Janaazah: Mazishi Ya Kiislamu
Janaazah: Mazishi Ya Kiislamu
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ
Himdi ni Zake Allaah, tunamtukuza Yeye, na tunamtaka msaada Yeye na tunamuomba msamaha Yeye. Tunajilinda kwa Allaah kutokana na maovu ya nafsi zetu na udhaifu wa vitendo vyetu. Aliyeongozwa na Allaah hakuna wa kumpoteza na aliyepotezwa na Allaah hakuna wa kumuongoza. Nashuhudia kuwa hapana apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allaah na nashuhudia kuwa Muhammad ni Nabiy Wake na Rasuli Wake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلا تَمُوتُنَّ إِلا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ
Enyi walioamini! Mcheni Allaah kama ipasavyo kumcha na wala msife isipokuwa nyinyi (mmeshakuwa) ni Waislamu. [Aal-‘Imraan: 102]
Na anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)
يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالأرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا
Enyi watu! Mcheni Rabb wenu Ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi moja (Aadam) na Akaumba kutoka humo mke wake (Hawwaa) na Akaeneza kutoka hao wawili wanaume na wanawake wengi. Na mcheni Allaah Ambaye Kwake mnaombana (haki zenu kwa kuunga) undugu. Hakika Allaah ni Mwenye kuwachunga daima. [An-Nisaa: 1]
Pia amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا ﴿٧٠﴾ يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٧١﴾
Enyi walioamini! Mcheni Allaah na semeni kauli nyofu ya haki. Atakutengenezeeni ‘amali zenu, na Atakughufurieni madhambi yenu; na anayemtii Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amefanikiwa mafaniko adhimu. [Al-Ahzaab: 70-71]
Kwa hakika maneno ya kweli kabisa ni yale ya Kitabu cha Allaah, na uongozi ulio bora zaidi ni uongozi wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na maovu yaliyo mabaya zaidi ni mambo ya kuzua (yaliyo mageni katika mafundisho ya Uislaam), na kila lenye kuzushwa katika dini ni bidaa (uzushi), na kila bidaa ni upotofu na kila upotofu mwisho wake ni katika moto.
Ndugu msomaji, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:
تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿١﴾ الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلا ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ ﴿٢﴾
Amebarikika Ambaye Mkononi Mwake umo ufalme Naye juu ya kila kitu ni Muweza. Ambaye Ameumba mauti na uhai ili Akujaribuni ni nani kati yenu mwenye ‘amali nzuri zaidi. Naye ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa kughufuria. [Al-Mulk: 1-2]
Nabiy Muhammad (Swalah na salaam za Allaah iwe juu yake) amesema:
“Sikuwa mimi katika hii dunia isipokuwa ni mfano wa msafiri jangwani aliyepumzika katika kivuli cha mti, kisha akaondoka na kukiacha kivuli kile”. [Hadiyth sahihi: Al-Albaaniy, namba, 438].
Ndugu msomaji, fahamu kuwa kwa mujibu wa mafundisho sahihi ya Uislaam, maiti ana haki nne anazopaswa kutendewa, ambazo ni:
1. Kuoshwa,
2. Kuvishwa sanda,
3. Kuswaliwa, na
4. Kuzikwa.
Hii ina maana kuwa Waislamu watawajibika kuyafanya haya kwa kila maiti Muislamu na si vinginevyo. Na watakapoacha kumfanyia maiti mambo hayo watapata dhambi Waislamu wote wa sehemu ile.
Ndugu msomaji, tunafahamu kuwa una hamu kubwa ya kuyajua kiundani mambo manne tuliyoyataja hapo juu. Shaka ondoa, makala hii iliyo mikononi mwako itakuonesha hayo kadiri utakapozidi kufungua kurasa zake.
Awali ya yote tunapenda kukujulisha itikadi ya Uislaam kuhusu maisha na uhai huu wa dunia.
Ndugu msomaji, Waislamu wanaitakidi kuwa, kila kilichopo katika dunia kitaondoka (kitakufa). Na hii ni kutokana na kauli ya Allaah Aliposema:
كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ
Kila aliyekuwa juu yake (ardhi) ni mwenye kutoweka. [Ar-Rahmaan: 26]
Kama ilivyozoeleka kuwa hakuna mwanzo usiokuwa na mwisho, wala hakuna mchana usiokuwa na usiku, kadhalika hakuna uhai usiokuwa na mauti. Allaah Anasema:
كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ
Kila nafsi itaonja mauti! [Al-Anbiyaa: 35]
Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameweka wazi katika Hadiyth tuliyoitanguliza hapo nyuma.
Ndugu msomaji, waweza kujiuliza kuwa umauti ni nini?
Nasi kwa kulifahamu hilo tuna haki ya kukufafanulia kama ifuatavyo:
Umauti ni mtengano au mfarakano kati ya mwili na roho ya kila kiumbe hai, kama mwanadamu, wanyama, majini n.k. Hapo huwa ndio mwisho wa kazi ya kila kiungo cha aliyekufa; macho, mdomo, sikio, mikono, mguu na mfano wake.
Si kama wanavyodai baadhi ya wasiokuwa na ufahamu sahihi na wasio na akili zenye kuwatosha kuwa eti kuna baadhi ya watu ambao huwa wanakufa baadhi ya viungo na baadhi havifi. Huu ni uongo wa wazi kabisa na kila mtu aliye na akili timamu atampa msemaji wa maneno haya moja kati ya sifa tatu zifuatazo:
1. Mjinga,
2. Punguani, hajui alisemalo,
3. Ni mtu aliyeamua kuifanya nafsi yake kuwa pumbavu, mfano wake ni
kama mtu anayedai mchana kuwa usiku na usiku kuwa mchana.
