Kusoma Qur-aan Katika Maji, Kuomba Haja Kwa Kusoma Mara Kadha Na Kadhaa
Kusoma Qur-aan Katika Maji Kuomba Haja Kwa Kusoma Mara Kadha Na Kadhaa
SWALI:
Assalamu Aleikum natoa shukurani nyingi kwa Allaah pia nawatakia kilala kheri namafanikio mema ndugu zangu kwa iman Alhidaaya Allaah atawalipa In shaa Allaah
BISMILLAH: suali yangu jee ukisoma aya za ALLAAH ktk maji halafu ukanyunyizia katika ukuta inafaa? pia kunakijitabu kidogo ina elezea fadhila ya surat fatiha kua ukitaka matatizo yaondoke sijui usome mara kadha pia ukitaka kitu omba mara kadha jee ni sawa? shukran kwa kunisikia nawatakia kilala kheri
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani kwako pia ndugu yetu katika Imani nasi tunakutakia kila la kheri katika mambo yako hapa. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atulipe sote ujira ulio bora kwa kutupatia Tawfiyq katika nyumba mbil; duniani na Aakhirah.
Swali lako hili halijaeleweka vyema kwani hakuna mahusiano yoyote yale baina ya kuyasomea maji na baadaye kunyunyiza katika ukuta. Je, katika kufanya hivyo umesikia kunaleta natija gani? Mambo yetu yote tunayoyafanya ni lazima yaafikiane na Shariy’ah na lau hayatakuwa ni yenye kuafikiana basi tutakuwa tunapata hasara. Jambo hilo halikuthibiti katika Dini yetu.
Ama kuhusu swali lako la kusoma Suwratul-Faatihah mara kadhaa na matatizo yako yatakuwa ni yenye kuondoka, hilo pia halikuthibiti katika Dini. Zipo Du’aa ambazo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuagizia tuzisome mara kadhaa na fadhila zake kwa mfano Suwrah Al-Ikhlaasw, Al-Falaq na An-Naas na pia baadhi ya Aayah. Ama kuhusu Suwrah Al-Faatihah haijathibiti kuwa inatakiwa uisome mara kadhaa ili uondokewe na matatizo yako, ila ina fadhila nyingi mojawapo ni ya kuponyesha magonjwa kama ilivyokuja katika Hadiyth ifuatayo
"Kundi la Swahaba walielekea katika safari hadi wakafika karibu na kabila fulani la Waarabu wakawaomba wawapokee kuwa wageni wao lakini walikataa kuwapokea. Mkuu wao akatafunwa na nyoka (au nge) na wakampa kila aina ya tiba lakini hazikumfaa. Baadhi yao wakasema: "Hebu waendeeni kundi la wasafiri walioteremka karibu yetu na waulizeni kama wanajua tiba yoyote?". Wakawaendea Swahaba na kuwaambia: "Enyi watu! Mkuu wetu ametafunwa na nyoka (ametafunwa na nge) na tummetibu kwa kila aina ya tiba lakini hakuna kilichomfaa. Je, kuna mmoja wenu anayejua cha kumfaa?" Mmoja wa Swahaba akasema: "Wa-Allaahi najua kutibu kwa Ruqyah. Lakini Wa-Allaahi nyie mmekataa kutupokea kama wageni wenu. Kwa hiyo hatutamtibu mgonjwa wenu hadi mtulipe".
Wakakubali kuwapa wasafiri (Swahaba) kundi la kondoo. Akaenda Swahaba (pamoja na watu wa kabila) akamtemea mate (alipotafunwa) na kumsomea Suwrah Al-Faatihah hadi mgonjwa akapata nafuu na akaanza kutembea kama kwamba hakuwa akiumwa. Kabila hili lilipowalipa malipo walioyokubaliana, baadhi yao (Swahaba) wakasema: "Gaweni (kondoo)" Lakini yule aliyefanya Ruqyah alisema: "Msifanye hivyo hadi kwanza tuelekee kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuelezea yaliyotokea ili tuone atatuamrisha nini". Wakaenda kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuelezea kisa chao naye akasema: ((Mmejuaje kuwa Suwrah Al-Faatihah ni Ruqyah? Mmefanya jambo la haki. Gaweni (mliyopewa) na munipe na mimi sehemu yangu)) [Al-Bukhaariy]
Bonyeza viungo vifuatavyo upate faida zaidi:
Ruqyah: Kinga Na Tiba Katika Shariy'ah
Du’aa Za Ruqyah (Kinga) Faida Na Sharh Zake
Na Allaah Anajua zaidi