06-Mapenzi Ya Ahlus-Sunnah Juu Ya Ahlul-Bayt: Elimu Ya Ghaibu Na Kukingwa

Elimu Ya Ghaibu Na Kukingwa

 

Sisi tunawaheshimu na tunawaenzi watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), lakini hatuamini kama wanavyoamini Shia kuwa wao wanajua elimu ya Ghaibu na wamekingwa hawafanyi makosa n.k. Tunaamini kuwa mwenye kujua ghaibu ni Allaah Peke Yake.

 

Allaah Anasema:

 

قل لا يعلم من في السموات والأرض الغيب إلا الله" [النمل: 65]

 

Sema: “Hakuna aliyeko katika mbingu na ardhi ajuaye Ghayb (yasiyotokea) ila Allaah." An Naml-65

 

Na Akasema:

 

قل لا أملك لنفسي نفعا ولا ضرا إلا ما شاء الله ولو كنت أعلم الغيب لاستكثرت من الخير وما مسني السوء إن أنا إلا نذير وبشير لقوم يؤمنون

 

Sema: “Sina mamlaka ya kujipa nafuu wala ya kujindolea madhara ila Apendavyo Allaah; na lau kama ningelijua ghaibu ningejizidishia mema mengi; wala isingalinigusa dhara. Mimi si chochote ila ni muonyaji na mtoaji wa habari njema kwa watu wanaoamini.” Al-A’araaf-188

 

Na tunaamini kuwa aliyekingwa ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) peke yake.

 

Allaah Anasema:

 

وَاللّهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ

 

Na Allaah Amekukinga Al-Maidah-67

 

Sisi tunaamini kuwa hapana yeyote aliyekingwa (Ma’aswuum معصوم), si katika watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wala katika Masahaba wake, kwa sababu zifuatazo:

 

1.     Hapana nassw iliyo wazi isiyopingika inayoeleza juu ya kukingwa kwao. Lau kama ingekuwepo basi tungelifuata bila matatizo wala kipingamizi.

 

2.     Hapana hata mmoja katika watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliyedai kuwa yeye amekingwa, akawataka watu waamini hivyo, isipokuwa katika vitabu ambavyo Maulamaa wote kama vile Ibni Kathiyr na Ibni Hajar na Adh-Dhahabiy na wengineo wamesema kuwa hadithi hizo si dhaifu tu, bali maudhui. (zimepachikwa).

 

3.     Hapana hata mwanachuoni mmoja katika Maulamaa wetu aliyesema hivyo, juu ya kukhitalifiana kwao katika mambo mengi, lakini juu ya jambo hili hapana hitilafu baina yao.

 

4.     Lau kama wangelikuwa wamekingwa, basi wasingelikubali kukosolewa na mtu yeyote katika Ijtihadi zao. Kwa mfano kama ‘Aliy (Radhiya Allaahu anhu) angelikuwa amekingwa, basi asingelikubali kukosolewa na Abu Bakr au ‘Umar au ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhum), na anapokosolewa angelisema kwa mfano; ‘Vipi mnanikosoa wakati mimi nimekingwa?’

Lakini ‘Aliy alikuwa akiwakosoa na wao walikuwa wakimkosoa, akiwaheshimu na wao wakimuheshimu, akiwapenda na wao wakimpenda.

 

5.     Maulamaa wanasema kuwa التطهير  ‘kusafishwa’ kama ilivyokuja katika aya, maana yake si kukingwa, bali ni kusafishwa na kutakaswa. Na  si kila aliyetakaswa amekingwa akawa hafanyi makosa, ama sivyo basi kila aliyesifiwa kuwa ametakaswa au amesafishwa atakuwa amekingwa. Kama ilivyokuja katika hadithi:

 

واجعلني من التوابين واجعلني من المتطهرين

 

Na unijaalie niwe miongoni mwa waliotubu na unijaalie niwe miongoni mwa wenye kujitakasa.

 

Na  Allaah Anawapenda wenye kutubu na Anawapenda wenye kujitakasa, lakini haimaanishi kuwa hao wamekingwa hawafanyi makosa.

 

6.     Kama Muislamu atachukua elimu yake kutoka katika Qur-aan na Mafundisho ya Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) peke yake bila ya kuchukua kutoka kwa watu wa Ahlul Bayt, huyo Uislamu wake unakuwa sahihi na hauna dosari yoyote. Wangelikuwa Ahlul Bayt wamekingwa ‘Ma’aswuumiyn’, basi ingelimuwajibikia kila Muislamu kuchukua elimu kutoka kwao.

 

7.     Kwetu Ahlus Sunnah, Abu Bakr na ‘Umar ni viumbe bora kupita wote  baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) mara zote alikuwa akiwatanguliza mbele ya ‘Aliy. Alikuwa akimuacha Abu Bakr aswalishe na ‘Aliy akiswali nyuma yake, na hapana hata mmoja katika Ahlus Sunnah aliyewahi kusema kuwa Abu Bakr amekingwa (Ma’aswuum معصوم). Itakuwaje basi awe mwengine asiyekuwa yeye?

 

8.     Imepokelewa kuwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwasifia waliojitenga katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, na alijuta kwa yaliyotokea katika vita vya ngamia na vita vya Swiffiyn. Angelikuwa amekingwa asingetenda matendo kisha akajuta.

 

9.     Imepokelewa kuwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipanda juu ya mimbari katika mji wa Al-Kuufa akasema:

«Namshitakia Allaah dhiki zangu na matatizo yangu.»  Kisha akasema:

«Wana daraja zao kwa Allaah Muhammad bin Maslamah na Usaamah bin Zayd na Sa’ad bin Abi Waqaas. Kama ni shari basi ndogo, na kama ni kheri basi ni nyingi (kwa kujitenga kwao na fitna).»

Naye ni mkweli (Radhiya Allaahu ‘anhu), lakini angelikuwa Ma’aswuuwm basi asingetamka haya. Asingewasifia waliojitenga na  fitna ile wakati yeye mwenyewe alikuwemo ndani yake.

 

10.             Siku ya Saqiyfah, siku ile baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kufariki dunia, wakati Waislamu walipojumuika na kumchagua Abu Bakr kuwa Khalifa wao, hapana hata mmoja aliyejitokeza akasema : «Jamani tunaye aliyekingwa hapa, kwa hivyo yeye ndiye anayestahiki kuchaguliwa.» Hilo halijatokea, na siku ile walikuwepo waliopigana vita vya Badr na pia walikuwepo wale ambao Allaah Alitangaza kuridhika nao chini ya mti. Inaingia akilini kweli kuwa watu wote hao waliosifiwa na Allaah ndani ya Qur-aan Tukufu, na wakasifiwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wafanye njama dhidi ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)?

 

 

Share