Haiingii akilini kabisa kuwa mtu afe halafu mguu wake usife au mkono wake au macho yake yasife au tupu yake isife. Hii haihitaji Aayah, Hadiyth, wala elimu kubwa wala muujiza, kwani akili inamtosha mwenye nazo na akazitumia. Ama yule asiyekuwa na akili basi Aayah, Hadiyth wala elimu yoyote pia haitamfaa.
Ndugu msomaji, katika hili tunaomba mchango wako wa kiakili na kujiuliza kuwa, Je, inawezekana kweli mtu afe baadhi na baadhi abaki kuwa hai halafu aitwe maiti? Jawabu liwe akilini mwako.
Mpendwa msomaji, baada ya kupata jawabu, sasa nikueleze yale mambo manne anayopaswa kufanyiwa maiti wa Kiislamu.
Jambo La Kwanza Ni Kuosha
Waislamu wanaosha maiti kwa sababu hayo ni mafundisho ya dini, na ni shari’ah.
Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha hayo katika Hadiyth ya Swahaba (mfuasi wa karibu) mtukufu Ibnu ‘Abbaas (Radhwi ya Allaah ziwe juu yake) katika kitabu cha [Imam Al-Bukhaariy na Muslim] kama alivyoeleza Shaykh Al-Albaaniy katika kitabu chake Ahkaamul Janaaiz, na Abuu Nu’am katika al-Mustakhraj Hadiyth namba, 139-140:
Maana ya Hadiyth:
“Siku moja mtu mmoja alikuwa amesimama ‘Arafah, ghafla mtu huyo akaanguka kutoka katika mnyama wake na yule mnyama akamkanyaga na kufa papo hapo. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Muosheni kwa maji na majani ya mkunazi na mumvishe sanda…”
Hivyo basi kwa mujibu wa mafundisho ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Waislamu wanawajibika kuosha maiti yao pale linapowezekana, kwa sababu hayo ndiyo mafundisho ya dini yao na si vinginevyo, wala si kama wasemavyo wenye chuki dhidi ya Uislaam kuwa eti Waislamu wanaosha maiti kwa sababu huenda ina janaba (yaani ilizini).
Swali la kujiuliza, Je ni kitabu gani kinachozungumzia hayo? Jibu ni hakuna ushahidi juu ya hayo katika kitabu chochote au mafunzo yoyote ya Uislaam wala hakuna ushahidi wowote wa kimazingira. Unaweza kujiuliza, kwa nini basi wanasema wasiyo na ushahidi nayo? Jibu linaloweza kupatikana ni moja tu, nalo ni chuki dhidi ya Uislaam.
Ndugu msomaji, ukweli ulio wazi ni kuwa chuki dhidi ya Uislaam imewapelekea watu (maadui) kuuzungumzia Uislaam na kuuzushia mambo ambayo hayapo na hayana ushahidi wowote. Muradi wao ni kuupiga vita Uislaam katika hali yoyote ile iwayo, na hili Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amelitanabahisha katika Qur-aan, Aliposema:
ولا يَزَالُونَ يُقَاتِلُونَكُمْ حَتَّىٰ يَرُدُّوكُمْ عَن دِينِكُمْ
Na wala hawatoacha kukupigeni vita mpaka wakutoeni katika Dini yenu wakiweza. [Al-Baqrah: 217]
Ndugu msomaji, suala la zinaa limekatazwa katika Qur-aan kuanzia katika hatua zake za mwanzo. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amesema:
وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَا ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا
Na wala msiikaribie zinaa. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya kabisa. [Al-Israa: 32]
Haifai kumtazama mwanamke kwa matamanio, imekatazwa pia kupeana mikono na mwanamke au mwanamume ambaye si ndugu yako wa karibu, si hilo tu, Uislaam hauruhusu wanaume kuchanganyika na wanawake katika hali yoyote ile. Kama hilo halitoshi, mwanamke katika Uislaam anatakiwa avae hijabu, vazi lisilo bana mwili wala lisilovutia na linalofunika mwili mzima. Katika hali hii na kwa mazingira haya, iweje Muislamu azini? Hapo ndipo utagundua kuwa aliyesema haya ima alitoka usingizini au hatumii akili.
Ndugu msomaji, fahamu kuwa hakuna mfumo au utaratibu wa maisha wenye kumuhimiza na kumuhitaji mtu kuwa mbali na zinaa kama utaratibu wa Kiislamu. Ndio maana Uislaam ukahimiza kuoa na ukakemea vikali uhuni na ukapera (kuto oa). Tunakushauri ndugu msomaji, uusome Uislaam, na hii ndio njia pekee ya kuujua ukweli, badala ya kusikiliza maneno ya watu wenye chuki na uadui dhidi ya Uislaam, ambao wengine wanadai kuujua Uislaam lakini kiukweli ni kuwa wanachotafuta ni kuwadanganya wasiokuwa Waislamu ili kupata muradi wao wa siku.
Namna Ya Kuosha Maiti
Ni nani mwenye haki zaidi ya kumuosha maiti? Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, mwenye haki zaidi ya kumuosha maiti ni yule mwenye ufahamu sahihi juu ya utaratibu wa kuosha maiti na Sunnah[1] zake, na hasa akiwa ni katika jamaa zake kama vile, mkewe/mumewe, mwanawe n.k.
Waoshaji huwa ni wawili au watatu kulingana na hali halisi. Watu hawa hawana majina maalum kishari’ah, kama wanavyodai baadhi ya watu kuwa eti kuna kiguzo, kigingi, na mshika kata; huu ni uzushi. Vitabu vinaonesha kuwa, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alioshwa na ‘Aliy akisaidiwa na Al-Fadhlu ibnu ‘Abbaas na Usaamah bin Zayd (Radhwi ya Allaah ziwe juu yao), wala hawakupewa majina maalumu. Haya yameelezwa na Abuu Daawuud kwa mapokezi sahihi juzuu ya pili (2) ukurasa wa 69.
