04-Jihaad: Fadhila Na Thamani Ya Jihaad
Fadhila Za Jihaad
Ibada Bora
Fadhila zinazopatikana katika Kupigana Jihaad isiyokuwa ya waajib kwa ajili ya kulinyanyua neno la Allaah na kuimakinisha hidaaya Yake juu ya ardhi, na kwa ajili ya kuimakinisha dini ya haki ni nyingi kupita fadhila zinazopatikana katika kuhiji Hija ya nyongeza baada ya mtu kuhiji Hija yake ya lazima, au ‘Umrah ya nyongeza, au Swalah za Sunnah au Swawm ya Sunnah.
Juu ya yote hayo, Jihaad imekusanya kila aina ya ibada za kiroho na kiwiliwili, kuikinai dunia, kuihama nchi na kuyahama matamanio na hii ndiyo maana ikapewa jina la ‘Uchaji Allaah’, kwani imekuja katika Hadiyth kuwa:
‘Ucha Mungu wa umma wangu ni Jihaad katika njia ya Allaah.”
Na ndani yake mna kuitakasa nafsi, kuitakasa mali, na kumuuzia Allaah nafsi, na haya yote ni matunda ya mapenzi na imani na yakini na kuelekea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).
Allaah Anasema:
إِنَّ اللّهَ اشْتَرَى مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُم بِأَنَّ لَهُمُ الجَنَّةَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللّهِ فَيَقْتُلُونَ وَيُقْتَلُونَ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا فِي التَّوْرَاةِ وَالإِنجِيلِ وَالْقُرْآنِ وَمَنْ أَوْفَى بِعَهْدِهِ مِنَ اللّهِ فَاسْتَبْشِرُواْ بِبَيْعِكُمُ الَّذِي بَايَعْتُم بِهِ وَذَلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ
“Hakika Allaah Amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwa kuwa wao watapata Pepo. Wanapigana katika Njia ya Allaah - wanaua na wanauawa. Hii ni ahadi Aliyojilazimisha kwa Haki katika Taurati na Injili na Qur-aan. Na nani atimizae ahadi kuliko Allaah? Basi furahini kwa biashara yenu mliyo fanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.”
At-Tawbah: 111
Dini ya Kiislamu imeitukuza ibada hii ya Jihaad, na ikatunabahisha juu umuhimu wake katika sura nyingi zilizoteremshwa Madina na ikawalaumu wanaoiacha na wanaoipinga na kuwapa sifa za unafiki na wenye maradhi moyoni.
Watu Bora
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Nikujulisheni juu ya aliye bora kupita wote? Mtu aliyeshika hatamu za farasi wake (akimuelekeza) katika njia ya Allaah (kupigana Jihaad). Nikujulisheni juu ya anayefuatia? Mtu aliyejitenga akiwa na mbuzi wake akitoa haki ya Allaah katika mbuzi hao. Nikujulisheni juu ya mtu muovu kupita wote? Mtu anayeombwa kwa jina la Allaah kisha hatoi (juu ya kuwa anao uwezo).”
Alipoulizwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): ‘Mtu yupi aliye bora?’
Akajibu: “Muislamu anayepigana Jihaad katika njia ya Allaah kwa nafsi yake na mali yake.”
Wakamuuliza: “Kisha yupi?”
Akasema: “Muislamu katika bonde mojawapo akimcha Allaah na anawaepusha watu na shari yake.”
Pepo Kwa Ajili Ya Mujaahidiyn
AmeHadiytha At-Tirmidhiy kuwa mtu mmoja alitamani ajitenge (awe mbali na watu huku akifanya shughuli za ibada peke yake), akamuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) juu ya jambo hilo, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:
“Usifanye hivyo, kwa sababu mmoja wenu anaposimama (tu) katika njia ya Allaah (wakati wowote anapokuwa katika Jihaad), ni bora kuliko akisali nyumbani kwake muda wa miaka sabini. Hampendi nyinyi Allaah akughufirieni kisha akuingizeni Peponi? Piganeni katika njia ya Allaah. Atakayepigana katika njia ya Allaah (muda wa) kiasi cha kumkamua ngamia maziwa tu, imemwajibikia Pepo.”
