Kuna Du'aa Khaswa Baada Ya Kumaliza Nifaas (Damu Ya Uzazi) ?

 

Kuna Du'aa Khaswa Baada Ya Kumaliza Nifaas (Damu Ya Uzazi)?

 

 

 

SWALI:

 

 

Baada ya kujifungua kwa mwanamke na kukaa siku 40 je dua yake ni ipi? ili niweze kuendelea na ibada 

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho 

 

 

Mwanamke anapotoka kujifungua uzazi huwa katika hali ya 'nifaas' (kutokwa damu ya uzazi). Na hali hii huwa inategemea kila mtu alivyojaaliwa kuwa nayo. Baadhi ya wanawake huwa katika hali hiyo kwa muda wa siku arubaini, wengine zaidi ya siku arubaini, wengine chini ya siku arubaini.

 

Anapomaliza tu mwanamke kutokwa na damu ya nifaas basi anatakiwa aendelee na ‘ibaadahh zake za kuswali na Swawm kama kawaida hata kama hakuchukuwa siku nyingi kuwa katika hali ya nifaas. Mfano hata kama alikuwa na damu ya nifaas kwa wiki mbili tu, basi pindi atakaposita damu na kuona maji meupe ya kutoharika atakuwa amemaliza nifaas na aendelee kufanya ‘ibaadah zake kama kawaida, na kutimiza mengine yote kama kawaida.

 

Na kurudia katika ‘ibaadah baada ya nifaas hakuna du'aa yoyote iliyo makhsusi katika mafundisho ya Sunnah, bali ni kukoga josho kama josho la hedhi au janaba, kwa kuweka niya moyoni (Na sio kutajwa mdomoni), na kuendelea na Swalaah yake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share