037-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kusujudu, Kwenda Chini Kusujudu Kwa Kutanguliza Mikono

 

 

KUSUJUDU

 

Kisha alikuwa  (صلى الله عليه وآله وسلم)akileta Takbiyr na kuporomoka chini kwa kusujudu([1]), na alimuamrisha aliyeswali vibaya afanye hivyo akimwambia: ((Swalah ya mtu ye yote haikamiliki hadi … aseme: 'Sami'a Allaahu Liman Hamidah' na mpaka anyooke sawa sawa, kisha aseme: 'Allaahu Akbar' kisha asujudu mpaka viungo vyake (vitulizane))).([2])

 

Pia alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) anapotaka kusujudu, huleta Takbiyr, (akitenganisha mikono yake mbali na ubavu wake) kisha ndio husujudu)([3])

 

Mara nyingine alikuwa akiinua mikono yake anaposujudu.([4])

 

 

KWENDA CHINI KUSUJUDU KWA (KUTANGULIZA) MIKONO

 

Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akitanguliza mikono yake ardhini kabla ya magoti yake.([5])

 

Alikuwa akiamrisha hivyo kwa kusema: ((Anaposujudu mmoja wenu, basi asiiname kama anavyoinama ngamia, bali atangulize mikono yake kabla ya magoti yake)).([6])

 

Na alikuwa pia akisema: ((Hakika mikono miwili inasujudu kama uso unavyosujudu, basi anapoweka mmoja wenu uso wake, aweke mikono yake na anapoinuka aiinue )).([7])

 

 

Na alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) viganja vyake (akivitanua)([8]) , akibana vidole vyake pamoja([9]) na kuvielekeza Qiblah.([10])

 

Na pia alikuwa akiviweka viganja vya mikono yake usawa na mabega yake([11]), na mara nyingine usawa na masikio yake([12]).  Alikuwa akiimakinisha pua yake na kipaji chake na ardhi.([13])

 

Alimuambia aliyeswali vibaya: ((Unaposujudu, makinisha sijda yako))([14]).  Na katika usimulizi mwingine: ((Unaposujudu, makinisha uso wako na mikono yako, hadi mifupa yako yote itulie mahali pake)).([15])

 

Na alikuwa pia akisema: ((Hakuna Swalah kwa ye ote yule isiyegusa pua yake ardhi kama kinavyogusa kipaji cha uso)).([16])

 

Alikuwa pia akimakinisha chini magoti yake na vidole vya miguu yake([17]), na akielekeza ncha za vidole vya mikono yake Qiblah([18]). Aliweka visigino vyake pamoja([19]). Aliweka miguu yake sawa sawa([20]) na aliamrisha hivyo.([21])

 

Hivi ni viungo saba ambavyo   (صلى الله عليه وآله وسلم) alisujudia; viganja viwili vya mikono, magoti mawili, miguu miwili, kipaji cha uso na pua.

 

Mtume  (صلى الله عليه وآله وسلم)  alivihesabu viungo viwili vya mwisho kama ni kiungo kimoja katika kusujudu kwani alisema: ((Nimeamrishwa kusujudu (katika riwaaya nyingine: Tumeamrishwa kusujudu juu ya viungo saba): Juu ya kipaji cha uso na akaashiria kwa mkono wake([22]), kwenye pua, na mikono, [katika riwaaya nyingine: viganja vya mikono], magoti na vidole vya miguu, na wala tusikunje([23]) nguo na nywele)).([24])

 

Alikuwa akisema: ((Mja anaposujudu, husujudu pamoja nae viungo saba: uso wake, viganja vya mikono yake, magoti yake, na miguu yake)).([25])

 

Na kuhusiana na mtu aliyeswali akiwa kafunga nywele zake([26]) kwa nyuma, Mtume  (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: ((Mfano wake hakika ni kama mfano wa mtu anayeswali huku amefunga mikono yake [nyuma ya mgongo wake]))([27]).  Akasema pia: ((Hiyo ni tandiko la Shaytwaan)), yaani anapokaa Shaytwaan, akikusudia mafundo ya nywele zake.([28])

 

Alikuwa  (صلى الله عليه وآله وسلم)  hailazi mikono yake([29]), bali alikuwa akiinyanyua mbali na ardhi na kuiweka mbali na mbavu zake kiasi kwamba weupe wa kwapa zake huonekana nyuma yake([30]), na pia kiasi kwamba lau mbuzi mchanga angelitaka kupita chini ya mikono yake angelipita.([31])

 

Alikuwa akifanya hivyo sana kiasi cha kwamba baadhi ya Swahaba zake walisema: "Tulikuwa tunahisi vibaya kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa sababu ya vile anavyoweka mikono yake mbali na mbavu zake anaposujudu.([32])

 

Alikuwa  (صلى الله عليه وآله وسلم)akiamrisha hivyo kwa kusema: ((Unaposujudu, weka viganja vyako (ardhini), na inua viwiko vyako ([33]). Na akisema: Kuweni sawa katika sujuud, na wala asitawanye mmoja wenu mikono yake mtawanyo wa [na katika riwaaya nyingine: kama anavyoitawanya] mbwa))([34]).

