Historia Fupi Ya Palestina

 

 Historia Fupi Ya Palestina

 

Muhammad Al-Ma’awy

 

Alhidaaya.com

 

 

Ulimwengu wetu wa sasa umekuwa ni wa utandawazi (ulimwengushi) kwa kiasi ambacho yaliyo ndiyo yamekuwa siyo na ya makosa yamechukuliwa kuwa ni ya makosa. Ulimwengu umekuwa ukipigwa makombora na vyombo vya habari kwa njia moja au nyingine.

 

Mwenye kumiliki chombo cha habari cha kilimwengu anaweza kupeperusha au kuandika ya kwake na yakaweza kuchukuliwa kama ukweli mtupu. Ulimwengu umekuwa ni wenye kuchukua yote na wenye sauti kubwa kwa kuwa na vyombo hivyo wameweza kusikika mbali  japokuwa hawana haki wa kupata wanayopata.

 

Kadhiya moja ambayo imeeleweka sivyo ni kadhiya ya historia ya Palestina. Waliojizatiti kuiweka katika hali hiyo iwe hivyo ni Wazeyuni bila kuwa na pingamizi kwa kuwa na sauti kubwa. Juhudi dhidi yao zimekuwa zikifanywa bila ufanisi wowote kwa sababu ya sauti kubwa waliyonayo wao. Taasisi kubwa na maarufu za vyombo vya habari zinamilikiwa nao kwa namna moja au nyingine. Mbali na hiyo hatufai kufa moyo kuhusu juhudi hizo kwani nusura hutokea baada tawfiki ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliyetukuka, kisha juhudi zetu kwa kutumia njia tofauti.

 

Kwa sababu ya sifa zake Palestina, kama hali ya hewa, rutuba ya ardhi na upatikanaji wa maji safi ndio wavamizi wengi wamejaribu kuiteka ardhi hii na kuitawala kimabavu.

 

Makao ya awali yalianzishwa Palestina katika miaka ya 14000 hadi 8000 KI (Kabla ya kuzaliwa kwa ‘Nabiy ‘Iysa) kwa utawala wa Tatwafi. Na katika mwaka 8000 KI, mji wa Ariha (Jericho) ulianzishwa huko Palestina. Mji huo ulijengwa na wenyeji ukajengeka kwa njia ya mipango kama ilivyo miji ya kisasa.

 

Makabila ya mwanzo kuja kuweka makazi yao katika nchi ya Palestina ni yale makabila ya Wayebusi, Waamori, Wahiti, Wakanaani, Waamalika na Wafiniki. Makabila haya yalikaa katika maeneo tofauti ya nchi hiyo: Wakanaani waliweka makazi yao katika eneo la Gaza ilhali Wayebusi walibuni mji wa Yebus, ambao kwa sasa unajulikana kama mji wa al-Quds. Makabila haya yalihamia huko kutoka kusini mwa Bara Arabu takriban mwaka 3000 KI.

 

Katika mwaka wa 1900 KI, Nabii Ibraahim ('Alayhis-salaam) alihamia kutoka Iraq na kuja kuweka makazi yake katika mji wa Khalil. Hapo ndipo alipomzaa Nabiy Ismaa‘iyl na Ishaaq ('Alayhim-salaam) na baadaye kuzaliwa Nabii Ya‘quub ('Alayhis-salaam).

 

Katika kipindi 1800 – 1600 KI, Palestina ilitawaliwa na Waheksosi. Ni katika kipindi hiki katika mwaka wa 1750 KI ndio Nabii Ya‘quub ('Alayhis-salaam) alizaliwa.

 

Katika karne ya 16 KI (yaani mwaka wa 1580 KI), Bani Israili waliokuwa Misri walitiwa utumwani na Firauni wa wakati huo kuvamia na kuitawala Palestina kwa muda kabla ya sehemu hiyo kuingia katika utawala wa Kiislamu.

 

Mwaka 1250 KI, Nabiy Muwsaa ('Alayhis Salaam) aliagiziwa na Allaah Aliyetukuka atoke Misri ambako wana wa Israili walikuwa ni watumwa waende wakaishi katika ardhi tukufu. Kwa ajili ya ukaidi wao (Qur-aan 5: 21 – 26), walipigwa marufuku kuingia katika ardhi hiyo. Mbali na hilo walipigwa adhabu kali ya kutangatanga katika jangwa kwa muda wa miaka arobaini (40). Katika kipindi hicho, wale wote waliokuwa wamebaleghe walikufa katika jangwa kikabakia kizazi ambacho kililelekea katika maadili ya Kiislamu, Imani na uchaji Allaah kuingia katika ardhi hiyo tukufu. Kizazi hicho kilipata darsa ya ukakamavu, utii, kujitolea mhanga na malezi bora, hivyo kwa tawfiki ya Allaah Aliyetukuka kuweza kuingia ardhi hiyo mwaka 1190 KI wakiongozwa na Yusha bin Nuwh ('Alayhis-salaam). Wakati huo tayari Nabiy Muwsaa ('Alayhis-salaam) alikuwa ameaga dunia hivyo kutoweza kuingia katika ardhi hiyo.

