Mume Anaweza Kumlipia Mke Kufanya Hijjah. Kuna Sharti Zozote Zinazopaswa Kutimizwa?

 

Mume Anaweza Kumlipia Mke Kufanya Hijjah. Kuna Sharti Zozote Zinazopaswa Kutimizwa?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

AAWW!

 

Nauliza:

 

Mume kumtolea nauli ya matumizi mke kwenda Hijjah inasihi? Kama jibu ni ndiyo, kuna pre-requisites e.g. Jee kama yeye mwenyewe an uwezo? Si Hijjah inamjuzu mwenye uwezo tu.

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza tunapenda kukumbusha ndugu muulizaji kuacha kufupisha salaam unapoandika, unapoteza fadhila na ujira kwa kufanya hivyo.

 

Kama tunavyoelewa kuwa Hijjah ni nguzo ya tano kwa Waislamu nayo ni Faradhi kwa waume na wake. Hiyo ni kuwa taklifu zote za amali katika Uislamu ni faradhi kwa wote. Allaah Anasema:

 

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً ۖ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٩٧﴾

Mwenye kutenda mema miongoni mwa wanamume au wanawake naye ni Muumin, Tutamhuisha uhai mzuri, na bila shaka Tutawalipa ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda. [An-Nahl: 97].

 

Na Hijjah imefaradhishwa kwa wote pindi yanapopatikana masharti Fulani. Allaah Anasema:

 

فِيهِ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ مَّقَامُ إِبْرَاهِيمَ ۖ وَمَن دَخَلَهُ كَانَ آمِنًا ۗ وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ ﴿٩٧﴾ 

Ndani yake kuna Aayaat (ishara, dalili) zilizo wazi; mahali pa kisimamo cha Ibraahiym. Na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Allaah imewajibika watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. Na atakayekufuru, basi hakika Allaah ni Mkwasi kwa walimwengu. [Al-'Imraan: 97].

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "…Na kwenda Hijjah ukiweza kufanya hivyo" [Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaaiy kutoka kwa ‘Umar bin al-Khatwaab  (Radhwiya-Allaahu ‘anhu)].

 

Ibara hii ya Aayah na Hadiyth ina maana ya kuwa kila Muislamu ni lazima ahiji mara moja katika maisha yake akiweza kufanya hivyo. Uwezo una tafswili nyingi na yaliyo muhimu ni: -

  1. Awe na afya nzuri ya kuweza kustahamili mazito ya safari.

 

  1. Kuwe na usalama njiani – kwenda na kurudi

 

  1. Awe na uwezo wa kutoa gharama za safari na kuacha masurufu yote ya wale wanaomtegemea. 

Ikiwa sharti moja katika hayo limekosekana basi Hijjah haijamlazimu mtu huyo. Hivyo,  jibu ni kwamba inafaa kwa mume kumpeleka mkewe Hijjah ikiwa atakuwa ana uwezo huo. Na inapendeza zaidi ikiwa watakwenda pamoja kwani hilo litaongeza mahaba baina yao. Na kwa ajili hiyo alipokuja mtu kwa Nabiy (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).) akamwambia kuwa mkewe anakwenda Hijjah naye amejiandikisha kwenda katika Jihadi, Nabiy (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia aende na mkewe kuhiji.

 

Na ni msingi wa Uislamu kuwa ((Yeyote mwenye kumuelekeza mtu mwengine katika kheri atapata thawabu sawa na mwenye kufanya hiyo amali)) [Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah kutoka kwa Ibn Mas‘uud na Abu Hurayrah (Radhwiya-Allaahu ‘anhumaa)]

 

Na hivyo hivyo ikiwa mke ni muweza kuliko mumewe anaweza kumsaidia mumewe kumpeleka Hijjah na pia atapata ujira mkubwa. Ikiwa mke ana uwezo anaweza kujipeleka mwenyewe baada ya kupata mahri wa kusafiri naye. Na wakati huo inakuwa ni lazima kwake kwa sababu masharti yote yametimia. Ikiwa hana uwezo haiwi ni lazima kwake lakini ikiwa atasaidiwa kutekeleza Faradhi hiyo basi hakuna tatizo lolote. Na hii ni ‘Ibadah ambayo ni tofauti na ‘Ibadah nyingine ambazo mtu hata akiwa mgonjwa anatakiwa afanye mwenyewe kama Swalaah, lakini Hijjah ikiwa  mgonjwa huwezi kwenda mwenyewe unaweza kumpatia mtu hela zinazohitajika akaenda kukuhijia.

 

Na Allaah Anajua zaidi

  

Share