003-Hakimu Wa Kiislamu: Umuhimu Na Faida Ya Kujifunza Sheria
UMUHIMU NA FAIDA YA KUIFAHAMU SHERIA
Uislamu umejengwa kwa mihimili mikuu kutoka katika Qur-aan na Sunnah ya Bwana wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Yeyote anayefuata nje ya mfumo huu basi atawajibika kueleza ni kwa nini alifanya hivyo. Kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) zinathibitisha:
{{Bila shaka Dini (ya haki) mbele ya Allaah ni Uislamu. Na waliopewa Kitabu (Mayahudi na Manaswara) hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ilimu. (Walikhitalifiana) kwa sababu ya uhasidi uliokuwa baina yao. Na anayezikataa Aya za Allaah (Allaah Atamuadhibu huko Akhera), na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.}}
[Suratu al-'Imraan: 19]
{{Na anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye khasara (kubwa kabisa).}}
[Suratu al-'Imraan: 85]
{{Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na kukutimizieni neema Yangu, na Nimekupendeleeni Uislamu uwe Dini yenu.}} [Surratu al-Maaidah: 3]
Kwa hakika Aayah hizo hapo juu zinatudhihirishia kwamba, Uislamu ndio Dini ya haki ya kufuatwa na viumbe vyote. Kupitia Uislamu wetu huu, ndio tunapata mfumo mzima wa maisha. Haitakikani kwa Muislamu kuwa na khiyari ya Uislamu wake; iwe ni kiuchumi, kisiasa au kijamii. Taratibu zote za maisha ya Muislamu yatakiwa kuegemezwa kupitia kwenye Uislamu wake. Ndipo hata tunapoona kwamba hata mwenendo wa kusikiliza na kutolea hukumu kwenye migogoro yatakikana kufuata mkondo wa Uislamu. Naye Allaah Ametuthibitishia hili kwa kauli Yake:
{{Enyi mlioamini! Ingieni katika hukumu za Uislamu zote…}}
[Suratu al-Baqarah: 208]
Waislamu wanashurutishwa kuitakidi amri zote za Uislamu kuwa ni stahiki juu yao kufuatwa. Wala si katika Muumini mwenye kuzikubali baadhi na kuzikataa baadhi. Hii ndio njia sahihi ya Uislamu. Hivyo basi, mwenye kutaka mafanikio duniani na Akhera anawajibika kushikamana na kamba ya Allaah Mtukufu.
Kabla ya kuja Uislamu, kulikuwa na upotevu wa hali ya juu kabisa; upotevu huu ama ulikuwa wa kuteleza na kuvuka mipaka katika kutafuta njia za kujikurubisha kwa Mola, au kwa kupotoka na kupindukia mipaka katika kumfuata Shaytwaan.
Ukaja Uislamu ukakuta upotevu na makosa katika utaratibu ulio nje ya maumbile ya mwanaadamu, haki ikifanywa batili na kinyume chake. Hivyo, jambo la kwanza ulilolifanya Uislamu ni kutengeneza sehemu hii muhimu ya Shari’ah. Sehemu hii ilitengenezwa kwa misingi mbali mbali ya Kishari’ah ambayo kupitia huko masala ya lipi la kufuatwa na lipi la kuepukwa yakatengenea.
