04-Matendo Mema Na Athari Yake Katika Utajiri Na Ukunjufu Wa Rizki: Sababu Ya Kudhikishiwa Rizki
C. SABABU YA KUDHIKISHWA KATIKA RIZIKI
Hakika kupata dhiki katika rizki kuna sababu, na Ametupa habari Allaah katika kitabu Chake, na ametufahamisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) kuna amali (matendo) atakayefanya atanyimwa riziki.
1. KUMKANUSHA ALLAAH (UKAFIRI)
Nayo ni sababu kubwa na muhimu katika kudhikishiwa rizki, ama anayesema makafiri wamepewa rizki pana hayo ni kuwasubirisha wazidishe maovu na baada ya hapo Atawaadhibu Allaah.
Amesema Allaah:
“Na atakayejiepusha na mawaidha Yangu (haya) basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki na siku ya Qiyaama tunamfufua hali ya kuwa kipofu) Twaahaa: 124
Atakuwa na maisha ya shida (duniani, hatopata utulivu wala ukunjufu wa kifua, hata akistarehe atakavyo, akavaa atakacho, aishi anapotaka, hakika moyo wake daima una hofu na dhiki na tabu pia kutangatanga.
2. MAKOSA NA MADHAMBI
Anasema Allaah:
“Hayo (ya kuwafika balaa hizi) ni kwa sababu Allaah Habadilishi kabisa neema Alizowaneemeshea watu hata wabadilishe wao yaliyomo moyoni mwao.” Al-Anfaal: 53
Anatupa habari Allaah katika ukamilifu wa uadilifu Wake katika hukmu Yake kwamba Allaah Habadilishi neema Aliyomneemesha yoyote ila kwa sababu ya dhambi alizochuma.
Kutoka kwa Thawbaan kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) amesema: “Hakika mtu ananyimwa rizki kwa dhambi aliyofanya wala hairudishi Qadar ila du’aa, wala haizidi katika umri ila wema) Musnad Ahmad
3. ZINAA
Anasema Allaah:
“Wala msikurubie zinaa hakika hiyo (zinaa) ni uchafu (mkubwa) na ni njia mbaya (kabisa).” Israa: 32
Anasema Allaah Akiwakataza waja Wake zinaa na kutoikaribia.
Kutoka kwa Ibn ‘Umar amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):
“Zinaa inarithisha umaskini (Ufakiri), dhiki katika rizki, na maradhi mengi ni adhabu kwa ajili ya zinaa.
4. UBAHILI NA KUTOTOA
Amekataza Allaah ubakhili katika sehemu nyingi kwani ni katika sifa mbaya, na mwenye kusifika na tabia hii ameahidiwa maangamivu.
Anasema Allaah:
“Na wala wasione wale ambao wanafanya ubakhili katika yale Aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kuwa ni bora kwao (kufanya ubakhili huko) la, ni vibaya kwao. Watafunwa kongwa (madude ya kunasa shingoni) za yale waliyoyafanyia ubakhili siku ya Qiyaama. Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Allaah. Na Allaah Ana habari za (yote) mnayoyafanya.” Al-'Imraan: 180
Yaani asidhani bakhili kukusanya kwake mali kutamfaa bali itamdhuru katika dini yake na huenda ikamdhuru pia duniani.
Anasema Allaah:
“Loo nyinyi mnaitwa mtoe (mali) katika njia ya Allaah na kuna wengine katika nyie wanafanya ubahili basi afanyaye ubahili anafanya ubakhili huo kwa (kuidhuru) nafsi yake mwenyewe. Na Allaah ni Mkwasi na nyinyi ndio makafiri. Na kama mkirudi nyuma (mkaupa mgongo Uislam), Allaah Ataleta watu wengine badala yenu nao hawatakuwa kama nyinyi (watakuwa bora).” Muhammad: 38
Kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) amesema:
“Ogopeni dhulma, hakika dhulma ni viza siku ya Qiyaama, na ogopeni ubakhili kwani umewaangamiza waliokuwa kabla yenu, iliwapelekea kumwaga damu zao na kuhalalisha haramu.”
Kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriy amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):
“Mambo mawili hayakusanyiki kwa Muumin, ubahili na tabia mbaya.” At-Tirmidhiy
Kutoka kwa Abu Hurayrah amesema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) amesema:
“Hakuna siku wanayopambazukiwa waja ila Malaika wawili wanashuka anasema mmoja wao, Ee Allaah mpe mtoaji badala, na anasema mwengine, Ee Allaah mpe anayezuia maangamizi.” Al-Bukhaariy