Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) Rahmah Kwa Walimwengu

 

Imekusanywa na:

Muhammad Faraj Saalim As-Sa’aiy

 

 

Yaliyomo

Utangulizi 4

Faida Za Kusoma Siyrah. 7

Bara Arabu Na Watu Wake. 8

Mataifa Ya Kiarabu. 10

Matawi Ya Waarabu. 11

Nabii Ibraahiym Awasili Makkah. 12

Haajar Na Kisima Cha Zamzam.. 15

Nguzo Za Al-Ka’abah. 20

Watoto Wa Ismaa’iyl 22

Utawala Wa Makkah. 23

Yemen. 24

Shaam na Iraq. 25

Dini Za Waarabu Kabla Ya Uislamu. 26

Wa Mwanzo Kufanya Shirk. 28

Dini Ya Kiyahudi 30

Dini Ya Kinasara. 32

Majusi 32

Sabaiya. 32

Dini Za Waarabu. 33

Walikuwepo Waongofu. 33

Tabia Nzuri Tabia Za Waarabu Kabla Ya Kuja Kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) 36

Tabia Mbaya. 37

Nasaba Yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) 40

Ukoo Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) 42

Mambo Adhimu Yaliyotokea Kabla Ya Kuja Kwa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) 45

Kufukuliwa Kisima Cha Zamzam.. 45

Kisa Cha Nadhiri aliyoweka ‘Abdul-Mutwallib Ya Kumchinja Mmoja Kati Ya Wanawe  48

