12-Mapenzi Ya Ahlus-Sunnah Juu Ya Ahlul-Bayt: Hitimisho

 

Hitimisho

 

Kwa kumaliza, hatusemi kuwa Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wamekingwa na kufanya makosa 'Maaswuwmiyn' au 'hawakosei'. Bali wao ni viumbe wanaokosea kama viumbe wengine. Tunachotaka na kusisitiza ni kuwanasihi ndugu zetu; ikiwa kweli wanautaka umoja wa Kiislamu, na wanapenda Waislamu waungane wawe kitu kimoja bila kujali madhehebu, basi waache kuwatukana na kuwalaani na kuwadhalilisha na kuwafanyia chuki Maswahaba hawa waliotukuzwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Maswahaba walioibeba Qur-aan hii tukufu tuliyonayo majumbani mwetu na Misikitini na kila mahali wakaifikisha kwetu na kuieneza kila pembe ya ulimwengu. Bila ya juhudi zao kubwa na kujitolea kwao mhanga kwa hali na mali, wakapigana jihadi dhidi ya maadui wa Allaah, dini isingeweza kutufikia, na tungelibaki hadi leo tukisujudia moto na masanamu na mizimu.

 

Walipotawala, dola kubwa kubwa zilisalimu amri mbele ya majeshi yao, na ulimwengu wote ulikuwa chini ya amri yao.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema juu yao:

 

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُواْ وَهَاجَرُواْ وَجَاهَدُواْ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللّهِ وَالَّذِينَ آوَواْ وَّنَصَرُواْ أُوْلَئِكَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاء بَعْضٍ وَالَّذِينَ آمَنُواْ وَلَمْ يُهَاجِرُواْ مَا لَكُم مِّن وَلاَيَتِهِم مِّن شَيْءٍ حَتَّى يُهَاجِرُواْ وَإِنِ اسْتَنصَرُوكُمْ فِي الدِّينِ فَعَلَيْكُمُ النَّصْرُ إِلاَّ عَلَى قَوْمٍ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُم مِّيثَاقٌ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿72﴾ وَالَّذينَ كَفَرُواْ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاء بَعْضٍ إِلاَّ تَفْعَلُوهُ تَكُن فِتْنَةٌ فِي الأَرْضِ وَفَسَادٌ كَبِيرٌ ﴿73﴾ وَالَّذِينَ آمَنُواْ وَهَاجَرُواْ وَجَاهَدُواْ فِي سَبِيلِ اللّهِ وَالَّذِينَ آوَواْ وَّنَصَرُواْ أُولَئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا لَّهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ

 

Hakika wale walioamini na wakahama na wakapigania Njia ya Allaah kwa mali yao na nafsi zao, na wale waliotoa mahala pa kukaa, na wakanusuru, hao ni marafiki na walinzi wao kwa wao. Na wale walioamini lakini hawakuhama, nyinyi hamna waajibu wa ulinzi kwao hata kidogo mpaka wahame. Lakini wakiomba msaada kwenu katika Dini, basi ni juu yenu kuwasaidia, isipo kuwa juu ya watu ambao yapo mapatano baina yenu na wao. Na Allaah Anayaona mnayoyatenda.

Na wale walio kufuru ni marafiki wenyewe kwa wenyewe. Msipofanya hivi itakuwako fitna katika nchi na fisadi kubwa.

Na walioamini wakahama na wakapigana Jihadi katika Njia ya Allaah, na waliotoa mahala pa kukaa na wakanusuru, hao ndio Waumini wa kweli. Watapata msamaha wa Allaah na kuruzukiwa kwema.

Al-Anfaal -72-74

 

Ndugu zangu Waislamu, aya hizi tukufu zinazungumza juu ya Maswahaba hawa (Radhiya Allaahu ‘anhum) walioamini wakahama (Watu wa Makkah) na walioamini wakatoa mahala pa kukaa (Watu wa Madiynah), kisha wakapigana Jihadi katika Njia ya Allaah wakiwemo Abu Bakr na ‘Umar na ‘Uthmaan na ‘Aliy na wenzao (Radhiya Allaahu ‘anhum jamiy’an).