Hatua Ya Kwanza:
Maiti itavuliwa nguo kwa upole na kufunikwa shuka ndefu baada ya kumfumba macho kama ilivyopokewa na Imaam Muslim, Ahmad na Al-Bayhaqiy kitabu cha tatu (3) ukurasa wa 334 na kama alivyoeleza Shaykh al-Albaaniy katika Ahkaamul Janaaiz ukurasa wa 12 katika Hadiyth ya Ummu-Salamah amesema:
“Aliingia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Abu-Salama akamkuta macho yake yapo wazi akamfumba, kisha akasema “hakika roho inapotolewa macho huifuata iendapo..”
Huu ni uthibitisho wa mwongozo sahihi wa Uislaam katika kumuosha maiti, si kama wanavyodai maadui wa Uislaam.
Hatua Ya Pili:
Baada ya kuvuliwa nguo, haraka iwezekananvyo, maiti itaoshwa. Yataandaliwa maji ambayo yatakuwa yamechanganywa na majani ya mkunazi[2] na kaafuur. Maji si lazima yawe ya moto, ila ikiwa kuna baridi kali maji yawe ya uvuguvugu. Atakayesema kuwa maji lazima yawe ya moto, huyo ni muongo kwani haya yameelezwa katika vitabu vya kishaafi’iy kama kitabu cha shekhe ‘Abdullaah bin Abdir-Rahmaan al-Hadharamiy (850-918) ukurasa wa 48 hadi 49, katika mlango wa Al-Janaaiz.
Maiti ataoshwa majosho matatu au matano kulingana na hali halisi ya maiti huyo. Hii ni kutokana na Hadiyth iliyosimuliwa na Ummu ‘Atwiyah kuwa:
“Aliingia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati tukiwa tunamuosha binti yake, Zaynab, akasema: Muosheni mara tatu au mara tano au mara saba au zaidi ya hapo ikiwa mtaona haja ya kufanya hivyo..”[3]
Ikiwa maiti ni wa kiume, nywele zake zitaachwa kama zilivyo ila zitaoshwa vizuri na wala hakitakatwa chochote kwenye mwili wake, si nywele wala kucha. Na ikiwa maiti ni wa kike, nywele zake zitafumuliwa ikiwa zimesukwa, kisha zitaoshwa, halafu zitasukwa tena njia tatu zikielekezwa kisogoni mwake. Na hii ni kutokana na Hadiyth iliyosimuliwa na Ummu ‘Atwiyah.[4]
Hatua Ya Tatu:
Ndugu msomaji, muoshaji atafunga kitambaa au atavaa kitu chochote mkononi mfano wa glovu, kisha ataosha sehemu za siri za maiti, baada ya kumpapasa tumboni kwa taratibu, ili kuondoa uchafu ulio karibu kutoka. Muoshaji atayafanya hayo bila kuangalia uchi wa maiti. Ni uzushi na ni uongo mkubwa kudai kuwa maiti wa Kiislamu hukamuliwa kwa Nguvu tumboni, kwani kufanya hivyo ni kinyume na mafundisho sahihi ya Uislaam.
Muoshaji atatupa kitambaa cha kwanza, kisha atachukua kingine na kuanza kusafisha meno ya maiti, baada ya kulowanisha kitambaa hicho kwa maji. Baada ya hapo, muoshaji na msaidizi wake watamtawadhisha[5] maiti, Wudhuu kamili. Watayafanya hayo yote kwa kuanzia kuliani kwa maiti na kumalizia kushotoni kwa maiti. Kwa mfano, wataosha mkono wa kulia halafu wa kushoto na mfano wa hayo.
Ndugu msomaji, fahamu kuwa maiti haitaingizwa maji mdomoni au masikioni au popote pale kwani hakuna ushahidi wowote juu ya hilo katika mafundisho ya Uislaam. Yeyote atakayeleta madai ya namna hii una haki ya kumtaka atoe ushahidi juu ya hilo.
Baada ya kutawadhishwa, maiti ataoshwa mwili wote mara tatu, tano, saba au zaidi ya hapo, kama tulivyoelezea hapo nyuma. Atamwagiwa maji upande wa kulia, kisha upande wa kushoto na kuoshwa vizuri kabisa. Na iliyo bora ni kuchanganya maji ya kuoshea kwa majani ya mkunazi kama tulivyokwisha elezea hapo awali katika Hadiyth ya Ummu ‘Atwiyah. Lililo bora katika osho la mwisho ni kuchanganya maji na kaafuur. Hii ni aina ya manukato yanayowekwa kwenye maji.
Kufikia hapa ndugu msomaji, tunataraji utakuwa umefahamu usahihi wa kuosha maiti, japo kwa ufupi.
Pamoja na hayo, ndugu msomaji, una haki ya kufahamu mambo yafuatayo:
Hataoshwa maiti aliyekufa shahidi,[6] bali atazikwa na nguo zake hizohizo. Hii ni kutokana na dalili nyingi, miongoni mwazo ni ile Hadiyth ya Jaabir (Radhwi za Allaah ziwe juu yake) pale Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema kuwaelekeza katika kuwazika Swahaba[7] waliofariki katika vita ya Uhudi kuwa, “Wazikeni na damu zao..”[8]
Fahamu pia kuwa, aliyekufa hali ya kuwa amehirimia (ameshakuwa tayari na amekusudia) kufanya hija, mtu huyo naye hatapakwa manukato wala hatafunikwa kichwa chake.
