Mashairi: Kwa Nini Tumeumbwa?
Kwanini Tumeumbwa?
Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)
Salaam zipokeeni, zinatoka Arabuni,
Ndugu wote na jirani, na rafiki wa zamani,
Na nyote mpo moyoni, nimehifadhi kichwani,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Sio bila ya sababu, Ametuumba Manani,
Kaumba Tumuabudu, Peke Yake Rahmani,
Wanyama hata wadudu, binadamu na shetani,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Wote Wanamuabudu, na samaki baharini,
Wote Wanamuabudu, na wanyama wa porini,
Wote Wanamuabudu, na ndege wote mwituni,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Kusujudu kakataa, Ibilisi malu'uni,
Kajiletea balaa, akatutia kundini,
Anachochea makaa, tuwe nae adhabuni,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Kamshawishi Adamu, akafukuzwa peponi,
Kaacha yote karamu, binadamu tazameni,
Mwenyewe kajilaumu, akaomba samahani,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Binadamu, Ibilisi, walifukuzwa mbinguni,
Kwa ajili ya maasi, na kukosa shukurani,
Tupo kwenye wasiwasi, tunaishi mashakani,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Ibilisi akasema, hatuachi asilani,
Sana atatuandama, atuingize motoni,
Hapo siku ya Qiyama, atajitenga pembeni,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Tupo nae hivi sasa, njiani na majumbani,
Hutufanyisha makosa, na hata msikitini,
Hatotuacha kabisa, mpaka tuzikwe shimoni,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Katuumba Subhaana, Tumuabudu yakini,
Si usiku si mchana, ibada tuwe makini,
Kwa marefu na mapana, tuizingatie dini,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Tupo hapa duniani, tumepewa mtihani,
Ili Aone mwishoni, ataepasi ni nani ?
Na yote Amebaini, tunayaona machoni.
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Mitume Aliwatuma, kuhubiri ardhini,
Maovu yote na mema, tulikanywa hadharani,
Na Mola Aliosema, yamo kwenye Qur-aani,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Ibada kitu cha kwanza, tuiweke akilini,
Haihitaji nyongeza, imekamilika dini,
Na wala kuipunguza, na kubadili maoni,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Hatukuja kutembea, kustarehe nchini,
Mola Ametuwekea, sheria tuziamini,
Yule Ataepotea, atajuta kaburini,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Majuto ni majukuu, mwisho yatafaa nini?
Ukipatwa na makuu, wa kukuokoa nani?
Kumbuka Alie juu, na hisabu na mizani,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Kwa hivyo na tukazane, thawabu zikusanyeni,
Kwa mema na tushindane, kila kizuri fanyeni,
Na usiku wa manane, kwa Mola sana ombeni,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Usisahau dunia, tule halali kazini,
Mali ukijipatia, ukumbuke masikini,
Usibadili tabia, kudharau walo duni,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Tukae tukikumbuka, maisha fupi jamani,
Mema tufanye haraka, tutakufa karibuni,
Hatutaishi miaka, tutarudi mchangani,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.
Hapa nafunga shairi, nimefika kikomoni,
Naomba kila la kheri, tukhitimu kwa amani,
Tuepukane na shari, na shetani tumlaani,
Ametuumba Manani, Pekee Tumuabudu.