Na katika tamshi jingine na Hadiyth nyingine: ((Na wala asilaze mmoja wenu mikono yake kama mlazo wa mbwa))([35]). 

Alikuwa pia akisema: ((Msitandaze mikono yenu [kama mtandazo wa mbuai (mnyama wa kuwinda). Lazeni mikono na tandazeni mikono mbali, kwani ufanyapo hivyo, huwa kila kiungo chako kinasujudu nawe)).([36])

 

 

 





[1] Al-Bukhaariy na Muslim.

[2] Abu Daawuud na Al-Haakim ambaye amekiri kuwa ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amewafikiana.

[3] Abu Ya'laa katika Musnad (284/2) ikiwa na isnaad nzuri na Ibn Khuzaymah (1/79/2) ikiwa na isnaad tofauti iliyo Swahiyh.

[4] An-Nasaaiy, Ad-Daaraqutwniy na Mukhlisw katika Al-Fawaaid (1/2/2) ikiwa na isnaad mbili Swahiyh. Kunyanyua mikono huku kumeripotiwa na Maswahaba kumi na Masalaf wengi wameona ni muono Swahiyh. Miongoni mwao ni Ibn 'Umar, Ibn 'Abbaas, Hasan Al-Baswriy, Twaawuus, mtoto wake 'Abdullaah, Naafi' mtumwa wa Ibn 'Umar aliyeachwa huru, Saalim mtoto wa Ibn 'Umar, Qaasim bin Muhammad, 'Abdullaah bin Diynaar na ‘Atwaa. Vile vile 'Abdur-Rahmaan bin Mahdi kasema: "Hii ni kutokana na Sunnah". Imefanywa na Maimamu wa Sunnah; Ahmad bin Hanbal, na imenukuliwa kutoka kwa Maalik na Ash-Shaafi'y.

[5] Ibn Khuzaymah (176/1), Ad-Daaraqutwniy na Al-Haakim ambaye amekiri ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubali. Hadiyth zote zinazopinga hii sio Swahiyh. Namna hii kumeidhinishwa  na Maalik, na ripoti kama hiyo  kutoka kwa Ahmad katika At-Tahqiyq ya Ibn Al-Jawzi (108/2). Al-Marwaz pia amenukuu kwa isnaad Swahiyh. Imaam Al-Awazaa'iy katika Masaail yake (1/47/1) akisema: "Nimewaona watu wakitanguliza mikono kabla ya magoti".

[6] Abu Daawuud, Tamaam katika Al-Fawaaid, na An-Nasaaiy katika Sunan As-Sughraa na Sunan Al-Kubraa (47/1) ikiwa na isnaad Swahiyh. 'Abdul-Haqq amekiri ni Swahiyh katika Al-Ahkaam (54/1) na akaendelea kusema katika Kitabu At-Tahajjud (56/1), "Ina isnaad madhubuti kuliko ya nyuma yake". Yaani Hadiyth ya Waail ambayo ni kinyume (magoti kabla ya mkono). Bali Hadiyth ya mwisho, pamoja nakuwa inapinga Hadiyth hii Swahiyh na iliyotangulia, sio Swahiyh katika isnaad wala katika maana, kama nilivyoelezea katika ‘Silsilatul-Ahaadiyth Adh-Dhwa'iyfah’ (Namba. 929) na katika Al-Irwaa (357).

Itambulikane kwamba njia ya kutofautisha na ngamia ni kutanguliza mikono kabla ya magoti kwa sababu ngamia anaanza kutanguliza magoti kwanza; magoti ya ngamia yako katika miguu yake ya mbele kama ilivyobainishwa katika Lisaan Al-'Arab na vitabu vingine vya Kiarabu, na kama ilivyotajwa na Atw-Twahaawiy katika Mushkil Al-Athaar  na Sharh Ma'aani Al-Athaar. Pia Imaam Qaasim As-Saraqutwniy (رحمه الله) katika Ghariyb Al-Hadiyth (2/70/1-2), ikiwa na isnaad Swahiyh, kauli ya Abu Huraryah, "Asipige magoti mtu kama afanyavyo ngamia anayekimbia". Akasema Imaam, "Hii ni katika sajdah. Anasema kwamba mtu asijitupe chini kama anavyojitupa ngamia anayekimbia (asiyefugwa) kwa haraka na bila ya utulivu, bali aende polepole chini akitanguliza kuweka mikono yake kwanza, kisha yafuatie magoti. Na maelezo ya Hadiyth marfuu' imesimuliwa kuhusu jambo hili". Kisha akataja Hadiyth za juu.

 

Ama kauli ya ajabu ya Ibnul-Qayyim, "Maneno haya hayaeleweki na hayafahamiki na mabingwa wa lugha", inajibiwa na vyanzo tulivyovitaja pamoja na vingi vinginevyo ambavyo maelekezo yanaweza kutafutwa. Nimelezea pia kuhusu hii katika kubainisha uongo dhidi ya Shaykh At-Tuwayjiriy ambayo imechapichwa.

