Anaweza Kuswali Ikiwa Atatokwa Na Manii Bila Ya Kitendo Cha Ndoa?

Anaweza Kuswali Ikiwa Atatokwa Na Manii Bila Ya Kitendo Cha Ndoa?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI

 

Je, mtu akishikana na mkewe mpaka akatoka manii bila ya kufanya tendo la ndoa anaweza kusali bila ya kuoga janaba?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Janaba inapatikana kwa hali ya kutokwa na manii sawa ikiwa manii yamekutoka kwa kuingiliana (yaani kwa kuzama kichwa cha dhakari ndani ya utupu wa mwanamke) au kuota, au kujichua n.k., na kwa hali hiyo huwezi ukaswali mpaka ujitwaharishe.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنتُمْ سُكَارَىٰ حَتَّىٰ تَعْلَمُوا مَا تَقُولُونَ وَلَا جُنُبًا إِلَّا عَابِرِي سَبِيلٍ حَتَّىٰ تَغْتَسِلُوا ۚ  

Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah na hali mmelewa mpaka mjue mnayoyasema, na wala mkiwa mna janaba isipokuwa mmo safarini mpaka muoge josho.  [An-Nisaa: 43]

 

Na katika Sunnah anasema Ummul-Muuminiyna ‘Aaishah (Radhwiya Allahu 'anhaa) kuna Mtu mmoja alimuuliza Nabiy (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu mtu anayemjamii mke wake kisha akakatisha ile jimai (katikati bila ya kushusha manii): Je, analazimika kuoga (janaba)? Na Bi ‘Aaishah wakati huo akiwa ameketi – Nabiy (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Kwa hakika mimi na huyu bibie hufanya hivyo kisha tunakoga" [Muslim]

 

Bonyeza  kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi ya maudhui hiyo:

 

Ikiwa Mtachezeana Tu Na Kutokwa Manii Inapasa Kukoga Josho?

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share