Sababu Kumi Za Kumtaka Muislamu Asitume Barua Pepe (Email/Forward) Kibubusa

 

Sababu Kumi Za Kumtaka Muislam Asitume

 

Barua Pepe (Email/Forward) Kibubusa

 

Imetayarishwa na: 'Abdun-Naaswir Hikmany

 

Alhidaaya.com

 

Ndani ya makala hii, tutajaribu kueleza ubaya uliojikita ndani ya jamii yetu kwenye masuala ya kupeleka mbele forwards za barua pepe (email). Mambo ambayo yamekithiri mno miongoni mwa Waislamu. Kabla ya kurukia kwenye orodha ya sababu za kuacha kutuma forwards hizo moja kwa moja, ni muhimu kueleza kwa ufupi kuhusu msingi mzuri wa chanzo cha Uislamu.

 

Uislamu umejengwa kutokana na misingi mikuu miwili ambayo ni Qur-aan na Sunnah ya kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Muongozo na mwenendo wowote unaokwenda kinyume na misingi hii ni batili moja kwa moja.

 

Uislamu sio tu dini kama zilivyo imani nyengine, bali ni mfumo mzima wa maisha ya mwanaadamu hapa duniani. Hakuna uchumi, siasa wala jamii itakayotoa kauli ambayo itakuwa juu ya Uislamu. Uislamu wetu unakuja mwanzo kuliko kitu chochote. Ni wa mwanzo kabla ya hiyo roho kupulizwa ndani ya kiwiliwili. Hivyo, Muislamu ni lazima ajivunie Uislamu wake kwa vitendo sahihi na wala sio kutuma barua pepe ambazo zinakwenda kinyume na mafundisho yetu.

 

Madaraka ya Muislamu yanatakiwa kutochupa mipaka. Kwani anatakiwa kukumbuka kwamba maisha yake yanamilikiwa na kile Rabb Anachokitaka. Hivyo, Muislamu hatakiwi kuongeza au kupunguza kwenye Uislamu kwa yale matakwa yake binafsi.

 

Utumiaji wa forwards zisizo na mashiko na zinazotumwa ovyo kutoka kwa Waislamu umezoeleka vibaya. Kwa hakika ni mtindo uliotokana na imani zisizo sahihi na matendo ya wasio kuwa Waislamu ama wale Waislamu wasioelewa elimu yao sahihi. Pia wengi ni wenye kufuata mkumbo tu, kuna baadhi ya Waislamu ni wageni katika utumiaji wa mitandao, wanapoona mambo hayo, basi nao hutaka kutuma tu bila ya kufikiria Uislamu wao.

 

Juu ya yote hayo, baadhi ya Waislamu wanafanya hayo kwa lengo la kutaka kwenda na wakati na pia kuepuka kuitwa Muislamu mwenye msimamo mkali (fundamentalist). Majina ya fundamentalistextremist na mengineyo si chochote isipokuwa ni kuwatia Waislamu pamba za masikioni ili wasifuate Uislamu wao kwa njia zilizo sahihi.

 

Sababu za kumtaka Muislamu asitume barua pepe kibubusa zimeorodheshwa hapo chini. Badala ya kutaja sababu hizo tu kwa juu juu, tumeegemeza dalili kutoka Qur-aan ama Sunnah na pia kutaja mifano ya barua pepe hizo. Hivyo, kila sababu inapewa mtindo ufuatao:

 

Maelezo Ya Sababu:

 

a)  -  Dalili ya Qur-aan/ Sunnah

 

Sababu Ya Kwanza

 

Angalia nini unachotuma; kwani tunatakiwa tuegemeze vitendo vyetu kwa mujibu wa mafunzo sahihi ya Qur-aan na Sunnah.

 

 قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi, Atakupendeni Allaah na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Aal-'Imraan: 31] 

 

Sababu Ya Pili

 

Soma na chunguza vizuri kila unachotumiwa kabla ya kuwatumia Waislamu wengine. Kiweke kwenye mizani ya: Kama Swahaba yeyote angelikuwa hai na kupokea barua pepe kama hii angeliifanya nini? (kuituma kwa Waislamu wengine au kuijibu kuwa haifai au kuifuta moja kwa moja?)

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Nakuusieni kumcha Allaah, usikivu na twaa hata ikiwa kiongozi wenu (Au atakayekuamrisheni) ni Mtumwa wa Ki-Habashi. Mtakaoishi miongoni mwenu mtaona ikhtilafu nyingi. Kwa hiyo shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa waliongoka baada yangu. Ziumeni kwa magego (zikamateni kwa nguvu wala msiziache). Na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila bid'ah ni upotofu.” [Abu Daawuud, At-Tirmidhiy kasema Hadiyth Hasan Swahiyh].