Kisa Cha Asw-Haabul Fiyl (Watu Wa Ndovu). 51

Alama Za Utume. 54

Bwana Anazaliwa. 55

Asubuhi Njema. 57

Kwa Bi Haliymah As-Sa’adiyah. 59

Mtoto Wa Ajabu! 63

Angelikuwa Yatima... 63

Kisa Cha Kupasuliwa Kifua. 63

Anarudi Kwa Mama Yake. 64

Ndugu Zake Wa Kunyonya. 66

Mama Yake Anafariki 67

Kwa Babu Yake Mwenye Huruma. 68

Kufariki Kwa Babu Yake. 69

Kwa Ami Yake. 70

Uso Wa Baraka. 71

Kabla Ya Kupewa Utume. 72

Mchaji Allaah Buhayrah. 74

Vita Vya Al-Fujaar (Waovu). 75

Muwafaka Wa Al-Fudhuwl 75

Shughuli Za Mwanzo. 77

Habari Za Kiwingu. 77

Anamuoa Bibi Khadiyjah. 79

Kuijenga Upya Al-Ka’abah. 81

Akihuzunika. 83

Chini Ya Kivuli Cha Utume. 84

Ndani Ya Pango La Hiraa. 84

Mpe Hongera Muhammad. 86

Jibriyl Anateremsha Wahyi 87

Zammiluuniy Zammiluuniy. 90

Wewe Ndiye Mtume Wa Umati Huu. 91

Mafunzo. 93

Kusimama Kwa Wahyi 93

Jibriyl Anateremka Tena. 94

Kulingania Kwa Siri 95

Walioanza Kusilimu. 95

Kusilimu Kwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu). 97

Miongoni Mwa Waliotangulia. 98

Kusilimu Kwa ‘Uthmaan Bin ‘Affaan. 99

Sa’ad Bin Abiy Waqaas. 99

Bilaal Bin Rabaah. 100

Nyumba Ya Al-Arqam.. 101

Hijra Ya Uhabashi 103

Kusilimu Kwa Hamzah. 109

Kusilimu Kwa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu). 110

Aila Yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). 114

Kulingania Kwa Jahara. 116

Mateso Mbali Mbali 117

Utumbo Wa Ngamia. 117

Nitamkanyaga Shingo Yake. 118

Oh! Mtamuua?. 119

Rudi Kwenu Ukawalinganie. 119

Wa Mwanzo Kuudhihirisha Uislamu. 120

Mafunzo. 121

Mbinu Mbali Mbali 123

Unaonaje Tukaabudu Unachoabudu. 124

Akitaka Mali Tutampa. 125

Makubaliano Ya Bani Haashim Na Bani Muttwallib. 127

Kupigwa Pande. 128

Makubaliano Ya Dhulma Na Uadui 128

Kuvunjika Kwa Mkataba. 129

Funzo. 130

Kufariki Kwa Abu Twaalib Na Bi Khadiyjah. 131

Safari Ya Twaaif 133

Funzo. 136

Israa Na Mi’iraaj 137

Fungamano La Mwanzo La ‘Aqabah. 143

Mafanikio ya Musw’ab. 144

Balozi Wa Uislamu Madiynah. 148

Funzo. 148

Fungamano La ‘Aqabah La Pili 149

Viongozi Kumi Na Mbili 152

Quraysh Wanapeleka Malalamiko. 153

Quraysh Wanapata Uhakika. 154

Funzo. 155

Mwanzo Wa Hijra. 156

Wa Mwanzo Kuhajir 157

Waliobaki Makkah. 160

Mkutano Wa Halmashauri Ya Maquraysh. 161

Kuhama Kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). 164

Nyumba Inazungukwa. 165

Anaondoka Nyumbani 166

Kutoka Nyumbani Kuelekea Pangoni 168

‘Aliy Na Hafswah (Radhiya Allaahu ‘Anhum) Wanaadhibiwa. 170

Njiani Kuelekea Madiynah. 171

Suraaqah Na Bangili Za Mfalme Kisraa. 173

Ummu Ma’abad Al-Khuza’iyah. 175

Kusilimu kwa Abu Buraydah. 176

Wanawasili Qubaa. 177

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu) Naye Anawasili Madiynah. 178

Kusilimu Kwa Salmaan Al-Faarisy (Radhiya Allaahu ‘Anhu). 179

Kuhama Kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Na Kwa ‘Umar Bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu). 180

Kuelekea Madiynah. 182

Kuingia Madiynah. 182

Mafunzo Juu Ya Hijra. 185

Ujenzi Wa Msikiti Wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). 189

Kuijenga Jamii Ya Madiynah. 192

Kufungisha Undugu. 194

Mkataba Wa Maridhiano Baina Ya Waislamu. 196

Mkataba Na Mayahudi 198

Kusilimu Kwa ‘Abdullaah Bin Salaam (Radhiya Allaahu ‘Anhu). 199

Kujenga Mwenendo Na Tabia Njema. 201

Mwaka Wa Mwanzo Wa Hijra. 203

Mwaka Wa Pili Wa Hijra. 205

Barua Ya Quraysh Kwa ‘Abdullaah Bin Ubay. 206

Vita Vya Badr 207

Sababu Za Vita. 207

Jeshi Dogo. 207

Jeshi Linaondoka Kuelekea Badr 208

Msafara Wa Abu Sufyaan. 209

Jeshi La Quraysh. 210

Jeshi La Waislamu. 211

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Aitisha Mkutano. 212

Majeshi Ya Kiislamu Yanafanya Uchunguzi 214

Habari Muhimu Kuhusu Jeshi La Quraysh. 215

Kuteremka Mvua. 217

Jeshi La Waislamu Linashika Sehemu Muhimu. 218

Makao Makuu Ya Jeshi 218

Usiku Kabla Ya Mapambano. 219

Jeshi La Watu Wa Makkah. 220

Majeshi Yanakabiliana. 221

Mubaaraza (Mapambano Kabla Ya Vita Kuanza). 223

Mashambulio. 223

Kifo Cha Abu Jahl 226

Mizoga Ya Makafiri 228

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Anawasemesha Maiti Wa Quraysh  228

Bishara Njema. 229

Kuondoka Badr 230

Matukio Mbali Mbali 230

Fundisho. 232

Mateka Wa Badr 234

Mpango Wa Kumuua Mtume Wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  235

Bani Qaynuqaa Wanavunja Mkataba. 237

Fundisho. 238

Vita Vya Uhud. 239

 

 

Utangulizi

Shukrani zote ni zake Allaah, tunamshukuru, tunategemea msaada Wake, tunafuata maongozi Yake, tunajilinda Kwake kutokana na shari za nafsi zetu na amali zetu zilizo ovu. Atakayeongozwa na Allaah hapana wa kumpotosha (kumpoteza) na Atakayeachwa kupotea (kwa sababu ya kukataa kwake kufuata uongofu), hatapata mwengine wa kumuongoza.

 

Nashuhudia kwamba hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni mja wake na mwisho wa Mitume yake na mjumbe Wake na kipenzi Chake na mbora wa viumbe Vyake. Ameulingania ujumbe, ameifikisha amana, amewanasihi umma na kuwaondolea dhiki, amewatoa watu kutoka katika kiza cha kufru na kuwaingiza katika Nuru ya Uislamu, na amepigana Jihaad katika njia ya Allaah kwa ukamilifu kama inavyostahiki.