Uislamu ukarudisha mambo haya kwenye asili yake, na kuweka mizani ya uadilifu na vipimo vya kupimia lililo halali na haramu. Kwa hivyo, Ummah wa Nabii Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ukawa katikati baina ya wale waliopotea na wale walioongoka. Yaani ukawa Ummah wa wastani na bora kuliko Ummah zote zilizopita, kama ulivyosifiwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni Umma bora ulioletwa kwa wanaadamu:
{{Nyinyi ndio Ummah bora kuliko ummah zote zilizodhihirishiwa watu (ulimwenguni) – mnaamrisha yaliyo mema na mnakataza yaliyo maovu, na mnamwamini Mwenyezi Mungu.}} [Suratu al-Ímraan: 110]
Na kwa hakika sio kazi nyengine tunayoifanya kwa wana jamii isipokuwa ni kujiengua miongoni mwa wenye kula khasara kutokana na kupoteza muda pamoja na kuacha kuamrisha mema na kukatazana maovu:
{{Kuwa binaadamu yuko katika hasara.}}
{{Isipokuwa wale walioamini na wakafanya vitendo vizuri, na wakausiana (kufuata) haki na wakausiana (kushikamana) na subira (kustahamiliana).}} [Suratul-Ásr: 2-3]
Ni wajibu wa Muislamu kuelewa kwamba kutafuta elimu ndani ya Uislamu ni faradhi kama ilivyo faradhi ya Swalah. Kwa hakika hawapo sawa wale wenye kujua na wasiojua:
{{Je wanalingana wale wanaojua na wale wasiojua?}} [Az-Zumar: 9]
Allaah pia Anaelezea daraja ya wale waliopata elimu:
{{“Atawainua Mwenyezi Mungu wale walioamini miongoni mwenu, na wale waliopewa elimu wana daraja kubwa.}} [Al-Mujaadalah: 11]
Pia Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) anatufahamisha kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Kutafuta elimu ni faradhi juu ya kila Muislamu.)) [Ibn Maajah, Shaykh Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Sunnan Ibn Maajah].
Hakika mwenye kuitafuta elimu hurahisishiwa njia ya kwenda Peponi kama alivyosema kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwenye kupita katika njia inayoshikamana ndani yake na elimu, Atamrahisishia Mwenyezi Mungu njia ya Peponi.)) [Al-Bukhaariy]
Na katika mapokezi mengine, amesimulia Abu Hurayrah:
Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Yeyote anayetoka katika njia akiitafuta kutokana nayo (njia hiyo) elimu, Humrahisishia Mwenyezi Mungu njia ya Peponi.)) [Imepokelewa na Muslim]
Elimu ndani ya Uislamu sio tu kusoma Qur-aan kama kasuku. Bali ni kuielewa, kuifanyia kazi pamoja na Sunnah alizokuja nazo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na ni nani anayesema kwamba elimu katika Uislamu ni ile tu inayomfikisha msomaji kuvaa vilemba vikubwa?! Uislamu umeweka kipaumbele katika elimu zote, iwe ni yenye kutoa vifungu vya sheria ama ni yenye kutibu ama inayorusha roketi na kadhalika. Tunatamka kwa vinywa vipana kwamba, elimu yoyote ambayo itakuwa na manufaa kwa Waislamu wenyewe na Ummah huu wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi tutaisaka, tutaisoma na tutaifanyia kazi kwa bidii zote bi idhni Llaah!
Uislamu umehimiza kusoma, na ndani ya hiyo elimu kuna mambo ya Shari’ah ambayo sio vyema kwa Muislamu kuiacha nyuma kwa kigezo kwamba haifanyiwi kazi. Popote inapopatikana fursa ya kuitumia basi na itumike Shari’ah. Muislamu anatakiwa kugida kila anachoweza kutokana na elimu aliyotuachia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
Imesimuliwa na Abu Muusa: Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Mfano wa uongofu na elimu ambayo Allaah Amenileta (kuifikisha) ni kama mvua kubwa inayoanguka juu ya ardhi, baadhi yake katika ardhi yenye rutba imenyonya maji ya mvua na ikaleta (kutokana nayo) mimea na majani kwa wingi. (Na) baadhi yake (ardhi) ilikuwa nzito na ikazuia maji ya mvua (kupenya katika ardhi) na Allaah Akawanemeesha watu kutokana nayo na wakaitumia kwa kunywa, kunyweshea wanyama wao na kwa ajili ya umwagiliaji na kilimo kwenye ardhi hiyo. (Na) baadhi yake (ardhi) ilikuwa sio yenye rutuba ambayo haikuweza kukamata maji wala kutoa mimea (hivyo ardhi hiyo haikutoa faida yoyote). (Ardhi) Ya mwanzo ni mfano wa mtu anayetambua dini ya Allaah na akapata faida (kutoka na elimu) ambayo Allaah Ameishusha kupitia kwangu (Mitume na wanazuoni) na akaisomesha kwa wengine. (Ardhi) Ya mwisho ni mfano wa yule mtu asiyeijali na hachukui (hafuati) uongofu wa Allaah Alioushusha kupitia kwangu (Ni mfano wa hiyo ardhi isiyo na rutuba).)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]
Udhalilifu tunaoupata hivi leo katika ulimwengu huu unatokana na kukosa elimu sahihi pamoja na kutoisimamisha hiyo elimu tunayoifuata. Maadui zetu wametugawa na tugawika vipande vipande kama kigae kilichovunjika. Hatukumalizia hapo tu, bali tukachaguliwa elimu za kuzisoma na zipi za kusimamisha. Hatimaye, tukawa hatusemi wala kutetea isipokuwa kile tulichokisoma mashuleni kupitia mitaala ya kikafiri.
