021-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Jirani Ana Haki Tusizisahau

 

JIRANI ANA HAKI TUSIZISAHAU

 

Familia ya Kiislamu haiishi peke yake kwa kujitenga na jamii bali ni lazima kuamiliana na jirani. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuusia kuchanganyika na watu na kuwa anayechanganyika na watu na akasubiria maudhi yao ni bora kuliko yule mtu ambaye hatangamani na watu na wala asiyesubiri maudhi yao.[1]

 

Jirani ndiye mtu wa mwanzo anayejiwa na mtu wakati wa shida hivyo kumfanyia wema ni wajibu na miongoni mwa wajibu mkubwa na kumfanyia ubaya ni jambo linalopelekea katika moto na adhabu ya Mwenyezi Mungu.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa,

“Mwanamke fulani namkumbuka kwa wingi wa Swalah zake, Swawm zake na sadaka zake azitoazo lakini anawaudhi jirani zake kwa ulimi wake…Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu, ‘Kwa hakika yeye ni mtu wa motoni’[2]

 

Hata hivyo ni muhimu kutahadhari na jirani muovu ambaye hajali kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa uwazi au mchana, na vile vile jirani mzushi (mtu wa bid’ah) ili watoto wasije wakaiga tabia za namna hizi na wakaenda kinyume na shari’ah za Mwenyezi Mungu.

Hata hivyo mlango wa nasaha na kuwaongoza watu hawa haujafungwa na kadhalika ikibidi kujadiliana nao kwa lile lililokuwa zuri hadi Allaah atakapotoa ruhusa ya kuongoka kwao, na siku zote usisahau kuwa, “Dini ni Nasaha.”

 





[1] At-Tirmidhiy

[2] Imepokewa na Ahmad

Share