Mawasiliano Na Mwanaume Asiye Na Maadili Ya Kiislamu Anayetaka Kunikurubia Bila Ya Ndoa
Mawasiliano Na Mwanaume Asiye Na Maadili Ya Kiislamu Anayetaka Kunikurubia Bila Ya Ndoa
Swali:
Assaalaam aleykum,
Nina mtihani naomba mnisaidie kuna mwanaume ananipenda lkn navyomuhisi nia yake Allaah anajua zaidi anataka kua na mimi kunyume na maadili yetu yaani anataka ukaribu na mimi pasipo ndoa kwanza kitu ambacho namuomba Allaah aninusuru. Mtihani wangu ni kwamba na mimi nimempenda huyo mwanaume lkn nampenda kwa ajili ya Allaah na ninatamani kama ana kheri na mimi awe mume wangu na ninaumia roho kumuona haswali na pia ananipenda kwa maasi natamani niwe karibu nae nanimshauri ktk mazuri na kwa uwezo wa Allaah awe mcha wa Allaah. Lakini sijui nifanye nini naomba msaada kwenu moja kama kuna dua yoyote nimsomee hata kwenye maji ili atakapo kunywa, abadili nia yake kwangu awe na nia njema, awe ananisikiliza pale nitapompa ushauri ktk mambo mema, aachane na starehe za dunia. Pia nisome dua gani ili niache kumpenda kwani pengine hajapangwa na Allaah kuwa mume wangu nitabaki naumia bure bora nimpende kama kaka kaka yangu tu.ntafurahi mkinisaidia.
Jibu:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Tambua kuwa mtihani kama huo wa kuwasiliana au kutaka kuwa na urafiki na mwanamume kinyume na sheria na asiye na maadili ya dini ni mitihani ya kujitakia mwenyewe. Jambo la kwanza ilipasa uepukane naye kabisa. Hakuna mapenzi ya Allaah ikiwa mtu hana maadili bali huwa ni kinyume chake. Kwa sababu mwenye mapenzi na Allaah ni yule mwenye kufuata amri Zake na amri za Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Ikiwa yeye anataka kukutumilia kwa kutaka mawasiliano bila ya kufunga ndoa, huyo amevuka mipaka ya dini na hivyo huyo sio mtu wa kutangamana naye bali ni kuepukana naye kabisa. Kwa hiyo kusema 'Nampenda kwa ajili ya Allaah' haina maana iliyokusudiwa katika 'mapenzi kwa ajili ya Allaah'.
Jambo ambalo unaweza kujaribu kufanya ni kumfahamisha ukweli kuwa hayo mahusiano si ya kisheria na yanapingana na maamrisho ya dini yetu. Na ikiwa huwezi kumkabili mwenyewe, basi tafuta mtu wa karibu naye aseme naye kwa kumpa mawaidha na amtambulishe kuwa wewe unataka kuungana naye kindoa ila haitowezekana hadi abadilishe maadili yake, na afuate sheria za Kiislamu ipasavyo katika mawasiliano. Amuulize kwanza kama anakutaka kikweli kwa ndoa au anataka kukuchezea tu. Hapo ndipo mtakapotambua nia yake na hapo ndio utakapoamua uamuzi wa mwisho ikiwa anakufaa au hakufai. Au unaweza kumkabili mwenyewe na kumuuliza akujulishe wazi wazi. Kama anakutaka kikweli basi haraka abadili maadili yake kisha ndio apeleke posa kwenu.
Ama kuhusu kumsomea du'aa au kumtilia katika maji kitu ni itikadi isiyo sahihi na haipasi kabisa kufanya hivyo. Haya ni kama wafanyao waganga ambayo hutumia njia zisizokubalika katika dini.
Inavyoonyesha kuwa tayari uko karibu naye hadi inafika kuwa unaweza kumpa maji. Tunakupa nasaha ya dhati dada yetu haraka ujiepushe naye, kwani Shaytwaan yuko pamoja na nyinyi na hatakuacheni hadi akutumbukizeni katika maasi. Hapo tena utakuja kujuta majuto makubwa kwani athari yake itakuwa ya milele kwako. Yeye atakugeuka atakapomaliza haja yake nawe, na hii ndio kawaida ya wanaume wengi. Kisha utabaki wewe na doa la maisha na kuathiri maisha yako kwa ujumla, pamoja na kuwa aibu itakupata mwenyewe, mbali familia yako, mbali itakapotokea kuwa umeshika mimba athari itabakia milele kwako, mtoto wako, na jamii nzima. Almuradi hutokuwa na raha maishani mwako mwote na utabaki na majuto milele. Achana naye kabisa na badala yake tafuta furaha ya moyo kwa Rabb wako Ambaye Pekee Ataweza kukupa faraja na hata kukujaalia kupata mume mwenye kheri na wewe utakayeridhika naye, utakayempenda kuliko huyo na utabakia katika usalama.
Amka usiku wa manane yaani thuluthi ya mwisho ya usiku, na omba sana du'aa. Tumia pia nyakati nyinginezo kama baina ya Adhaan na Iqaamah, n.k. Funga Swawm na uombe sana kwani du'aa ya mwenye kufunga hukubaliwa. Soma sana Qur-aan na adhkaar upate furaha na utulivu wa moyo. Na kumbuka kwamba Allaah Anakupenda hadi Amekutanabahisha kuwa huyo mtu sio mzuri hadi utafute nasaha kabla ya kujitumbukiza katika maasi naye. Hivyo inapasa umshukuru Allaah na tambua kuwa utakapojiepusha na jambo ovu kwa ajili Yake, Atakubadilishia lililo bora kuliko hilo.
Tunatumai utafuata nasaha zetu hizi haraka na tunakuombea taqwa na Allaah Akupe furaha na Akupe utakalo lenye kumridhisha Yeye Subhaanahu wa Ta'aalaa.
Na Allaah Anajua zaidi