Ukweli ni kwamba kuna fadhila kubwa za kusoma. Mwenye elimu ndani ya Uislamu umemtukuza zaidi kuliko yule anayefanya ibada bila ya elimu. Fadhila hizi hazikuishia hapo tu, bali huombewa maghfira na viumbe vyote vilivyomo mbinguni na ardhini:
Kutokana na Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema: Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Fadhila za mwenye elimu juu ya mwenye kufanya ibada kama fadhila za aliye chini yenu))
Kisha akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Hakika ya Mwenyezi Mungu na Malaika Wake na viumbe vya mbinguni na ardhini hata wadudu ndani ya mashimo yao na hata samaki wanamswalia mwenye kusomesha watu khayr.)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy]
Qur-aan na Sunnah pia zinatuonesha kwamba mali na watoto havina umuhimu mbele ya elimu, kwani hata Mitume hawakurithisha mali kwa taifa lao isipokuwa elimu. Elimu ndio mirathi waliyotuachia Mitume wetu, kwani wao hawarithishi makasri wala dhahabu wala pesa:
Kutokana na Abu Dardaai (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwenye kuifuata njia kuitafua elimu, Allaah Humfanyia wepesi njia ya Peponi, na hakika ya Malaika wanagubika mbawa zao kwa mwenye kutafuta elimu, wapo radhi kwa anayoyafanya, na hakika ya mwanazuoni anaombewa maghfira kwa aliyepo katika mbingu na ardhi hata samaki baharini, na fadhila za mwanazuoni juu ya mwenye kufanya ibada ni kama fadhila za mwezi juu ya nyota nyengine, na hakika ya wanazuoni ni warithi wa Mitume, na hakika Mitume hawarithishi dinari wala dirham, na hakika (wao) wanarithisha elimu. Basi yeyote atakayechukua (elimu hiyo), amechukua kitu bora.)) [Imepokewa na Abu Daawuud na Tirmidhiy]
Leo ulimwengu wetu umegubikwa na tatizo la kuwaweka madarakani viongozi wenye ukosefu wa elimu sahihi na wasio wacha Mungu, waliopo ni wachache sana wenye sifa hizo, ama wengi ni wenye elimu ya kubahatisha, wenye kutumia elimu yao kwa maslahi ya kilimwengu na wenye kutumiwa kuuvuruga Uislamu.
Imesimuliwa na 'Abdullaah bin 'Amr bin Al-'Aas kwamba: Nimemsikia Mjumbe wa Allaah akisema:
((Allaah haichukui elimu kwa kuichukua kutoka kwa (mioyo ya) watu, lakini anaichukua kwa kufariki Maulamaa hadi hakuna yeyote (‘Aalim) atakayebaki, watu watawafanya viongozi wao wajinga ambao watakapoulizwa watatoa fatwa zao bila ya elimu. Hivyo watapotea na watawaongoza watu kwenye upotevu)) [Al-Bukhaariy]
Elimu na Uislamu ni vitu vinavyokwenda sambamba ndani ya mfumo wetu huu wa maisha hapa duniani. Kuna khayr kubwa kwa yule mwenye kupatiwa elimu inayotokana na diyn hii ya Uislamu, kwani zipo elimu nyingi na chungu nzima zisizo na asili yoyote na Uislamu. Mfano wa somo la historia kuwasomesha wanafunzi ya kwamba binadamu asili yake ni sokwe! Subhaana Allaah.
