Mashairi: Adabu Na Tabia Njema
Adabu Na Tabia Njema
‘Abdallah Bin Eifan (Rahimahu Allaah)
Nawapa nyingi salaamu, kama maji ya kisima,
Hapa nashika kalamu, nina machache kusema,
Ninaandika kwa hamu, kuwaelezeni umma,
Adabu, tabia njema, pambo la Waislamu.
Pambo la Waislamu, adabu, tabia njema,
Tumefundishwa elimu, dini yetu imesema,
Kumbuka wetu Imamu, Mtume kwa wake wema,
Adabu, tabia njema, pambo la Waislamu.
Viumbe kuwaheshimu, tulifundishwa mapema,
Wadogo na wamakamu, wote hupewa heshima,
Twakatazwa kudhulumu, hata porini wanyama,
Adabu, tabia njema, pambo la Waislamu.
Twaheshimu binadamu, walokufa na wazima,
Wote walio timamu, na hata wenye vilema,
Na hata wendawazimu, tuwaonee huruma,
Adabu, tabia njema, pambo la Waislamu.
Maswahaba ni walimu, sifa zao zinavuma,
Walifundisha kaumu, kuishi kwa usalama,
Maisha yao magumu, ona hawakulalama,
Adabu, tabia njema, pambo la Waislamu.
Usisahau binamu, usifanye kuwanyima,
Kuwazuru maalumu, Mungu (Allaah) hayo Amesema,
Hilo ni kubwa jukumu, kuwakumbuka ni vyema,
Adabu, tabia njema, pambo la Waislamu.
Hata mavazi muhimu, vaa nguo kwa kupima,
Dini itakulaumu, kuigiza kina mama,
Mwisho wake jahanamu, haraka usipokoma,
Adabu, tabia njema, pambo la Waislamu.
Jirani kumuheshimu, kumuuliza daima,
Ni wajibu kuhudumu, anapotaka huduma,
Kwa machungu na matamu, kuwa nae fanya hima,
Adabu, tabia njema, pambo la Waislamu.
Milango usihujumu, kupiga hodi lazima,
Ukialikwa karamu, uroho uweke nyuma,
Mgeni kumkirimu, wajibu huo tazama,
Adabu, tabia njema, pambo la Waislamu.
Wagonjwa kuwasalimu, na kwenda kuwatazama,
Wajibu huu fahamu, thawabu utazichuma,
Hao walo mahamumu, uwaombee uzima,
Adabu, tabia njema, pambo la Waislamu.
Uongo kitu haramu, dharau hukuandama,
Na watu kuwashutumu, kuwabebesha lawama,
Adabu kuwa adimu, mambo yako husimama,
Adabu, tabia njema, pambo la Waislamu.
Na watu kutabasamu, ni adabu na hekima,
Bila adabu kudumu, mambo mengi yatakwama,
Husimama gurudumu, mambo huenda mrama,
Adabu, tabia njema, pambo la Waislamu.
Dini ya Kiislamu, ni Dini yenye neema,
Mola Amesha hukumu, Qura-ani tumesoma,
Ya kwamba Uislamu, ya mwisho ndio hatima,
Adabu, tabia njema, pambo la Waislamu.
Shairi nalikhitimu, naomba Rabbi salama,
Ikipigwa baragumu, hapo siku ya Qiyaama,
Aturehemu Rahimu, kwa nyingi Zake Rehema,
Adabu, tabia njema, pambo la Waislamu.