Maana Ya Talqiyn Kwa Mtu Anayekata Roho - Je, Vipi Inamfaa Maiti?

 

Maana Ya Talqiyn Kwa Mtu Anayekata Roho - Je, Vipi Inamfaa Maiti?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Nashukuru kwa ilmu yenu ambayo nami najaribu kuisambaza kwa baadhi ya ndugu zetu waislaamu In shaa Allaah. Kwanza kabisa ningependa mnifafanulie hili neno TALAQIN. Pili je ni wakati gani itamfaa mtu kama ameshakata roho au kwenye sakaratul mauti. Nitashukuru kwani kuna ubishi miongoni mwa wasilaam sehemu hii.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Talqiyn ni neno la Kiarabu lenye maana ya imla, mafunzo, elekezo. Na katika sheria ni elekezo au mafunzo ambayo Muislamu anampatia nduguye, Muislamu inapobainika kuwa yuko katika sakarati (umauti).

 

Kurudia hilo elekezo au imla ni kwa Muislamu aliye karibu na Muislamu aliye katika Sakaraatul-mawt sio baada ya kuaga dunia. Na hiyo Talqiyn wakati huo ni kurudia rudia kumtamkia mbele yake huyo mwenye kukaribia kukata roho kwa kusema Laa ilaaha illa Allaah. Inatakiwa ayakariri maneno hayo, ili naye aliye katika sakarati ayakumbuke na aweze kuyatamka. Na endapo atafanikiwa kuyasema maneno hayo mwishoni basi yatamuondoshea yote na endapo aliye katika sakarati atasema maneno mengine basi mwenye kumsemea itabidi arudie   maneno hayo kwa kutaraji kuwa atatamka na yawe ni maneno yake ya mwisho. Kuna fadhila kubwa sana kwa aliye katika sakarati kusema maneno hayo mwisho. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

"Yule atakayekuwa maneno yake ya mwisho ni Laa ilaaha illa Allaah ataingia Peponi" [Ahmad na Abuu Daawuud].

 

Na wala si kumsomea au kumlaqinia anayekufa Suwrah Yaasiyn kama wengine wanavyoitakidi kutokana Hadiyth dhaifu:

 

"Someni Yaasiyn kwa maiti wenu"  

 

‘Maiti wenu' hapo wengine wamefahamu kuwa ni wale wanaokata roho, na wengine wamefahamu kuwa ni wale tayari waliokwishakufa. Ndio maana utakuta mtu anapotaka kukata roho watu hukimbilia kumsomea Yaasiyn, na wengine baada ya kumzika humsomea maiti wao Yaasiyn kwa ufahamu wao wa Hadiyth hiyo ambayo ni dhaifu. - Maimaam An-Nawawiy, Ibn Hajar, Adh-Dhahabiy, Ibn Al-Qattwaan, Al-Albaaniy na wengineo wamesema Hadiyth hiyo ni dhaifu.

 

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kwa maelezo zaidi:

 

Kumsomea Maiti Surat Yaasiyn Anapooshwa, Au Akishazikwa Pamoja Na Du'aa Inafaa?

 

 

Kwa hivyo, iliyo sahihi ni kumlaqinia anayekata roho maneno haya: ‘Laa Ilaaha Illa Allaah’. Na kufanya hivyo ndio kushikamana na mafunzo sahihi ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na kudhihirisha mapenzi kwake kwa kufuata yale aliyotufundisha na kuacha yale ya kutungwa na kuzuliwa.

 

Na hiyo inamfaa mtu huyo kabla hajafariki, na akishafariki yanayomfaa ni du’aa kutoka kwa Waislam, na yale mambo matatu yaliyotajwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

"Anapokufa mwanaadamu hukatika ‘amali zake isipokuwa matatu: sadaka inayoendelea, elimu inayoendelea kunufaisha au mtoto mwema anayemuombea". [An-Nasaaiy na At-Trimidhiy].

 

Ikiwa aliyefariki aliyaacha mambo hayo wakati wa uhai wake, basi yatamnufaisha huko Akhera In Shaa Allaah.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share