Kumpa Mtoto Jina Lisilokuwa La Kiislamu Inafaa?

 

SWALI:

 

Assalam Aalleykum, ndugu zangu waislam

Swali langu ni hili je kumpa mtoto wako jina lolote zuri la ki kiristo je ni dhambi? Kama ni muislam, na kama mzazi anayefuata sheria zote za kiislam. KWA SABABU NAONA SIKU HIZI MAJINA YAMECHANGANYIKA KWA WAISLAM NA WARISTO NAOMBA JIBU TAFADHALI.


 

 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 

.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumpa mtoto jina lisilokuwa la Kiislamu

.

Uislamu ni mfumo kamili wa maisha kwa kuwa kila tunachotaka limeelezwa kinaganaga katika machimbuko yetu ya Shari’ah. Na kwa hilo katika kupeana majina hasa ya watoto ni jukumu la Muislamu kumpatia mtoto jina zuri ambalo litamletea taathira njema katika maisha yake. Hiku kupatiwa jina zuri kwa mtoto ni haki yake kabisa ambayo mtoto anapatiwa na sheria ya Kiislamu.

 

Muislamu ni kiumbe mnyenyekevu na mtiifu kwa sheria zilizowekwa na Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa hiyo, haiyumkini na haiwezekani kwa Muislamu wa kweli mwenye kufuata sheria zote za Kiislamu akakiuka na kupuuza sheria hii ya kumpa jina zuri kwa mtoto wake. Huenda labda kwa kutofanya hivyo ni kutokujua kanuni za Kiislamu kuhusu kumpatia mtoto jina.

 

Linalopasa kwa mlezi kuchukulia uzito wakati wa kumpa jina mtoto; na huko ni kumchagulia jina zuri kama alivyosisitiza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Abu ad-Dardaa’ (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Kwa yakini siku ya Qiyaamah mtaitwa kwa majina yenu na kwa majina ya baba zenu. Basi yaboresheni majina yenu” (Abu Daawuud).

 

Vile vile anawajibika mlezi (mzazi) kutompa jina baya litakaloweza kumharibia heshima yake na iwe ndio kivutio cha istihzai na kuchezwa shere. Mama wa Waumini ‘Aa’ishah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akilibadilisha jina baya” (at-Tirmidhiy).

 

Na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema: “Binti fulani wa ‘Umar akiitwa ‘Aasiya (muasi). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwita Jamyilah (mwema, mzuri)” (at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

 

Vilevile asimuite mtoto jina linaloashiria ukorofi na kisirani ili mtoto aweze kusalimika na ukorofi huo.

 

Ingia kwenye viungo vifuatavyo usome zaidi mas-ala yenye kuhusiana na majina:

 

Majina Ya Watoto Na Maana Yake

 

Fiqh Ya Kuwaita Majina Watoto

 

Pia Muislamu haifai kujifananisha kwa hali yoyote ile na wasiokuwa Waislamu, kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza hilo. Mfano mmoja ni kuita majina ambayo si ya Kiislamu. Na kuhusu majina hatuna haja kabisa ya kuiga majina ya makafiri wowote wawao kwani majina yetu mazuri ni mengi sana yasiyohesabika.

 

Kwa hivyo kuwaita watoto kwa majina hayo haifai katika Uislamu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share