 

Sababu Ya Tatu

 

Jaribu kuchunguza kwa umakini wa hali ya juu nini unachotaka kuwatumia Waislamu wengine. Mara nyingi utashuhudia kutumiwa Hadiyth au du’aa au visa ambavyo havina usahihi. Dua hizo zina asili ya kutoholewa kutoka dini za Kikafiri na kubadilishwa ili ziendane na mazingira ya Uislamu. Kitu ambacho hakikubaliki kabisa kabisa.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا الَّذِينَ اتَّخَذُوا دِينَكُمْ هُزُوًا وَلَعِبًا مِّنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ وَالْكُفَّارَ أَوْلِيَاءَ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ إِن

 

كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

Enyi walioamini!  Msiwafanye wale walioifanya Dini yenu mzaha na mchezo - miongoni mwa wale waliopewa Kitabu kabla yenu, na makafiri kuwa marafiki wandani. Na mcheni Allaah, kama nyinyi ni Waumini. [Al-Maaidah: 57]

 

Pia imepokewa kwa Abu Muhammad al-Hasan bin ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘Anhuma) kuwa alisema:

 

“Nimehifadhi kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Acha lenye kukutia shaka kwa lisilokutia shaka.” [At-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy].

  

Sababu Ya Nne

 

Kuna Hadiyth nyingi zilizo dhaifu lakini zinafanywa kuwa na nguvu ndani ya mitandao hii. Pia kuna Hadiyth za uongo anazozushiwa Nabiy wetu Muhammad (Swallah Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam). Hilo utalielewa utakapokuwa makini pamoja na kufuatilia kila unachotumiwa.

 

Kutokana na ‘Abdullaah bin 'Amruu bin Al-'Aasw (Radhwiya Allaahu ‘Anhuma) amesema: Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Fikisheni kutoka kwangu japo Aayah (moja), na hadithieni habari za Bani Israaiyl wala hakuna kosa, na yeyote atakayenizulia uongo moja kwa moja, basi ajitayarishie makaazi yake ndani ya moto.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy].

 

Sababu Ya Tano

 

Bila ya shaka itakuwa umepata kupokea barua pepe au hata ujumbe mfupi wa simu (SMS) ndani ya simu yako inayosema: Tuma Kwa Watu 10 Utapata Habari Nzuri au Tuma Kwa Watu 5 Kama UTapuuza Kitu Kibaya Kitakupata. Ni vyema ukapuuzia mbali ujumbe kama huo kwani kama kweli aliyekutumia ni Muislamu hakuwa na haja ya kukulazimisha bali wajibu wake ni kutoa ushahidi wa Qur-aan na Hadiyth ili Muislamu aelewe umuhimu wa hilo analokutumia. Sio wajibu wake kukulazimisha kutii kwa kuipeleka mbele forward. Hiyo ni khiyari yako. Na kuhusu mambo yatakayotokea baadaye (Ghayb) ni mambo yaliyo mikononi mwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Hakuna kiumbe chenye kumiliki ghaibu ya kukwambia utapata habari nzuri ama litakukuta jambo baya. Hata Rusuli, Malaika na Majini hawajui elimu ya ghaibu. Jibriyl (‘Alayhis-salaam) alimuuliza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “…Hebu nipe habari ya Qiyaamah”. Akasema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Mwenye kuulizwa si mjuzi kuliko mwenye kuuliza.” (Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy).

 

Pia tamko la Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Linasema:

 

إِنَّ اللَّـهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ

 

تَمُوتُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ

Hakika Allaah Ana elimu ya Saa (Qiyaamah), na Anateremsha mvua na Anajua yale yaliyomo katika tumbo la uzazi, na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho, na nafsi yoyote haijui itafia katika ardhi gani, hakika Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Luqmaan: 34].

 

Sababu Ya Sita

 

Kuna mambo mengi ndani ya mtandao yenye kuunganishwa na madhehebu yasiyo sahihi lakini yakafanywa kuwa ni yenye asili ya Uislamu. Kwa mfano unaweza kupokea barua pepe yenye kisa cha kifo cha Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kikataja majina ya ‘Aliy na Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘Anhuma) tu kuwa ndio waliokuwepo wakati Nabiy anakufa. Hapo ni lazima ujiulize na kukumbuka vyema kisa cha kifo cha Nabiy wetu. Kwani alikuwepo Mcha wa Allaah muhimu ambaye wapotoshaji wa Uislamu hawataki hata kumsikia, naye ni Mama wa Waumini Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa). Hivyo haifai kutuma barua pepe kama hiyo kwa Waislamu wengine kwani barua na visa kama hivyo vimetungwa na wale wenye mapenzi na watu fulani tu wa nyumba ya Nabiy na kuwaacha wengine muhimu.

 

Katika Hadiyth ya Ibn Mas‘uud (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: “Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituchorea mstari. Kisha akasema: ‘Hii ndio njia ya Allaah’. Kisha akachora mistari kuliani na kushotoni kwake na akasema: ‘Hivi ni vijia, katika kila njia kuna Shaytwaan ambaye anawaita watu katika njia hiyo”. Hapo akasoma:

 

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa. [Al-An’aam: 153]

 

[Imepokewa na Imam Ahmad, at-Twabariy na al-Haakim ambaye ameisahihisha na kukubaliana naye adh-Dhahabiy].

