055-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kuomba (Du’aa) Kabla Ya Kutoa Salaam Na Aina Zake

 

 

Kuomba (Du’aa) Kabla Ya Kutoa Salaam Na Aina Zake

 

Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Swalah yake akiomba aina mbali mbali za du’aa.”([1]) Akiomba wakati mwingine kwa du’aa hizi na wakati mwingine zile, na akazikubali du’aa nyingine na “akamuamrisha mwenye kuswali achague azipendazo”([2])  Nazo ni:

 

 

1- اللّهُـمَّ إِنِّـي أَعـوذُ بِكَ مِـنْ عَذابِ القَـبْر، وَأَعـوذُ بِكَ مِـنْ فِتْـنَةِ  المْسيحِ الدَّجّـال، وَأَعـوذُ بِكَ مِـنْ فِتْـنَةِ  المْحْـيا وَالمْمـات. اللّهُـمَّ إِنِّـي أَعـوذُ بِكَ مِنَ المْأْثَـمِ وَالمْغْـرَم

 

Allaahumma inniy a’uwdhu Bika min ‘adhaabil qabri, wa a’uwdhu bika min fitnatil Masiyhid Dajaal wa a’uwdhu bika min fitnatil mahyaa wal- mamaat, Allaahumma inniy ‘a’uwdhu bika minal ma-athami wal-maghrami

 

“Ee Allaah!  Hakika mimi najikinga Kwako kutokana na adhabu ya kaburi, na najikinga Kwako kutokana  na fitna ya Masihid-dajjaal, na najikinda Kwako kutokana na fitna ya uhai na ya mauti, Ee Allaah, hakika mimi najikinda Kwako kutokana na dhambi([3]) na deni”([4]) ([5])

 

 

2-  اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ مَا عَمِلْتُ، وَمِنْ شَرِّ مَا لَمْ  أَعْمَلْ (بَعْدُ)

 

Allaahumma inniy a’uwdhu Bika min sharri ma ‘amiltu wamin sharri ma lam a’amal (ba’ad)

 

“Ee Allaah, hakika mimi najikinga Kwako kutokanan na shari nilizozitenda na shari nisizozitenda([6]) [bado]([7])

 

 

3-  أللَّهُمَّ حَاسِبْنِي حِسَاباً يَسِيراً

 

Allaahumma Haasibniy hisaaban yasiyran

 

“Ee Allaah, nihesabie hisabu nyepesi”([8])

 

 

4- اللّهُـمَّ بِعِلْـمِكَ الغَـيْبِ وَقُـدْرَتِـكَ عَلـى الْخَلقِ، أَحْـيِني ما عَلِـمْتَ الحـياةَ خَـيْراً لـي، وَتَوَفَّـني إِذا كَانَتِ الوَفـاةَ  خَـيْراً  لـي، اللّهُـمَّ  وَأَسْـأَلُـكَ خَشْيَتَـكَ في الغَـيْبِ وَالشَّهـادَةِ، وَأَسْـأَلُـكَ كَلِمَـةَ الحَـقِّ (وفي رواية: الْحُكْم) وَالْعَدْلَ فِي الْغَضَبِ وَالرِّضَى، وَأَسْـأَلُـكَ القَصْدَ في الفَقْـرِ وَالغِنَـى، وَأَسْـأَلُـكَ  نَعـيماً لاَيَبِيدُ، وَأَسْـأَلُـكَ قُـرَّةَ عَيْـنٍ (لاَ تَنْفَذَُ وَ) لا تَنْـقَطِعْ  وَأَسْـأَلُـكَ الرِّضَـى بَعْـدَ القَضـاءِ، وَأَسْـأَلُـكَ بًـرْدَ الْعَـيْشِ بَعْـدَ الْمَـوْتِ، وَأَسْـأَلُـكَ لَـذَّةَ النَّظَـرِ إِلـى وَجْـهِكَ (وَأَسْأَلُكَ) الشَّـوْقَ إِلـى لِقـائِـكَ، في غَـيرِ ضَـرّاءٍ مُضِـرَّة، وَلا فِتْـنَةٍ مُضـلَّةٍ، اللّهُـمَّ  زَيِّـنّا بِزينَـةِ الإيـمان، وَاجْـعَلنا هُـداةً مُهْـتَدين

 

