Baba Ameacha Mke, Watoto 4 Wa Kike, 3 Wa Kiume, Bibi, Shangazi, Ma-Ammi Na Wajukuu
SWALI:
Mimi ni binti nimezaliwa katika familia ya watoto saba wakike wanne na wakiiume watatu baba amefariki toka mwaka 2000 na kuacha nyumba 4 na shamba moja zote mali zake mwenyewe maswali yangu ni kama yafuatayo
1. Hizi mali zipo chin ya mama toka kipind hicho je mama ana radhi mbele ya Allah?
2. Ningependa kufaham mgawanyo wa hiz mali kwa mujib wa allah?
3. Kuna bib mzaa baba, shangazi na baba wadogo nao wanastahili kupata na wajuukuu je?
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu Miyraath. Ama kuhusu kipengele chako cha kwanza ni kuwa mama hana haki kumiliki mali yote hiyo ambayo inafaa igawanywe kama anavyotaka Allaah Aliyetukuka au warithi wajadiliane namna ya kuendesha mali hiyo na kugawa baina yao kulingana na mgao waliopatiwa na Muumba wetu.
Ama mgao unavyotakiwa kufanywa kama anavyotaka Allaah Aliyetukuka ni kama ifuatavyo:
1. Bibi mzaa baba atapata sudusi (1/6 = 16.7%).
2. Mke (mama yenu) atapata thumuni (1/8 = 12.5%).
3. Kila binti atapata 17/240 = 7.08%.
4. Kila mtoto wa kiume atapata 17/120 = 14.16%.
Ama shangazi, baba wadogo na wajukuu hawatarithi kwa kuwepo kwa watoto wa aliyefariki.
Na Allaah Anajua zaidi