035-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kusimama (Kuitadili) Kutoka Katika Rukuu Na Anachokisema Ndani Yake

 

 

KUSIMAMA (KUITADILI) KUTOKA KATIKA RUKUU NA ANACHOKISEMA NDANI YAKE

 

Kisha, alikuwa   (صلى الله عليه وآله وسلم) akiunyanyua mgongo wake kutoka rukuu huku akisema:

 

 

 

Sami’a Allaahu liman Hamidah

Allaah Amemsikia mwenye kumsifu([1])

 

 

Alimuamrisha pia aliyeswali vibaya kufanya hivyo alipomwambia: ((Swalah ya mtu haitimii hadi… amesema Takbiyr … kisha akarukuu …. Kisha akasema 'Allaah Amemsikia mwenye kumsifu' hadi asimame kwa kunyooka sawa sawa))([2]).

 

Aliponyanyua kichwa chake, alikuwa akisimama wima na kunyooka sawa sawa hadi kila pingili ya uti imerudi sehemu yake.([3])

 

 

Kisha alikuwa akisema huku akiwa amesimama wima:

 

 

 

Rabbanaa Walakal-Hamdu

Ee Mola Wetu! Na Zako Sifa njema na shukrani za dhati.([4])

 

 

Aliwaamrisha wanaoswali wote sawasawa wakiweko nyuma ya Imaam au wasiweko nyuma ya Imaam kufanya hivyo, wanapoinuka kutoka rukuu kwa kusema: ((Swalini kama mlivyoniona nikiswali)).([5])

 

Alikuwa akisema pia: ((Imaam amewekwa kwa ajili ya kufuatwa …, anaposema ' Sami’a Allaahu liman Hamidah’ (Allaah Amemsikia mwenye kumsifu), basi semeni: '[Allaahumma] Rabbanaa Walakal-Hamd'. Allaah Atakusikilizeni, kwani hakika Allaah (تبارك وتعالى) Amesema katika ulimi wa Mtume Wake, (صلى الله عليه وآله وسلم), Allaah Anamsikiliza mwenye kumsifu)).([6])

 

Pia ametoa sababu ya kuamrisha hivi katika Hadiyth nyingine kwa kusema: ((... kwani mwenye kuwafikiana kauli yake na kauli ya Malaika, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)).([7])

 

 

Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم)  akiinua mikono yake katika huku kusimama([8])  kwa namna zilizotangulia kuelezwa katika 'Takbiyra Ya Kufungulia', na husema hali ya kuwa amesimama - kama ilivyotajwa kabla- :

 

1.      

 

 

Rabbanaa Walakal-Hamd'

Ewe Mola Wetu! Na Zako sifa njema na shukrani za dhati([9]). Na mara nyingine husema:

 

2.

 

 

Rabbanaa Lakal-Hamd'

Ewe Mola Wetu! Ni Zako sifa njema na shukrani za dhati([10]). Na mara nyingine huongezea matamshi mawili haya tamshi:

 

Allaahumma

Ee Allaah!([11])

 

 

3.

 

 

 

Allaahumma Rabbanaa Walakal-Hamd'

Ee Allaah! Mola Wetu! Na Zako sifa njema na shukrani za dhati.

 

 

 

4.

 

 

 

 

 

 

Allaahumma Rabbanaa Lakal-Hamd'

Ee Allaah! Mola Wetu! Ni Zako sifa njema na shukrani za dhati.

 

 

Alikuwa akiamrisha (wengine) kufanya hivi kwa kusema: ((Imaam anaposema 'Sami'a Allaahu Liman Hamidah' semeni: 'Allaahumma, Rabbanaa Lakal-Hamd', kwani mwenye kuwafikiana kauli yake na ya Malaika ataghufuriwa madhambi yake yaliyopita)).([12])

                                                                     

Mara nyingine alikuwa akiongeza:

 

5.

 

 

 

Mil-as Samaawaati, wamil- al Ardhi, wamil-a maa shi-ita min shayin ba’du

Zimejaa mbingu, na zimejaa ardhi, na zimejaa (sifa Zako) kwa Ulichokitaka baada yake.([13])

 

 

Au:

 

6.