Allaahumma bi ‘Ilmikal-ghaybi, wa Qudratika ala khalqi. Ahyiniy maa ‘alimtal-hayaata khayran liy wa Tawafaniy idhaa kaanatil wafaatu khayran liy. Allaahumma wa As-aluka Khashyataka fil ghaybi wash-shahaadah, wa As-aluka kalimatal haqqi, [al-hukmu], wal-‘adla fil ghadhwabi war-ridhwaa, wa As-alukal qaswda fil faqri wal-ghinaa, wa As-aluka na'iyman laa yabiydu, wa As-aluka quratan ‘aynin [laa tanfadhu wa] la tanqatwi’u, wa As-alukar-ridhwaa ba'dal-qadhwai, wa As-aluka bardal-‘aysha ba'dal mawti, wa As-aluka ladhatan nadhwari ilaa Wajhika, wa [As-aluka] ash-shawqa ilaa Liqaaika, fiy ghayri dhwaraain mudhwirratin, wa la fitnaatin mudhwillah. Allaahumma Zayinnaa bi ziynatil iymaani, wa Ja'alnaa hudaatan muhtadiyn.

 

“Ee Allaah, Kwa ujuzi Wako wa mambo yaliyofichikana, na uwezo Wako wa kuumba, niweke hai iwapo Unajua kwamba uhai ni bora kwangu, na nifishe iwapo kufa ni bora kwangu, Ee Allaah, nakuomba pia khofu yako kwa siri na dhahiri na ninakuomba neno la haki [na katika riwaaya: hukmu], na uadilifu wakati nimefurahi na wakati nimekasirika, na ninakuomba matumizi ya wastani wakati wa utajiri na wakati wa umaskini, na ninakuomba neema isiyokwisha na ninakuomba kituliza jicho (moyo) [kisicho toweka na] kisichokatika, na ninakuomba  kuridhia baada yakuwa umeshanipangia, na ninakuomba maisha ya utulivu baada ya kufa, na ninakuomba ladha ya kukutizama uso Wako, [na nakuomba] shauku ya kukutana Nawe, pasina madhara yanayodhuru, wala fitna yenye kupoteza.  Ee Allaah, Tupambe kwa kipambo cha imani, na Tujaalie tuwe waongozi wenye kuongoka”([9])

 

 

5-Amemfundisha Abu Bakr As-Swiddiyq (رضي الله عنه) kusema:

 

اللّهُـمَّ إِنِّـي ظَلَـمْتُ نَفْسـي ظُلْمـاً كَثـيراً وَلا يَغْـفِرُ الذُّنـوبَ إِلاّ أَنْت، فَاغْـفِر لي مَغْـفِرَةً مِنْ عِنْـدِكَ وَارْحَمْـني، إِنَّكَ أَنْتَ الغَـفورُ الرَّحِـيمُ

 

Allaahumma Inniy dhwalamtu nafsiy dhwulman kathiyran walaa yaghfirudh-dhunuuba illa Anta, fa-Ghfirliy maghfiratan min ‘indika, wa-Rhamniy Innaka Antal-Ghafuurur-Rahiym

 

“Ee Allaah, hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu, dhulma nyingi, na hasamehe madhambi ila Wewe, basi Nisamehe msamaha kutoka Kwako, na Unirehemu, hakika Wewe ni mwingi wa kusamehe, mwingi wa kurehemu”([10])

 

 

6- Amemuamrisha ‘Aaishah (رضي الله عنها) aseme:

 

 اللَّهُمَّ إِني أسْأَلُكَ مِنَ الْخَيْرِ كُلِّهِ (عَاجِلِهِ وَآجِلِه) مَا عَلِمْتُ مِنْهُ وَمَا لَمْ أعْلَمْ، وَأعُوذُ بِكَ مِنَ الشَّرِّ كُلِّهِ، (عَاجِلِهِ وَآجِلِهِ) مَا عَلِمْتُ مِنْهُ وَمَا لَمْ ‏‏ أعْلَمْ، وَأسْأَلُكَ (وَفي رواية: اللَّهُمَّ إِنِّي أسْأَلُكَ) الْجَنَّةَ وَمَا قَرَّبَ إلَيْهَا مِنْ قَوْلٍ أوْ عَمَلٍ، وَأعُوذُ بِكَ مِنَ النَّارِ وَمَا قَرَّبَ إِلَيْهَا مِنْ قَوْلٍ أوْ عَمَلٍ، وَأسْأَلُكَ (وَفي رواية: اللَّهُمَّ إِنِّي أسْأَلُكَ) مِنَ (الْ) خَيْرِ مَا سَألَكَ عَبْدُكَ وَرَسُولُكَ (مُحَمَّدٌ وَأعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ مَا اسْتَعَاذَكَ مِنْهُ عَبْدُكَ وَرَسُولُكَ مُحَمَّدٌ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) (وَ أسْأَلُكَ) مَا قَضَيْتَ لِي مِنْ أَمْرٍ أنْ تَجْعَلَ عَاقِبَتَهُ (لي) رُشْداً

