Ana Matatizo Na Mumewe, Anataka Kuachika Ili Nimuoe Mimi Nami Nna Mke Tayari

SWALI:

As-salamu alaikum ndugu zangu katika uislamu, Nipo na mwanamke aliyeolewa takriban miaka 10 na zaidi na tunakutana kazini mara kwa mara,al-hamdulillahi pia mimi nimeowa.Mda wote ninamchukulia kwa nia safi kama dadangu katika uislamu,walakin analalamika sana kuhusu mumewe.Anasema kuwa ndoa yake ililazimishwa na kwa dhati ya nafsi yake hana mapenzi wala raha na mumewe,maana anapenda kucheza kamari na anafuja pesa za mkewe kwa kulipa madeni ya watu na wala hamshughulikii ipasavyo.

Anahisi yeye ni kama mtumwa na hana hadhi ya uke pale nyumbani na hana raha kabisa japo atakuwa anafanya jimai na mumewe.Anasema kuwa dhati ya penzi lake lipo kwangu. Na yupo tayari kuwa mke wangu wa pili ikiwa nipo tayari kumuoa. Ikhwaani, nimefikia wakati mimi pia nimeangukia kumpenda japo mke wa watu. Nahofia yasije yakatokea haya, aitoe nafsi yake au aombe talaka yake sababu yangu. Na nimejaribu kumnaswihi lakini haisaidii kitu!

Insha-allah nakuombeni naswiha, na jaza yenu ipo kwa M/Mungu.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Asli kukaa tu na mwanamke bila ya kuwepo Mahram wa huyo mwanamke pamoja na mwanaume huyo anayekaa na mwanamke kwa kuzungumza ni jambo lisilokubalika kisheria kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Hairuhusiwi kukaa mwanamume na mwanamke peke yao isipokuwa yuko pamoja nao Mahram wa mwanamke “Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha ndoa, mlango wa hakai mwanamume peke yake na mwanamke isipokuwa pawepo Mahram wake.

 

Hivyo basi kuwa au kukaa peke yako na mwanamke hakuruhusiwi na hii ni kwa asiyeolewa na kwa aliyeolewa huwa zaidi kwani fitina huwa kubwa kuliko asiyeolewa.

 

Kwani kukaa nae kunapelekea Munkar ulio wazi na ndani yake kuna matatizo -mafaasid- mengi kwani Shaytwaan huwa ni watatu wao na pahala penye Shaytwaan kutokea uchafu na maasi ndio pake kwani kazi ya Shaytwaan ni kuamrisha machafu na kuwapambia watu uchafu kuuona kuwa ni bustani zenye maua yenye kunukia na kuvutia na wakishaingia katika uchafu Shaytwaan huwakimbia na kuwaacha; na kwa hakika hakuna mwanamume anayeridhia haya kwa Mahram wake achilia mbali kwa mkewe, kwani huyo ni katika wenye imani dhaifu na ni katika walio na upungufu katika uume wao.

Kukutana mwanamume na mwanamke kama mnavyokutana huko makazini kuna fitna kubwa hivyo ni vyema mtu ajitahidi kujiepusha kadiri awezavyo; kwani makutano baina ya mwanaume na mwanamke yana hali tatu:

Moja: Kukutana mwanamume na mwanamke huku kukiwepo Mahaarim wa huyo mwanamke Hali hii inaruhusiwa haina tatizo.

 

Mbili: Kukutana mwanamume na mwanamke kwa lengo la ufisadi na uharibifu bali kutaka kutimiza uchafu Hali hii hairuhusiwi ni haramu.

 

Tatu: Kukutana mwanamume na mwanamke katika sehemu za kutafuta elimu, makazini, hospitalini, kwenye sherehe za harusi au nyenginezo na kadhalika Hali hii imefafanuliwa na Maulamaa na kama kuna ulazima basi unaruhusiwa na kama hakuna ulazima ni haramu pia.

 

Hivyo basi kukutana na mke wa watu kazini si jambo lenye kuruhusiwa na kukubalika kwani ni sawa au zaidi ya kuwa naye peke yako katika nyumba, kwani ikiwa mnakutana kazini na kuzungumza na kupanga kila kitu basi inawezekana pia ukawa unakwenda naye na kurudi naye kazini katika gari peke yenu jambo ambalo linakupa nafasi ya kumdhibiti utakavyo awe anaridhia au vyenginevyo kwani wewe ndiye mshika mpini na hili ndio linalosababisha fitna kubwa.

