005-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Mapokezi Mazuri Huingiza Furaha Moyoni
MAPOKEZI MAZURI HUINGIZA FURAHA MOYONI
Wakati mume anaporudi nyumbani na kumkuta mumewe amejiandaa na watoto humkabili kwa nyuso za bashasha, jambo hilo humuingizia furaha moyoni mwake. Katika Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tunasoma ya kuwa,
“Atakayekutana na nduguye Muislamu kwa alipendalo ili amfurahishe kwa hilo basi Mwenyezi Mungu Atamfurahisha siku ya Qiyaamah”[1]
Ummu Sulaym, mke wa Abu Twalhah pindi alipofiwa na mwanawe aliwaambia watu wa nyumbani kwake,
‘Msimwambie Abu Twalhah hadi mimi mwenyewe nitakapomweleza’ Abu Twalhah aliporejea kutoka katika safari zake akamkuta mkewe katika hali nzuri na sura iliyochangamka. Abu Twalhah akakaribishwa vizuri na kisha wakazungumza wakiwa faragha kiasi cha mume kumaliza haja yake kwa mke wake. Baada ya hapo ndipo alipomweleza habari ya kifo cha mwanawe. Abu Twalhah alikasirika kwa jambo hili (kufichwa habari kwa muda kisha kuelezwa baadaye) kwa hiyo akaenda kushitakia kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Baada ya Mtume kusikia mashitaka yale aliunga mkono kitendo cha mke wa Abu Twalhah na kumwambia, “Mwenyezi Mungu Awabariki kwa usiku wenu ule.”[2]
Alisema kweli Mtume wa Allah na wakabarikiwa kupitia usiku wao ule, watoto kumi na wote wakawa wasomaji wazuri wa Qur-aan.
Ewe mke wa Kiislamu! Usiwe kama ambaye humpokea mumewe wakati wa kurudi nyumbani kwa uso uliojawa na huzuni kwa sababu amechelewa kurudi nyumbani, au kwa mapokezi yanayoanza kwa salamu za mashitaka kwa hali yake ya siku ile au ya watoto na matatizo yao. Kwa hakika yote haya yanarudi kwa watoto na huathirika kwa tabia hizi na yanayotokea baina ya wazazi wao hali inayowafanya kuathiri afya zao za nafsi kwa siku za mbele.