 

Allaahumma inniy As-aluka minal-khayri kullihi ‘aajilihi wa aajilihi maa `alimtu minhu wa maa lam a`lam, wa a’uwdhu Bika mina-sharri kullihi `aajilihi wa aajilihi maa `alimtu minhu wa maa lam a`lam. Wa As-aluka

 

[Allaahumma inniy As-aluka] Al-Jannata wamaa qarraba ilayhaa bi qawlin au ‘amal. Wa a’uwdhu Bika minan-naari wamaa qarraba ilayhaa min qawlin au ‘amal. Wa As-aluka  [Allaahumma inniy As-aluka] minal-khayri ma sa-alaka ‘Abduka wa Rasuuluka Muhammadun, wa a’uwdhu Bika min sharri ma sta’aadhaka minhu ‘Abduka wa Rasuuluka Muhammadun Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam. [Wa As-aluka] maa qadhwayta liy min amrin an Taj’ala ‘aqibatahu [liy] rushdaa.

 

“Ee Allaah hakika mimi nakuomba mema yote [karibu na mbali] ninayoyajua na nisiyoyajua, na najikinga Kwako na shari zote [karibu na mbali] ninazozijua na nisizozijua, na nakuomba [na katika riwaaya: Ee Allaah hakika mimi nakuomba] Pepo na kila kauli au kitendo kinachokaribisha nayo, na najikinga Kwako na moto na kila kauli na kitendo kinachokaribisha nao, na nakuomba [na katika riwaaya: Ee Allaah, hakika hakika mimi nakuomba] kutokana na kheri alizokuomba Mja Wako na Mjumbe Wako [Muhammad na najikinga Kwako na shari alizojikinga nazo Mja Wako na Mjumbe Wako Muhammad SwallaLlaahu ‘alayhi wa sallam], [na nakuomba] kwa mambo yote uliyonikidhia Ujaalie matokeo yake [kwa ajili yangu] yawe ya uongofu([11])

 

 

7- Alimuuliza mtu: ((Unasema nini katika Swalah?)) Akasema: “Nakiri kwamba (yaani nashuhudia) kisha nauomba Allaah Pepo, na najikinga Naye kutokana na moto. Lakini Naapa, hakuna dandana (mnong’ono)([12]) mzuri kama wako au wa Mu’aadh”. Hivyo akasema: ((Dandana [mnong’ono] wetu ni kama wako))([13])

 

 

8-Amemsikia mtu akisema katika Tashahhud yake:

 

اللّهُـمَّ إِنِّـي أَسْأَلُـكَ يا اللهُ  (وَفِي رواية: بِاللّه) (الْواحِدُ) الأَحَـدُ ،الصَّـمَدُ الَّـذي لَـمْ يَلِـدْ وَلَمْ يولَدْ، وَلَمْ يَكـنْ لَهُ كُـفُواً أَحَـدٌ-   أَنْ تَغْـفِرَ لي ذُنـوبي إِنَّـكَ أَنْـتَ الغَفـورُ الرَّحِّـيمُ

Allaahumma inniy As-aluka yaa Allaah  [BiLlahi] [Al-Waahidu] Al-Ahad As-Swamadu Alladhiy lam Yalid walam Yuwlad walam Yakun Lahu kufuwan ahad-an Taghfira liy dhunubiy Innaka Antal-Ghafuwrur Rahiym.

 

“Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba Ee Allaah, [na katika riwaayah: Naapa kwa Allaah] [Wewe ni Mmoja] Uliye  Pekee, Mwenye kutegemewa kwa haja zote, Ambaye Hakuzaa wala Hakuzaliwa, na wala hakuna mfano Wake na kitu chochote, Unisamehe makosa yangu, hakika Wewe ni Mwingi wa Kusamehe, Mwenye Kurehemu”.

