Posa Zake Hazifanikiwi – Anapata Matamanio Na Kujishika Sehemu Zake Hadi Atulie

 

Posa Zake Hazifanikiwi – Anapata Matamanio Na Kujishika Sehemu Zake Hadi Atulie

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalam Aleykum.

 

Mimi ni msichana wa miaka 25 lkn bado sijaaliwa nimekua nikipata wachumba mara nyingi lkn ndoa haisimami wanaowa kwingine bila sbb sasa je kuna tatizo kwangu au bado tu rizki? Maana kuna watu wananiambia lbd nina jini mahaba au husda je nifanye nini kwa kweli natamani sana na mimi kustirika kwa kuolewa. Nashkuru Allaah sijawahi kuzini naiogopa sana dhambi yake na aibu ingawa kuna wakati napata shida sana kutamani jambo hilo mimi simtazamaji wa filamu za ngono lkn nashangaa hali ya kutamani inanijia mara nyingi sijui kama ntakua nakosea au vipi kwani ninapo tamani huwa najishika mwenyewe sehemu zangu nakutulia sasa sijui ninakosea au? Na kama nakosea inabidi nikoge janaba au? Na je nifanyaje kuepukana na hili. Ntashkuru mkinifahamisha kwani naogopa sana kumkosea mola wangu.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kupata wachumba kisha wakavunja posa na kwenda kuoa pahali pengine ni moja ya mitihani ambayo huwakumba wasichana au wanawake au pengine pia huwa mwanamme huyo si kheri nawe. Ikiwa ni mtihani inabidi uupite ili upate rehema ya Allaah Aliyetukuka kwa kuwa Anasema:

 

أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لَا يُفْتَنُونَ ﴿٢﴾وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۖ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّـهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ ﴿٣﴾

Je, wanadhani watu kwamba wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao ndio wasijaribiwe?  Kwa yakini Tuliwajaribu wale wa kabla yao, ili Allaah Awatambulishe wale walio wakweli na ili Awatambulishe walio waongo. [Al-‘Ankabuut: 2-3].

 

 

Kushindwa kuupita ni kumaanisha kuwa umepata hasara hapa duniani na Kesho Aakhirah.

 

 

Ama kwa sababu ya pili ni kuwa ikiwa si kheri kwako basi pia unatakiwa uvumilie kwani kwa kuvumilia Allaah Aliyetukuka Hatokuacha bali Atakuletea yule mwenye kheri. Ama uwezekano wa jini hauwi hivyo rahisi kwa kusema tu bali inatakiwa ufanyiwe dawa kujua hilo. Na hilo linaweza kujulikana kwa mwanzo kuangalia maisha yako kabla ya kuanza kuposwa na baada ya hapo. Jambo la pili ambalo inawezekana kujua hilo ni kusomewa Aayah zinazoweza kutambulisha kukumbwa na jini. Na hiyo ni kusomewa Aayah na Suwrah zinazohusiana na majini na ukipatikana na ishara baada ya kusomewa basi kweli utakuwa na jini la hukupatikana na alama yoyote utakuwa huna majini. Ama kuondoa husuda ikiwa kweli ni husuda inafaa uwe unasoma asubuhi na jioni Suwrah Al-Ikhlaasw, Al-Falaq na An-Naas mara tatu kila moja na baadhi ya Adhkaar ambazo unaweza kuzipata katika kijitabu Hiswn al-Muslim kinachopatikana hapa Hiswnul Muslim. Kufanya hivyo kutakusaidia sana pamoja na kuwa na ada ya kusoma Qur-aan kwa ujumla kila siku.

 

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akuweke katika hali njema hata usifikirie kuzini, kwani kufanya hivyo ni kuonyesha kutoogopa kwako Muumba wako. Na zinaa ni dhambi kubwa ambayo tumeagiziwa hata tusiikaribie. Na ama kutamani ni jambo la kawaida kabisa kwa kila mmoja wetu – mvulana au msichana miongoni mwetu. Lile ambalo tunafaa kulitilia maanani ni kujaribu kuyazuia matamanio kadiri tuwezavyo kwani ukitofanya hivyo kunaweza kukuingiza wewe katika zinaa ambayo unaiogopa sana. Matamanio hayo yanaweza kupunguzwa kwa kufunga kama alivyotuagizia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Jaribu kujenga ada ya kufunga Jumatatu na Alkhamiys na pia kujaribu kusoma kwa wingi Qur-aan pamoja na kuleta Adhkaar na na kufanya mazoezi ya mwili sana, pamoja na kumuomba sana Muumba Akulinde na zinaa na Akuletee mume wa kheri mwenye Dini na maadili mema ya Kiislamu.

 

 

Wakati unapojiwa na matamanio kule kushika sehemu zako za siri ndio kunazidisha matamanio. Kwa hiyo, ni vyema ujiepushe na kushika sehemu hizo kwa kujishughulisha na mambo mengine yatakayokunufaisha wewe. Na lau utashika sehemu hizo na ukatokwa na maji ya uzazi (manii) basi itabidi uoge josho la janaba. Na ikiwa si maji ya uzazi bali ni maji yanayoitwa madhii yanayotoka kwa matamanio kabla ya manii, itabidi tu uoshe sehemu zako za siri na kisha uchukue wudhuu kwa ajili ya Swaalah.

 

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akuepushe na hayo matamanio pamoja na ndugu zetu wote katika Uislamu. Na tunamuomba Muumba wetu, Awapatie wake wenye kheri wanaume wasiokuwa na wake na wanaume wa kheri wanawake wasio na waume.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share