Uzazi: Mjamzito Anatapika Swawm Yake Inafaa?

SWALI:
 

Assalaamu Alaykum, kwanza hongereni kwa michango yenu munayotowe kwa jamii, suala langu ni kuwa mimi nina mimba na huwa natapika baadhi ya muda, je nikitapika wakati nina funga ya ramadhaani, ramadhaani yangu bado imo au itakuwa haimo.  Nategemea nitapata jibu zuri.


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Asli katika hukumu za Swawm ni kuwa mwenye mimba au mwenye kunyonyesha na akajiogopea nafsi yake au kilichomo katika tumbo lake hutakiwa afungue; ameruhusiwa kula na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipenda sana kuchukuwa ruhusa anayopewa na Allaah, hivyo ushauri ni kuwa chukua ruhusa na udhuru wake utapoondoka itamlazimu kulipa siku alizofungua.

 

Asli katika hukumu za kutapika kwa mwenye funga ni kama hivi:

 

1.     Kujitapisha kwa makusudi, hili linabatilisha funga kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Abu Hurayrah kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ataeghilibiwa na matapishi na kushinda kuyadhibiti kwa kuwa yamemjia kwa nguvu na kumshinda mpaka akatapika pasina hiyari yake, haitoharibika swawm yake; na atae jitapisha kwa makusudi atalipa” lmepokelewa na At-Tirmidhiy, Kitabu cha Swawm kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), mlango yaliyokuja katika aliyejitapisha kwa makusudi.

 

2.    Kujiwa na matapishi kwa nguvu na kushindwa kuyazuia na ikiwa halikurudi ndani hata kidogo, hili halibatilishi funga.

 

Kama hali yako iko katika hizo mbili basi hukumu ndio kama hivyo, na lililo bora ni kutojikalifisha kwani mwenye mimba ni katika walioruhusiwa kula kwani anahisabika kuwa ni mgonjwa kama kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

(Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine)) [Al-Baqarah: 185]

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share