Mu'aawiyah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesimulia kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Mwenyezi Mungu Akimtakia khayr (mja Wake) Humpa ufahamu (elimu) katika diyn.)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Kazi hizi tuzifanyazo kwa jamii si chochote ila ni kutafuta radhi za Muumba. Kwani hili ni jukumu la kila Muislamu kumsomesha mwenziwe kwa kile alichokipata. Hata gari la shilingi milioni mia moja halina thamani mbele ya yule aliyemuongoza mja mmoja tu:
Kutokana na Sahal bin Sa'ad (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema: Hakika ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kumwambia 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu):
((Ninaapa kwa Allaah kwamba Akimuongoza Allaah mja kupitia kwake mtu mmoja ni bora kwake kuliko ngamia mwekundu.)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Pia katika Hadiyth nyengine, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema mwenye kulingania uongofu, atapata ujira wa anayemfuata bila ya kupunguziwa chochote:
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema: Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Yeyote anayelingania katika uongofu, atakuwa na ujira mfano ujira wa anayemfuata, hatapunguziwa kutokana ujira huo chochote.)) [Muslim]
Muhimu kuelewa kwa makini kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amempatia dhamana ya moto kwa yule anayemsingizia uongo:
Kutokana na 'Abdullaah bin 'Amruu bin Al-'Aas (Radhiya Allaahu ‘Anhuma) amesema: Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Fikisheni kutoka kwangu japo Aayah (moja), na hadithieni habari za Bani Israaiyl wala hakuna kosa, na yeyote atakayenizulia uongo moja kwa moja, basi ajitayarishie makaazi yake ndani ya moto.)) [Imepokelewa na Al-Bukhaariy]
Hichi ni kibarua kikubwa kwa waandishi wa Kiislamu, kwani Ulimwengu wa Hadiyth umejaa simulizi za uongo chungu nzima. Hata hivyo, tunarudia kusema kwamba mwenye kutafuta elimu Allaah Humfanyia wepesi mambo yake.
Ni mengi ambayo tunayasikia na kuyasoma kutoka vyanzo mbalimbali. Uislamu kwa upande wake umehimiza Muislamu kusoma na kusomesha. Kuifikisha elimu kwa wengine ndio jamii inapotengenea. Elimu hii ifikishwe bila ya kujali huyo unayemfikishia iwapo anaelewa au laa:
Kutoka kwa Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema: Nimemsikia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
((Mwenyezi Mungu Amemtakia khayr aliyesikia maneno kutoka kwetu, basi akayafikisha kama alivyoyasikia, pengine aliyefikishiwa ni mjuzi kuliko aliyefikisha.)) [Imepokewa na at-Tirmidhiy]
Ndio maana waandishi kadhaa wanahitaji mawazo ya wengine. Kwa sababu huenda huyo anayefikishiwa elimu ni mjuzi zaidi kuliko mfikishaji. Na tunasema kwamba, muongozo uliomo ndani ya kitabu hichi cha Mwenendo wa Kesi Baina ya Shari’ah (za Allaah) Na sheria (za mwanaadam) si jambo geni wala sio jipya. Wapo wajuzi zaidi wa kuandikia maelezo haya kwani wao ni wenye elimu zaidi. Tunachokifanya ni kufikisha kwa jamii ili upatikane ufahamu kwa wepesi huku tukipatiwa fafanuzi za makosa yetu. Kwani kila binaadamu ni mwenye kukosea.
Ufikishaji huu kama tulivyosema awali, ni mzigo kwa aliyepatiwa elimu. Kwani kuna adhabu kubwa mbele ya Allaah kwa anayeficha elimu sahihi. Adhabu ambayo ni ya kurajmiwa kama anavyofanyiwa punda au farasi au ngo'mbe kwa kuingiziwa kamba puani aendeshwe kwa namna bwana anavyotaka. Ni udhalilifu wa aina gani huu kwa mwenye kuficha elimu?
Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Mwenye kuulizwa juu ya elimu akaificha, atafungwa mdomo na kifungo cha moto siku ya Qiyaamah.)) [Imesimuliwa na Abu Hurayrah; Imepokewa na Ahmad na at-Tirmidhiy]
Tuweke akili sawa kwamba kutafuta elimu kwa kupata cheo hapa duniani sio sahihi kabisa. Tusome elimu kwa ajili ya kupata radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Kwani hapo tutapata yote – dunia na Akhera.
Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Mwenye kujifunza elimu (isiyokuwa) ya kutafuta fadhila za Allaah 'Azza wa Jalla, hajifunzi isipokuwa kupata cheo ndani ya dunia, hatoipata (hata) harufu ya Pepo siku Qiyaamah.)) [Imesimuliwa na Abu Hurayrah; Imepokewa na Abu Daawuud]
Muislamu wa kweli hatosheki katika kufanya khayr, na hakuna fadhila kubwa kama za kuitafuta elimu pamoja na kuisomesha.
Kutoka kwa Abu Sa'iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema: Amesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Hatosheki Muumini katika (kutenda) khayr mpaka atakapomalizia Peponi.)) [Imepokewa na at-Tirmidhiy]
Na hivyo tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ajaalie kazi hizi za kuifikishia jamii elimu sahihi ni yenye manufaa. Manufaa ambayo yatajaalia kuzaa matunda hapa duniani pamoja na hapo tutakapokuwa katika maisha ya barzakh (kaburini). Hii ni kwa uthibitisho wa Hadiyth aliyonukuliwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
((Atakapokufa mwanaadamu hukatika amali zake isipokuwa mambo matatu: swadaqah yenye kuendelea, au elimu yenye kumnufaisha, au mtoto mwema anayemuombea.)) [Imesimuliwa na Abu Hurayrah; Imepokelewa na Muslim]
Kwa upande wa Tawhiyd tunaelezwa kwamba Shahadah ya Mwenyezi Mungu Ndiye Anayestahiki kuabudiwa na kwamba Muhammad ndiye Mjumbe Wake wa mwisho inafanyiwa kazi kwa kufuata Shari’ah ya Kiislamu. Hata kwa wasiokuwa Waislamu walio chini ya himaya ya Taifa la Kiislamu (dhimmi) wanawajibika kufuata Shari'ah hizi:
Imesimuliwa na Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma): Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Nimeamrishwa (na Allaah) kupigana dhidi ya watu hadi waape kwamba hakuna mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mjumbe Wake, na kusimamisha Swalah na kutoa Zakaah, hivyo wakiyatekeleza hayo, basi maisha yao na mali zao zinahifadhiwa kutokana na mimi isipokuwa kwa Shari’ah za Kiislamu na hisabu yao itafanywa na Allaah.)) [Al-Bukhaariy]
Shari’ah hizo ni lazima zitokane na Qur-aan pamoja na Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwani Shari’ah yoyote isiyotokana na Muumba basi hiyo haifai kufuatwa na yaeleweka kuwa ni baatwil kwani itakuwa inaenda kinyume na maumbile (fitrah) ya mwanaadamu.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Yeyote anayeweka masharti (Shari’ah) ambayo hayamo ndani ya Kitabu cha Allaah, masharti yake yatakuwa si sahihi hata kama atayalazimisha mara mia moja.)) [Imesimuliwa na mama wa Waumini 'Aaishah; Imepokewa na Al-Bukhaariy]
Na kutoa hukumu kwa mujibu wa Shari’ah za Allaah ndio mwenendo unaotakiwa kufuatwa na kuhimizwa kutekelezwa. Kisa hichi ni vyema tukakinukuu ili kufahamu ni namna gani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa makini kabisa katika kusimamisha hukumu za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
