Ana Rafiki Wa Kiume, Mama Yake Mdogo Anamtisha Kuwa Akiolewa Naye Atamtangazia Kuwa Amezini Naye

 

Ana Rafiki Wa Kiume, Mama Yake Mdogo Anamtisha Kuwa

Akiolewa Naye Atamtangazia Kuwa Amezini Naye

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Asalam alekum warahmatulah wabarakatuh.

 

Mimi nilikuwa na boyfriend kwa muda mrefu kidogo. Mamake mdogo ambae ameshika dini sana na anaaminika katika familia yao kasema akiskia tunataka kufungua ndoa atawaambia ukoo mzima kama tumezini na atahakikisha ndoa haifungwi. Sisi tunajiamini kama hatujazini na ndoa yetu itakuwa halali lakini tunaogopa aibu ya kupakaziwa hili jambo ambalo halina ukweli wowote. Naomba ushauri wenu na In shaa Allaah Allaah atakulipeni. Tufanye nini ili tuweze kufanikisha ndoa yetu kwa misingi ya dini inavyosema kwasababu bado tunapendana sana.

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kabla hatujaingia katika swali lenyewe ambalo kwayo unajiweka katika hali ya kuonewa na mama mdogo wa rafiki yako wa kiume. Mwanzo tunataka kukukumbusha kuwa ni makosa kwa Muislamu kuwa na rafiki wa jinsia nyingine. Kwa maana hiyo, hufai wewe kama msichana Muislamu kuwa na rafiki wa kiume kwa muda mdogo hata kwa nukta moja au muda mrefu. Kuwa na rafiki ni njia ya kuingia katika zinaa hata ukisema kuwa hamjafanya chochote.

 

Allaah Aliyetukuka Anasema:

وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا ﴿٣٢﴾

Na wala msiikaribie zinaa. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya kabisa. [Al-Israa: 32].

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia kuwa kila kiungo cha miili yetu, kama macho, mikono, miguu, masikio na kadhalika kinatekeleza zinaa kwa njia moja au nyingine. Macho zinaa yake ni kutazama, masikio ni kusikia, mikono ni kushika, yote yakiwa ni ya haramu yaliyokatazwa. Kwa hivyo, jambo la kwanza ambalo unatakiwa ufanye ni kutokutana na huyo rafiki yako wala kutokutana naye kwani huko ni kupata madhambi kwako.

 

Hatujui unamaanisha nini unaposema mama yake mdogo ameshika Dini? Kushika Dini ni kufuata maagizo ya Uislamu na kuacha makatazo yake. Kulingana na maelezo yako ni wazi kuwa inawezekana kuwa mama huyo ana Dini lakini bila ya elimu ambayo ni muhimu kukuza Dini yake. Kama angekuwa kweli ameshika Dini angemsaidia mtoto wake huyo kuweza kukamilisha Dini yake kwa kuoa mke anayempenda na kumtaka. Kitu ambacho huyo anayetaka kukuoa anafaa afanye ni kuja kwa wazee wako na kukuposa rasmi ikiwa kweli anakutaka. Ikiwa anataka kukuchezea basi atabaki kuwa ni rafiki yako tu kinyume cha shari’ah bila kuja kwenu.

 

Ikiwa anakutaka kweli anatakiwa huyo mume aje kwenu na kukuposa na kukuoa bila kujali watakayosema watu. Ikiwa kweli hamjazini Allaah Aliyetukuka Atawahifadhi kabisa na maneno ya watu. Ikiwa mama huyo atafanya jambo hilo atakuwa na dhambi kubwa sana mbele ya Allaah, kwani Aliyetukuka Anasema:

 

وَالَّذِينَ يَرْمُونَ الْمُحْصَنَاتِ ثُمَّ لَمْ يَأْتُوا بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاءَ فَاجْلِدُوهُمْ ثَمَانِينَ جَلْدَةً وَلَا تَقْبَلُوا لَهُمْ شَهَادَةً أَبَدًا ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿٤﴾

Na wale wanaowasingizia wanawake watwaharifu kisha hawaleti mashahidi wanne; basi wapigeni mijeledi themanini. Na wala msipokee ushahidi wao abadani. Na hao ndio mafasiki. [An-Nuwr: 4].

 

Hii Aayah inatakiwa aonyeshwe mama huyo kuonyesha dhambi kubwa anayofanya yeye na madhara kwake hapa duniani na kesho Aakhirah. Kungekuwa na Dola ya Kiislamu basi mama huyo angehitajika kuleta mashahidi wanne, akishindwa kufanya hivyo:

 

1.     Ataadhibiwa kwa kupigwa bakora themanini.

2.     Ushahidi wao hautakubaliwa tena, mpaka watubie kweli kweli.

3.     Watakuwa ni miongoni mwa mafasiki, waliopotea njia.

 

Nasaha ambazo tunaweza kukupatia ni kama zifuatazo:

 

a.    Mtake shauri Allaah Aliyetukuka kwa kuswali Swalah ya Istikhaarah

 

b.  Je, kukataa kwa mama mdogo wa rafiki ni kwa ajili wewe hujashika Dini kama wanavyotaka? Hata kama hukushika Dini haimaanishi kuwa mama huyo anaweza kukusingizia mambo ambayo hujayafanya, hilo ni kosa kwake. Ikiwa unaona umeshika Dini inavyopasa unahitaji kuzungumza kwa mara ya mwisho na mchumba wako aweze kuzungumza na wazazi wake, wazee wengine au hata Mashaykh waweze kuzungumza na mama mdogo huyo kwa njia nzuri ili abadilishe msimamo wake kuhusu ndoa hiyo.

 

c.  Je, huyo mume anayetaka kukuoa ameshika Dini inavyopasa? Ikiwa hakushika Dini utakuja kupata shida kwani hatajua haki zako kama inavyotakiwa katika Dini. Lau hujajua kuhusu hilo jaribu kumuulizia kwa wanaomjua ili usiingie katika tatizo. Usishike msemo wa Kiswahili unaosema kuwa kipendacho moyo ni dawa.

 

d.  Taka shauri kwa wazazi wako na wazee na jamaa zako kuhusu suala hilo na utilie maanani ushauri wao.

 

Ukifanya hayo twataraji ya kwamba utapata kwa wepesi ufumbuzi wa tatizo lako hilo. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akutimizie kila jema na zuri.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share