 

Tunakuomba Ee Mola wetu Umpe rahmah na Umpe amani Mtume wako huyu mtukufu uliyemleta akiwa ni Rahma kwa walimwengu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Allaah Anasema:

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ

“Na hatukukutuma (hatukukuleta) ila uwe rehema kwa walimwengu.”

Al-Anbiyaa- 107

 

Swala na salaam za Allaah zimfikie yeye pamoja na aali zake na Swahaba zake wema (Radhiya Allaahu ‘anhum).

Amma baad –

Nilianza kukifasiri kitabu cha Siyrah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kiitwacho Ar-Rahiyq Al-Makhtuum, lakini baada ya kujulishwa kuwa wapo waliokwisha ifanya kazi hiyo, nikaamua kuacha kuendelea kukifasiri na badala yake kuandika Siyrah iliyotwaharika ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuongezea mafunzo tunayoweza kuyapata ndani ya Siyrah hii adhimu. Nikaamua pia kunukuu kutoka vitabu mbali mbali ili msomaji apate ladha na fani za wanavyouni tofauti walioandika Siyrah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Faida kubwa sana nimeipata katika kitabu ‘Waqafaat Tarbawiyah’ kilichoandikwa na Shaykh Ahmad Fariyd, hiki ni kitabu maarufu sana kwa wenye kufuatilia elimu hii ya Siyrah.

Na pia nimefaidika sana na maelezo katika kitabu ‘Haadhal Habiyb’ na mengi zaidi nimeyapata katika kitabu nilichotangulia kukitaja ‘Ar-Rahiyq Al-Makhtuum’.

  

Faida Za Kusoma Siyrah

Maisha ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni somo adhimu sana baada ya somo la Qur-aan tukufu, na hii ni kwa sababu ndani yake tunapata faida nyingi sana, zikiwemo zifuatazo:

        Kujua sababu za kuteremshwa kwa aya mbali mbali za Qur-aan jambo litakalotuwezesha kukifahamu vizuri kitabu cha Allaah pamoja na kuzifahamu hukmu zake na hadithi zake, na kuifahamu vizuri Sunnah iliyotakasika ya Mtume wa Allaah Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

        Kufahamu namna gani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyoshirikiana na Swahaba zake watukufu (Radhiya Allaahu ‘anhum) walivyoipigania Dini ya Allaah kwa hali na mali na kuieneza kila pembe ya dunia, na pia mafundisho ya hekima, pamoja na maarifa mbali mbali aliyowafundisha Maswahaba wake kwa ajili ya majukumu hata wakaweza kusubiri na kustahamili mashaka na tabu mbali mbali mpaka pale Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) alipowapa yale aliyowaahidi kwa kuitiisha dunia yote ikawa chini ya amri yao.

 

        Maisha ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni muujiza katika miujiza ya Allaah, kwani katika kuidurusu Siyrah yake, tutaona namna gani alivyozaliwa na kulelewa katika mazingira ya kiajabu na ya kimiujiza na pia namna Alivyoelimishwa na Kulindwa na Mola wake (Subhaanahu wa Ta’alaa).

 

        Tunapata kuwajua zaidi watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na namna gani walivyoshirikiana na Maswahaba wake watukufu (Radhiya Allaahu ‘anhum), tokea siku za mwanzo, wakahuzunika na kufurahi pamoja, na wakati huo huo msomaji wa Siyrah anafurahi kwa furaha zao na anahuzunika kwa huzuni zao.

 

        Katika somo hili, tunaweza kujua namna gani Maswahaba walivyojifunza katika madrasa ya Mtume wao mtukufu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), akawalea vizuri na kuwafanya wawe umma bora kuliko umma zote zilizowahi kuteremshiwa watu. Kwani wao ndio walioisimamia Dini hii na kupiga mifano mema katika kujitolea nafsi zao mhanga kwa ajili ya kuutetea Uislamu, kupigana Jihaad na kuwalingania watu katika njia ya Allaah, kuonyesha ushujaa, ustahamilivu na uadilifu mbele ya adui, pamoja na mapenzi na huruma na ukarimu na kila sifa njema mbele ya wenzao.

 

        Katika kuyadurusu maisha ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tutaweza pia kuona na kuonja ladha ya Jihaad na namna gani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Swahaba zake watukufu (Radhiya Allaahu ‘anhum) walivyosimama kidete katika kuipigania Dini hii tukufu na namna walivyoweza kusubiri mbele ya adui na kuvumilia mateso na shida mbali mbali.