At-Tirmidhy
Daraja Mia Peponi
Kutoka kwa Abu Sa’iyd al-Khudry (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Ewe Abu Sa’iyd! Atakayeridhika kuwa Mola wake ni Allaah, na Islamu dini yake, na Muhammad Mtume wake, amewajibika kuingia Peponi.”
Abu Said akastaajabu kwa maneno hayo akasema:
“Yarudie tena (maneno hayo) kwa ajili yangu ewe Mtume wa Allaah.”
Kisha (Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)) akasema:
“Na mengine anamnyanyua kwayo mja wake daraja mia, na baina ya kila daraja mbili (umbali wake) sawa na umbali wa mbingu na ardhi.”
Akauliza;
“Nini hicho ewe Mtume wa Allaah?”
Akasema:
“Ni Jihaad katika njia ya Allaah, ni Jihaad katika njia ya Allaah.”
Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Hakika huko Peponi zipo daraja mia, Allaah amewatayarishia wapiganao Jihaad katika njia ya Allaah, na baina ya kila daraja mbili umbali wake sawa na umbali wa mbingu na ardhi. Na mnapomuomba Allaah, muombeni (Pepo ya) Al Firdaus, kwani hiyo ipo kati kati ya Pepo, sehemu ya juu ya Pepo, na juu yake ipo Arshi ya Al Rahman, na kutoka hapo inapasuka (inaanzia) mito ya Peponi.”
Thamani ya Jihaad
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:
“Aliulizwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
“Kipi chenye thamani kupita Jihaad katika njia ya Allaah?”
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
“Hamukiwezi.”
Akaulizwa suali hilo mara mbili au tatu na kila anapoulizwa alikuwa akijibu;
“Hamukiwezi.”
Mara ya tatu akasema:
“Mfano wa anayepigana Jihaad katika njia ya Allaah ni mfano wa aliyefunga (aliyebaki akiwa amefunga), (na) akasali nyakati za usiku huku akiomba na kusoma aya za Allaah bila kuchoka katika Sala yake wala kuacha kufunga mpaka atakaporudi yule aliyekwenda kupigana Jihaad katika njia ya Mwenyezi.”
Maimamu watano
Kufa Shahiyd
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Hajeruhiwi mtu (anapopigana Jihaad) katika njia ya Allaah, na Allaah anamuelewa kila anayejeruhiwa katika njia ya Allaah, isipokuwa atakuja siku ya kiama huku jeraha lake likiwa linamwaga damu, na rangi ni rangi ya damu lakini harufu ni harufu ya miski.”
Amesema Muhammad bin Ibraahiym katika Hadiyth ndefu yenye shairi refu ndani yake kuwa:
“Kisha nikakutana na al-Fudhayl bin ‘Iyaadh akanambia:
“Wewe ni katika wanaoandika Hadiyth?”
Nikamwambia; “Ndiyo’.
Akaniambia; “Basi iandike Hadiyth hii (kama) ujira wako kwa kutuletea kitabu cha Abi Abdir-Rahmaan. Kisha al-Fudhayl bin ‘Iyaadh akaanza kunihadithia yafuatayo:
“Amenihadiithia Mansuur bin Al-Muatamir, kutoka kwa Abu Swaalih, kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa mtu mmoja alimwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam); “Ewe Mtume wa Allaah nifundishe jambo nitakalopata ndani yake thawabu ya mpigana Jihaad katika njia ya Allaah.”
Akasema:
“Unaweza uwe unaswali (moja kwa moja) bila kuchoka, na ufunge (moja kwa moja) bila kula chakula?”
