06-Jihaad: Simba (Mmarekani) Na Chui (Umoja Wa Mataifa)
Simba na Chui
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Mtakapouziana kwa riba, mkajishughulisha na biashara, mkaridhika na kilimo, na mkaiacha jihadi (wakati wenzenu wanauliwa), Allaah atakuteremshieni udhalilifu mtakaoshindwa kuuondoa mpaka (pale) mtakaporudi katika dini yenu.” (Abu Daawuud na Imam Ahmad)
Na imetolewa na Muslim na Abu Daawuud na An-Nasaaiy na Al-Haakim na Al-Bayhaqiy kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) pia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Atakayekufa bila kupigana (jihadi) na wala (hata) kumpitikia moyoni mwake (nia ya kupigana) jihadi, (akifa) anakufa akiwa na sehemu ya unafiki.”
Waislamu ni umma uliochaguliwa na Allaah kwa ajili ya kuuongoza ulimwengu na walimwengu na kulinyanyua juu neno la Allaah, lakini Waislamu leo wamekuwa watu dhalili kupita umma zote zinazotembea juu ya ardhi. Kila anayetaka kuzifanyia silaha zake majaribio au kujipima nguvu, anazielekeza silaha hizo na nguvu hizo kwa Waislamu. Tumeyaona hayo yakitokea sehemu mbali mbali ulimwenguni, zikiwemo Bosnia, India, Afghanistan, Palastina na sasa Iraq, na hivi karibuni Gaza (Palestina).
Kote huko na katika sehemu mbali mbali ulimwenguni Waislamu wanadhalilishwa, wanauliwa, watoto kwa wakubwa, wanawake kwa wanaume, na majumba yao yanabomolewa mbele ya kamera za television na mbele ya macho ya kila mtu, bila watu kujali wala hata nyoyo kusituka. Kisha Waislamu hao hao eti wanakimbilia kupeleka mashitaka yao Umoja wa Mataifa wakitegemea kupata msaada, wakati wote hao (Marekani, Mayahudi na Umoja wa Mataifa) ni kitu kimoja.
Na hii inanikumbusha kile kisa cha chui na kima:
Inasemekana kuwa chui alikuwa akipenda kumuonea kima na kumpiga bila sababu yoyote, na kila anapomuona alikuwa akitafuta kisingizio chochote cha kumpiga makofi ya uso kima yule.
Alikuwa mara nyingine akimwambia;
“Kofia yako iko wapi! Mbona leo hujavaa kofia, si nilikwambia lazima uivae? Kesho lazima nikuone nayo,” humwambia hivyo huku akimtandika makofi na mateke.
Siku ya pili kima anapokuja akiwa amevaa kofia, chui yule yule humvamia na humpiga makofi huku akimwambia:
“Kwa nini umevaa kofia! Si nilikwambia usiivae?” akiivaa anapigwa na asipoivaa anapigwa.
Hali ikaendelea hivyo mpaka siku ile kima alipochoka kuonewa, akaamua kumshitaki chui kwa mfalme simba bila kujuwa masikini kuwa simba na chui wote ni kitu kimoja.
Mfalme simba akamwita chui pembeni na kumwambia kwa kumnong'oneza:
“Wewe vipi ndugu yangu! unampiga mwenzio bila kumtafutia kisingizio kinachokubalika? Tizama mimi kwa mfano; ninapotaka kumpiga punda nafanya nini? Humtuma aniletee matufaha, na yeye bila kuniuliza hukimbia na kuniletea matufaha mekundu, mimi hapo humtandika makofi na kumwambia:
“Nani aliyekuaambia uniletee matufaha mekundu?”
Hapo yeye hukimbia na kurudi haraka akiwa ameniletea matufaha ya kijani, na hapo namtandika tena makofi na kumwambia:
“Nani aliyekwambia uniletee matufaha ya kijani?” na kwa njia hii namtandika makofi kwa raha zangu.”
Chui akaona kuwa hii ni fikra nzuri, akaondoka na kwenda moja kwa moja mpaka kwa kima akamwambia:
“Nenda kaniletee matufaha sasa hivi, tena mbiyo!”
Lakini kima anakhitalifiana na punda, kima alimuuliza chui:
“Unata nikuletee matufaha rangi gani? Mekundu au kijani au manjano?
Chui kuona ameshindwa hila akarudia pale pale:
“Mbona leo hujavaa kofia eh?”, Ngumi! Teke!
Na hii ndiyo hali yetu Waislamu baada ya kuyaacha mafundisho ya dini yetu, na kuiacha jihadi na kuyakimbilia maisha ya dunia, Allaah Ametusalitishia udhalili ikawa kila safihi anapotaka kujipima nguvu zake anakuja kututandika sisi ngumi na makofi yake, na sisi tunakimbilia kwa mfalme Simba (Mmarekani) au kwa chui (Umoja wa Mataifa) na kumbe wote hao ni kitu kimoja waliokwishaamua kumpiga vita kila anayetaka kuisimamisha bendera ya Laa ilaaha illa Allaah.
Tunamuomba Allaah Atusimamishie kiongozi wa kheri, awe katika utawala wake kiongozi huyo anaheshimiwa kila mwenye kumuogopa Allaah, na anadhalilishwa kila mwenye kumuasi Allaah. Awaunganishe umma chini ya bendera ya Laa ilaaha illa Allaah na kuihuisha Jihadi ambayo kwayo pekee umma huu utarudisha heshima yake - Aamiyn.