Imesimuliwa na Abu Hurayrah na Zayd bin Khaalid al-Juhaani: Bedui mmoja alikuja na kusema: "Ewe Mjumbe wa Allaah! Hukumu baina yetu kwa mujibu wa Shari’ah za Allaah." Mpinzani wake akasimama na kusema: "Yupo sahihi. Hukumu baina yetu kwa mujibu wa Shari’ah za Allaah.' Bedui akasema: "Mwanangu wa kiume alikuwa ni mfanyakazi akifanya kazi kwa bwana huyu, na akatenda kitendo cha ndoa kisicho halali na mkewe. Watu wameniambia kwamba mwanangu apigwe mawe hadi kifo; hivyo kwa uzito wa hilo, nikalipa fidia ya mbuzi mia moja na mtumwa wa kike ili kumuokoa mwanangu. Kisha nikawauliza wanazuoni ambao walisema: "Mwanao apigwe mijeledi mia moja na atengwe kwa mwaka mmoja." Mtume akasema:
((Hapana shaka nitahukumu baina yenu kwa mujibu wa Shari’ah za Allaah. Huyo mtumwa wa kike na mbuzi mia moja warudi kwako, na mwanao atastahiki mijeledi mia moja na mwaka mmoja wa kutengwa.)) Baadaye akamuamrisha mtu:
((Ewe Unays! Nenda kwa mke wa huyu (mtu) na mpige mawe hadi afariki.)) Hivyo, Unays akaenda na kumpiga mawe hadi kufa. [Al-Bukhaariy]
Kufuata Shari’ah sio tu kazi ya Hakimu, bali hata kwa mashahidi na wenye kupeleka kesi zao wanawajibika kuwa makini katika kufuata mwenendo sahihi utakaopelekea hukumu ya haki na uadilifu kutolewa. Mwenendo huu ni pamoja na kufuata maelekezo ya Mahkama iliyo 'aadil pamoja na kujiweka mbali na vitendo vya dhulma kama vile utapeli, wizi na rushwa.
Juu ya migogoro na migongano yote inayotokezea baina ya watu, la muhimu ni kukumbuka kwamba Muumba wetu ni Ghafuurun Rahiym (Mwenye Kuswamehe na Mwenye Huruma). Kama Yeye Mola wetu yupo tayari kutupokelea dhambi zetu hata ziwe na ukubwa wa mbingu na ardhi, kwanini basi wanaadamu wanashindwa kuwa wasemehevu baina yao? Ni vyema tukajifunza kutokana na kisa kifuatacho:
Binti wa An-Nadr alivunja jino la mtoto wa kike, jamaa wa Ar-Rabi’ wakaomba jamaa wa mtoto wa kike kukubali Irsh (fidia kutokana na maumivu) na kumsamehe (mtenda kosa), lakini wakakataa. Hivyo, walikwenda kwa Mtume aliyeamrisha kufanya kisasi. Anas bin An-Nadr akauliza: "Ewe Mjumbe wa Allaah! Je jino la Ar-Rabi’ litavunjika?" "Hapana kwa Yule Aliyekuleta wewe pamoja na Ukweli, jino lake halitavunjika." Mtume akasema:
((Ewe Anas! Shari’ah ya Allaah inaamrisha kisasi)) Baadaye jamaa za mtoto wa kike wakakubali na kumsamehe. Mtume akasema:
((Kuna baadhi ya watumwa wa Allaah, ambao wakila kiapo kwa jina la Allaah, kinajibiwa na Allaah, (yaani kiapo chao kinatimizwa)) Anas akaongeza: "Watu wameelewana na kukubali Irsh." [Imesimuliwa na Anas; Imepokelewa na Al-Bukhaariy]
Bahati mbaya ndani ya jamii za Waislamu, utakuta migogoro isiyo na kichwa wala miguu. Waislamu wanafika kupelekeshana Mahakamani kwa sababu ya nazi zenye kuhesabika na kugombania ulezi wa mtoto wa mwaka mmoja? La hawla walaa quwwata illa bi Llaah! Hii ni aibu na fedheha kubwa. Waislamu wanatakiwa kuwa ni mfano kwa wasio Waislamu kwa kuwa na moyo wa kusamehe na huruma. Njia hii itarahisisha kutatua migogoro pamoja na kupunguza magonjwa yanayotokana na kuweka kitu moyoni sana kama presha au magonywa ya moyo.