Zingatio: Subira Katika Kumtii Allaah

 

Zingatio: Subira Katika Kumtii Allaah

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

Maisha yanapokosa muongozo sahihi huweza mara moja kuharibu jitihada zote alizozifanya mwanaadamu. Uharibifu huu huanza kwa akili wenyewe, hufuatiwa na mwili na humalizia kwa ulimwengu mzima.

 

Bila ya shaka muongozo mkuu tunaoufuata Waislamu ni kutokana na Qur-aan pamoja na Sunnah. Subra ndiyo iliyotawala ndani ya maandiko hayo. Ikionesha kwamba mwenye kushikamana nayo basi atakuwa miongoni mwa wenye kufanikiwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatuamrisha:

 

وَاصْبِرْ نَفْسَكَ مَعَ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ ۖ وَلَا تَعْدُ عَيْنَاكَ عَنْهُمْ تُرِيدُ زِينَةَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَا تُطِعْ مَنْ أَغْفَلْنَا قَلْبَهُ عَن ذِكْرِنَا وَاتَّبَعَ هَوَاهُ وَكَانَ أَمْرُهُ فُرُطًا ﴿٢٨﴾

Na isubirishe nafsi yako pamoja na wale wanaomuomba Rabb wao asubuhi kabla jua kucha na jioni, wanataka Wajihi Wake. Na wala macho yako yasiwavuke kwa kutaka pambo la uhai wa dunia. Na wala usimtii Tuliyemghafilisha moyo wake na Ukumbusho Wetu akafuata hawaa zake, na jambo lake limekuwa la kuzidi kuvuka mipaka. [Al-Kahf: 28]

 

Kwa hakika ni wengi tumewaona wakisema wameachana na maovu wakitaraji kurejea kwa Allaah 'Azza wa Jalla. Lakini hatimaye tunawaona wakirudi kule kule kwenye maasi yao. Wapo ambao walijaribu kutubia wakihitaji kuachana na kuimba. Tulisikia hadi adhana zikighaniwa kwenye idhaa mbali mbali na hadi kivazi cha mtu kinabadilika kabisa kabisa, kikawa kuliko cha mcha wa Allaah wa kweli kweli. Walakin! Mara anarudi kwenye kibarua chake cha miziki. Hii yote inatokana na kukosa subra ya kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Subra katika Kumtii Rabb Mlezi haina masikhara hata kidogo. Yatakikana kuelewa kwamba sote ni watenda maovu. Maovu ambayo hata tukiomba toba vipi hatupati uhakika wa asilimia mia kwamba tumesamehewa hadi tufike mbele ya Mahkama ya Allaah. Yabidi Muislamu ajipinde akitaka asitake kutubu pamoja na kufanya matendo mema bila ya kukatisha njiani.

 

Wala hakuna siri kubwa ya kushikamana na kamba ya Allaah. Kinachotakikana ni kuwa karibu na wanao mcha Allaah wenye muongozo sahihi kama tulivyoinukuu Aayah ya 28 ya Suwrah Al-Kahf. Waislamu wenzangu kwani hatuoni Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba aliwateua Swahaba waongofu kuwa ni watu wake wa karibu? Swahaba ambao walimshauri na kumuongoza pale anapoghafilika. Kama yeye mbora wa viumbe amewaweka wacha wa Allaah mbele, sisi Waislamu wa leo tunaoidharau dira ya Uislamu tuwaweke wapi kama sio kwenda nao bega kwa bega?

 

Tukumbuke hekima za Waswahili wa kale waliposema: "Moyo wa subira haufanyi ghira" Yaani sio wenye kutapa tapa ukitafuta mambo yasiyo na maana. Unakuwa ni wenye kutulia na kufuata yale yenye maana na yeye. Huo ndio moyo wa Muislamu unavyotakiwa kuwa katika kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Tumalizie Hadiyth iliyosimuliwa na Abu Sai'yd al-Khudriy (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) kwamba amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “…Hakuna mtu anayepewa rahmah bora na nyingi kuliko subira.” [Imepokewa na Muslim, kitabu 24, Hadiyth 548]

 

Kwa hivyo ni wajibu wetu kushikamana na subira katika kumtii Allaah Rabb Mlezi wa viumbe vyote. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atuongoze kushikamana na kamba yake pamoja na wale walioghafilika wakashindwa kustahamili.  Amiyn!

 

 

Share