Mashairi: Aashuraa
'Aashuraa
Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)
Natuma zangu salaamu, zivuke yote mipaka,
Ni mwezi wa Muharramu, hakika umesifika,
Huu mwezi ni adhimu, ni minne imetajika,
Aliokolewa Muusa, ni siku ya ‘Aashuraa.
Ni siku ya 'Aashuraa, ndio Muusa kaokoka,
Alipiga kwa bakora, bahari ikafunguka,
Ikawa ni barabara, wafuasi walivuka,
Aliokolewa Muusa, ni siku ya ‘Aashuraa.
Kafatwa na Firiauni, bahari ikafungika,
Na wakazama majini, wote walihalakika,
Kwa kudra zake Manani, Muusa akanusurika,
Aliokolewa Muusa, ni siku ya ‘Aashuraa.
Walifunga Mayahudi, saumu kuikumbuka,
Waliifanya ni Iddi, siku kuu kutukuka,
Na Mtume Muhammadi, habari ilimfika,
Aliokolewa Muusa, ni siku ya ‘Aashuraa.
Tufungeni siku mbili, Mtume alitaamka,
Tuwe nao mbalimbali, kwa siku kuongezeka,
Muusa kwangu ni awali, maneno yalisikika,
Aliokolewa Muusa, ni siku ya ‘Aashuraa.
Tufungeni kwa imani, madhambi yatafutika,
Tisa na kumi fungeni, tumuombe Mtukuka,
Ni siku zenye thamani, tena zilizosifika,
Aliokolewa Muusa, ni siku ya ‘Aashuraa.
Kwingine tukitazama, hakika twasikitika,
Mashia wakilalama, na maovu kufanyika,
Wanajipiga kwa vyuma, na damu kutiririka,
Aliokolewa Muusa, ni siku ya ‘Aashuraa.
Kifo cha Al-Husseini, sote tunahuzunika,
Lakini tufanye nini, Mungu Alishaandika,
Huzuni yote ya nini, ajali ilishafika,
Aliokolewa Muusa, ni siku ya ‘Aashuraa.
Kuvaa nguo nyeusi, na misiba kufanyika,
Kuwatukana matusi, Maswahaba wasifika,
Vitendo vya Iblisi, Mungu Anaghadhibika,
Aliokolewa Muusa, ni siku ya ‘Aashuraa.
Ajali iliokuja, imeshapita miaka,
Zaidi ya elfu moja, miaka imekatika,
Karbala wanakuja, na bado hawajachoka,
Aliokolewa Muusa, ni siku ya ‘Aashuraa.
Mungu Atawaongoza, wapate kuelimika,
Na sana wakichunguza, mwisho watabadilika,
Sina haja kuongeza, hapa mwisho naondoka.
Aliokolewa Muusa, ni siku ya ‘Aashuraa.