 

Allaah Mwenye kujuwa yaliyodhihirika na yaliyojificha aliangalia ndani ya nyoyo zao akawapa sifa hizo wanazostahiki.

Allaah Anasema :

 

ألا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ {14)

 

Oh! Asijue Aliyeumba! Naye ndiye Avijuaye visivyojulikana na vinavyojulikana?

Al-Mulk - 14

 

Ndugu zangu Waislamu, zile kauli zisemazo kuwa ulikuwepo uadui baina ya Maswahaba na Watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) si sahihi. Hizi ni kauli zilizoingizwa ndani ya baadhi ya vitabu kwa ajili ya kujenga chuki baina yetu Waislamu na kututenganisha na kutudhoofisha. Msighururike nazo.

Na hapa tunakuleteeni mtiririko wa kauli mbali mbali kutoka kwa Maulamaa wa Kishia wenye kuonyesha mapenzi ya hali ya juu yaliyokuweo baina ya Maswahaba na baina ya Watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

 

Imam Hasan Al-Askariy ambaye ni Imamu wa kumi na moja katika madhehebu ya Shia Ithnaashariy akihadithia juu ya siku ya Hijrah allisema:

« Baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kumtaka ‘Aliy alale juu ya tandiko lake, alimuambia Abu Bakr  Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu): «Utakuwa radhi uwe pamoja nami ewe Abu Bakr ukitafutwa kama ninavyotafutwa na ukijulikana kuwa wewe ndiye mwenye kunisaidia katika haya ninayowalingania watu ndani yake, na utabebeshwa kwa ajili yangu kila aina ya adhabu?» Abu Bakr akasema: «Ewe Mtume wa Allaah, ama mimi hata kama nitaishi duniani nikaidhibishwa maisha yangu yote adhabu kali kali, bila ya kufa kifo cha uhakika na bila ya furaha, na yote haya yawe kwa ajili ya kukupenda wewe, basi hayo ni bora kwangu kuliko kuneemeka duniani nikiwamiliki wafalme wote dhidi yako. Kwani mimi na mali yangu na watoto wangu ni kitu gani isipokuwa ni kwa ajili yako.»

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: «Bila shaka Allaah Ameangalia ndani ya moyo wako akaona kuwa unakubaliana na yanayotamka ulimi wako. Akujaalie uwe mfano wa masikio yangu na macho yangu katika mwili, na roho katika nafsi.»

Tafsiri ya Al-Hasan Al-Askariy na Bihaar Al-Anwaar

 

Imepokelewa pia kuwa ‘Aliy bin Abi Twaalib alimuambia ‘Uthmaan (Radhya Llahu ‘anhum:

 

«Na WAllaahi sijui nikuambie nini. Hapana ninachokijua mimi usichokijua wewe, na hapana ninachoweza kukufundisha usichokifahamu, hatukukutangulia katika jambo lolote hata tuweze kukupa habari zake, wala hapana kilichofichika kwao tukakujulisha nacho. Umeona tuliyoyaona, na umeyasikia tuliyosikia, na umekuwa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kama tulivyokuwa pamoja naye, na wala si mwana wa Quhafa, (Abu Bakr Asw-Swiddiyq) wala si mwana wa Al-Khattwaab, (‘Umar bin Khattwaab) waliokutangulia katika haki. Na wewe umehusiana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) zaidi kuliko wao, kwa sababu umeoa kwake zaidi kupita walivyofanya wao. Kwa hivyo Allaah Allaah katika nafsi yako…»

Nahjul-Balaghah

 

Anasema Al Majlisiy kutoka kwa At-Tuwsy kuwa Imam ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwaambia sahibu zake :

 

«Nakuusieni juu ya sahibu zake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), msiwatukane kwani hawa ni Swahibu zake Mtume wenu, na ni Swahibu zake ambao hawajaongeza uzushi wowote katika dini, wala hawamuogopa mwenye kuleta uzushi. Ndiyo! Ameniusia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) juu yao hawa.»