 

 

 

 

Mil-as Samaawaati, [wamil-a]l Ardhi, wamaa baynahumaa, wamil-a maa shi-ita min shayin ba’du

Zimejaa mbingu na (zimejaa) ardhi na vilivyomo ndani yake sifa Zako, na zimejaa (sifa Zako) kwa Ulichokitaka baada yake.([14])

 

Mara nyingine aliongeza zaidi:

 

7.

 

 

 

Ahlath – thanaai wal Majdi, laa maani’a limaa a’twayta, wala mu’twiya lima mana’ta, walaa yanfa’u dhal jaddi minkal jaddu

Wewe ni Mstahiki wa sifa na Utukufu, hapana anayeweza kukizuia Ulichokitoa, wala mwenye kutoa Ulichokizuia, na wala haumnufaishi mwenye utajiri, kwani kwao Wewe ndio utajiri.([15])

 

Au mara nyingine ziada ilikuwa:

 

8.

 

 

 

Mil-as Samaawaati, wamil-al Ardhi, wamaa baynahumaa, wamil-a maa shi-ita min shayin ba’du, ahlath-thanaai wal Majdi, ahaqqu maa qaalal ‘abdu, wakullunaa laka ‘abdun, [Allaahumma] laa maani’a lima a’twayta, [wala mu’twiya lima mana’ta], walaa yanfa’u dhal jaddi minkal jaddu

Zimejaa mbingu na zimejaa ardhi na vilivyomo ndani yake sifa Zako, na zimejaa (sifa Zako)  kwa Ulichokitaka baada yake, Wewe ni Mstahiki wa Sifa na Utukufu, ni kweli aliyoyasema mja Wako, na sote ni waja Wako, (Ee Allaah)  hapana anayeweza kukizuia Ulichokitoa, (na wala kutoa Ulichokizuia), na wala haumnufaishi mwenye utajiri, kwani Kwako Wewe ndio utajiri.([16])

 

Mara nyingine alikuwa akisema katika Swalah ya usiku:

 

9.

 

 

LiRabbiyl Hamdi, li Rabbiyl Hamdu,

Kwa Mola wangu Sifa zote, Kwa Mola Wangu Sifa zote na shukrani za dhati.

 

Akikariri hadi kisimamo chake kilikuwa kirefu kama rukuu yake ambayo ilikuwa inakaribiana kwa urefu na kisimamo chake cha mwanzo, na alikuwa amesoma ndani yake Suratul-Baqarah.([17])

 

 

10.

 

 

 

Rabbanaa walakal Hamdu, Hamdan Kathiyran Twayyiban Mubaarakan fiyh [Mubaarakan ‘alayhi, kamaa Yuhibbu Rabbunaa Wayar-dhwaa]

Ee Mola wetu! Ni zako sifa njema sifa nyingi, nzuri, zenye Baraka (Baraka juu yake kama Anavyopenda Mola wetu na Kuridhika)([18])

 

 

Matamshi haya aliyasoma mtu aliyekuwa akiswali nyuma yake   (صلى الله عليه وآله وسلم). Aliyasoma baada ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kunyanyua kichwa chake kutoka kwenye rukuu na alisema: 'Sami'a Allaahu Liman Hamidah'. Alipomaliza Mjumbe wa Allaah  (صلى الله عليه وآله وسلم) kuswali, alisema: ((Nani aliyesema hivi sasa?)) Yule mtu akasema: "Ilikuwa ni mimi ewe Mjumbe wa Allaah!" Hivyo Mjumbe wa Allaah  (صلى الله عليه وآله وسلم)akasema: ((Nimewaona Malaika zaidi ya thelathini wanakimbilia kuwa wa kwanza kuyaandika)).([19])

 

 

 

[1] Al-Bukhaariy na Muslim.

[2] Abu Daawuud na Al-Haakim ambaye amesema ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubaliana naye.

