Kula Pamoja Na Wasio Waislamu Wanaokula Nguruwe Na Vyakula Vinapakuliwa Kwa Pamoja
SWALI:
Assalam W W! kabla ya yote natoa shukrani zangu za zatu kwa kutusaidia kutufungulia iyi website ambayo inanufaisha wengi sanaa.Hatuna cha kuwalipa ila inshaAllah tunawaombea kwa Allah awalipe pepo.(amin)
Swali: mimi nikijana ambae naishi sweeden na ni mwanafunzi. Tunapataga lunch shuleni kwetu lakini mimi silagi kwasababu niliwai kuambiwa na masheikh wa2 kwamba si vizuri kula na wale manaswara kwa sababu nyingi alizonipa. ya kwanza nikusema kuwa wakati tunakula, tunakuwa sehemu moja na wale manaswara baya zaidi wanakula nguruwe na nyamafu kwa hiyo inakuwa haipendezi kwa muisilam. Na istoshi japokua panakua chakula cha waisilam (halal) lakini vyombo vya zile nguruwe na vyombo vya chakula chetu cha halali binakuwa sehemu moja yaani bahati mbaya mtu wakati anapakua ile nguruwe mchuzi unaweza kudondokea ndani ya chakula chetu. Nilimuelewa na ikabidi nikawa nimeacha kula masomoni, lakini juzijuzi nimeambiwa na masheikh wengine wa2 kuwa si makosa kula chakula chao ingawa pako cha waisilam na akanipa sababu nyingi... sasa ningelipenda mnisaidie kunipa mwangaza kwa kua mpaka sasa nashindwa nimuamini yupi?
Na nitafurahi
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu kula pamoja na wasio Waislamu wanaokula nguruwe, na tunakupongeza kwa tahadhari zako na uchungaji wako wa Shari’ah ya dini yetu tukufu.
Suala
Kwa hiyo, kutumia vyombo vya kupikia vya Manaswara havikatazwi lau vitaoshwa vizuri. Kwa hiyo, lau chakula chenu kitapikwa katika vyombo vingine au vyombo hivyo ambavyo viatoshwa vyema kabisa mnaweza kula chakula hicho bila ya tatizo. Kwa vile tayari idara imeruhusu nyinyi kupikiwa chakula chenu ambacho ni halali mnaweza kuzungumza nao tena ili wasiwe ni wenye kuwatilia chakula hicho sehemu moja.
Hata hivyo, linaweza kuwa hilo ni gumu kutekelezeka na kwa hiyo tunakushauri ununue vyombo vyako na ukae navyo chumbani kwako, na wakati wa chakula uwe unakwenda na vyombo vyako na kupakuliwa humo kisha unakwenda kulia chumbani kwako au kwenye meza pamoja na Waislam wenzako. Haipendezi kukaa meza moja na wanaokula nguruwe au haraam nyinginezo.
Vizuri pia ufahamu kuwa ikiwa utakula pamoja na Manaswara haifanyi chakula chako cha halali kuwa haramu. Kitu ambacho inatakiwa ni Waislamu kuchukua vyakula vyao na kula ima vyumbani au mkae kwenye meza yenu mkila nyinyi kivyenu.
Kuhusu vyakula vyao ambavyo si vile vilivyoharamishwa wazi na Shari’ah, Allaah Aliyetukuka Anatuambia:
“Leo mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula cha wale waliopewa Kitabu ni halali kwenu” (5: 5). Kwa hiyo, chakula cha Mayahudi na Manaswara ambacho ni halali kwetu havina tatizo kuvila ukiondosha nyamafu na nguruwe na vingine vilivyokatazwa na Shari’ah.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaagiza Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) walipokuwa wanakwenda jihadi watapita sehemu ambazo wanaishi Manaswara kwa hiyo wanaweza kula vyakula vyao na kutumia vyombo vyao pia.
Bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:
Kuchanganya Vyombo Pamoja Na Vile Vinavyotumika Kwa Nguruwe
Tunawaombea usahali katika kuyapigania hayo na kuweza kupewa haki zenu na taratibu nzima za kutekeleza mambo yote ya dini yenu vizuri.
Na Allaah Anajua zaidi