010-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Hamu Yako Kubwa Iwe Kujifanyia Islahi Na Kuendesha Nyumba Yako

 

Hamu Yako Kubwa Iwe Kujifanyia Islahi Na Kuendesha Nyumba Yako

 

 

 

Nafsi ya mwanadamu inapenda uzuri na inapenda kuonesha uzuri kwa anayempenda, tunasoma katika Hadiyth: “Ni yule ambae ukimuangalia atakupendeza.”

 

Kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) vile vile amesema:  “Kwa hakika Allaah Ni Mzuri Anapenda vitu vizuri.”[1]

 

‘Aliy bin Abi Twaalib amesema: “Mbora wa wanawake wenu ni mzuri wa harufu, mwenye kupika chakula kizuri kitamu na akitoa hutoa kwa wastani na akizuia huzuia kwa wastani”

 

Moja katika usia wa Umaamah bint Al-Haarith kwa mwanae Ummu Iyaas bint ‘Awf wakati wa ndoa yake: “Jicho lake lisiangukie kwenye eneo lako lenye kuchukiza, na wala asinuse kwako isipokuwa harufu nzuri.”

 

Kwa hakika usafi binafsi wa mwanamke ni jambo muhimu sana: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mwanamme kurudi safarini usiku kisha kumgongea mke wake mlango usiku, ili aweze kujitayarisha kwa kuchana nywele na kunyoa vinywele vya mwili.[2]  

 

Katika Hadiyth nyingine tunajifunza: “Usafi unalingania kwenye imani”[3]  

 

Hapa tutaonesha kwa ufupi baadhi ya mambo makhsusi ya mapambo ya mwanamke.[4]

 

1-Kuunga nywele: kuunga nywele za mwanamke kwa nywele nyinginezo ni haramu kwa maafikiano ya Wanachuoni[5] na katika kuziunga na kitu kingine, wanachuoni wametofautiana.

 

2-Kupunguza Nywele: inaruhusiwa kwa kutopungua chini ya masikio mawili, ama chini ya hapo kuna tofauti ya wanachuoni katika hilo.[6]

 

3-Kuondosha Nywele za Uso: Kuna tofauti ya maamuzi ya uhalali na uharamu wake lakini kilichokubaliwa zaidi ni kuwa inafaa, kama haitokuwa tatizo kwa mume (kwa maana akiruhusiwa na mume wake zaidi ikiwa mwanamke huyo kazoea kunyoa mara kwa mara hapo kabla, ikiwa hali haipo dhahiri hivyo yaani mume hakereki na mke kuwa na nywele nyingi basi ni bora aache nywele na asinyoe.[7] WaAllaahu A’alam.

 

4-Kuondosha nyusi: (Ingawa) baadhi ya watu wa madhehebu ya Hanbali na ya Shaafi’iy wanaona kuwa ni sawa kufanya hivyo ikiwa idhini ya mume wake imepatikana na wengineo wanasema kuwa ni haramu kwani imeingia katika jumla ya maana ya An-Nams [8]kwa kuwepo ila nyinginezo sio illa ile ya Taghriyr inayoharamisha kuondosha kwake nyusi. (Pamoja na wanaoona hivyo, ila lililo sahihi kutokana na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyo wazi ni kuwa jambo hilo ni Haraam; liwe kwa idhini ya mume au bila idhini ya mume)[9]

 

5-Kuondosha Nywele zingine katika mwili.[10]  

 

Kwa ujumla inaruhusiwa bila ya kuwepo mambo yenye kuchukiza. Hivyo inajuzu kwa mwanamke kuondosha nywele zake mwilini mwake kwa njia anayoiona kuwa ni sawa.[11] 

 

Kinachokamilisha pambo la mwanamke na uzuri wake ni uzuri wa nyumba yake, usafi wa makazi yake na kumhudumia mume wake, anaweza kuiga mfano wa Asmaa bint Abi Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhaa) aliposema: “Az-Zubayr alinioa wakati ambapo hakuwa na mali mbali na farasi wake mmoja na ngamia wake anayemnywesha maji, nilikuwa na tabia ya kumlisha farasi wake na kumuongoza na ninamsagia ngamia wake, na ninashona kiriba chake cha maji, ninakanda unga, na nilikuwa nikichukua mbegu kichwani mwangu kwa masafa ya theluthi ya maili (farsakh) nilipumzika na hayo yote pindi baba yangu Abu Bakr aliponitumia mfanyakazi aliyenitosheleza na kumuongoza farasi nikaona kuwa nimekombolewa.”[12]

 

Huu ni mfano wa mwanamke mkweli aliyekuwa akimhudumia mume wake kiasi cha kumuongoza farasi wake na kumsimamia nalo ni jambo lisilowezekana ila kwa wanaume na wanawake majasiri kama Asmaa hadi alipokirimiwa na Allaah kwa kupewa mfanyakazi ili aweze kufanya kazi zingine za kumhudumia mume wake na kusimamia nyumba yake.

 

 

[1]  Imepokelewa na Muslim

 

[2] Al-Bukhaariy na Muslim

 

[3] Imepokewa na At-Twabaraaniy

 

[4] Fungu hili limetoka katika kitabu, ‘Min Qadhwaaaya Az-Ziwaaj’ cha Jaasim bin Muhalhal Al-Yaasin]

 

[5] Angalia Fat-hul Baariy, Juzuu ya 1

 

[6] Swahiyh Muslim, sharh ya An-Nawawi, Juzuu ya 4

 

[7] Naylul Awtwaar cha Ash-Shawkaaniy, Juzuu ya 6

 

[8] Ishara ya Hadiyth   ‘Abdullaah Bin Mas’wud ambaye amesema: “Allaah Amewalaani wenye kuchanja na wenye kuchanjwa, na wenye kunyoa nyusi, na wenye kuchonga meno kwa urembo, na wenye kubadilisha umbile la Allaah” [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

 

[9] Maneno ya kwenye mabano ni ya Mpitiaji.

 

[10] Ni juu ya mwanamke mwenyewe kunyoa nywele zake za mwilini na asiifanye kazi hiyo mtu mwengine zaidi yake kwa dalili ya Hadiyth ya Mtume inayosema, “Mwanamme haangalii uchi wa mwanamme mwenzake, na mwanamke haangalii uchi wa mwanamke mwenzake” imepokewa na Muslim na Ahmad

 

[11] Kutoka katika kitabu, ‘Qadhwaaya Az-Ziwaaj’ cha Jaasim bin Muhalhal Al-Yaasin

 

[12] Al-Bukhaariy na Muslim.

 

Share