Ikiwa maiti itaharabika kutokana na namna ya kifo chake, kama vile kutokana na ajali ya gari, kuungua moto, kuangukiwa na nyumba, n.k, basi maiti huyo atatayamamishwa (yaani badala ya kutumika maji utatumika udongo ulio safi na twahara), na kama itashindikana basi, uwajibu (ulazima) wa kufanya hivyo utaondoka. Allaah, Mtukufu, anasema katika Suwrah Al-Baqarah: 286
لا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلا وُسْعَهَا
“Allaah Hakalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya uwezo wake. …” [Al-Baqarah: 286]
Pia Wanachuoni wa kanuni za Fiqh (Usuul al-Fiqhi) wana msemo usemao:
“Hakuna uwajibu endapo hauwezekani (hautekelezeki)…” (La waajiba ma’al ‘ajzi). Na Allaah ni Mjuzi zaidi.
Hutokea baadhi ya nyakati kuwa, mathalani, mtu kafariki na baadhi ya viungo vyake, kama mikono au mguu, vimekosekana. Na maiti huyu ameoshwa, kaswaliwa, na hatimaye kuzikwa akiwa hana viungo vyote. Mara tu baada ya kuzikwa kikaonekana kiungo au baadhi ya viungo vilivyokosekana, Je, kiungo au viungo hivyo vitaoshwa na kuswaliwa? Ndugu msomaji, suala hili aliwahi kuulizwa Shaykh Muhammad bin Swaalih Al-‘Uthaymiyn[9] (Allaah Amrehemu), akajibu:
“Viungo vidogo vidogo kama mikono na miguu vitakapopatikana na maiti ameshaswaliwa, viungo hivi havitaoshwa wala kuswaliwa kwa kuwa ameshaswaliwa.”
Akaendelea kusema:
“Ama itakapokuwa maiti haikupatikana bali kimepatikana kiungo katika mwili wake kama vile kichwa au mguu au mkono, basi kitaswaliwa na kuzikwa kilichopatikana baada ya kuoshwa vizuri na kuvishwa sanda[10].
Mpaka hapa tuna imani kuwa tumeondoa kiu yako juu ya moja kati ya mambo mane anayopaswa kufanyiwa maiti. Hatua inayofuata baada ya hii ni kuvishwa sanda.
Kuvishwa Sanda
Baada ya maiti kuoshwa vizuri, hatua inayofuata ni kuvishwa sanda, nguo au shuka ndefu yenye uwezo wa kufunika mwili wote wa maiti. Ni bora zaidi na inapendeza shuka hiyo ikiwa nyeupe. Na hii ni kutokana na Hadiyth sahihi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)aliposema:
”Pendeleeni kuvaa mavazi meupe kwani hayo ni katika mavazi bora kwenu na mukafini (muwavishe) maiti wenu kwa hizo sanda”.[11]
Sanda huwa ni shuka tatu (3) tu, na si zaidi, kutokana na Hadiyth iliyosimuliwa na mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwi ya Allaah ziwe juu yake) aliyesema:
“Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)alikafiniwa (alivishwa sanda) katika nguo tatu..”[12]
Ndugu msomaji, hakuna tofauti kati ya sanda ya maiti mume na sanda ya maiti mke, na hii ni kutokana na kukosekana ushahidi sahihi juu ya hilo, na kama upo, basi ni Hadiyth ambazo hazikusihi upokezi (sanadi) wake. Mfano wa Hadiyth dhaifu inayotumiwa na baadhi ya watu ni Hadiyth ya Layla bint Qaaif Ath-Thaqafiy inayoeleza kuwa sanda ya kike ni nguo tano zikiwa shuka mbili, kikoi, kanzu, na kilemba. Hadiyth hii upokezi (isnadi) yake ni dhaifu. Ndani ya msururu wa wapokezi (isnadi) kuna mtu mmoja, anaitwa Nuuh bin Haakim Ath-Thaqafiy, ambaye hajulikani zaidi ya jina lake tu, kama alivyoelezea al-Haafidh bin Hajar na wengineo.[13]
Uandaaji Wa Sanda
Shuka hizo kwa ajili ya sanda zitatandikwa sehemu safi. Kisha zitafukizwa udi na manukato mazuri mara tatu, kama alivyoelekeza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Mtakapoweka manukato ya maiti basi wekeni mara tatu.”[14] Isipokuwa sanda ya aliyehirimia kufanya hija haitapakwa manukato wala haitafukizwa udi.”
Hii imeesimuliwa na Ibn ‘Abbaas (Radhwi ya Allaah ziwe juu yake) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“…Msimpake manukato wala msimfunike kichwa chake kwani huyo atafufuliwa siku ya kiama hali ya kuwa analeta talbiya”[15] [Al-Bukhaariy na Muslim].
Baada ya kutandikwa sanda, maiti atalazwa juu yake. Itachukuliwa ncha ya upande wa kulia na iletwe hadi kifuani mwake, na ncha ya kushoto itafanywa hivyo hivyo. Utaratibu huo utafuatwa kwa shuka ya pili na ya tatu. Kisha itachukuliwa kuanzia kichwani na itafungwa na miguuni pia itafungwa. Pia itawekwa pamba iliyolowanishwa manukato mazuri na itawekwa juu ya macho yake na mdomoni mwake kama alivyoelekeza Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn. Mpaka hapa, maiti itakuwa tayari kwa ajili ya kutekelezewa jambo la tatu ambalo ni kuswaliwa.
Kumswalia Maiti
Ndugu msomaji, ni wajibu kumswalia kila maiti wa Kiislamu isipokuwa hawa wafuatao:
1. Mtoto mdogo ambaye hajafikia kubalehe. Na hii tunaipata katika Hadiyth iliyosimuliwa na bi Aaisha (Radhwi ya Allaah ziwe juu yake) kuwa:
“Alikufa Ibraahim mtoto wa Rasuli wa Allaah na hali ya kuwa ana miezi minane na Nabiy hakumswalia.”[16]
2. Mtu aliyekufa shahidi (aliyekufa vitani) kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwaswalia waliokufa katika vita vya Uhud.