[3] Al-Bukhaariy na Abu Daawuud. "Al-Faqaar" ni uti – "mifupa inayounda uti wa mgongo kutoka mwanzo wa shingo hadi kitokono" kama ilivyo katika Kamusi. Taz. pia Fat-h Al-Baariy (2/308).

[4] Al-Bukhaariy na Ahmad.

[5] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.

[6] Muslim, Abu 'Awaanah, Ahmad na Abu Daawuud.

 

TANBIHI: Hadiyth hii haithibitishi kwamba Maamuma hawashirikiani na Imaam katika kusema: 'Sami'a Allaahu Liman Hamidah'. Pia haithibitishi kuwa Imaam hashirikiani na Maamuuma wanaosema: 'Rabbanaa Walakal-Hamd', yote kwa kuwa Hadiyth hii haikuja kubainisha yale khaswa ambayo Imaam na Maamuma wanapaswa kuyasema katika nguzo hii, bali imekuja kueleza kwamba tahmiyd (Rabbana Walakal-Hamd) ya Maamuma inatakiwa isemwe baada ya tasmiy' (Sami'a Allaahu Liman Hamidah) ya Imaam. Hii imetiliwa nguvu kutokana na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema tahmiyd hali ya kuwa yeye ni Imaam, na pia kwa ujumla wa kauli yake: ((Swalini kama mnavyoniona nnaswali)) ambayo inaonyesha kwamba Maamuuma waseme anayoyasema Imaam kama (Sami'a Allaahu Liman Hamidah) na mengineo. Wale ndugu waheshimiwa waliorejea kwetu kuhusu mas-ala haya watilie maanani haya, labda katika tuliyotaja kuna yenye kukinaisha. Na yeyote atakayetaka kujadii zaidi mas-ala haya arejee katika makala ya Al-Haafidh As-Suyuutwiy katika mas-ala hii kwenye kitabu chake Al-Haawy lil Fataawa (1/529).

 

[7] Al-Bukhaariy na Muslim. At-Tirmidhiy amesema ni Swahiyh.

 

[8] Al-Bukhaariy na Muslim. Huku kunyanyua mikono ni mutawaatir kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), na ni kauli ya Maulamaa wengi na baadhi ya Mahanafi. Taz. Tanbihi za nyuma katika (mlango wa) Rukuu.   

[9] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.

[10] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.

[11] Al-Bukhaariy na Ahmad. Na kwa hakika Ibnul-Qayyim (رحمه الله) alikosea (katika nukta hii,) pale alipokanusha katika Zaad Al-Ma'aad usahihi wa riwaayah hii yenye kukusanya baina ya 'Allaahumma' na 'wa' pamoja na kuwepo kwake katika Swahiyh Al-Bukhaariy, Musnad Ahmad, An-Nasaaiy na Ahmad tena kupitia njia mbili (za usimulizi) kutoka kwa Abu Hurayrah, na katika Ad-Daaraimiy kutokana na Hadiyth ya Ibn 'Umar, na katika Al-Bayhaqiy kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriyy, na katika An-Nasaaiy tena kutokana na Hadiyth ya Abu Muusa Al-Ash'ariyy.

[12] Al-Bukhaariy na Muslim. At-Tirmidhiy amesema ni Swahiyh.

[13] Muslim na Abu 'Awaanah.

[14] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.

[15] Jadd: Bahati, Utajiri, Utukufu, nguvu, yaani Mwenye mali, watoto, cheo, uwezo na nguvu katika dunia hii. Hatoweza kunufaika navyo mbele Yako; Anavyomiliki havitomuokoa kutoka Kwako, lakini kitachomnufaisha na kumuokoa ni amali njema pekee.

[16] Muslim na Abu 'Awaanah.

[17] Muslim, Abu 'Awaanah na Abu Daawuud.

[18]    Abu Daawuud na An-Nasaaiy kwa isnaad Swahiyh. Imetolewa katika Al-Irwaa (335).

[19]    Maalik, Al-Bukhaariy na Abu Daawuud.

Share