Mashairi 4: Ramadhani Imefika, Mola Tusamehe Dhambi
Mashairi 4: Ramadhani Imefika, Mola Tusamehe Dhambi
‘Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)
Alhamdullaah nashukuru, namshukuru Qudusi,
Kutwa tunamdhukuru, kwa wingi bila kiasi,
Apate kutunusuru, na adui ibilisi,
Ramadhani Imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Hili ni Kumi la kwanza, litapita kwa upesi,
Sote tunabembeleza, rehema Zake Mkwasi,
Dua tumeziongeza, Tunamuomba halisi,
Ramadhani imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Tusije tukateleza, kuyarudia maasi,
Mola Atatuongoza, Atutoe wasiwasi,
Mola Atupe Mwangaza, tuone kwa urahisi,
Ramadhani Imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Walokufa Warehemu, peponi Wape nafasi,
kaburini Wakirimu, upweke wasiuhisi,
Wewe Mola ni Adhimu, kwa Kusamehe Mwepesi,
Ramadhan Imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Mola ondoa magonjwa, khasa ule wa ukimwi,
Watoto kuambukizwa, kosa lao hawajuwi,
Mayatima wamekuwa, na tena hawaulizwi,
Ramadhani imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Mola ondoa ukame, Waokoe wakulima,
Mvua Usiwanyime, mazao yatasimama,
Dua zote tuzisome, leo, kesho na daima,
Ramadhani imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Waongoze wasichana, wapate kujifunika,
Hijaab ni kinga sana, wapate kusitirika,
Ni vazi lenye heshima, tena limewajibika,
Ramadhani imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Waongoze wavulana, wapate kunusurika,
Uhuni kuepukana, tabia kubadilika,
Waongoze Subhaana, dini yao kuishika,
Ramadhani imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Mola Walipe vipofu, Uwaingize peponi,
Bubu awe kwenye safu, na kiziwi masikini,
Wamesubiri pungufu, na shida zote mwilini,
Ramadhani imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Mtukufu huu mwezi, viumbe tuwe azizi,
Ni mwezi wenye malezi, na mwezi wa mazoezi,
Huku tukifanya kazi, na ibada tuienzi,
Ramadhani imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Tusamehe Mola wetu, sisi viumbe dhaifu,
Tufutie dhambi zetu, Tunakuomba Raufu,
Tusafishe kila kitu, tusibakize uchafu,
Ramadhani imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Wakati unakupita, unakimbia kwa kasi,
Wakati utakukata, kama kanga na mkasi,
Omba sana utapata, tulia na ujilisi,
Ramadhani Imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Mola Anapenda sana, Anaemuomba sana,
Kwa hivyo tuombe sana, ili Atupende sana,
Akishatupenda sana, Atatupa nyingi sana,
Ramadhani imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Hitimisha Qur-ani, ni mwezi uloteremshwa,
Uende msikitini, tarawih ikiswalishwa,
Qiyaamul-Llayl swalini, kama tulivyofundishwa,
Ramadhani imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Fanyeni mambo ya kheri, anza ndugu na jirani,
Toa sadaka kwa siri, usitaje asilani,
Ghadhabu Zake Qahari, zinapozwa kwa yakini,
Ramadhani imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Jitolee kwa futari, peleka msikitini,
Apate kula fakiri, pamoja na masikini,
Au katoka safari, mlishe huyo mgeni,
Ramadhani imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Uwaombe msamaha, wale ulowakosea,
Hapo utahisi raha, deni umeshalipia,
Epukana na karaha, viumbe kuwaonea,
Ramadhani imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Mtu akikutukana, usimjibu nyamaza,
Ukianza kugombana, saumu utapoteza,
Ni mwezi wa kupatana, subira kutekeleza,
Ramadhani imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Mola wetu na Muumba, Pokea zetu amali,
Radhi Zako tunaomba, dua zetu Zikubali,
Sote tumeshika kamba, tunaomba tunaswali,
Ramadhani Imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Nafunga shairi langu, tutazidi kuonana,
Nisameheni wenzangu, kama tumekoseana,
Atatusamehe Mola, ikiwa tumeshikana
Ramadhani Imefika, Mola Tusamehe Dhambi.