  

Sababu Ya Saba

 

Jaribu sana kusoma kwenye darsa madhubuti za Kiislamu ama mitandao yenye mafundisho sahihi badala ya kusubiri tu barua pepe ndani ya inbox yako. Utaratibu huu utakupa umakini zaidi kwani utatuma kitu ambacho nawe umekitafuta, umekisoma na umekielewa.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

 

هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ۗ

Je, wanalingana sawa wale wanaouja na wale wasiojua? [Az-Zumar: 9]

 

يَرْفَعِ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَالَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ دَرَجَاتٍ

Allaah Atawainua wale walioamini miongoni mwenu na waliopewa elimu daraja za juu. [Al-Mujaadalah: 11].

  

Pia Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anatufahamisha kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Kutafuta elimu ni faradhi juu ya kila Muislamu.” [Ibn Maajah, Shaykh Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Sunnan Ibn Maajah].

 

Sababu Ya Nane

 

Muziki, pombe, kamari, shirki, picha za utupu na mengine yanayofanana nayo ni haramu ndani ya Uislamu. Hivyo, barua pepe yoyote yenye mnasaba wowote wa kulinganisha na mambo hayo haifai kutumwa wala kutumiwa kwa Muislamu. Mfano ni barua pepe inayosema “beautiful download! Attachment” yenye kumkumbusha Muislamu juu ya masuala Atakayouliza Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Siku ya Qiyaamah.  Kitu kikubwa ambacho kimo ndani ya kiambatanisho hii ni muziki ambao unakwenda kama kwaya za kanisani. Hapo utaelewe namna Waislamu wasivyokuwa makini na wanavyounganisha Uislamu wao ulio kamili na ukafiri ulio na mashaka chungu nzima. Na nyakati nyingine utakuta zinatumwa ‘slide show’ ambazo asli yake ni za kutoka kwa Wakristo zenye kutaja maombi yao ya kumuomba ‘Jesus’, Waislam wakazigeuza neno ‘Jesus’ na ‘Lord’ na kuandika Allah kisha wakazituma zionekane kama ni du’aa za Kiislam!!

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

Enyi walioamini! Hakika pombe na kamari na masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli; ni najisi na chukizo kutokana na kitendo cha shaytwaan; basi jiepusheni navyo, mpate kufaulu. [Al-Maidah: 90].

 

Sababu Ya Tisa

 

Muislamu hatakiwi kupoteza muda wake kwenye mambo yasiyo na msingi. Hivyo sio vyema kumpotezea Muislamu mwengine kusoma mambo ya kitwaghuti na mizaha iliyochupa mipaka ya Kiislamu. Mfano ni kumtumia Muislamu barua pepe inayomtaka kufumba macho kama vile anasinzia na kusoma ujumbe unaomwambia kwamba Ana Macho Mabaya – Bad Eyes. Je, tunaweza kuyaweka kwenye mizani gani hayo maneno? Je, ni macho mabaya kwa Alichokiumba Rabb ama macho mabaya kwa uoni wa mwanaadamu?

 

Mzaha na matani yenye kuchupa mipaka ni vitu vinavyotengua Uislamu wa binaadam. Allaah Anasema: 

 

وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ ۚ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ﴿٦٥﴾لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ ۚ إِن نَّعْفُ عَن طَائِفَةٍ مِّنكُمْ نُعَذِّبْ طَائِفَةً بِأَنَّهُمْ كَانُوا مُجْرِمِينَ﴿٦٦﴾

Na ukiwauliza, bila shaka watasema: Hakika tulikuwa tunaporoja na tunacheza. Sema: Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayaat Zake na Rasuli Wake? Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu. Tukilisamehe kundi miongoni mwenu, Tutaliadhibu kundi (jingine), kwa kuwa wao walikuwa wakhalifu. [Tawbah: 65-66].

 

Naye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Chukua faida ya mambo matano (5) kabla ya matano (5): ujana wako kabla ya uzee wako, afya yako kabla ya maradhi yako, mali yako kabla ya ufukara wako, faragha yako kabla ya wakati utakaoshughulishwa na mambo mbali mbali, na maisha yako kabla ya kifo chako.” [Al-Haakim].

  

Sababu Ya Kumi

 

Mwisho kama ni barua pepe nzuri yenye mafundisho sahihi ya Qur-aan na Sunnah usiache kuituma kwa Waislamu wengine pamoja na kumuombea du’aa mtumaji.

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) amesema: Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Yeyote anayelingania katika uongofu, atakuwa na ujira mfano ujira wa anayemfuata, hatapunguziwa kutokana na ujira huo chochote.” [Muslim].

 

Tunawanasihi tuwe tunajihesabia matendo yetu na 'amali zetu kabla hazijakuja kuhesabiwa siku ya Qiyaamah. Na tutambue kuwa tupo hapa duniani kwa maisha ya kupita na kila tunalolifanya liko katika Hisaab. Khatmah yetu hatuijui tutaangukia Jannah ama Motoni. Tujitahidi kusoma vyema mafunzo sahihi ya Kiislamu na kutenda mema kabla ya kutufikia yakini (mauti).

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atughufurie sote kwa yale tunayoyajua na tusiyoyajua.

 

Share