 

Umesema, Al-hamdulillahi pia mimi nimeowa. Ni vyema ashukuriwe Mjuzi wa siri na dhahiri kila wakati na kwa dhati kwani shukurani hapa tunaona kama sipo pahala pake, kwani kama ungeelewa kuwa huyu mwanamke ni mke wa ndugu yako kwa kauli yake huyo unayemshukuru basi usingekaa nae wala usingeshukuru; Quraan inasema:

“Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Allaah ili mrehemewe.” Al-Hujuraat:10.

 

Vipi unakaa na mke wa ndugu yako peke yenu bila ya hata kuona vibaya wala kuhisi kuwa ufanyavyo si halali kwako, jifikirie kama ingelikuwa ni mkeo ndie yuko katika hali hiyo ya kukaa na wanaume, jifikirie kama mkeo angelikuwa anazungumza habari zenu na mwanamume anayesikia sauti tu ya mwanamke husimika wachilia mbali awe anamuona na huku wakiwa wako wao peke yao kama unavyokuwa wewe na huyo mke wa ndugu yako?!

 

Kisha umesema, Mda wote ninamchukulia kwa nia safi kama dadangu, mwenye nia safi na mwenye kuhisi bali kuamini udugu wa uislamu udugu alioutaja Allah katika Qur-aan, ni yule anaempendelea mwenzake bali ndugu yake Muislamu anayoyapendelea nafsi yake kama ilivyothibiti katika Hadiyth nyingi tu za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); kama kweli ulikuwa na nia safi na kumchukulia kama ndugu yako basi ilikuwa ni jukumu lako kama Muislamu umnasihi kidhati na kikweli badala ya kukaa na kuanza kusikiliza siri na matatizo ya nyumba ya ndugu yako Muislamu siri au matatizo ambayo wewe huna uwezo au huna haja  ya kuyatafutia ufumbuzi kwa sababu nyingi uzijuazo.

 

Na ikiwa kweli alilazimishwa kuolewa, basi alikuwa na haki ya kujikomboa –khul’u- au hata kuomba talaka kwani kinachotakiwa ni utulivu na mapenzi katika nyumba na hayo hayapo.

 

Umsema anahisi kama mtumwa na si mke, ikiwa dhana yake kama kweli anasema hivyo, na kubwa ni kuwa katika Uislamu hakuna mtumwa wala muungwana bali watu wote ni sawa sawa mbele ya Allaah na hukumu zake; na kama kweli alikuwa hana hadhi ya uke, basi wewe ilikuwa haki yake kwako kama ni dada yako Muislamu na mumewe ni ndugu yako katika Uislamu umnasihi na umshauri apeleke malalamiko yake kwa wahusika, kama inavyoshauri Qur-aan:

“Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke. Wakitaka mapatano Allaah Atawawezesha. Hakika Allaah ni Mjuzi Mwenye khabari” An-Nisaa: 35.

 

Kwani yeye alikuwa na nia safi -sio wewe- alikukinai na kudhania kuwa utaweza kumsaidia kutatua matatizo yake na mumewe, lakini wewe hukuelewa hivyo ulikuwa uko katika ulimwengu wa pili ulimwengu wa kujitafutia maziwa bila kununua ng’ombe, kwani uwezo wa kuyatatua matatizo huna bali una uwezo wa kuyapalilia tu.

 

Umesema, Anasema kuwa dhati ya penzi lake lipo kwangu. Kila mtu ameandikiwa sehemu au nasibu yake katika zinaa, na wewe ulishachukuwa nasibu yako kwa kukaa naye kumtazama uzuri wake, hiyo ilikuwa zinaa ya macho yako, kuzungumza naye ilikuwa zinaa ya masikio yako kutaladhadh na sauti yake wakati mwengine kumgusagusa au kusalimiana naye kwa kupeana mkono hiyo ni zinaa pia ya kumgusa asiyestahiki kuguswa na wewe na kadhalika na hayo yote huthibitishwa na utupu wako kwa kusimika na hata wakati mwengine kutokwa na maji.  Ndugu yetu, Qur-aan imetushauri hivi, wala msiukaribie uzinzi, kwa kuziingilia sababu zinazopelekea uzinzi. Jambo hilo ni jambo la aibu na uovu usiofichikana, na hapana njia mbovu kama hiyo, wewe umeikaribia zinaa kwa kutekeleza sababu zake karibu zote na sasa ndio uko tayari kuivamia.

