05-Kukata Undugu: Fadhila Za Kuunga Undugu

 

FADHILA ZA KUUNGA UNDUGU

 

1. Kuunga undugu ni alama ya kumuamini Allaah na siku ya mwisho:

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

“Mwenye kumuamini Allaah na siku ya mwisho amkirimu mgeni wake, na mwenye kumuamini Allaah na siku ya mwisho aunge undugu wake.” Al-Bukhaariy.   

 

 

2. Ni sababu ya kuzidi umri na kukunjuliwa rizki.

 

Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

“Mwenye kupenda kutanuliwa rizki yake, na azidishiwe baraka katika umri wake aunge undugu wake.” Al-Bukhaariy

 

Na kuongezewa umri ni kubarikiwa kupewa nguvu katika mwili akili kuwa salama na maisha mazuri (chakula bora, hewa safi)

 

3. Mwenye kuunga undugu anakuwa karibu na Allaah

 

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

“Hakika Allaah Ameumba viumbe mpaka Alipomaliza ulisimama undugu, ikasema; huyu amesimama anajikinga Kwako na anayemkata, Akasema ndio hivi huridhii Nikimuunga anayekuunga na Ninamkata anayekukata? Akasema sawa. Akasema hilo lako (umekubaliwa ombi lako).” Al-Bukhaariy.

 

4. Kuunga undugu ni sababu kubwa ya kuingia peponi

 

 Kutoka kwa Abu Ayuub al- Answaariy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba mtu alisema;

“Ewe Mtume wa Allaah, nifahamishe tendo litakaloniingiza peponi na litakaloniepusha na moto.” Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): “Umuabudu Allaah wala Usimshirikishe na chochote, usimamishe Swalaah utoe Zakaah na uunge undugu” Al-Bukhaariy.

 

5. Kuunga undugu ni katika kumtii Allaah, kwani unafuata uloamrishwa.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

 “Na wale ambao huyaunga Aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanaikhofu hisabu mbaya.” Ar-Raa’d: 21

 

6. Nayo ni katika mazuri ya dini, Uislam ni dini ya kuunganisha dini ya wema huruma inaamrisha undugu na inakataza kukatana.

 

Inapelekea makundi ya Waislam wenye kushikamana kuzoeana kuoneana huruma kinyume na vikundi vingine visivyochunga haki hii wala kutilia umuhimu.

 

7. Sheria zote za dini za mbinguni zimeafikiana kuhusu kuunga undugu na kuhadharisha ukataji wake. Na hili linaonesha umuhimu wake.

 

8. Kuunga undugu kunapelekea kutajwa vizuri na kusifiwa hata watu wa enzi ya ujahilia (ujinga) walikuwa wanawasifia waunga undugu.

 

9. Kunapelekea wema na ni dalili ya uzuri wa nafsi na ukweli katika kuishi na watu. Palisemwa asiyewafaa ndugu zake hawezi kukufaa…

 

10. Inaeneza upendo baina ya ndugu.

 

Kwasababu inaenea mapenzi na mazoea mazuri, ndugu wanakuwa kitu kimoja, hivyo maisha yao yanakuwa safi na furaha inazidi.

 

11. Kunyanyuliwa muunga undugu.

 

Mwanadamu akiwaunga Ndugu zake,na akachunga katika kuwatukuza, watamkirimu, watamheshimu, watakuwa ni wenye kumsaidia.

 

12. Kuwa na cheo wenye kuungana.

 

Ndugu wenye kuungana kupendana wataheshimika kila mtu ataogopa kuwafanyia ubaya kinyume na hivyo wakikatana kufanyiana vitimbwi watadharaulika watadhalilika baada ya utukufu na kuwa juu. 

Share