Zingatio: Kama Wewe Humuoni Yeye Anakuona
Zingatio: Kama Wewe Humuoni Yeye Anakuona
Naaswir Haamid
Iwapo unatambua nguzo tano za Kiislamu, nguzo sita za Imani, basi elewa fika kwamba kuna nguzo moja ya Ihsani anayotakiwa Muislamu kuifanyia kazi.
Katika Hadiyth maarufu ya Jibriyl (‘Alayhis-salaam) iliyosimuliwa na Sayyidna 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) na kupokelewa na Muslim, tunaelezwa kwamba Ihsani ni kumuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kana kwamba unamuona, na ikiwa wewe humuoni, basi Yeye Anakuona.
Muumba wetu Ndie Ajuaye yanayopita ndani ya nyoyo zetu na kila tendo tunalolifanya. Wala hahitajii msaada wa binadamu, majini wala malaika kuyafanya Ayatakayo. Kauli Yake ni kusema: 'Kuwa' na jambo hilo likawa bila ya kikwazo chochote. Iwapo yupo mwenye cheo, mali, elimu na uwezo basi Ashindane na Muumba wake kwa kukimbia kuhifadhiwa vitimbi vyake, na kama hawezi basi ajisalimishe mbele Yake kabla ya makubwa kumfikia.
Rabb wetu Hatutakii mabaya wala madhara, Ameiumba dunia na kila vilivyomo ndani yake kwa kuridhisha maumbile ya mwanaadamu, naye Akamfanya kuwa ni kiongozi wa ulimwengu huu. Akiuzunguka na kuufanya atakavyo. Basi kuwa ni mwenye kushukuru kwa neema hii. Kwani bila ya hivyo, hata ngo'mbe ungelishindwa kumchinja, kwani naye angelitaka kutoa amri zake za kukaidi kuchinjwa. Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amemfanya dhalili mbele ya wanaadamu.
Katika visimamo vyetu vya Swalaah na utelekezaji wa ibada zetu zote, tuelewe kwamba tunatizamwa matendo yetu na ipo siku tutakuja kulipwa. Hivyo, hatuna budi kuwa na unyenyekevu, utulivu na upole mbele ya Swalaah. Kwani hapo ndipo mwanaadamu anapowasiliana na Muumba wake moja kwa moja bila ya kizuizi chochote.
Kukithiri kwa madhambi kutoka kwa viumbe inatokana na kutojali kwamba Yupo Rabb Ambaye Anayaona matendo yote. Liwe kubwa mfano wa ulimwengu hata dogo mfano wa mdudu chungu yote yanawekwa kumbukumbu. Iwapo Muislamu amechukua haki ya mwenziwe kwa njia ya utapeli, wizi, hadaa au nyenginezo zisizokuwa halali, basi aelewe kwamba hiyo ni haki iliyochungwa na isiporejeshwa atakwenda kuilipa mbele ya Hisabu.
Nao wapo dada zetu wenye kuweka kijihijabu katika mabega tu, lakini ni ajabu pale wanapopita mbele za wanaowaheshimu au hata mbele ya Misikiti huurudisha mbio kwenye kichwa kuficha nywele zao. Wengine wanaposikia adhana mikono yao hupapara kila kona ya mtandio huo ili kusitiri viji nywele vyake. Sasa huu mtandio uliuchukua kwa lengo gani? Hii yote ni ushahidi wa kukosa (au kudharau) mafunzo sahihi na kwamba Muislamu huyo haamini kwamba Muumba wake Anamuona.
Waswahili wanatuambia: Ndege mjanja hunasa kwenye tundu bovu. Hivyo, hao wanaoweka vijishungi kwenye mabega na waovu wa madhambi mengine wanaofanana nao, wanakuja kuadhirika mbele za kadamnasi za watu. Na wala hakuna ujanja wa kujidai mwanaadamu kwamba hataenda kulipwa siku ya Hesabu. Kwani mwisho wake atarudi tu mbele ya Muumba.
Wenye kuamini na kuitakidi kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anawaona ni wale wenye kuchunga matendo yaokama lilivyo Tamko Lake Muumba:
قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿٢﴾ وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ ﴿٣﴾ وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ ﴿٤﴾ وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٥﴾
Kwa yakini wamefaulu Waumini. Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea. Na ambao wanajiepusha na mambo ya upuuzi. Na ambao wanatoa Zakaah. Na ambao wanazihifadhi tupu zao. [Al-Muuminuwn: 1-5]
Na pia katika Tamko Lake Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa katika suwrah hiyo hiyo:
أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾ الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١﴾
Hao ndio warithi. Ambao watarithi (Jannah) ya Al-Firdaws, wao humo ni wenye kudumu. [Al-Muuminuwn: 10-11]
Na malipo ya mwenye kuifanyia kazi nguzo ya Ihsani ni Jannah. Hivyo, tujitahidi kuwa karibu na Muumba wetu kwa kufanya mema na kujiepusha maovu. Tuelewe kwamba Rabb wetu hashikwi na usingizi wala kuchoka, Anashuhudia yote tuyatendayo, na mbora wetu ni yule anayeogopa ghadhabu Zake akatekeleza amri Zake.