Hii (صلى الله عليه وآله وسلم) alisema: ((Amesamehewa, Amesamehewa))([14])

 

 

9-Alimsikia mtu mwingine akisema katika Tashahhud yake:

 

اللّهُـمَّ إِنِّـي أَسْأَلُـكَ بِأَنَّ لَكَ الْحَـمْدُ لا إِلـهَ إِلاّ أَنْـتَ (وَحْـدَكَ لا شَـريكَ لَـكَ) (المَنّـانُ) (يا) بَديـعَ السَّمواتِ وَالأَرْضِ يا ذا الجَلالِ وَالإِكْـرام، يا حَـيُّ يا قَـيّومُ  (إِنِّـي أَسْأَلُـكَ) (الجَـنَّةَ وَأَعـوذُ بِـكَ مِنَ الـنّار)

Allaahumma inniy As-aluka bianna Lakal-hamdu, laa ilaaha illa Anta [Wahdaka laa shariyka Lak], [Almannaan], [yaa] Badiy’a s-samawati wal-ardhwi, yaa Dhal-Jalaali wal-Ikraami, yaa Hayyu yaa Qayyuum, [inniy as-aluka] [al-Jannata, wa a’uwdhu Bika minan-Naari]

 

“Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba, kwa vile sifa njema zote ni Zako, hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe, [Peke Yako Huna mshirika] [mwingi wa kuneemesha].  [Ee] Mwanzishi (muumbaji) wa mbingu na ardhi,  Ee mwenye Utukufu na  Ukarimu, Ee Uliye Hai Mwenye kusimama kwa dhati  Yako, [hakika mimi nakuomba]  [Pepo, na najilinda  Kwako kutokana  na moto”].

 

Hivyo Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akawaambia Maswahaba: ((Mnajua kaomba nini?)) Wakasema: “Allaah na Mjumbe Wake wanajua zaidi”. Akasema: ((Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake, amemuomba Allaah kwa Jina Lake tukufu)) [katika riwaaya nyingine: Tukufu kabisa]([15]) ambalo Anapoombwa Anajibu na Anapoombwa Hutoa)).([16])

 

10- Kitu cha mwisho alichokuwa akisema baina ya Tashahhud na tasliym ilikuwa ni:

 

اللّهُـمَّ اغْـفِرْ لي ما قَدَّمْـتُ وَما أَخَّرْت، وَما أَسْـرَرْتُ وَما أَعْلَـنْتُ، وَما أَسْـرَفْتُ، وَما أَنْتَ أَعْـلَمُ بِهِ مِنِّي. أَنْتَ المُقَـدِّمُ، وَأَنْتَ المُـؤَخِّـرُ لا إِلهَ إِلاّ أَنْـتَ

 

Allaahumma-Ghfirliy maa qaddamtu wamaa akhartu, wa maa asrartu, wamaa a’lantu, wamaa asraftu, wamaa Anta A’lamu bihi minniy, Antal Muqaddimu, wa Antal Muakhiru, laa ilaaha illa Anta.

 

“Ee Allaah! Nisamehe niliyoyatanguliza, na niliyoyachelewesha, na niliyoyafanya kisiri, na niliyoyafanya kwa dhahiri na niliyoruka mipaka, na ambayo Wewe Unayajua zaidi kuliko mimi, Wewe Ndiye Mwenye kutanguliza na Wewe Ndiye Mwenye kuchelewsha, hakuna apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe”.([17])

 

 

 

 



[1]  Hatukusema “ ….katika Tashahhud yake”, kwa sababu matini ni “…katika

Swalah yake”, bila ya kuelezea kama Tashahhud au sehemu nyingine. Hivyo inajumuisha sehemu zote zifaazo kwa du’aa mfano katika Sujuud na Tashahhud. Amri ya kuomba du’aa katika vikao viwili zimetajwa kabla.

[2]   Al-Bukhaariy na Muslim. Amesema Al-Athram: “Nilimuuliza Ahmad:

Niombe na nini baada ya Tashahhud? Akasema: Kama ilivyosimuliwa. Nikasema: Kwani Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hakusema: ((Achague du’aa zozote azipendazo?)) Akasema: Achague katika zilizosimuliwa. Nikakariri swali, akasema: Kutoka zilizosimuliwa. Hii imenukuliwa na Ibn Taymiyyah (Majmuu’a Al-Fataawa 69/218/1), ambaye amenukuu akiongeza: ‘Hivyo, ‘du’aa zozote’ zinakusudiwa Anazozipenda Allaah, na sio du’aa yoyote…” Kisha akasema: ‘Hivyo ni bora kusema zile zilizokubaliwa, du’aa zilizothibiti, na hizi ndizo zilizosimuliwa na zenye manufaa”.  Ndivyo hivyo, lakini kutambua du’aa gani hakika zenye manufaa inategemea na elimu Swahiyh, nayo ni nadra kupatikana kwa watu. Kwa hivyo ni bora kushikilia du’aa zilizonukuliwa khaswa zikiwa zinajumuisha zile anazopenda mwenye kuswali. Na Allaah Anajua zaidi

 

 

[3] "Ma-tham" ni yale yanayomsababisha mtu kutenda dhambi au dhambi yenyewe.

