002-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Mwanzo Mzuri Wa Maisha Ya Ndoa

 

MWANZO MZURI WA MAISHA YA NDOA

 

Kwa hakika mwanzo mzuri uko katika uchaguzi mzuri, atakayefanya uchaguzi mzuri atakuwa ameweka mguu wake katika njia ya uokozi na furaha.

Uislamu ni dini ya maumbile, umemuongoza mwanamke wa Kiislamu katika misingi sahihi ya kuchagua mume, mwanamke ambae akiongoka kwa uongofu wake basi maisha yao ya ndoa yatakuwa mepesi yenye baraka, na hivyo kuwa na familia njema yenye mapenzi, huruma na mambo mazuri.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Atakapokujieni mnayeridhika na dini yake na akhlaqi yake basi muozeni, na kama hamkufanya hivyo itakuwa ni fitna kwenye ardhi na ufisadi mkubwa”[1]

 

Hizi ni sifa za Mume mwema, dini na tabia njema.

 

Angalia ewe dada wa Kiislamu yule anayekuja kukuposa, akiwa mtu mwenyewe amelazimiana na sifa nzuri za Kiislamu na mwenye kuhifadhi Swalah zake, yupo mbali na mambo machafu na watu wenye tabia mbaya na kufuata hawaa, mwenye kusuhubiana na waja wema wa Allaah, hupata chumo la halali basi usimuache mtu huyo.

 

Al-Hasan Al-Baswry amemuusia mtu mmoja kwa kumwambia,

“Muozeshe Binti yako mtu mwenye Dini, Kwani mtu mwenye dini akimpenda binti yako atamkirimu, na akimchukia hatomdhulumu”

 

Baadhi ya watu wanaangalia ndoa kana kwamba ni mkataba wa kibiashara, mshindi na mwenye kupata faida ni yule anayepata kiasi kikubwa cha mali, bila ya kujali matokeo yake mabaya yenye kuangamiza familia, hawajali tabia wala dini ya mume, lakini wanachojali zaidi ni kiasi gani cha mali au fedha alichonacho. Ewe dada wa Kiislamu huu usiwe mtazamo wako kwa mume, ukaonja machungu na hasara kupita kiasi. Angalia tabia yake, maadili aliyokuwa nayo na yasikuhadae mandhari yake ya kupendeza.

 

Mwangalie Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ni kigezo chetu anapopita mtu mbele ya watu alikuwa akiuliza, “Mnamuonaje mtu huyu, Husema: huyu kwa hakika akiposa ataozeshwa, na akiombewa atakubaliwa, na akisema atasikilizwa, kisha akanyamaza, akapita mtu katika mafukara Waislamu akasema, ‘Mnasemaje katika haya kuhusu huyu? Wakasema, kwa Hakika huyu akiposa haozeshwi, na akiombewa hakubaliwi na akisema hasikilizwi, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, ‘Huyu ni bora ujazo wa ardhi kuliko yule’[2]     

 

Hii haina maana kuwa mimi nakulingania ewe dada yangu Muislamu katika kuchagua mume fukara, lakini kumbuka kuwa fukara mwema ni bora kuliko tajiri muovu. Kama ambavyo mwanamume ana haki ya kuangalia dini ya mwanamke. Ni vyema kwa walii wa mwanamke aangalie dini ya kijana anayekuja kuposa hali yake na tabia zake na pindi atakapomuozesha binti yake mwanamume fasiki, au mwenye bid’ah, basi mtu huyu atakuwa amemkosea binti na yeye mwenyewe.[3]

 

Salafus Swaalih (watangulizi wema) walitupigia mifano mizuri sana katika uchaguzi wa mume mwema, huyu hapa Sa’iyd bin Al-Muswayyib ambaye ni Tabii maarufu, alikuwa ni mwanachuoni mwenye zuhdi, anakataa kumuoza binti yake (ambae watu wanajua uzuri na usomi wake) kwa Waliyd bin ‘Abdil-Malik (mtoto wa Khalifa wa Waislamu wakati ule) na akaamua kumuoza kijana wake kwa mwanafunzi wake ambae akiitwa Abu Wadaa’a kwa Dirham mbili au tatu tu.

 

 

 

[1] Hadiyth hii imepokewa na At-Tirmidhiy na wengineo na ameifanyia Tahsiyn Al-Al-Baaniy

[2] Al-Bukhaariy

[3] Minhaaj al-Qaswidiyn

Share