Ndugu msomaji, fahamu kuwa tunaposema kuwa si wajibu kuwaswalia watu wa aina hii hatuna maana kuwa ni haraam kuwaswalia, bali tunamaanisha kuwa hakuna ulazima au uwajibu wa hilo. Lakini wakiswaliwa inafaa kwa kuwa kuna ushahidi juu ya hilo kama alivyosimulia ‘Aaishah, mama wa waumini, anayesimulia:
“Aliletwa mtoto kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) miongoni mwa watoto wa answaar (watu wa Madiynah) na Nabiy akamswalia”.[17]
Ndugu msomaji, ni matarajio yetu kuwa utangulizi huu utakuwa ni mwanzo wa kuifahamu vizuri Swalah ya Jeneza.
Namna Ya Kumswalia Maiti
Maiti huswaliwa kwa kufuata utaratibu huu:
Atasimama Imaam (kiongozi wa Swalah) upande wa kichwa, kama maiti ni mwanaume, na hii imethibiti katika Hadiyth ya Abu Ghaalibi al-Khayyaat, amesema:
“Nimemshuhudia Anas bin Maalik akiswalia maiti ya kiume akasimama usawa wa kichwa chake.”
Pia Imaam atasimama usawa wa katikati wa ikiwa maiti ni mwanamke, kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Samurah bin Jundub, anasema:
“Nimeswali nyuma ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye akimswalia mama wa Ka’ab…akasimama katikati yake.”
Kisha, Imaam ataleta takbira kwa kusema, ‘Allaahu Akbar’, (Allaah ni mkubwa) mara nne au tano au tisa, kwani aina zote hizi zimethibiti kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Lakini mara nyingi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alileta takbira nne (4).
Katika takbira ya kwanza, itasomwa suratul-Faatihah, baada ya kumlaani Shaytwaan, bila kudhihirisha sauti.
Katika takbira ya pili, itasomwa Swalah ya Nabiy kwa ukamilifu wake.
اَللّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى اِبْرَاهِيمَ وَعَلَى آلِ اِبْرَاهِيمَ و بارك على محمدٍ وعلى آلِ محمدٍ كما باركتَ على إِبراهيم وعلى آلِ إبراهيمَ إِنَّكَ حَميدٌ مَجيد
Katika takbira ya tatu itasomwa du’aa ya kumuombea maiti, nazo ni nyingi zilizothibiti kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Katika takbira ya nne, ambayo ni ya mwisho, itasomwa du’aa yoyote au atanyamaza (anayeswali) na kisha atatoa salamu. Namna zote hizi mbili zimethibiti.[18]
Ndugu msomaji, ni muhimu ufahamu kuwa kuna nyakati tatu muhimu ambazo haifai kuswali ndani yake ila kwa dharura. Nyakati hizo zimebainishwa katika Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir (Radhwi ya Allaah ziwe juu yake) anayesimulia:
“Alikuwa Nabiy (Rehma na amani za Allaah iwe juu yake) anatukataza kuswalia au kuzika maiti katika nyakati tatu:
Kwanza - wakati wa kuchomoza jua mpaka linyanyuke juu,
Pili – wakati anaamka aliyelala qayluulah (yaani saa 6:00 mchana wakati jua linapokuwa utosini au katikati mpaka lihame kuelekea upande wa Magharibi).
Tatu – wakati jua linapokaribia kuzama mpaka lizame kabisa.”[19]
NB: Suala hili lina mitazamo tofauti miongoni mwa wanachuoni wa Ahlus Sunnah wal-Jama’ah[20] juu ya kufaa kuswalia jeneza na kuzika katika nyakati hizi. Lakini wengi kati yao wanaliona hilo halipendezi kishari’ah (makruhu) nao ni kama vile ‘Atwaa, An-Nakha’iy, Al-Awza’iy, Ahmad, Is-haaq, na Ath-Thawriy. Ash-Shaafi’iy yeye anaona kuswalia wakati wowote na kuzikwa inafaa[21].Kauli ya jamaa (ya kwanza) ni bora kwa kuwa imeafikiana na Hadiyth.
Kuzikwa
Jambo la nne analopaswa kutekelezewa maiti ni kuzikwa. Kaburi ni lazima liwe refu kwenda chini na liwe pana. Kina cha kaburi kiwe sawa na kimo cha mtu mzima na kunyoosha mkono, na litachimbwa kiasi maiti akilazwa kwa ubavu wa kulia atakuwa anaelekea Qiblah.[22]
Kaburi likiwa tayari, maiti atachukuliwa katika jeneza na kuwahishwa katika kaburi. Wakati wa kusindikiza jeneza (kumpeleka maiti kaburini), mambo yafuatayo yanapaswa kuchungwa:
Kwanza, lisifuatwe jeneza kwa sauti wala kwa moto. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hadiyth iliyosimuliwa na Abu Hurayrah:
“Msifuate jeneza kwa sauti wala kwa moto.”[23]
Hapa inamaanisha sauti yoyote ya mwanadamu. Pia haifai kubeba chetezo cha ubani chenye moto wakati wa kusindikiza jeneza.
Pili, jeneza lisifunikwe na chochote. Kufunika jeneza au kaburi wakati wa kuzika ni miongoni mwa mambo yasiyokuwa na ushahidi[24]. Baada ya maiti kuwasilishwa kaburini, watatakiwa watu baadhi washuke ndani ya kaburi, na iliyo bora zaidi ni kuwa watakaoingia ndani ya kaburi wawe ndugu wa aliyefariki.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:
وَأُولُو الأرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ
Na ndugu wa uhusiano wa damu wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe (kwa kurithiana), katika shariy’ah ya Allaah. Hakika Allaah ni Mjuzi wa kila kitu. [Al-Anfaal: 75]
Maiti atalazwa kama tulivyoelezea katika uandaaji wa kaburi, huku wakisema wanaomlaza maiti kwenye mwana-ndani:
“Kwa jina la Allaah na juu ya mila ya Rasuli wa Allaah” au “Kwa jina la Allaah na juu ya Sunnah ya Rasuli wa Allaah.” Haya yamethibiti kwa riwaya zote.