 

Yusha bin Nuwh ('Alayhis-salaam) ndiye mwana Israili wa kwanza aliyeanzisha dola katika maeneo ya Palestina. Hata hivyo, wana wa Israili chini ya uongozi wa Yusha bin Nuhw ('Alayhis -salaam) hawakuweza kuliteka eneo lote la Palestina katika mipaka yake ya sasa na hata mji wa al-Quds haukuingia mikononi mwake. Ifahamike kuwa dola hiyo haikuwa katika misingi ya Kiyahudi kwani dini ya Kiyahudi ilikuwa haijabuniwa kamwe wakati huo bali ilikuwa ikipekeshwa katika misingi ya Kiislamu.

 

Dola hii haikukaa kwa muda kwani vurugu liliingia kati baada ya kuaga dunia Yusha bin Nuwh ('Alayhis-salaam), hivyo kushikiliwa na Ma-Qaadhi kabla ya kusambaratika kabisa kabisa. Kufikiwa na hayo, Bani Israili waliingia katika utawala wa Wapalestina ambayo asili yao ni Wakanaani. Kudhalilishwa kwao huko kuliwafanya watake msaada kutoka kwa Allaah Aliyetukuka ili warudi katika enzi zao (Qur-aan, 2: 246). Allaah Aliyetukuka Aliwateulia Twaaluut kuwa mfalme wao wa kuwaongoza wao kwenda kupambana na Wapalestina wakiongozwa na Jaaluut (Qur-aan, 2: 247). Bani Israili waligomba sana kuhusu uchaguzi huo, hata hivyo wapo waliokuwa na Imani ambao walisalimu amri na kujizatiti kwenda  kupambana na Wapalestina. Wakati huo, Nabii Daawuud ('Alayhis-salaam) alikuwa kijana mdogo aliyejiunga na jeshi hilo ambalo kwa tawfiki ya Allaah Aliyetukuka liliweza kulishinda jeshi la Jaaluwt (Qur-aan, 2: 248-251). Ushindi huo ulipatikana mwaka wa 1025 KI. Twaaluut aliweza kuanzisha tena dola ya Kiislamu Palestina ikiwa inaongozwa na Bani Israili mpaka kufa kwake mnamo 1004 KI.

 

Baada ya kuaga dunia tu, hatamu za uongozi zilishikwa na Nabiy Daawuud (‘Alayhis-salaam) ambaye aliipanua dola hiyo kwa kasi kubwa sana. Ni wakati wake ndio mji wa al-Quds uliweza kutekwa. Nabiy Daawuud ('Alayhis-salaam) aliaga dunia mwaka wa 960 KI na kumuacha mtoto wake, Nabiy Sulaymaan ('Alayhis-salaam) katika utawala. Kwa upande wake naye, Nabiy Sulaymaan ('Alayhis-salaam) aliipanua dola hiyo lakini haikufika katika mipaka yake ya sasa. Nabiy Sulaymaan ('Alayhis-salaam) aliimarisha sana dola hiyo, akiwa yeye na babake wameitawala kwa misingi ya Kiislamu. Ilibaki hivyo hadi mwaka wa 922 KI pale naye alipoaga dunia.

 

Kufariki kwake kuliifanya dola hiyo igawanywe sehemu mbili: Dola ya Yuda  (kusini) na Kizeyuni (kaskazini). Bani Israili waligawanyika katika koo zao kwa kiasi ambacho walianza kupigana wao kwa wao (baina dola mbili hizo) na ufisadi ukakithiri kwa kiasi kikubwa sana. Wakati huo ndio alitokea mtu kwa jina la Yuda aliyekiuka mipaka ya Dini na kuasi. Alipata wafuasi wengi na hapo kukazaliwa Dini ya Uyahudi.