Hayaat al-Quluub kilichoandikwa na Al-Majlisi- uk. 122

 

Na kutoka kwa Ja’afar Asw-Swaadiq kutoka kwa wazee wake kutoka kwa ‘Aliy amesema:

 

«Nakuusieni juu ya Swahibu zake Mtume wenu. Msiwatukane. Hawa hawajaongeza uzushi wowote, wala hawajampa ulinzi mwenye uzushi. Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ameusia juu yao kila la kheri. »

Bihaar al-Anwaar - 305 na Ash-Shi’ah al-Imaamiyah, kilichoandikwa na Dr. Al-Qifary - uk. 935

 

Na siku ile Ibni Muljam (mwenye kustahiki kutoka kwa Allaah kile anachostahiki) alipompiga upanga ‘Aliy bin Abi Twaalib na ‘Aliy alipohisi kuwa anafariki dunia, alimuusia mwanawe Al-Hasan akimuambia ; ‘Allaah Allaah (nakuusia) juu ya wake wa Mtume wenu, wasidhulumiwe wakati mpo hai. Na Allaah Allaah (nakuusieni) juu ya Sahibu zake Mtume wenu, kwa sababu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ameusia (mema) juu yao.’

Kashf al- Ghummah - 2/59 na Muqaatil atw-Twaalibin kilichoandikwa na Al-Asfahaani uk.39

 

Kutoka kwa Urwa bin ‘Abdillaah alisema :

 

Nilimuuliza Abu Ja’afar Muhammad bin ‘Aliy juu ya kuzipamba panga, akasema ; ‘Hapana ubaya, hata Abu Bakr Asw-Swiddiyq alikuwa akiupamba upanga wake (Radhiya Allaahu ‘anhu)’ Nikamuambia : ‘Na unamuita ‘ Asw-Swiddiyq ?’ anasema : ‘Aliinuka kwa haraka sana akaelekea Qiblah, kisha akasema ; ‘Naam (namuita) Asw-Swiddiyq Naam (namuita) Asw-Swiddiyq Naam (namuita) Asw-Swiddiyq, na asiyemuita kwa sifa hii basi hana ukweli wowote duniani wala akhera.’

Kashf al-Ghummah - 2/360.

 

Anasema ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu):

«Nilipokwenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kumposa Faatwimah aliniambia: ‘Uza ngao yako kisha niletee thamani yake ili nipate kukutayarishia wewe na binti yangu Faatwimah kitakachoweza kukufaeni.» Anasema ‘Aliy : «Nikaichukua ngao yangu nikaenda nayo moja kwa moja mpaka sokoni nikamuuzia ‘Uthmaan kwa Dirham mia nne. Na baada ya kupokea pesa zangu na baada ya ‘Uthmaan kuipokea ngao yangu, akasema: Ewe Baba yake Hasan, ngao hii si imekuwa yangu na Dirham zimekuwa zako ?» Nikamuambia: «Ndiyo.» Akaniambia: «Basi ngao hii ni zawadi yako kutoka kwangu. »  Nikaichukua ngao na Dirham nikaenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) nikaiweka ngao pamoja na pesa mbele yake, nikamhadithia aliyonitendea ‘Uthmaan, akamuombea dua ya kheri. »

Al-Manaaqib/Al-Khawarizmi uk. 252 na Kashf al-Ghummah 1/359 na Bihaar al-Anwaar/Al-Majlisi uk. 39-40

 

Tunamuomba msomaji arudie marejeo yote upate kumbainikia ukweli na ili apate kufikiri na kutanabahi juu ya msimamo wa wenye kuwalaani Maswahaba wakiwemo Makhalifa watatu wa mwanzo wa Waislam.

 

Baada ya kuzisoma kauli hizi za Maimamu wa Ahlul Bayt zinazowapa Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) sifa zao wanazozistahi, kilichobaki hivi sasa ni kwa kila mwenye kudai kuwa anawapenda watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) nao pia wazitambue haki za Maswahaba hawa (Radhiya Allaahu ‘anhum) kama zilivyotambuliwa na Maimam wao.

Hili ni tumaini letu kwa kila mwenye kuitafuta haki na mwenye kujinasibisha na Ahlul Bayt.

Na baada ya kuujua  ukweli huu asije mtu akaanguka tena ndani ya shimo la kuwalaani na kuwatukana Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kuwatuhumu kwa ukafiri na unafiki.

Tunamuomba Allaah Atuepushe na shari ya ukafir na unafik.

Wabillahi tawfiyq

 

 

 

Share