[4] "Maghram" ni mzigo. Hapa ina maana deni kama ilivyothibiti katika Hadiyth nyingine ambayo ‘Aaishaah amesema: “Mtu alimwambia: “Kwa nini kila mara unajikinga kutokana na maghram ewe Mjumbe wa Allaah?” Akajibu: ((Hakika mtu anapokuwa na deni, husema uongo na anaaahidi na kuvunja ahadi yake)).

[5]  Al-Bukhaariy na Muslim.

[6] Yaani kutokana na shari ya vitendo viovu nilivyovitenda, na kutokana na  shari ya maovu ya kutokutenda vitendo vyema.

[7]  An-Nasaaiy ikiwa na isnaad Swahiyh na Ibn Abi ‘Aaswim katika kitabu

chake As-Sunnah (Namba. 370- ikiwa na utafiti wangu). Ziada ni kutoka kwake.

[8] Ahmad na Al-Haakim ambaye amekiri ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubali.

[9] An-Nasaaiy na Al-Al-Haakim ambaye amekiri ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubali.

[10]   Al-Bukhaariy na Muslim.

[11] Ahmad, Atw-Twayaalisiy, Al-Bukhaariy katika Al-Adaab Al-Mufrad, Ibn

Maajah na Al-Haakim ambaye amekiri ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubali. Nimetoa takhiryj yake katika Silsilatul-Ahaadiyth As-Swahiyhah (1542).

[12] "Dandanah" ni kusema kwa sauti ndogo isiyosikika, lakini maneno yasiyofahamika – katika hali hii ni maneno ya kimya ya du’aa. Kauli ya mwisho ina maana: “Maneno yetu ni kama yako”.

[13] Abu Daawuud, Ibn Maajah na Ibn Khuzaymah (1/87/1) ikiwa na isnaad Swahiyh.

[14]  Abu Daawuud, An-Nasaaiy, Ahmad na Ibn Khuzaymah. Al-Haakim amekiri ni Swahiyh,na Adh-Dhahaby amekubali.

[15] Tawassul hii (kujikurubisha) kwa Allaah kwa kutumia Majina Yake mazuri

na sifa Zake, ni amri ya Allaah تعالى  ((وَلِلَّهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا)) [Al-A’raaf 7: 180]. Ama kumuomba Allaah kwa kukurubia vitu vingine mfano, ‘kwa kumtaja fulani na fulani’ au ‘kwa makarama ya fulani na fulani’ au ‘masharifu’ n.k – matini ya Imaam Abu Haniyfah (رحمه الله ) na Maswahaba zake, wametaja kuwa desturi hii ni makruuh (inachukiza). Kwa ujumla imeharamishwa. Hivyo inasikitisha kwamba watu wengi miongoni mwao MaShaykh, wamedharau tawassul zilizokubaliwa – hutowasikia wakijikurubisha kwa Allaah kwa tawassul hizo, bali wamebobea katika aina za tawassul za bid’ah ambazo angalau kwa uchache zinasemwa kuwa zimekhitilafiana wanazidumisha kama kwamba nyinginezo hazifai. Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah ameandika makala ndefu kuhusu maudhui hii yenye kichwa cha habari: At-Tawassul Wal-Wasiylah (Kujikurubisha kwa Allaah na njia zake) ipasayo kufuatwa, kwani ni muhimu sana hakuna mfano wake katika maudhui hii. Pia kuna makala yangu "Tawassul Anwaa'uhaa wa Ahkaamuhaa" ambayo pia ni muhimu katika maudhui yake na mfumo wake, na pia inakanusha shubuhaat mpya kutoka kwa baadhi ya Madaktari wa kisasa wa dini. Allaah Atuongoze pamoja nao.

[16] Abu Daawuud, An-Nasaaiy, Ahmad, Al-Bukhaariy katika Al-Adaabu Al-

Mufrad, At-Twabaraaniy na Ibn Mandah katika Tawhiyd (44/2, 67/1, 70/1-2) ikiwa na isnaad Swahiyh.

[17] Muslim na Abu ‘Awaanah.

 

Share