 

Wapi umesikia katika tarehe yote ya Kiislamu mke kuwa na mume zaidi ya mmoja?! Kinachoeleweka ni kuwa mume huwa na wake hadi wane kwa wakati mmoja.

 

Ukasema, Na yupo tayari kuwa mke wangu wa pili ikiwa nipo tayari kumuoa. Bila shaka uko tayari kwani utupu wako ushathibitisha hayo siku nyingi tu, hivyo basi kila kitu ushakamilisha kilichobakia ni tendo lenyewe tu la ndoa, lakini utamuoa vipi na bado hujamuachisha kwa mumewe au hajaachwa na mumewe?  Uislamu unatutaka tuwapatanishe watu hasa mke na mumewe kama hawana mafahamiano na haututaki tumuachishe mke kwa mumewe kwa sababu ya kutaka kumuoa, na imethibiti katika Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa

 

“Hayuko pamoja na sisi mwenye kumchukiza mwanamke kwa mume wake, au mtumwa kwa bwana wake” pia “Mwanamke yoyote atakayeomba talaka kwa mume wake bila ya sababu (inayokubalika) basi Allaah Atamuharamishia harufu ya Pepo”.

 

Uislamu umeruhusu katika muda wa eda kwa mwanamke aliyefiwa –huyu wako ana mume- mkiwaonyesha dalili kuwa mnadhamiria kutaka kuwaoa waliomo edani, lakini hayo yawe ni kudhamiria ndani ya moyo tu. Kwa hivyo mmepewa ruhusa kuashiria bila ya kubainisha kwa maneno. Basi msiwape ahadi ya kuwaoa ila iwe ishara isiyo ovu wala ya uchafu.

 

Wewe ushatoa ishara ovu na chafu tena kwa mke wa mtu hilo bila ya shaka yo yote ile ni kosa kubwa kwani ndoa haifungwi mpaka baada ya kwisha eda kama inavyoshauri Qur-aan kwa waumini wake:

“Wala si vibaya kwenu katika kupeleka posa kwa ishara tu kwa wanawake waliomo edani au mkadhamiria katika nyoyo zenu. Allaah anajua kwamba nyinyi mtawakumbuka. Lakini msiwaahidi kwa siri, ila mnene maneno mema. Wala msiazimie kufunga ndoa mpaka eda ifike mwisho wake. Na jueni kwamba Allaah Aanajua yaliyomo katika nafsi zenu. Basi tahadharini naye. Na jueni kwamba Allaah ni Mwenye kusamehe na Mpole” Al-Baqarah: 235.

 

Ndugu yetu, makosa uliyoyafanya ni mengi kama tulivyojaribu kwa ufupi kuyaelezea na kuyataja kadiri ya uwezo tuliowafikishwa na mengi huenda yakatokea kama unavyodhania kama ulivyosema kuwa, Nahofia yasije yakatokea haya, aitoe nafsi yake au aombe talaka yake sababu yangu. Na nimejaribu kumnaswihi lakini haisaidii kitu! Fahamu ikitokea hivyo basi tambua kuwa sababu bila ya shaka yo yote ile utakuwa wewe; la kufanya ni kurudi kwa Mola wako kwa kuachana tena mara moja bali kuufuta na kuung’oa uhusiano wako na huyo mke wa ndugu yako Muislamu na kuisemesha nafsi yako kuwa huyo mwanamke hatokuwa mke wako hata kama ataachwa na mumewe na hiyo ndio huenda ikawa tawbah yako ya kweli kwa Mola wako inshaAllaah kama utakuwa mkweli wa nafsi yako kwani yote hayo hayatotokea kama utakuwa huonani wala huzungumzi nae, acha kazi yako na tafuta nyingine kwa ajili ya Allaah na Allaah Atakukubalia tawbah yako.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share