03-Kukata Undugu: Sababu Za Kukata Undugu

 

SABABU ZA KUKATA UNDUGU

 

 

1. UJINGA

 

Ujinga unapelekea kukata undugu.

 

 

2. UDHAIFU KATIKA UCHA MUNGU (TAQWA)

 

Itakapodhoofika Ucha Mungu hajali mtu kukata Aliyoamrisha Allaah kuunga wala hatamani ujira wa uungaji na hajali matokeo ya ukataji.

 

 

3. KIBRI

 

Baadhi ya watu wakipata cheo cha juu au akapata nafasi nzuri au akawa mfanyibiashara mkubwa anafanya kibri kwa ndugu wa karibu; anaacha kuwatembelea na kuwapenda anaona yeye ndiye mwenye haki na yeye ni bora kutembelewa na kuijiwa.

 

 

4. KUPOTEA KWA MUDA MREFU

 

Kuna baadhi ya watu wanawapotea ndugu zao muda mrefu anaanza kusema nitawazuru mpaka anazoea kuwa mbali nao na anawakata.

 

 

5. KULAUMU SANA

 

Baadhi ya watu anapofanyiwa ziara na mmoja wa ndugu baada ya kupoteana muda mrefu, anamshushia mvua ya lawama na amepuuza katika haki yake na anafanya taratibu katika kumzuru hili linapelekea ndugu kuogopa kumzuru kwani atalaumiwa.

 

 

6. KUJIKALIFISHA ZAIDI

 

Mwingine anapozuriwa na ndugu anajilazimisha kuliko inavyohitajika na anajitia hasara kwa mali nyingi anajiandaa kumkirimu na anaweza kuwa hali yake ni duni. Hivyo ndugu anapunguza ziara anaogopa kumtia nduguye katika matatizo.

 

 

7. KUTOWAJALI WANAOKUZURU

 

Miongoni mwa watu, anapotembelewa na ndugu hajali wanapozungumza, hawasikilizi katika mazungumzo yao, wala hafurahii kuja kwao, wala hawashukuru kwa kuja kwao, hawapokei kwa furaha, anajivuta jambo linalopelekea ndugu kutomtembelea.

 

 

8. UCHOYO NA UBAHILI

 

Baadhi ya watu Allaah Anapowaruzuku mali au cheo anawakimbia ndugu, sio kwa kibri, ila anaogopa kufungua mlango na nduguze wataanza kumtembelea na kutaka msaada au linginelo.

 

Badala awafungulie mlango awakaribishe na awahudumie kwa analoweza au kuomba samahani kwa asiloliweza, bali anawaepuka anawahama ili wasimsumbue kwa kutaka misaada mingi kama anavyodai.

 

Ni nini faida ya mali au cheo akiwanyima nduguze?

 

Amesema Zuhayr bin Abi Sulma:

 

ومن يك ذا فضل فيبخل بفضله

علي قومه يستغن عنه ويذ مم

 

“Mwenye kuwa na uwezo akafanya ubahili kwa watu wake, akafaidika nao mwenyewe na kulaumiwa.”

 

 

Na uzuri ulioje wa aliyoyasema Al-Baaruudiy:

 

فلا تحسبن المال ينفع

اذا هو لم تحمد قراه العشائر

 

“Usihesabie (usidhani) mali inanufaisha, ikiwa yeye hatosifiwa na wa karibu”

    

Na katika yaliyosemwa:

 

ومن ذا الذي ترجو الأباعد نفعه

اذا كان لم يصلح عليه الأقارب

 

“Ni kitu gani tunachosubiria wa mbali kutunufaisha, ikiwa ndugu wa karibu hawawezi kutunufaisha?”

 

 

9. KUCHELEWESHA KUGAWA MIRATHI

 

Inaweza kuwa baina ya ndugu Mirathi haijagaiwa ama kwa uvivu wao au baadhi wana makusudi ya kuchelewesha au mfano wake.

 

Kila unapochelewa ugawaji wa Mirathi na muda kupita, kunaenea uadui na bughdha baina ya ndugu huyu anataka haki yake katika Mirathi atajirike, mwengine anakufa, na wanapata tabu walio baada yake kukusanya wakala wapate fungu lao, mwengine anamdhania mwenzie vibaya, yanazidi matatizo na inaenea kuhamana.

 

 

10. USHIRIKA BAINA YA NDUGU

 

Mara nyingi ndugu wanashirikiana katika mradi au shirika fulani bila kuafikiana katika misingi madhubuti na bila ya kusimamia Ushirika kwa uwazi, bali kwa kuridhishana ya uongo na kutodhaniana vizuri.