Akasema:
“Ewe Mtume wa Allaah mimi ni dhaifu nisiyeweza kufanya yote hayo.”
Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:
“Basi naapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, lau kama utafanya yote hayo basi (bado) hutouifikia (daraja) ya mpigana Jihaad katika njia ya Allaah.
Hujaelewa bado kuwa Mpigana Jihaad anapokuwa juu ya farasi (akiwa amekaa tu juu yake) huku amezishika hatamu anaandikiwa thawabu?.”
Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliwahi kuwaambia Maswahaba wake:
“Walipofariki ndugu zenu katika vita vya Uhud, Allaah alizijaalia roho zao ndani ya mwili (mfano) wa ndege wa kijani wanaiendea mito ya Peponi na wanakula katika matunda yake na wanakaa katika tundu za dhahabu zilizotundikwa katika kivuli cha Arshi. Walipoona ladha nzuri ya vyakula vyao na vinywaji vyao na makazi yao wakasema:
“Nani atakayewajulisha ndugu zetu (waliopo duniani) juu yetu kuwa tuko hai Peponi tunaruzukiwa, ili wasije kufanya ulegevu katika Jihaad?”
Allaah Akasema:
“Mimi nitawajulisha juu yenu.”
Ndipo Alipoteremsha kauli Yake:
وَلاَ تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُواْ فِي سَبِيلِ اللّهِ أَمْوَاتًا بَلْ أَحْيَاء عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ . فَرِحِينَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ وَيَسْتَبْشِرُونَ بِالَّذِينَ لَمْ يَلْحَقُواْ بِهِم مِّنْ خَلْفِهِمْ أَلاَّ خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلاَ هُمْ يَحْزَنُونَ 0 يَسْتَبْشِرُونَ بِنِعْمَةٍ مِّنَ اللّهِ وَفَضْلٍ وَأَنَّ اللّهَ لاَ يُضِيعُ أَجْرَ الْمُؤْمِنِينَ
“Wala kabisa usiwadhanie waliouliwa katika Njia ya Allaah kuwa ni maiti. Bali hao ni wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi.
Wanafurahia aliyo wapa Allaah kwa fadhila Yake, na wanawashangilia wale ambao bado hawajajiunga nao, walio nyuma yao, ya kwamba haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.
Wanashangilia neema na fadhila za Allaah, na ya kwamba Allaah Hapotezi ujira wa Waumini.”
Aal-‘Imraan: 169-171
Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Roho za mashahidi zimo ndani ya miili (mfano wa miili) ya ndege (yenye rangi ya) kijani, wanatembezwa (wanaingia na kutoka) Peponi wanavyotaka.”
Na akasema:
“Shahidi hahisi maumivu ya kuuliwa ila kama mmoja wenu anavyohisi maumivu ya kufinywa.”
Na akasema:
“Jihaad iliyo bora, ajeruhiwe farasi wako na imwagike damu yako.”
Kutoka kwa Jaabir bin ‘Aatiq kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Mashahidi ni (aina) saba gheri ya aliyeuliwa katika njia ya Allaah:
Aliyekufa kwa maradhi ya tauni ni shahidi, aliyezama (aliyekufa kwa kuzama) shahidi, mwenye maradhi yanayosibu sehemu za mbavu ni shahidi (aliyekufa kwa maradhi hayo), aliyekufa kwa maradhi ya tumbo ni shahidi, aliyekufa kwa kuungua - shahidi, aliyekufa kwa kuangukiwa na nyumba - shahidi, na mwanamke aliyekufa katika uzazi - shahidi.”
Ahmad – Abu Daawuud – An-Nasaaiy kwa isnadi iliyo sahihi
Na kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Wepi mnaowahesabu kuwa ni mashahidi miongoni mwenu?”
Wakasema:
“Ewe Mtume wa Allaah, aliyeuliwa katika njia ya Allaah ni shahidi.”
