Mumewe Amefariki Tokea Miaka Miwili Nyuma Hakugaiwa Mirathi Yake Na Wanaohusika

SWALI:

 

Salaam Aleikum Warahamatullah Taaalah Wabarakatu.

 

Nashukuru kwa kutupa wasaa wa kuuliza maswali ya URITHI: Dada yangu Amefiwa Mume mwaka 2006 mwezi wa 9, lakini mpaka sasa sijaona mgao wa mirathi, Mume huyo ameacha Baba na Mama, Mke, watoto wanne, na ana wadogo zake 9 wa kike na wa kiume. Aliyefariki ameacha gari na linafanya kazi.

 

Msimamizi wa mirathi ni Mdogo wa kiume wa Aliyefariki. Lakini Mali ya aliyefariki ipo na Baba yake pamoja na watoto, mke amerudi kwao hana kitu chochote zaidi ya nguo zake, je ni halali? Naomba nijibiwe ili niweze kumsaidia dada yangu, ambaye hupo kwenye mtihani mkubwa.


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mirathi ya aliyefiliwa na mumewe. Hakika ni kuwa mtu anapofariki anatakiwa ashughulikiwe kwa kuzikwa, kulipiwa madeni na kutoa kiasi alichokitoa kwa ajili ya watu wasiorithi au kwa mikakati ya Kidini. Na kiasi cha wakfu hakifai kuzidi thuluthi (1/3).

 

Baada ya masurufu hayo kutolewa na kukabakia kitu au vitu vitahitajika kugaiwa wenye kurithi pekee. Na kulingana na listi yako wale ambao wanarithi kisheria ni baba mzazi wa aliyefariki, mama, watoto wake na mke aliyeachwa na kumkalia eda. Ama fungu la mke ni makhsusi alilopewa na Allaah Aliyetukuka pindi aliyefariki anapokuwa na watoto kama ilivyo kwa dadako, hivyo fungu lake litakuwa ni thumuni (1/8) kwa kilichobaki.

 

Kwa hiyo, mfanyie bidii dada yako awe ni mwenye kupata haki yake aliyopewa na Allaah Aliyetukuka katika Qur-aan. Na kufanya hivyo tunakuomba ufuate utaratibu ufuatao:

 

  1. Jaribu mwanzo kuzungumza na baba wa aliyefariki kuhusu suala hilo la mgao, ikiwa haikuwezekana, basi;
  2. Jaribu kuzungumza na ma-Shaykh walio katika kijiji au mji mnaoishi kuhusu hilo. Ikiwa hamkufanikiwa,
  3. Itabidi mwende kwa Qaadhi, ikiwa yupo katika mji mnaoishi.

 

Tunakuombea kila aina ya mafanikio katika kumpatia dada yako haki yake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share