Wanaotakiwa kuyasema maneno haya ni wale wanaomuweka maiti katika mwanandani (sehemu ndogo inayochimbwa ndani ya kaburi kwa ajili ya kumlaza maiti kwa ubavu wake wa kulia) na sio walio juu ya kaburi. Haya yameelekezwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyosimuliwa na Swahaba mtukufu Al-Bayadhi kuwa:
“Maiti anapolazwa katika kaburi basi aseme yule anayemuweka katika kaburi wakati wa kumuingiza katika mwanandani; Kwa jina la Allaah na kwa ajili ya Allaah na juu/kwa kufuata mila ya Rasuli wa Allaah.”[25]
Baada ya maiti kulazwa katika mwanandani, kaburi litafukiwa na mwisho litainuliwa kiasi cha shibri[26] moja tu. Na hili linathibitika kutokana na Hadiyth ya Jaabir (Radhwi ya Allaah ziwe juu yake) amesema:
“Kwa hakika Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwekwa katika lahdi (mwanandani) na yakawekwa nyuma yake matofali na likanyanyuliwa kaburi lake kiasi cha shibri moja.”[27]
Kujengea Kaburi
Kwa taratibu na mafunzo sahihi ya Kiislamu, kaburi halitajengewa. Haikupata kuonekana zama za Nabiy (Swalah na salaam za Allaah iwe juu yake) kaburi likajengewa na yeye akiwa hai, bali alionekana na kusikika kwa kinywa chake akilikemea vikali suala hili. Dalili juu ya hili zipo nyingi, mojawapo ni Hadiyth hii ambayo ameisimulia Abuu Ya’ala akisema,
“Amekataza Rasuli wa Allaah kujengwa juu ya kaburi na kukaa au kukanyaga juu yake na kuswali kwa kuyaelekea makaburi.”[28]
Ndugu msomaji, jua ya kwamba makaburi ya Baqiy (sehemu walikozikwa Waislamu wa mwanzo, Swahaba) mpaka sasa yapo na Waislamu wanaendelea kuzikwa katika eneo hilo. Waliojaaliwa kwenda Hijja ni mashahidi kwani huwa wengi wanayazuru makaburi haya na hayajajengewa. Suala la kujiuliza ni Je, kama makaburi hayo yangekuwa yanajengwa ingewezekana leo kuwepo eneo la kuzikia hadi sasa? Hasa ukizingatia kuwa kutoka Nabiy (Juu yake Swalah na salaam za Allaah) alipokufa mpaka sasa ni zaidi ya miaka 1400 imeshapita? Ni wazi kuwa kusingekuwa na nafasi tena ya kuzikia.
Kwa msingi huu tunatumia fursa hii kumuusia kila asomaye Makala haya kuwa maiti hanufaiki na na wala hana haja na vitu vya duniani, si vigae, marumaru, wala jengo la aina yoyote katika kaburi, bali anachohitaji zaidi maiti ni du’aa yako. Mkumbuke, kisha muombee msamaha kwa Allaah Ampunguzie adhabu za kaburi bila kutumia utaratibu maalum, hapo utakuwa umemfanyia jambo kubwa sana.
Kutokana na Hadiyth tuliyoinukuu punde tunajifunza mambo kadhaa ambayo huwa tunayafanya bila kujua ubaya wake. Mfano wa hayo ni kama kukalia na/au kukanyaga makaburi. Haya tunayashuhudia wakati maiti anapofikishwa katika eneo la makaburi, watu husimama juu ya makaburi na wengine huyakalia. Hili ni suala la kuwa makini nalo na kujichunga wakati tukiingia makaburini tusiyakanyage wala kuyakalia.
Kuzika Maiti Msikitini
Ndugu msomaji, miongoni mwa makatazo ni kuzika maiti Misikitini. Imekuwa kasumba ya baadhi ya watu kuacha wasia kuwa wakifa wazikwe Misikitini kwa kuwa pengine wao ndiwo waliotoa maeneo yaliyojengwa Misikiti hiyo au vinginevyo. Hii inawapelekea watu kuswali kwa kuyaelekea makaburi, jambo ambalo limekatazwa na shari’ah ya Kiislamu. Jambo hili limekuwa ni fitna kubwa miongoni mwa Waislamu kwani miongoni mwa madhara makubwa yatokanayo na jambo hili ni kwa watu kuanza kuomba na kufanya tawassul (kumuomba Rabb kupitia makaburi hayo) na hatimaye kuabudiwa kabisa makaburi hayo. Haya ni masikitiko makubwa.
Aliulizwa mmoja wa wanachuoni, Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn kuwa ni ipi hukumu ya Swalah kwenye Msikiti wenye kaburi?
Akajibu akasema:
“Ikiwa kaburi limeutangulia Msikiti (yaani kaburi lilikuwepo kabla Msikiti haujajengwa) basi ni wajibu kuuhama Msikiti huo na ubomolewe na liachwe kaburi. Na kama Msikiti umelitangulia kaburi basi ni wajibu kufukuliwa (kuhamishwa) kaburi hilo na maiti akazikwe makaburini.”