 

[7] Ibn Khuzaymah (1/79/2), Ahmad na Siraaj. Al-Haakim amekiri ni Swahiyh na Adh-Dhahabiy ameikubali. Imetolewa katika Al-Irwaa (313).

[8] Abu Daawuud na Al-Haakim ambaye amekiri ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubali.

[9] Ibn Khuzaymah, Al-Bayhaqiy na Al-Haakim ambaye amekiri ni Swahiyh, na Adh-Dhahaby amekubali.

[10] Al-Bayhaqiy ikiwa na isnaad Swahiyh. Ibn Abi Shaybah (1/82/2) na Siraaj wamehusisha kuelekeza vidole vya mguu katika usimulizi mwingine.

[11] Abu Daawuud na At-Tirmidhiy ambaye amekiri ni Swahiyh, kama alivyokiri Ibn Al-Mulaqqin (27/2). Imetolewa katika Al-Irwaa (309).

[12] Abu Daawuud na An-Nasaaiy ikiwa na isnaad Swahiyh.

[13] Abu Dawuud na At-Tirmidhiy ambaye amekiri ni Swahiyh kama alivyokiri Ibn Al-Mulaqqin (27/2). Imetolewa katika Al-Irwaa (309).

[14]  Abu Daawuud na Ahmad ikiwa na isnaad Swahiyh.

[15] Ibn Khuzaymah (1/10/1) ikiwa na isnaad nzuri.

[16] Ad-Daaraqutwniy, Atw-Twabaraaniy (3/140/1) na Abu Nu'aym katika Akhbaar Isbahaan.

[17] Al-Bayhaqiy ikiwa na isnaad Swahiyh, Ibn Abi Shaybah (1/82/2) na Siraaj. Wamehusisha nia kuelekeza vidole vya mguu katika usimulizi mwingine.

[18] Al-Bukhaariy na Abu Daawuud. Ibn Sa'd (4/157) amesimulia kutoka kwa Ibn 'Umar kwamba alipenda kuelekezea Qiblah kila sehemu ya mwili wake awezavyo wakati wa kuswali hata vidole gumba.

[19] Atw-Twahaawiy, Ibn Khuzaymah (Namba 654) na Al-Haakim ambaye amekiri kuwa ni Swahiyh, na Adh-Dhahaby amekubali.

[20] Al-Bayhaqiy ikiwa na isnaad Swahiyh.

[21] At-Tirmidhy na Siraaj. Al-Haakim amekiri ni Swahiyh na Adh-Dhahaby amekubali.

[22] Kuashiria huku kwa mkono kumefasiriwa kutokana na sarufi ya matini ya Kiarabu (Fat-h Al-Baariy).

[23] Yaani kuvikusanya na kuvizuia kutawanyika, kwa maana, kukusanya nguo au nywele kwa mikono katika rukuu na sujuud (An-Nihaayah). Makatazo haya sio katika Swalah, bali hata kabla ya Swalah imekatazwa kama walivyoongeza Maulamaa wengi katika makatazo. Hii imetiliwa nguvu zaidi kwa kuwakataza wanaume kuswali wakiwa wamefunga nywele zao, ambayo inafuatia baadaye.

[24] Al-Bukhaariy na Muslim. Imetolewa katika Al-Irwaa (310).

[25] Muslim, Abu 'Awaanah na Ibn Hibbaan.

[26] Yaani kubanwa juu au kusukwa.

[27] Muslim, Abu 'Awaanah na Ibn Hibbaan. Ibn Al-Athiyr amesema: "Maana ya Hadiyth hii ni kwamba kama nywele zake ingelikuwa zimelegea, zingelianguka ardhini katika sajdah; hivyo mtu atalipwa thawabu za kusujudu nywele. Lakini nywele zikifungwa, zitamaanisha kuwa hazikusujudu, kwani kamlinganisha na mtu ambaye mikono yake imefungwa pingu pamoja, kwa vile haitogusa ardhini kusujudu.

Inaelekea amri hii imewekewa mipaka kwa wanaume pekee na haiwahusu wanawake kama Ash-Shawkaaniy alivyonukuu katika Ibn Al-'Arabi.

[28]  Abu Daawuud na At-Tirmidhiy ambaye amekiri ni nzuri. Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan amekiri ni Swahiyh. Taz. Swahiyh Abu Daawuud (653).

[29]    Al-Bukhaariy na Abu Daawuud.

[30]    Al-Bukhaariy na Muslim. Imetolewa katika Al-Irwaa (359).

[31]    Muslim, Abu 'Awaanah na Ibn Hibbaan.

[32]   Abu Daawuud na Ibn Maajah ikiwa na isnaad Hasan.

[33]    Muslim na Abu 'Awaanah.

[34]    Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud na Ahmad.

[35]    Ahmad na At-Tirmidhiy ambaye amekiri ni Swahiyh.

[36]   Ibn Khuzaymah (1/80/2), Al-Maqdisy katika Al-Mukhtaarah na Al-Haakim ambaye amekiri ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubali.

Share