 

Uzalishaji utakapoongezeka na kutanuka mzunguko wa kazi, kunazuka hitilafu na ubaya pia dhana mbaya, na haswa ikiwa wana uchache wa Ucha Mungu na kujitolea au ikiwa baadhi yao wanang’ang’ania rai zao au upande mmoja ukawa unashughulika zaidi.

 

Na hapa uhusiano unakuwa mbaya na kufarakana na inaweza kufikia kushtakiana mahakamani.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

“ … Na hakika washirika wengi hudhulumiana wao kwa wao, isipokuwa walioamini na wakatenda mema. Na hao ni wachache…” Swaad: 24.

 

 

11. KUSHUGHULIKA NA DUNIA

 

 

12. TALAKA BAINA YA NDUGU

 

Inaweza kutokea talaka baina ya ndugu, yanazidi matatizo baina ya ndugu zao ama kwa sababu zinazohusiana na talaka au mengineo.

 

 

13. UMBALI WA MASAFA NA KUFANYA UVIVU KATIKA ZIARA

 

 

14. KUWA KARIBU KATIKA MAKAZI BAINA YA NDUGU

 

Huenda hili likasababisha kukatana. Imepokelewa kutoka kwa ‘Umar bin Al-Khattwwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

“Waamrisheni wenye undugu watembeleane wala wasiwe majirani.”

 

Ameongezea Ghazaali kutokana na maneno ya ‘Umar “amesema hivyo kwani ukaribu unaleta msongamano katika haki na huenda likarithisha chuki na kukatana.”

 

Amesema Aktham bin Asw-Swayfi:

 

“Kuweni mbali katika majumba  kuweni karibu katika mapenzi.”

 

Kisha kuwa karibu katika masafa kunaweza kusababisha matatizo, na yanatokea matatizo kwa sababu inaweza kuwa baina ya watoto mashindano na yanaweza kuhama hadi kwa wazazi, kila mzazi anajitahidi kumtetea mwanae na kunaanza uadui na mwisho kutengana.

 

 

15. UCHACHE WA KUWASTAHAMILIA NDUGU NA KUWASUBIRIA

 

Baadhi ya watu hawawezi kustahamili kitu kidogo kutoka kwa ndugu kosa dogo tu au kulaumiwa na mmoja wa ndugu anafanya haraka kukatana na kuhamana.

 

 

16. KUWASAHAU NDUGU KATIKA SHUGHULI NA HARUSI

 

Inaweza kuwa kwa mmoja wa wanafamilia ana harusi au sherehe fulani, anawaalika ndugu kwa mdomo au kadi au kwa simu, huenda akamsahau mmoja katika ndugu au huenda aliyesahauliwa ni dhaifu wa nafsi au ana tabia ya dhana mbaya; anafasiri kusahaulika kwamba wamempuza na kumdharau anaamua kwa dhana hiyo kuwahama.

 

 

17. HASADI

 

Kuna aliyeruzukiwa elimu au cheo au mali au kupendwa, na wengine unakuta anawahudumia ndugu zake anawafungulia moyo wake mwema, kwa hilo huenda baadhi ya ndugu wakawa wanamhusudu na wanamsababishia uadui na kutia shaka katika uaminifu wake.

 

 

18. MIZAHA MINGI

 

Mizaha mingi ina athari mbaya,huenda ikatoka neno la kujeruhi kwa mtu, hachungi hisia za wengine, ikampata mtu anayeathirika haraka, ikazaa chuki bughdha kwa muongeaji.

Na hili linatokea sana baina ya ndugu kwa kukutana kwao sana.

 

Amesema Ibn ‘Abdil-Bariy:

 

“Kundi la Ulamaa limechukia kuzama katika mizaha, kutokana na mwisho mbaya…”

 

 

19. UCHONGANISHI

 

Katika watu kuna ambaye katika tabia yake Allaah Atuepushe anaharibu uhusiano ulio baina ya wapendanao, unamkuta anapupia baina ya wapendanao kuwatenganisha na kuchafua usafi wao, ni ndugu wangapi wametengana kutokana na mchonganishi, mmbeya.

 

Anasema Al-‘Aashiy:

 

“Mwenye kumtii mchonganishi hatomuachia rafiki hata kama alikuwa ni kipenzi aliye karibu.”

 

 

20. TABIA MBAYA KATIKA BAADHI YA WAKE

 

Baadhi ya watu wanaweza kuwa na mtihani na mke mwenye tabia mbaya hawezi kumstahamilia yeyote, hataki ndugu au yeyote washirikiane naye kwa mumewe, anamzuia akitaka kuwakaribisha, na wanapomzuru ndugu wa mume haonyeshi furaha, hili linasababisha ndugu kukatana.

 

Baadhi ya waume wanampa uongozi mke akiwaridhia ndugu zake anawaunga na ndugu asiowataka mke anawakata na huenda akamtii katika kuwakata wazazi.

 

Share