 

Hali hiyo halisi ya mapambano baina ya Bani Israili iliwapelekea dola zao mbili hizo kudhoofika na mwisho katika mwaka wa 722 KI, dola ya Israili ilianguka na eneo hilo kutawaliwa na Wa-Asiria. Nayo dola ya Yuda ilivamiwa na mfalme Nubukadneza wa Babeli (Iraq) mwaka 586 KI, na dola hiyo kuingia katika utawala wa Kibabeli. Wana wa Israili wote walipelekwa uhamishoni huko Iraq kama watumwa. Hapo wengine wao walipata kukimbia na kuingia Ufursi (Iran) ambapo walijaribu kufanya mahusiano ya karibu na utawala wa huko hadi wakamtoa msichana wao kwa ajili ya kuolewa na mfalme wa Iran. Mafungamano hayo yalimfanya mfalme Cyrus wa Iran aunde jeshi kwa usaidizi wa Mayahudi ili kuivamia Palestina na kuwang’oa Wababeli. Cyrus alifanikiwa kuwashinda Wababeli kutoka Palestina na kuwapatia ruhusa Mayahudi kurudi katika nchi hiyo lakini hata hivyo waliorudi hawakuwa wengi, walikuwa wachache sana. Wengi miongoni mwao walibakia katika nchi ya uhamisho wao. Kushinda kwao kulitokea mwaka wa 538 KI. Hata hivyo, Mayahudi wakati wa utawala wa Kifursi hawakuwa na mamlaka wala madaraka yoyote lakini walipatiwa uhuru wa kufanya Ibadah zao bila kufuatiliwa, kuingiliwa wala kubughudhiwa na Wafursi.

 

Na katika mwaka 332 KI, Palestina ilivamiwa na kutekwa na Warumi wakiongozwa na Alexander kutoka Macedonia. Hata hivyo, Warumi hawakuweza kukaa huko kwa muda mrefu pale wafalme wa kutoka Syria walipovamia sehemu hiyo na kuitia katika utawala wao mwaka 198 KI.

 

Wayunani nao waliiteka ardhi hiyo mwaka wa 175 Ki na kuitawala. Mayahudi waliweza kujizatiti na kuiteka sehemu hiyo ya ardhi mwaka wa 166 KI na ikabaki mikononi mwao kwa kipindi cha miaka 4. Wasyria walirudi tena kwa kishindo na kuwashinda Mayahudi mwaka wa 162 KI. Hata hivyo, nao Mayahudi walijizatiti kwa mara nyingine tena wakaja wakawang’oa Wasyria kutoka sehemu hiyo mwaka 143 KI. Hapo waliweza kuibakisha ardhi hiyo katika utawala wao hadi mwaka 70 KI.

 

Kwa miaka saba baada ya huo mwaka wa 70 kukawepo vurugu kubwa hadi mwishowe Warumi wakaweza kuwashinda Mayahudi mnamo 63 KI. Kuanzia mwaka huo hadi mwaka wa 616 BI (Baada ya kuzaliwa kwa Nabii ‘Iysa) Palestina ilibaki katika utawala wa Warumi isipokuwa kile kipindi cha mapinduzi ya Mayahudi cha mwaka 66 BI na 132 – 135 BI. Hata hivyo, katika kipindi cha mapinduzi hayo ya Mayahudi serikali ya Roma ilituma wanajeshi wake wengi ili kuyasagasaga hayo mapinduzi. Ni wakati huo ndio serikali ya Kirumi ilipitisha sheria kuwa mji wa al-Quds haufai kukaliwa na Mayahudi.

 

Utawala wa Kirumi ulisitishwa kidogo na ule wa Wafursi mwaka wa 616 BI. Lakini utawala wa Wafursi haukukaa kwa muda mrefu kwani katika mwaka wa 624 BI walishindwa na Warumi katika vita ambavyo Allaah Amevizungumzia katika Suwrah Ruwm (30): Aayah 1 – 5. Warumi waliweza kusonga mbele hadi kuuteka mji wa al-Quds katika kipindi cha muda miaka 3 hadi 4.

 

Kipindi baada ya Sulhu ya Hudaybiyah ndicho kile ambacho Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alianza kupeleka barua kwa mataifa mbali na ndio barua hiyo ikamfikia mfalme wa Warumi, Hiraql (Heraclius) akiwa al-Quds mwaka wa 628 BI. Hapo ndio yalianza mapambano baina ya Waislamu wakiongozwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Warumi. Mji wa al-Quds uliingia mikononi mwa Waislamu wakati wa ukhalifa wa 'Umar bin al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye alifunga safari kwenda kuchukua funguo za mji kutoka kwa kasisi Sophronius mwaka wa 638 BI na hapo miji mingi ya Palestina ikaingia katika Dola ya Kiislamu. Nchi hiyo pamoja na nchi za Shaam zote zilibakia katika utawala wa Kiislamu hadi mwaka wa 1099 BI wakati ambapo Wakristo walikuja kuzivamia ardhi hizo katika vita vya Msalaba.

