Nani Vipenzi Vya Allaah (سبحانه وتعالى)?
Nani Vipenzi Vya Allaah (سبحانه وتعالى)?
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
أَلا إِنَّ أَوْلِيَاء اللّهِ لاَ خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلاَ هُمْ يَحْزَنُونَ ﴿٦٢﴾ الَّذِينَ آمَنُواْ وَكَانُواْ يَتَّقُونَ ﴿٦٣﴾ لَهُمُ الْبُشْرَى فِي الْحَياةِ الدُّنْيَا وَفِي الآخِرَةِ لاَ تَبْدِيلَ لِكَلِمَاتِ اللّهِ ذَلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿٦٤﴾
“Tanabahi! Hakika vipenzi wa Allaah hawana khofu juu yao, na wala hawatohuzunika. Ambao wameamini na wakawa wana taqwa. Watapata bishara katika uhai wa dunia na ya Aakhirah. Watapata bishara katika uhai wa dunia na wa Aakhirah. Hakuna mabadiliko katika Maneno ya Allaah. Huko ndiko kufuzu adhimu.” [Yuwnus: 62-64]
Aayah hizi tukufu zinataja 'Vipenzi Vya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Ni nani basi hao vipenzi Vyake Mola Mtukufu? Je, ndugu Muislamu, unamiliki sifa za kuwa ni waliyyu-Allaah? (kipenzi cha Allaah)?
Vipenzi vya Allaah ni kila aliyekuwa na sifa ya Aayah namba 63 nazo ni kuamini na kuwa na Taqwa, kwa maana kwamba wanafuata waliyoamrishwa na kujiepusha na waliyokatazwa.
Huenda ikawa ni yeyote mmoja wenu madamu tu umetimiza sifa hizo basi umeshakuwa ni 'Walii Wa Allaah', na si kama wanavyodhani watu wengine kuwa ni watu makhsusi kama masharifu na mashekhe wala si watu wa kabila makhsusi au wenye kuvaa nguo makhsusi au kuishi mahali makhsusi.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema kuwa hao 'Awliyaa-Allaah' (Vipenzi vya Allaah) hawatokuwa na khofu wala hawatohuzunika.
Kama ilivyosemwa, kwamba huenda wakawa ni waja wowote na sio watu khaswa, wala wasiwe ni Manabii au Shuhadaa kama alivyotujulisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عن أبي هريرة، رضي الله عنه، قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((إن من عباد الله عبادا يغبطهم الأنبياء والشهداء)). قيل: من هم يا رسول الله؟ لعلنا نحبهم. قال: ((هم قوم تحابوا في الله من غير أموال ولا أنساب، وجوههم نور على منابر من نور، لا يخافون إذا خاف الناس، ولا يحزنون إذا حزن الناس)). ثم قرأ: أَلا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّهِ لا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴿٦٢﴾ الطبري ورواه النسائي ورواه ابن حبان في صحيحه
Imetoka kwa Abuu Hurayrah ((Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Miongoni mwa waja wa Allaah, watakuweko wale ambao Manabii Na Shuhadaa watawadhania kuwa ni wenye bahati)). Akaulizwa "Nani hao ee Rasuli wa Allaah ili tuwapende?" Akasema: ((Hawa ni watu waliopendana kwa ajili ya Allaah bila ya sababu ya maslahi ya kifedha au undugu (ujamaa), nyuso zao zitaang'ara katika jukwaa la nuru. Hawatakuwa na khofu (siku hiyo) watakapokuwa na khofu watu wengine, wala hawatahuzunika watakapohuzunika watu wengine)). Kisha akasoma: ((Sikiliezeni! Vipenzi vya Allaah hawatakuwa na khofu (siku ya Qiyaamah) wala hawatohuzunika)) [Atw-Twabariy, Abuu Daawuwd, Ibn Hibbaan katika Swahiyh yake]
Kisha Anaendelea Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kusema:
لَهُمُ الْبُشْرَى فِي الْحَياةِ الدُّنْيَا وَفِي الآخِرَةِ لاَ تَبْدِيلَ لِكَلِمَاتِ اللّهِ ذَلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿٦٤﴾
“Watapata bishara katika uhai wa dunia na wa Aakhirah. Hakuna mabadiliko katika Maneno ya Allaah. Huko ndiko kufuzu adhimu.” [Yuwnus: 64]
Maana ya bishara njema katika maisha ya dunia na Aakhirah:
عن عبادة بن الصامت؛ أنه قرأ لرسول الله صلى الله عليه وسلم: لَهُمُ الْبُشْرَى فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الآخِرَةِ ..﴿٦٤﴾ ثم قال: فقد عرفنا بشرى الآخرة الجنة، فما بشرى الدنيا؟ قال: ((الرؤيا الصالحة يراها العبد أو تُرَى له، وهي جزء من أربعة وأربعين جزءا أو سبعين جزءا من النبوة)).
'Ubaadah Bin Swaamit alimsomea Rasuli wa Allaah Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam:(Watapata bishara katika uhai wa dunia na wa Aakhira) kisha akasema: "Tunajua bishara ya Aakhirah kuwa ni Pepo, lakini nini bishara ya dunia?" Akasema (Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ni ndoto. njema (inayotokea kweli) anayoota mja au anayooteshwa. Ndoto hii ni sehemu moja kutoka sehemu arubaini na nne au sabiini za Unabii)) [Atw-Twabariy 15:132]
Vile vile imesemwa kuwa bishara njema ni ile anayoletewa Muumini na Malaika wakati wa mauti yake. Humletea bishara njema ya Jannah na maghfirah kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلائِكَةُ أَلا تَخَافُوا وَلا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنْتُمْ تُوعَدُونَ﴿٣٠﴾ نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الآخِرَةِ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنْفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ ﴿٣١﴾ نُزُلا مِنْ غَفُورٍ رَحِيم﴿٣٢﴾
Hakika wale waliosema: “Rabb wetu ni Allaah.” Kisha wakathibitika imara; Malaika huwateremkia: (kuwaambia): Msikhofu, na wala msihuzunike, na pokeeni bishara njema ya Jannah ambayo mlikuwa mkiahidiwa. Sisi ni rafiki zenu walinzi katika uhai wa dunia na katika Aakhirah. Na mtapata humo yale yanayotamani nafsi zenu, na mtapata humo yale mtakayoomba. Ni mapokezi ya takrima kutoka kwa Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu.” [Fuswswilat: 30-32]
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atujaalie ni katika Awliyaa Wake. Aamiyn.