Baba Kaacha Watoto Saba Wa Kike – Je, Ndugu Za Huyo Baba Watapata Chochote?
SWALI:
Assalam nauliza swali langu ktk urithi sisi ni watoto 7 wa kike baba yetu hakujaaliwa kupata mtoto wa kiume. Jee urithi alotuachia, ndugu zake baba watarithi na kama watarithi ni asilimia ngapi. Shukran
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Mirathi.
Hakika ni kuwa maswali mengi yanayoulizwa kuhusu Mirathi huwa hayakamiliki. Kulingana na swali hili tumeelewa kuwa hao waliotajwa ndio pekee waliobaki wanaohusiana na baba yenu aliyefariki. Kwa hiyo, Aliyefariki hakuacha mke wala wazazi. Ikiwa ni hivyo, mgao wa urithi wa aliyefariki utakuwa kama ifuatavyo:
1. Dada saba (7) waliobaki watagawa sawa sawa fungu lao la thuluthi mbili (2/3). Kwa hivyo kila mmoja atapata 2/21.
2. Ndugu wa baba watagawa sehemu iliyobaki, thuluthi moja (1/3). Mgao utakuwa ndugu wa kiume anapata sehemu mbili kwa moja ya ndugu wa kike.
Na Allaah Anajua zaidi