Akasema:
“Basi mashahidi katika umati wangu watakuwa wachache.”
Wakasema:
“Wepi hao basi ewe Mtume wa Allaah?”
Akasema:
“Atakayeuliwa katika njia ya Allaah ni shahidi, na atakayekufa katika njia ya Allaah ni shahidi (yaani akiwa katika kumtii Allaah), na atakayekufa kwa maradhi ya tauni ni shahidi, na atakayekufa kwa maradhi ya tumbo ni shahidi na aliyezama ni shahidi.”
Muslim
Na kutoka kwa Sa’iyd bin Zayd kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Atakayeuliwa kwa ajili ya (kuihami) mali yake ni shahidi, na atakayeuliwa kwa ajili ya (kuipigania) dini yake ni shahidi, na atakayeuliwa kwa ajili ya (kuwahami) watu wake ni shahidi.”
Ahmad na At-Tirmidhiy na akaisahihisha.
Wanasema wanavyouni kuwa watu wote hawa wanahesabiwa kuwa ni mashahidi juu ya kuwa hawakufa katika vita vya Jihaad ya kuipigania dini ya Allaah na kuwa siku ya Akhera watapata thawabu sawa na waliokufa katika Jihaad, isipokuwa hapa duniani wataoshwa na kusaliwa (kama maiti wa kawaida).
Kulinyanyua Neno La Allaah
Anayepigana Jihaad ya kweli ni yule ambaye nia yake ni kulinyanyua neno la Allaah na kuinyanyua bendera ya Haki na kuiondoa batili na kujitolea mhanga nafsi yake kwa ajili ya kutaka radhi za Allaah.
Ama ikiwa nia ya kupigana Jihaad ni nyingine katika mambo ya kidunia tofauti na hayo yaliyotajwa, basi hiyo haiwezi kupewa jina la Jihaad.
Kwa hivyo atakayepigana kwa ajili ya kupata cheo, au kwa ajili ya ngawira, au apate kuonekana ushujaa wake, au kwa ajili ya kujulikana, basi huyo hana chake katika ujira wowote utokao kwa Allaah na wala hatopata thawabu.
Kutoka kwa Abu Musa (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:
“Alikuja mtu kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema (akauliza):
“Mtu anapigana kwa ajili ya kujipatia ngawira (mali inayotekwa katika vita), na mwengine apate kusifiwa, na mwengine apate kuonesha ushujaa wake, yupi kati yao (anahesabiwa kuwa) yupo katika njia ya Allaah?”
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
“Atakayepigana ili neno la Allaah liwe juu, huyo yupo katika njia ya Allaah.”
Imesimuiwa na Abu Daawuud na An-Nasaaiy kuwa mtu mmoja alisema:
“Ewe Mtume wa Allaah, unaonaje mtu anayepigana kwa ajili ya kutaka ujira na umaarufu, anapata nini?”
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
“Hapati chochote.”
Akauliza suali hilo mara ya tatu ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipomwambia:
“Hapati chochote. Hakika Allaah haikubali amali (matendo) yoyote ikiwa haikuwa halisi kwa ajili ya kutaka radhi Zake.”
Nia ni uhai wa ‘amali yoyote ile, na chochote kinachotendwa bila ya nia basi amali hiyo inakuwa amali isiyo na uhai wala uzito wowote mbele ya Allaah.
Amesimulia Al-Bukhaariy kutoka kwa Abullaahi bin ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Hakika ‘amali zote (huhesabiwa kutokana) na nia, na hakika ana kila mja (malipo) ya aliyoyanuwia.”
Nia ndiyo yeye kunyanyua daraja ya matendo, kwani mtu anaweza kuifikia daraja ya waliokufa shahidi hata kama hakufa vitani.
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Atakayemuomba Allaah kwa nia ya kweli afe shahidi, Allaah Atamfikisha katika daraja za waliokufa shahidi hata kama atakufa kitandani pake.”
