Zingatio: Liwapi Chozi?
Zingatio: Liwapi Chozi?
Naaswir Haamid
Giza litakapotanda ndani ya kaburi lako, hakuna mwengine wa kuja kukusaidia. Upo peke yako, kule chini kabisa, chini ya ardhi, hakuna anayesikia sauti yako zaidi ya Rabb wako. Ulimkimbia sasa Amekutia Mkononi.
Ulikuwa ni chembe ya manii, Allah Akakupatia umbo zuri, sasa unaliringia na hutaki kumsujidia? Sasa ndio unalitumia sikio kwa kusikilizia miziki? Subhaana Llaah, wapi utaipata rehema za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)?
Roho itakapovutwa mfano wa zizi lisilotaka kung’oka. Malaika wamepewa amri wala hawaikaidi. Nao wataitoa roho kwa kuikomoa tena kwa nguvu. Namna ulivyomuasi Rabb wako ndivyo uchungu utakavyozidi. Je umewahi kufikiria uchungu wa maumivu wa mwanaadamu aliyechunwa ngozi yake, kisha akagaragizwa katika mchanga umoto? Hiyo ndio hali ya kutolewa roho.
كَلَّا إِذَا بَلَغَتِ التَّرَاقِيَ﴿٢٦﴾وَقِيلَ مَنْ ۜ رَاقٍ﴿٢٧﴾وَظَنَّ أَنَّهُ الْفِرَاقُ﴿٢٨﴾وَالْتَفَّتِ السَّاقُ بِالسَّاقِ﴿٢٩﴾إِلَىٰ رَبِّكَ يَوْمَئِذٍ الْمَسَاقُ﴿٣٠﴾
26. Laa, hasha! Itakapofika (roho) mafupa ya koo. 27. Na itasemwa: Ni nani wa tabibu kumponya? 28. Na atakuwa na yakini kwamba hakika hivyo ni kufariki. 29. Na utakapoambatishwa muundi kwa muundi. 30. Siku hiyo kuendeshwa ni kwa Rabb wako tu. [Al- Qiyaamah: 26-30]
Unamwita mama/baba... yuwapi kukusaidia? Unamwangalia mkeo... yuwapi kukuliwaza? Unamwita mwanao... yuwapi kukufadhili? Waite ndugu zako, rafiki, maraisi, mapolisi na wengineo, hakuna wa kukusaidia. Dakika zako za kuishi zimekwisha ndugu yangu. Pumzi na riziki zako zimeshafikia sifuri. Huna kitu tena. Leo ndio siku yako ambayo ulikuwa unaikimbia, nayo imefika kwani ahadi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni kweli.
Wapi basi unakimbilia ewe ndugu yangu Muislamu? Hiyo ndio nyumba yako ya muda ukisubiri kufufuliwa kwenda kuhisabiwa. Hakuna kwengine isipokuwa ni Moto ama Jannah. Motoni ndimo wengi wa viumbe watamalizikia. Ya Allaah tunaomba hifadhi Yako.
Wala bado mambo hayajaanza, kivumbi kipo siku ya kufufuliwa hiyo ya Qiyaamah. Iwapo wakati wa kutolewa roho ulikuwa ukitaka msaada wa ndugu, basi wakati huo ndio:
وَصَاحِبَتِهِ وَبَنِيهِ ﴿٣٦﴾ وَأُمِّهِ وَأَبِيهِ ﴿٣٥﴾ يَوْمَ يَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ أَخِيهِ ﴿٣٤﴾لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُمْ يَوْمَئِذٍ شَأْنٌ يُغْنِيهِ ﴿٣٧﴾
34. Siku mtu atakapomkimbia ndugu yake. 35. Na mama yake na baba yake. 36. Na mkewe na wanawe. 37. Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na hali ya kumtosheleza. [Abasa: 34-37]
Ni khasara iliyoje, kwa kutumia wakati katika mambo ya upuuzi na ya uzushi. Uliambiwa hichi usifanye ni haramu, ukajibu ‘ni makruhu tu, sio haramu.’ ama ‘kila mmoja na kaburi lake.’ Ukasisitizwa kutenda mema, nawe ukajibu ‘usinifuatilie wakati wangu.’
Uendapo hupajui khatari yake, bado unadhani utaishi milele hapa duniani. Wako wapi wafalme na matajiri waliosifika kutoka kila pembe ya dunia? Wako wapi wabadhirifu waliobadili maumbo yao? Hakuna mwengine wa kukusaidia zaidi ya Allaah (‘Azza wa Jalla). Kama ulimkana duniani, wala usitaraji rehema zake.
Hiyo ndio siku ambayo itakugharimu sio mabilioni wala kilo za dhahabu, bali ni amali njema. Iwapo ulimfanyia mzaha Allaah, ukamkasirisha kwa kutenda maovu, ukashirikiana na wanafiki pamoja na makafiri katika kuudidimiza Uislamu, basi utamkuta Allaah Akiwa Amekukasirikia.
Kumbuka kwamba lengo la kuishi duniani ni kumuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), sio kuanzisha vipindi vya komedi wala kuifanya runinga kuwa ndio Qur-aan. Balaa sivyo hivyo. Weka makini kabisa Aayah ifuatayo:
فَلْيَضْحَكُوا قَلِيلًا وَلْيَبْكُوا كَثِيرًا جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ﴿٨٢﴾
.Basi na wacheke kidogo (duniani), na watalia sana (Aakhirah); jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyachuma. [At-Tawbah: 82]
Rabb wetu! Hakika Wewe ni Mpole sana. Mwenye rehema mno. Rabb wetu! Tumetegemea kwako, na tumegeuka kuja Kwako, na Kwako tu ndiko marejeo (ya viumbe wote). Tuswamehe makosa yetu na utuongoze katika njia iliyonyooka.