Kuhudhuria Darsa Msikitini Wanawake Wenye Hedhi

 

SWALI:

Jee unweza kuhudhuria darsa msikitini  sehemu ya wanawake  ukiwa katika hedhi, Na  kuweza kusomesha wanafunzi bila ya kuishika?

 


JIBU:

Wanachuoni wengi wamekubaliana kuwa kupita msikitini kwa dharura kunakubalika. Na wengine wameonelea mwanamke mwalimu au mwenye kusoma (mwanafunzi) anaweza kuhudhuria madarasa hayo kwa sababu asipoteze ile elimu kwa wanaoihitaji, na kwa mwenye kusoma ili asisahahu au kupitwa na mafunzo muhimu kwa sharti tu awe amejistiri vizuri ili asichafue msikiti.

Wanaopinga mwanamke kuingia msikitini na wakaruhusu tu kupita kwa dharura, wanatoa hoja ya Aayah hii:

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ تَقْرَبُواْ الصَّلاَةَ وَأَنتُمْ سُكَارَى حَتَّىَ تَعْلَمُواْ مَا تَقُولُونَ وَلاَ جُنُبًا إِلاَّ عَابِرِي سَبِيلٍ حَتَّىَ تَغْتَسِلُواْ

{{Enyi mlio amini! Msikaribie Swalah, hali mmelewa, mpaka myajue mnayoyasema, wala hali mna janaba - isipo kuwa mmo safarini - mpaka mkoge...}} An Nisaa: 43

Pia baadhi wachache wanatoa hoja ya Hadiyth isemayo: ((Siruhusu mwenye janaba au mwenye hedhi kuingia msikitini)) Lakini Hadiyth hii ni dhaifu kwa mujibu wa wanachuoni wa Hadiyth, miongoni mwao Al-Khatwaabiy, 'Abdul-Haqq Al-Ishbiyliy, An-Nawawy, Al-Albaaniy, na  Ibn Hazm kasema ni Hadiyth batili.

Na wanaoona hakatazwi mwanamke mwenye hedhi kuingia msikitini wanaona kuwa Aayah hiyo haihusiani na mwenye hedhi na vilevile wanatilia nguvu hoja yao kwa ushahidi wa Hadiyth ya ((bi 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) ielezayo kuwa siku moja Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa msikitini akamtuma bi 'Aishah (Radhiya Allaahu 'anha) tandiko la kuswalia (Mswala) na bi 'Aaishah akamjibu "lakini niko kwenye hedhi". Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia,"Bali hiyo hedhi haiko mikononi mwako!))  (na akikusudia kuwa ile hedhi si amri yake au khiyari yake bali ni amri ya Allaah [Subhaanahu wa Ta'al])) imepokewa Hadiyth hii na Imaam Muslim, An-Nasaaiy na wengineo.

Wa Allaahu A'alam

 

Share