Na akasema:
“Hakika katika mji wa Madina kuna makundi ya watu ambao hamkwenda mwendo (yaani vitani), na hamkuyakata mabonde isipokuwa walikuwa mabondeni (sawa kama nyinyi), yamewazuia maradhi.”
Ama ikiwa nia ya kupigana Jihaad si kwa ajili ya kutaka radhi za Allaah, bali kwa ajili ya kutafuta manufaa ya kidunia, basi si kama mtu huyo atakosa thawabu tu, bali atakuwa amejitafutia adhabu siku ya Kiama.
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:
“Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:
“Wa mwanzo kuhesabiwa siku ya Kiama ni mtu aliyekufa shahidi katika vita, ataletwa na kujulishwa neema alizoneemeshwa na baada ya kuzijuwa ataulizwa:
“Umezifanyia kazi gani neema hizi?”
Atasema:
“Nimepigana Jihaad kwa ajili yako mpaka nikafa shahidi.”
Ataambiwa:
“Umesema uongo, bali ulipigana ili pasemwe kuwa wewe ni mjasiri na pashasemwa.”
Kisha pataamrishwa abururwe kwa uso wake na kuingizwa motoni.
Na mtu (mwengine) aliyejifundisha elimu akaijuwa (vizuri), akasoma na Qur-aan, (mtu huyo) ataletwa na kujulishwa neema alizoneemeshwa, kisha ataulizwa;
“Umezifanyia kazi gani neema hizi?”
Atasema:
“Nimejifunza elimu nikafundisha na kwa ajili yako nikasoma Qur-aan.”
Ataambiwa:
“Umesema uongo, bali ulijifunza elimu ili pasemwe kuwa wewe ni aalim. Ukasoma Qur-aan ili pasemwe kuwa wewe ni msomaji mzuri, na pashasemwa.”
Kisha pataamrishwa abururwe kwa uso wake na kuingizwa motoni.
Na mtu (mwengine) Allaah Amempa wasaa, akampa kila aina ya mali, ataletwa na kujulishwa juu ya neema alizoneemeshwa, kisha ataulizwa:
“Umezifanyia kazi gani neema hizi?”
Atasema:
“Sijaacha njia unayopenda mtu atoe katika mali yake ila mimi nimetoa kwa ajili yako.”
Ataambiwa:
“Umesema uongo, bali umetoa ili pasemwe kuwa wewe ni mkarimu na pashasemwa. Kisha pataamrishwa abururwe kwa uso wake na kuingizwa motoni”.
Fadhila Za Kulinda Mipaka
Kwa kawaida panakuwa na upenyo katika mipaka baina ya ardhi ya Waislamu na ya makafiri, upenyo ambao adui anaweza kuutumia kwa ajili ya kujipenyeza na kuingia ndani ya ardhi ya Waislamu. Kwa hivyo ni wajibu kwa Waislamu kuzilinda vizuri sehemu hizo ili adui asiwezi kuzitumia na kuwashambulia kwa urahisi.
Uislamu umetilia mkazo sana kuzilinda sehemu hizo na pia umetilia mkazo kuwatayarisha Waislamu ili wawe wapiganaji hodari, na kwa ajili hiyo kazi hii ya kulinda kwa ajili ya kupigana Jihaad katika njia ya Allaah ikapewa jina la (Al Ribaat), na uchache wake ni muda wa saa moja na ukamilifu wake ni siku arubaini, na fadhila nyingi sana zinapatikana katika kuzilinda sehemu zenye hatari zaidi.
Maulamaa wamekubaliana kuwa fadhila zake ni nyingi kupita fadhila za kuswali Msikiti wa Makkah.
Hadiyth zifuatazo zinatujulisha juu ya fadhila za jukumu hili:
Kutoka kwa Salmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa alimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:
“Ribaat ya siku moja na usiku wake ni bora kuliko kufunga mwezi mzima na kusali usiku wake, na mtu akifa (akiwa katika jukumu hilo), amali zake zitaendelea kuandikwa na riziki yake ataendela kupata na atasalimika na fitna (za kaburi).”
