Zingatio: Qur-aan Na Sunnah Hazina Mpinzani

 

Zingatio: Qur-aan Na Sunnah Hazina Mpinzani

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Allaah Ameutofautisha Ummah wetu kwa kuihifadhisha Qur-aan na kuifahamisha. Mataifa kabla yetu walikuwa wakisoma vitabu vyao bila ya kuweza kuisoma kwa moyo. Hivyo, alipokuja 'Uzayr na kuisoma Taurati kwa moyo walisema: "Huyu ni mtoto wa Allaah".

 

Hakika hayo ni maneno matamu na yenye maana aliyoyasema Imaam Ibn Al-Jawziy pale alipojadili namna Ummah huu ulivyotofautishwa na Ummah kabla yetu: Kwa kuwa na Qur-aan.

 

Ni namna gani sisi Waislamu, tunaweza kumshukuru Muumba wetu kwa watoto wa miaka saba kuweza kuisoma Qur-aan kwa moyo?!

 

Basi, hakika hakuna taifa, zaidi yetu sisi, waliokusanya simulizi za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wao kwa matendo na maneno kwenye namna ambayo inaeleweka na yenye kuaminika. Hadiyth zimefikishwa kwetu kutoka vizazi vilivyopita, na wao walipokea kutoka kwa wazee wao.

 

Ni mfumo ambao ulirithishwa kizazi baada ya kizazi kwa uangalifu wa hali ya juu, na ndio tunaona msururu wa wasimulizi hadi kumrudia Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mataifa yote hapo kabla walikuwa wakieleza kutoka vitabuni mwao, hali ya kuwa hawajui nani aliyeandika au aliyesimulia.

 

Tuna haja ya kuilinda zawadi hii, na kuihifadhi kwa kuisoma ili kwamba iendelee kubaki salama. Wamekuwepo watu wengi kabla yetu waliohifadhi elimu nyingi sana, baadaye elimu yao ikarithiwa na watu ambao hawakuifanyia mapitio kwa sababu ya uvivu wao. Hivyo, pale mtu alipotaka kunukuu kitu, alishindwa kufanya hivyo.

 

Huko enzi za kale, elimu ilikusanywa kwa heshima kutoka kwa wanachuoni, kwa njia ya simulizi na kwa kuinamisha magoti mbele ya wanachuoni. Hata hivyo, leo elimu inachukuliwa kutoka vitabuni, magazetini, mtandaoni na hata kwenye simu. Hivyo elimu imedhoofika, pia umakini na ufahamu umeanguka. Makosa mengi na kasoro nyingi zinajitokeza.

 

Na tunaona sasa, wametokezea watu wasioweza kutofautisha kondoo na ngamia, au baina ya ngano na mbegu za maua. Hawa ndio wametambulika kwa dunia ya leo kuwa ni Imamu na wanachuoni, wenye kufikia kusema: "Wao ni watu na sisi ni watu."

 

Hakuna shaka yoyote kwamba, kuna haja ya Waislamu kukaa kitako na kutafakari urithi wa elimu yao iliyo bora. Na njia iliyo bora ni kuendelea kuisoma kwa ikhlaasw (kwa kutegemea radhi za Allaah) kutoka kwa wanachuoni wenye ucha wa Allaah.

 

 

Share