Kuna Tatizo Lolote Kishari’ah Kwa Mwanamke Kutaka Kuolewa Na Mume Ampendaye?
SWALI:
asalamu aleykum ndugu wa islamu na uliza kama kuna hadithi inayo sema ni sawa kuhongeza ikiwa mume wangu hakutaka huyo bibi wa pili lakini huyo binti alimtaka na aka sema ni yowe niwe bibi yako wa pili sababu ninakutaka na bwana yangu akamwowa je angelikata bana yangu ingelikuwa anadhabi sababu ya kumkata ataadibiwa aw anayo haki kukata bibi huyo anasistiza ili aolewe asate
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu msichana Muislamu kujipeleka kwa mume Muislamu mwenye mke ili amuoe.
Kishari’ah, Uislamu hakuna tatizo lolote kwa msichana kujipeleka kwa kumtaka mwanamme Muislamu amuoe. Kitendo kama hiko kilifanyika wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale mwanamke alipokuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili amuoe. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa hamtaki kwa kutosema kitu, Swahaba mmoja aliyekuwa yupo hapo alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa hamtaki basi amuoze yeye (al-Bukhaariy).
Ila tu katika kufanya hivyo msichana ahakikishe kuwa yule ambaye anataka aolewe naye awe ni mwenye Dini na maadili. Na baada ya hapo kuwe na posa za kawaida ya kishari’ah na kuwe na Nikaah inayotekeleza masharti yote yaliyowekwa.
Na Allaah Anajua zaidi