019-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Jamaa Za Mume Wako Ndio Jamaa Zako…Wakirimu

 

JAMAA ZA MUME WAKO NDIO JAMAA ZAKO…WAKIRIMU

 

Kwa hakika miongoni mwa mambo ambayo yananyanyua hadhi na shani yako kwa mume wako ni kuwakirimu jamaa za mume wako na haswa zaidi mama yake mzazi na kutangamana naye matengamano mazuri na kumuita kwa jina analopenda kuitwa nalo na kumsaidia mume wako aweze kuwafanyia wema wazazi wake wawili.

 

Ole wako, tena ole wako, kukikosoa jambo la mama yake kwa mume wako (wala pembeni) jambo hilo hatofurahia na litamkera na kumpa dhiki, jaribu kusubiri kwa muamala wa mama wa mume wako ikiwa hujavutiwa nae au wewe mwenyewe binafsi humpendi na kumbuka ya kuwa, ‘Kama unavyofanya utafanyiwa’ wahurumie watu waliokuwa dhaifu na wazee, na jua ya kwamba chochote utakachowafanyia basi nawe utafanyiwa na watoto wako au wake za wanao.

 

Kadhalika kumbuka kauli ya Allaah,

Na Mola wako Ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa heshima. (17:23)

 

Pamoja na kuwa mume wako ameamrishwa kuwafanyia wema wazazi wake wawili lakini nawe kama mke wake una wajibu wa hilo pia, nalo ni kuhakikisha kuwa unamsaidia mume wako katika kuwafanyia wema wazazi wake wawili, usiwe kikwazo katika kufikia hilo, kama vile wewe kuzua matatizo pamoja na mama yake na kumuweka mume wako katika hali ngumu. Katika kuona kwamba umeshindwa kumsaidia hilo ni pindi mume wako anapokufadhilisha wewe kuliko hata mama yake na hivyo kupata hasara kubwa, na kadhalika hasara hiyo utaipata nawe kadhalika kwani wewe ndie uliyesababisha hilo. Mtu yeyote atakayelingania katika upotofu naye ana dhambi na dhambi za watakaomfuata katika upotofu ule hadi siku ya Qiyaamah, kuwaasi wazazi wawili ni katika madhambi makubwa nayo ni sababu ya kukosa rehema kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Tunasoma katika Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam),

“Watu watatu hawatoingia peponi; Atakayewaasi wazazi wake wawili, Dayuuth[1], na Yule mwenye kujifananisha na wanaume”[2]

 

Je, baada ya hapo dada yangu kuna marejeo mema?!! Kwa hakika kuwakirimu wazazi wawili, na kuwalingania katika kufanya wema ni katika jambo litakalokusaidia katika kupata furaha hapa duniani na Akhera na hivyo kheri itaweze kuenea katika nyumba yenu na rehema na Baraka za Mwenyezi Mungu Hakika Yeye ni Mwingi wa Kuhimidiwa, Mwingi wa Kutukuzwa.

 





[1] Dayuuth ni yule mtu asiyeona wivu kwa mke wake hata akifanya jambo baya

[2] Imepokewa na An-Nasaaiy, Al-Haakim na wengineo

Share