Al-Wahn
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Hivi karibuni mtakuja zungukwa na mataifa, mfano wa walaji wanavyokizunguka chakula chao (wanavyokaa kuizunguka sinia ya chakula)." Tukasema: "Kwa sababu ya uchache wetu ewe Mtume wa Allaah siku hiyo?" Akasema: "Hapana, nyinyi siku hiyo mtakuwa wengi, lakini mtakuwa (mumegawanyika) muko mbali mbali mfano wa takataka zinazokumbwa na maji ya mvua. Allaah Ataondoa haiba yenu kutoka katika vifua vya adui yenu, na ataingiza ndani ya nyoyo zenu Al-Wahan (udhaifu)." Mmoja akauliza: "Ewe Mtume wa Allaah, ni kitu gani hiki Al-Wahan?" Akasema: "Kuipenda kwenu dunia na kuyachukia mauti." (Imam Ahmad katika Musnad yake)
Hadithi hii ni muujiza katika miujiza ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) juu ya hali yetu hivi sasa. Kama kwamba alipokuwa amekaa pale Msikitini kwake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akihadithia hadithi hii, alikuwa akiiona hali yetu hivi sasa kama tulivyo.
Maadui wa Waislamu wanatutuhumu kuwa tunaongezeka kwa wingi, na wanazihadaa serikali zetu zikubali kutupa dawa za kuzuia uzazi. Hii ina maana kuwa idadi yetu inaongezeka, lakini juu ya wingi wetu, hatuna maana yoyote. Hatuna faida yoyote. Maadui wa Allaah wanatuuwa, wanatudhalilisha, wanatutenganisha, wanatugawa, wanatugombanisha, na sisi hatuna la kufanya, bali hatuwezi kufanya kitu. Wanatusukuma wanapotaka, na wanatuendesha wanavyotaka. Tumekuwa mfano wa takataka zinazokumbwa na kusukumwa na maji ya mvua huku na kule.
Na muujiza mwingine uliomo ndani ya hadithi hii ni kule kuungana dhidi yetu kwa mataifa yote. Wamarekani, wazungu wa Ulaya, Mayahudi, Wajapani na maadui wa Allaah walioko Magharibi na Mashariki ya ulimwengu, wote wamejikusanya na kutuzunguka, mfano wa walaji wanavyokizunguka chakula chao. Wote wamekula kiapo kuupiga vita Uislamu. Wakati huo huo sisi tumo katika starehe zetu, kama kwamba hapana kinachotokea. Kila mmoja anakiogopea kiti chake, anaiogopea mali yake, anauogopea mustakbali wake, anaiogopea nafsi yake. Tunaipenda dunia na tunayachukia mauti.
Tunafaidika na hadithi hii pia ile balagha, ule ubingwa wa kutumia lugha uliotumika katika kuwaelezea maadui wa Allaah, pale (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema: "mfano wa walaji wanavyokizunguka chakula chao." Na hii inatuonyesha njaa waliyonayo maadui hawa, na tamaa yao kubwa juu ya mali za Waislamu na utajiri wao. Wanakuja kwa nguvu zao zote na kwa ujabaruti na ujeuri mkubwa na kibri huku wakiwasaidia Mayahudi kwa nguvu zao zote ili waweze kuzinyakua mali hizo na uchumi huo na ardhi.
Na muujiza mwengine ni kule kufanya kwao wanavyotaka bila kujali masikitiko yetu wala huzuni zetu wala lawama zetu wala hata vilio vyetu. Wanafanya wanavyotaka. Wanapiga wanavyotaka, wanabomoa wanavyotaka, kama kwamba ardhi yote na Waislamu wote ni milki yao. "Mfano wa walaji wanavyokizunguka chakula chao."
Hata Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) walishangazwa waliposkia, wakauliza:
"Kwa sababu ya uchache wetu ewe Mtume wa Allaah siku hiyo?" Walishangaa vipi tutakuwa katika hali hii, vipi maadui wataweza kutupiga wakati idadi yetu ni kubwa kupita yao. Bila shaka tutakuwa wachache wakati huo. Lakini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akawaambia: "Hapana, (bali) nyinyi siku hiyo mtakuwa wengi, lakini mtakuwa mumefarakana mfano wa takataka zinazokumbwa na maji ya mvua."
Izingatie vizuri kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema "nyinyi siku hiyo mtakuwa wengi", na hii maana yake ni kuwa mwili wa Waislamu ni mwili mmoja. Tokea wakati ule mpaka wakati huu, sisi sote ni kitu kimoja.
"مثل المؤمنين في توادهم وتراحمهم كمثل الجسد الواحد إذا اشتكى منه عضو تداعى له سائر الجسد بالحمى والسهر"
Mfano wa Waislamu katika kupendana kwao na kuhurumiana kwao ni mfano wa mwili mmoja, kinapoumia kiungo kimoja basi viungo vyote vilivyobaki vinashirikiana (nacho kiungo hicho) kwa homa na kukesha. (Al-Bukhaariy na Muslim)
Hivi ndivyo alivyotufundisha Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)
Na katika hadithi hii ya kuzungukwa na maaduwi tunaweza kuujuwa ugonjwa wetu na pia kuijuwa dawa yetu.
Maradhi yetu ni kuwa mbali na Allaah, mfarakano wetu, na kuipenda kwetu dunia.
Na dawa yetu ni kurudi kwa Mola wetu (Subhaanahu wa Ta’ala). Turudi katika dini yetu. Tuirudishe imani yetu na kumtegemea Allaah peke Yake. Tumuogope Yeye tu, na tuache kuuogopa uluwa na mali na ufalme na vitu kama hivi visivyo na thamani yoyote mbele ya Allaah. Tuache kuuthamini ulimwengu na kuyaogopa mauti.
Tuwalee watoto wetu malezi ya Kiislamu na mafundisho ya Allaah na ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Tuwafundishe taariykh yetu.
Kurudi kwa Allaah na kurudi katika mafundisho ya dini Yake ndiyo jambo la pekee linaloweza kuturudishia heshima yetu na utukufu wetu.