Nini Maana ya Kibri Iliyotajwa Katika Mas-ala Ya Isbaal?
SWALI:
Assalam alykum,
ni nini maana ya kisheriah ya kibri? Nimesoma makala ya kuvaa nguo ya chini isiyopita kongo mbili za mguu. Katika hadith za isbaal, zinafahamisha atakae vaa nguo yake ya chini yenye kupita kongo mbili za mguu kwa kibri basi motoni. Sasa hii kibri maana yake ya kisheria ni ipi?
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu maana ya kibri kisheria.
Kwa Lugha nyepesi labda kabla ya kuja katika sheria ni kujiona au kuwa na majivuno.
Maana ya neno hilo kisheria limeelezewa na mwenyewe Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kutwambia kuwa ni kuwatweza na kuwadharau watu na kukataa haki. Na hakika ni kuwa hakuna haki kama maneno ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na yeyote atakayeyapinga maneno hayo atakuwa ni mwenye kiburi cha hali ya juu.
Na ikiwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufahamisha kuwa haifai kwa Muislamu mwanamme kuvaa nguo yenye kupita kongo/fundo mbili za miguu na yeyote atakayefanya hivyo basi atakuwa amefanya kosa la kumuingiza Motoni. Baada ya hayo, Muislamu akawa anafanya hivyo ni kuashiria kiburi cha hali ya juu.
Huenda mtu akauliza huku kuvaa nguo ndefu kuna mahusiano gani na kibri. Tufahamu kuwa si kila jambo la sheria tunapata hekima yake moja kwa moja lakini kila linalokatazwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huwa kuachwa kwake kuna maslahi na Muumini wa kweli.
Kuburuza nguo ilikuwa ni ada ya kijahiliya, mabwanyenye wa Ki-Quraysh walikuwa wakivaa hivyo kwa kiburi na hivyo mwenye kufanya hivyo leo ni sawa na kuwaiga wao na mwenye kuwafuata watu atafufuliwa na wao. Na kwa sababu tumeambiwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu hilo basi inaweza mtu kwa kuvaa nguo ndefu akaingia katika kiburi.
Na hivyo, Muumini wa kweli anapaswa kujiepusha na kuvaa vazi lenye kuvuka mafundo ya miguu yake miwili kwa kuwepo Hadiyth nyingi zenye makemeo na makatazo ya kufanya hivyo kwa kiburi na bila kiburi kama zinavyoonyesha Hadiyth zifuatazo:
Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Kilicho chini ya fundo mbili katika shuka hicho kitakuwa motoni" (al-Bukhaariy na an-Nasaa'iy).
Na imepokewa tena kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Allaah Hamuangalii mwenye kuburuza nguo yake kwa kiburi" (al-Bukhaariy, Muslim na Maalik).
Na imepokewa katika riwaya nyingine kutoka kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Allaah Hatozungumza na watu aina tatu Siku ya Qiyaamah wala Hatowaangalia na wala Hatowatakasa na watakuwa na adhabu iumizayo". Akasema: "Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliikariri kauli hii mara tatu". Akasema Abu Dharr: "Watu hao wamehasirika, ni kina nani ewe Mtume wa Allaah?" Akasema: "Mwenye kuburuza nguo kwa kiburi; na mwenye kujionyesha kwa fadhila aliyomfanyia mtu mwengine; na mwenye kuuza mali duni kwa kiapo cha uongo" Muslim. Na katika riwaya nyengine: "Mwenye kuburuza kikoi chake kwa kiburi".
Na imepokewa kwa Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhuma) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Allaah Hatowaangalia wale watu walioburuza nguo zao kama kikoi na kanzu na kilemba kwa kiburi" (Abu Daawuud na an-Nasaaiy kwa Isnadi iliyo sahihi).
Hivyo Muislamu mzuri ni yule mwenye kusikia na kutii na kuyatekeleza yale yaliyotoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa hiyo haifai Muislam kuvaa suruali, kanzu, kikoi au vazi lenye kuburuza (kuvuka mafundo ya miguu) lenye kujulikana kama 'Isbaal'.
Hivyo inatakiwa tuwe macho katika kutekeleza tunayoamrishwa na sheria na kuepukana na makatazo ili tuwe mahali pazuri hapa duniani na kesho Akhera.
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuepushe na kiburi, kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwa kututahadharisha:
"Haingii Peponi ambaye ndani ya moyo wake uzito wa atomu (chembe ndogo) wa kiburi" (Muslim, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy).
Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate manufaa zaidi:
Isbaal - Hukmu Ya Nguo Inayovuka Mafundo Ya Miguu Ya Mwanaume
Isbaal – Vazi La Mwanamme Lenye Kuvuka Mafundo Ya Miguu (Uburuzaji Au Kuburura) - 1
Isbaal – Vazi La Mwanamme Lenye Kuvuka Mafundo Ya Miguu (Uburuzaji Au Kuburura) - 2
Na Allaah Anajua zaidi