Ufafanuzi Kuhusu Aayah Inayosema “Mali Zenu Na Watoto Wenu, Wake Zenu Fitna”

 

Ufafanuzi Kuhusu Aayah Inayosema "Mali Zenu Na Watoto Wenu,

Wake Zenu Fitna"

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Assalamu aleykum warahmatullah wabarakat

 

Imetajwa katika Qur-ani tukufu kuwa mali zenu, wake zenu, na watoto ni fitna kwenu. Kama mume anaichukulia aya hii moja kwa moja tu bila hata kuona hiyo fitna ya mke na watoto, madam imetajwa tu basi kwake yeye mke na watoto ni jamii au ni kitu cha mwisho katika maisha yake wala hakipi umuhimu wake inavyotakiwa na ilivyosunniwa, na pia kwake yeye ni watu wa kuwa sacrificed for anything at anytime. Je hii ni sawasawa? Naomba ufafanuzi wa jambo hili na aayah yenyewe katika Qur-aan na makusudio yake kiwazi kwani ina affect not only the motherhood, but hata the social behaviour and the self esteem (confidence) of the innocent growing children.

 

Kwanza kabisa natoa shukurani kwa waanzilishi na wahusika wote wa Alhidaya, Allaah atawajaalia kila lenye kheri fildunia wal akhira. Niliwahi kutuma suala langu kuhusu mada ya hapo juu "vipi mke na watoto huwa ni fitna?"Lakini sikuona jibu bado. Naomba radhi kwa kuchanganya lugha. Shukran

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ufafanuzi wa Aayah inayosema kuwa wake na mali zenu, na watoto wenu ni fitna. Hakika Aayah hii imeeleweka vibaya kama vile zilivyoeleweka nyingine ambazo kwa kuzielewa vibaya kunaleta athari mbaya katika jamii yetu ya Kiislamu.

 

Mwanzo kabisa Aayah yenye maana hiyo japokuwa hazikujumlishwa aina zote hizo tatu. Na maana ya Fitnah iliyotumika ni mitihani. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ مِنْ أَزْوَاجِكُمْ وَأَوْلَادِكُمْ عَدُوًّا لَّكُمْ فَاحْذَرُوهُمْ ۚ وَإِن تَعْفُوا وَتَصْفَحُوا وَتَغْفِرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١٤﴾

Enyi walioamini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu ni maadui kwenu, basi tahadharini nao. Na mkisamehe na mkapuuza na mkayafutilia mbali, basi hakika Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [At-Taghaabun: 14]

 

Katika Aayah hii inatueleza makundi mawili uliyotaja hapo juu; wake na watoto ni maadui zenu kwa kuwa lau hamtokaa nao vyema basi watakwenda kuwashitaki Kesho Aakhirah mbele ya Allaah Aliyetukuka. Waume wamepatiwa majukumu ya kukaa na wake zao kwa wema kwa kuwapatia yote ambayo wanafaa wapewe. Ikiwa hayo hayatofanyika atakwenda kushitakiwa Siku ya Qiyaamah, siku ambayo kila mmoja atamkimbia mwenziwe. Ndio kwa ajili ya hiyo Allaah Aliyetukuka Akasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ

Enyi walioamini! Jikingeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe [At-Tahriym: 6]

 

Ama kuwa watoto ni fitnah (jaribio) ni kuwa baba ana wajibu kumlea mtoto wake kwa njia nzuri, kwa kumlisha vyema, kumsomesha na kumpatia maadili. Kutofanya hivyo ni kufeli (kuanguka) mtihani. Na vile vile mali, mali inatakiwa itumiwe katika kumridhisha Allaah Aliyetukuka na kutoitumia katika maasi. Kwa ajili hiyo Akasema Aliyetukuka:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا زَحْفًا فَلَا تُوَلُّوهُمُ الْأَدْبَارَ﴿١٥﴾

Enyi walioamini! Mtapokutana na wale waliokufuru vitani, msiwageuzie migongo (kukimbia). [Al-Anfaal: 15]

 

Na kama Muislamu ataweza kuupita mtihani huu basi atapata ujira mkubwa kama Alivyosema Aliyetukuka:

وَاعْلَمُوا أَنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ وَأَنَّ اللَّـهَ عِندَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ﴿٢٨﴾

Na jueni kwamba mali zenu na watoto wenu ni jaribio, na kwamba kwa Allaah uko ujira adhimu.  [Al-Anfaal: 28]

 

Linalotakiwa ni kuwa haifai wake, watoto na mali kumsahaulisha mmoja wenu na kukosa kufanya mema kama kumtaja Allaah kwa wingi kutekeleza ‘Ibaadah Zake na mambo mengine mema. Kwa ajili hiyo, Allaah Aliyetukuka Akawahutubu Waumini kwa kuwaambia:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُلْهِكُمْ أَمْوَالُكُمْ وَلَا أَوْلَادُكُمْ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ﴿٩﴾

Enyi walioamini! Zisikupurukusheni mali zenu na wala watoto wenu mkaacha kumdhukuru Allaah. Na yeyote atakayefanya hivyo basi hao ndio waliokhasirika. [Al-Munaafiquwn: 9]

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share