Muslim
Na akasema:
“Kila maiti amali zake zinakatika ila aliyekufa akiwa analinda mipaka ili adui asiweze kuingia katika nchi ya Kiislamu (Muraabitan), kwa hakika huyu amali zake zinaendelea kuandikwa mpaka siku ya Kiama, na anaepushwa na mitihani ya kaburi.”
Fadhila Za Kurusha 'Ar-Ramyi'
Uislamu umetilia mkazo kujifunza kurusha (mkuki, mshale, kupiga risasi, mabomu nk.), na pia kujifunza fani mbali mbali za kupigana kwa nia ya Jihaad katika njia ya Allaah, na ukapendekeza pia kufanya mazoezi ya viungo na ya kutumia silaha kwa nia hiyo hiyo.
Kutoka kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:
“Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akiwa juu ya mimbari akisema:
وَأَعِدُّواْ لَهُم مَّا اسْتَطَعْتُم مِّن قُوَّةٍ
“Basi waandalieni (wawekeeni tayari) nguvu mnazoweza (silaha).” At-Tawbah: 60
‘Hakika nguvu ya kweli ni kurusha, hakika nguvu ya kweli ni kurusha, hakika nguvu ya kweli ni kurusha.”
Muslim
Na kutoka kwa ‘Uqbah (Radhiya Allaahu ‘anhu) pia alisema:
“Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:
“Mtawezeshwa kuziteka nchi nyingi, mmoja wenu asishindwe kuutumuia mshale wake (asijifunze kuutumia kwa ajili ya mchezo tu – bali kwa ajili ya kupigana Jihaad). Hakika Allaah huwaingiza Peponi watu watatu kwa mshale mmoja - aliyeutengeneza (kwa nia ya Jihaad), anayempa (anayekaa nyuma yake au pamoja naye na kumpa pale mishale inapomalizika), na mrushaji katika njia ya Allaah.”
Uislamu umeshadidia sana katika kuchukizwa na mtu anayejifunza kutumia upinde au silaha yoyote kisha akasahau namna ya kuitumia silaha hiyo bila udhuru unaokubalika kishari’ah.
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Atakayejifunza kutupa, kisha akasahau hayupo pamoja nasi.”
Na akasema:
“Mchezo wowote anaocheza mtu ni batil (yaani hapati thawabu ndani yake), isipokuwa (mchezo wa) upinde (na mshale), na kumzowesha farasi wake (pamoja na kumfundisha), na kucheza na watu wa nyumba yake (kwa kuzungumza na mkewe na kutaniana naye), hayo ni katika mambo ya haki (anayopata thawabu ndani yake).”
Anasema Al-Qurtubiy:
“Maana ya Hadiyth hii na Allaah ndiye ajuwae zaidi, ni kuwa; Kila mchezo unaopoteza wakati wa mtu usio na faida, hauna thawabu yoyote ndani yake, na kuachana nao ni bora zaidi, isipokuwa mambo matatu haya, juu ya kuwa ni mchezo, lakini yanampatia mtu thawabu kwa sababu ya faida inayopatikana ndani yake. Kwa sababu katika kutumia upinde na mshale na kumfundisha farasi mbinu mbali mbali za kivita, na mtu kuzungumza na kutaniana na mkewe kunaweza kumfanya awe mcha Mungu wa kweli. Na kwa ajili hii mambo matatu haya yakawa yanaweza kumpatia mtu thawabu.”
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema:
“Enyi wana wa Isma’iyl! rusheni (mishale) kwani baba yenu alikuwa mrushaji.”
Na kujifunza kupanda farasi na kutumia silaha ni katika fardhi kifaya inayoweza kuwa fardhi 'ayn.