 

Watu wa Msalaba kutoka bara Ulaya waliweza kuwaua Waislamu 70,000 ndani ya eneo la Msikiti wa Aqswa. Wakristo waliweza kuitawala ardhi hiyo kwa muda wa miaka 88 ambapo harakati za kuikomboa zilipamba moto. Harakati hizo zilianzishwa na Nuurud-Diyn Zinkiy, mwanae Nuurud-Diyn Mahmuud na baadaye Swalaahud-Diyn Hasan al-Ayyuubiy ambaye aliweza kwa tawfiki ya Allaah kuirudisha Palestina kuwa katika Dola ya Kiislamu mwaka 1187 BI.

 

Kuanzia mwaka huo wa 1187 BI, Palestina ilibakia kuwa katika Dola ya Kiislamu hadi baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia (1917) ndio Palestina iliingia katika utawala wa Uingereza. Wenyeji wa al-Quds hawakusadiki masikio yao pale walipokusanyika kumsikiliza jemadari Allenby katika uwanja wa al-Quds. Allenby alisema kwa uwazi kabisa: "Leo ndio vita vya Msalaba vimekwisha". Kabla hata ya kuiteka na kuitawala ardhi hiyo, serikali ya Uingereza tayari ilikuwa imewaahidi Wazeyuni kuwa wakiondoka watawazawadia wao kipande hicho cha ardhi. Hayo yanapatikana katika ahadi au tangazo la Waziri wa Nje, Arthur James Balfour ya tarehe 2 Novemba 1917.

 

Na kweli kwa ahadi yao, Uingereza ilipoondoka Mei 1948 waliwaachia ardhi hiyo Wazeyuni wasiokuwa na mafungamano na ardhi hiyo. Hakika ni kuwa Mayahudi wakati huo na kabla ya hapo hawakuwa na kitambulisho cha aina yoyote ile. Hii ni kwa mujibu wa barua aliyoiandika Dkt Chaim Weizman ya 18 Aprili 1918 kwa mkewe: “Ni masikitiko makubwa kuona kuwa hapa hatuna chochote. Hapa hakuna hata taasisi moja ya Kiyahudi, lakini kumejaa minara (kumaanisha wingi wa Misikiti)”.

 

Ndugu zetu walianzisha harakati ya kutaka kujikomboa na minyororo ya ukoloni. Harakati ya kwanza ni ile iliyoongozwa na Sh. Abdul-Qaadir al-Qassaam, kutoka Syria mwaka 1925. Mwaka wa 1929 kulikuwa na Intifadha ya al-Buraaq, naye Sh. Al-Qassaam akauliwa mwaka wa 1935 alipokuwa anapambana na jeshi la Muingereza katika maeneo hayo matakatifu.

 

Kuanzia mwaka wa 1948, kumekuwa na vita baina ya Waarabu na Wazeyuni, lakini Waarabu wakashindwa sana kwa kutokuwa na kuwa wamoja na kauli moja, kutokuwa na mipango mizuri na wakati mwengine kushirikiana na dola haramu ya Kizeyuni. Hata hivyo, sababu kubwa ya kushindwa ni kule Waarabu kuichukulia kuwa hiyo ni kadhiya ya Waarabu tu na kutowajumuisha Waislamu wengineo.

 

 

Rejea:

 

  1. Quds Qadhwiyah Kull Muslim.
  2. Mustwafa Muhammad atw-Twahhaan, Filistwiyn wal Muaamaratul Qubraa.
  3. Al-Islaam wal Qadhwiyatul Filistwiyniyah.
  4. Dkt. Muhsin Muhammad Swaalih, atw-Twariyq ilal Quds.
  5. Dkt. Muhammad Siddiq Qureishi, Zionism and Racism.
  6. Dkt. Mohsen M. Saleh, The Palestinian Issue.
  7. Mawlana Mawdudi, Tafhiymul Qur-aan.
  8. Raymond Caroll, The Palestine Question.
  9. Maryam Jamiylah, Islam versus Ahl al Kitab: Past and Present.
  10. Dkt. Bhatt, Zionism and Internal Security.
  11. Dkt. Muhsin Muhammad Swaalih, al-Haqaaiq al-Arba'una fil Qadhwiyatil Filistwiyniyah.
  12. Tovuti: www.palestine-info.info 

 

 

Share