Pia Shaykhul Islaam amesema:
“Wala haitaswihi (haitafaa) Swalah kwenye makaburi au kwa kuyaelekea makaburi, na katazo hili ni kwa kuziba mianya ya shirki”[29]
Kuhusu Kaburi La Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
Maswali huja kuwa mbona kaburi la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) liko ndani ya Msikiti na limejengewa? Katika kulifafanua hili inahitajika kwa wewe msomaji kuzingatia kwa umakini, kwani jambo hili linatatiza wengi katika watu.
Historia inaonesha kuwa Msikiti wa Madiynah haukujengwa juu ya kaburi lolote kwani Msikiti ulijengwa mwaka wa kwanza wa Hijrah (mwaka wa Kiislamu) na wakati huo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa hai.
Pia haikushuhudiwa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kumzika yeyote katika Swahaba zake katika Msikiti.
Tatu, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuzikwa ndani ya Msikiti, na yeye mwenyewe alikemea hilo la kuzika watu Misikitini kwa kusema katika Hadiyth iliyosimuliwa na ibn Mas’uud (Allaah amuwie radhi) kuwa,
“Hakika miongoni mwa viumbe waovu ni wale ambao kitafika Qiyamah hali ya kuwa wapo hai na wale ambao wameyaweka makaburi Misikitini (wamezika watu ndani ya Misikiti).”[30]
Swahaba ni mfano bora wa kuigwa kwani wao waliyazingatia vilivyo na kuyafanyia kazi maneno na mafunzo ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kiasi waliweza kufikia kutoa mali zao na nafsi zao kwa ajili yake. Unaweza kujiuliza, inawezekana kweli watu hawa (Swahaba) wakakiuka maelekezo ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hatimaye wamzike Msikitini? Kama hawakumzika Msikitini, je ni nani aliyeliingiza kaburi la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Msikitini, na wapi lilikuwa kabla?
Jawabu ni kuwa aliyeliingiza Msikitini kaburi la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ‘Umar bin Abdil-‘Aziyz kwa amri ya mtawala wa zama hizo aitwaye Al-Waliyd bin ‘Abdil-Malik katika mwaka wa 88 H.
Inafahamika kuwa nyumba ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa inapakana na Msikiti kwa kutengwa na ukuta mmoja upande wa kushoto na hasa chumba cha Bibi ‘Aaishah (Allaah awe radhi naye) ambacho ndiko alikozikwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), pamoja na Swahaba zake wawili, Abu Bakr na ‘Umar (Allaah awawie radhi wote wawili). Baada ya Msikiti kupanuliwa, makaburi hayo yakaingizwa Msikitini, na hii ni kwa sababu Al-Waliyd bin ‘Abd-l-Malik alikuwa hana elimu juu ya hilo. Baadhi ya wafuasi wa Swahaba (Taabi’iyn) walipojaribu kulipinga hilo walionekana hawana kauli. Miongoni mwao ni Sa’iyd bin al-Musayyib, yeye alijaribu kushauri kuwa basi chumba cha Bibi ‘Aaishah (Allaah awe radhwi naye) (Mke Wa Nabiy), ambako alizikwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kisiingizwe ndani ya Msikiti, bila mafanikio. Kwa kuwa Al-Waliyd alikuwa ndiye mwenye mamlaka, akamlazimisha ‘Umar bin ‘Abdil-Aziyz kubomoa ukuta uliokuwa unatenganisha makaburi hayo na Msikiti na kwa hiyo makaburi yakajumuishwa ndani ya Msikiti. Kwa ufafanuzi huu mfupi, ni wazi kuwa hakuna hoja ya kudai kuwa inafaa kuzika au kujengea makaburi.[31]
Kuwekea Alama Makaburi
Je, ni namna gani unaweza kulitambua kaburi au kuliwekea alama kaburi? Hilo linajibiwa katika Hadiyth iliyosimuliwa na Swahaba mtukufu Al-Mutwallib bin Abi Wadaa (Allaah amuwie radhi) kuwa, pindi alipokufa ‘Uthmaan bin Madh’uun, ndugu wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kunyonya ziwa moja, baada ya kumaliza kufukia kaburi, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alibeba jiwe na akaliweka upande wa kichwani kisha akasema,
“Nimeliweka jiwe hili ili nipate kulijua kaburi la ndugu yangu na nizike pembeni yake atakayekufa katika jamaa zangu”[32]
Baada Ya Kuzika
Ndugu msomaji, kinachofuatia baada ya kufunika kaburi ni kumuombea maiti kimya kimya, kama alivyofanya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ya Al-Baraa bin ‘Aazib iliyopokelewa na Jama’ah.[33]
Fahamu kuwa hakuna kitu kinachoitwa talaqini baada ya maziko, kwani mapokezi juu ya jambo hilo ni dhaifu na hayakusihi kabisa. Hadiyth inayozungumzia talaqini ni dhaifu na haifai kuitumia katika hoja, na yeyote anayefanya talaqini anahesabika kuwa ni mzushi[34].
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Alikuwa Akifanya Nini Alipomaliza Kuzika?
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akishamaliza kuzika (yaani baada ya kufukia kaburi) alikuwa akisimama na kisha husema maneno haya:
“Muombeeni msamaha ndugu yenu na mumuombee uthabiti, kwani hakika sasa hivi anaulizwa maswali”[35] kama ilivyokuja katika Hadiyth ya ‘Uthmaan bin ‘Affaan.
Pia ifahamike kuwa, haifai kwa Muislamu kuzikwa katika makaburi ya wasiokuwa Waislamu, wala wasiokuwa Waislamu kuzikwa katika makaburi ya Waislamu[36].
Kufikia hapa mpendwa msomaji, tunataraji kuwa, kwa mapenzi ya Allaah, utakuwa umefahamu, japo kwa ufupi, ukweli kuhusu mazishi sahihi ya Kiislamu.
Tunataraji pia kuwa, utakuwa umebaini uzushi na uongo kuhusu mazishi ya Kiislamu. Utaufahamu uongo huo pale utakapoona au kusikia watu wanasema au kufanya kinyume na haya tuliyoeleza, halafu yakawa hayana ushahidi, au ushahidi upo lakini ni dhaifu.
Tukupe changamoto ndugu msomaji, pindi ikitokea unahudhuria muhadhara wake, fanya kumuomba akupe ushahidi kutoka katika Qur-aan au katika Hadiyth za Nabiy, kama ambavyo tumekuwa tukibainisha katika makala hii. Hapo ndipo utakapogundua hila yake yeye pamoja na wengine wanoupaka matope Uislaam.
Fahamu pia kuwa, ibada yoyote utakayoona inafanywa na Muislamu lazima iwe na uthibitisho kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kinyume chake huo utakuwa ni uzushi katika dini.
Tunamuomba Allaah Ajaalie Makala hii iwe chachu ya Waislamu kuipenda dini yao na kujifunza na kuyatekeleza yaliyo sahihi katika dini.
Tunamuomba Allaah Atusamehe madhambi yetu na walio kufa kabla yetu katika Imani.
Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.
[1] Sunnah ni matendo aliyoyafanya Nabiy Muhammad (Swalah na Salamu Za Allaah Ziwe Juu Yake) au aliyashuhudia yakifanywa.
[2] Aina ya majani yanayochanganywa katika maji
[3] Al-Bukhaariy (3/99-104), Abuu Daawuud (2/60-64), An-Nasaaiy (1/266-267)
[4] Shaykh Al-Albaaniy katika Ahkaamul Janaaiz uk.48, Shaykh Bin ‘Uthaymiyn katika Min Ahkaam Al-Fiqhiyah, uk. 68
[5] Kutawadha (Wudhuu) ni utaratibu maalum wa kuosha viungo vya mwili, viganja vya mikono,kusukutua, kusafisha pua,kuosha uso, mikono miwili mpaka vifundoni, kupaka maji kichwani na kusafisha masikio, kuosha miguu miwili mpaka kwenye kongo za miguu, pale Muislam anapotaka kutekeleza ibada yoyote maalum.
[6] Shahidi ni mtu aliyekufa katika Jihaad, vita takatifu vya kupigania Uislaam. Kujilipua kwa kujitoa muhanga haifai katika Uislaam na anayekufa katika hali hii si shahidi, wala si katika Jihaad kujihusisha na vitendo vya kigaidi.
[7] Swahaba ni wafuasi wa mwanzo waliomkubali Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), n ani wa mwanzo kuukubali na kueneza Uislaam.
[8] Al-Bukhaary 3/165, An-Nasaaiy 1/277
[9] Alizaliwa Nchini Saudi Arabia sehemu iitwayo ‘Unayzah tar. 27 Ramadhwaan 134/H na kufa 142H.
[10] Fataawa Arkaanil Islaam uk 406
[11] Imepokelewa na Jamaa: Abuu Daawud 2/176, na wengineo kama Bin Maajah, Al-Bayhaqiy
[12] Imepokelewa na Imamu sita na A-Baqiy na Al-Bayhaqiy na Ahmad katika Hadithy namna 93. Imesahihisha na Al-Abaaniy.
[13] Nisbur Raayat 2/258
[14] Al-Albaaniy katika Ahkaamul Janaaiz uk 64 chapa ya Beirut yam waka 1406H sawa 1966AD
[15] Talbiyah ni matamshi maaluma ayasemayo anayehiji wakati wa kuhiji
[16] Abuu Daawuud 2/166, Bin Hazm 5/158, Ahmad 6/267 na wengineo.
[17] Muslim 9/55, An-Nasaaiy 1/476, Tazama pia kitabu Ahkaamul-Janaaiz uk. 80-82
[18] Ahkaamul Janaaiz uk. 123
[19] Muslim 2/208, Abuu Awaanah ameisahihisha, 1/396
[20] Ahlus Sunnah: Waislam wenye kufuata mafundisho ya Uislaam kulingana na Qur-aan, Sunnah, na (wakafuata njia ya) ufahamu na walivyouelewa Swahaba na wafuasi wao kutoka katika watangulizi wetu wema.
[21] Ahkaam uk. 131 katika maandishi madogo chini ya ukurasa.
[22] Qiblah ni muelekeo ambao Waislamu huelekea wanapokuwa wanaswali au kuchinja, nao ni mwelekeo ulipo mji mtukufu wa Makkah
[23] Ahmad 2/427,528,532
[24] Abu Shaamah katika kitabu Al-Baa’ithu ‘alaa inkaar Al-Bid’ah uk. 67
[25] Al-Haakim na ameipa daraja ya Hasan katika Ahkaam uk. 152
[26] Shibri ni kipimo cha kiganja kimoja…
[27] Ibn Hibbaan katika sahifa yake uk.2160, Al-Bayhaqiy 3/410, na isnadi ya Hadiyth ni hasan (nzuri).
[28] Amepokea Imam Al-Haythamiy katika Majmu’ Az-Zawaaid 3/61 na amesema wapokezi wa Hadiyth hii ni waadilifu.
[29] Ikhtiyaarat al-‘llmiyya uk. 25
[30] Ibn ‘Uthaymiyn katika Fataawa uk. 302. Ahmad 1/405-435
[31] Fataawa uk. 301
[32] Abuu Daawuud 2/69, Al-Bayhaqiyy 3/412, Ahkaam uk. 155
[33] Ahkaam uk. 156-159
[34] Tazama kitabu Zaadul-Ma’aad cha bin-al-Qayyim 1/206, tazama pia kitabu Subulus Salaam cha Imaam Asw-Swana’aniy 2/161
[35] Abuu Daawuud 2/70, Al-Haakim 1/370, na Adh- Dhahabiy ameikubali