 

        Tutaweza pia kuujua uchaMungu wao na namna gani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyoweza kuzibadilisha na kuzijenga nyoyo na nafsi zao kwanza, kabla ya kuziendea nyoyo na nafsi nyingine, na hii ni tafisiri ya kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) isemayo:

إِنَّ اللّهَ لاَ يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّى يُغَيِّرُواْ مَا بِأَنْفُسِهِمْ

“Hakika Allaah habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao Yaliyomo katika nafsi zao”.

Ar-Ra’ad - 11

 

 

Bara Arabu Na Watu Wake

Kwa vile Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekuja na ujumbe uliowatoa watu kutoka katika giza la ushirikina na kuwaingiza katika nuru ya Uislamu, kuwatoa katika dhulma za viumbe na kuwaingiza katika Rahma ya Mola wa viumbe, kuwatoa katika ujahili wa kuwaabudu viumbe na kuwatia katika neema ya kumuabudu Mola wa viumbe, basi hatutoweza kufaidika vizuri ikiwa tutayadurusu maisha yake bila ya kwanza kuidurusu hali ya mambo ilivyokuwa huko bara Arabu kabla ya kuja kwake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  karibu ya kuja kwake, na baada ya kuja kwake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  kisha tukapambanisha baina ya hali hizo.

 

Bara Arabu imelala katika sehemu muhimu sana ya ulimwengu inayounganisha Mashariki ya ardhi na Magharibi yake, Kusini na Kaskazini.

Upande wa Magharibi unamalizikia Bahari nyekundu (Red sea) pamoja na jangwa la Sinai, na Mashariki yake inamalizikia katika Ghuba ya Arabuni (Arabian Gulf) na sehemu ya Kusini ya nchi ya Iraq. Ama Kusini mwa bara hili, ipo bahari ya Arabu (Arabian sea) napo ni mahali panapoanzia bahari ya India (Indian ocean), na Kaskazini mwake inamalizikia nchi ya Sham na sehemu ya nchi ya Iraq.

 

Juu ya kuwa sehemu kubwa ya ardhi yake ni jangwa na majabali, jambo lililowasaidia sana watu wake wasiweze kutawaliwa na Mataifa mengi, lakini sehemu ya nje ya bara hili imelala katika sehemu muhimu sana kijografia, kwani Magharibi ya Kaskazini mwake ni mlango wa kuingia katika bara la Africa, na sehemu ya Mashariki ya Kaskazini ni mlango wa kuingia chi za Ulaya (Europe), na Mashariki yake ni mlango wa kuingia nchi ya Iran, India, Uchina na sehemu mbali mbali za mashariki ya mbali (Far east).

 

Kwa ajili hii, kupitia karne mbali mbali bara hili liliweza kufikiwa na ustaarabu wa Mataifa yote ulimwenguni.

 

 

Mataifa Ya Kiarabu

Asili ya waarabu wote inatoka Yemen, na wengi wao waliihama nchi yao hiyo na kuenea katika sehemu mbali mbali za bara Arabu baada ya mafuriko makubwa yaliyotokea huko Yemen yaliyosababishwa na kubomoka kwa boma maarufu la kuzuia maji lililokuwepo mji wa Ma’arib (Ma’arib dam), kwa Kiarabu linajulikana kwa jina la ‘Sid Ma’arib’.

 

Mafuriko hayo yametajwa katika Qur-aan tukufu.

Allaah Anasema:

فَأَعْرَضُوا فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ سَيْلَ الْعَرِمِ وَبَدَّلْنَاهُم بِجَنَّتَيْهِمْ جَنَّتَيْنِ ذَوَاتَى أُكُلٍ خَمْطٍ وَأَثْلٍ وَشَيْءٍ مِّن سِدْرٍ قَلِيلٍ

“Lakini walipuuza (amri ya Allaah); Tukawapelekea mfuriko mkubwa (wa maji ukagharikisha mashamba hayo)”.

Sabaa – 16

Boma hilo ambalo ni ukuta mkubwa uliojengwa baina ya majabali mawili kwa ajili ya kuyazuia na kuyakusanya maji ya mvua yanayotoka sehemu mbali mbali za majabalini na kuishia hapo, lilijengwa tokea zama za Yuarub bin Yashjab bin Qahtwaan kwa ajili ya kufaidika na maji hayo katika kilimo na matumizi mengine mbali mbali.

 

Anasema Ibn Kathiyr katika Al-Bidaayah wan-Nihaayah:

“Maji Yaliyokuwa yakijikusanya mahali hapo yaliweza kuwasaidia sana watu wa Yemen katika kuyamwagilia mashamba yao na katika matumizi yao ya kila siku”.[1]

 

Inasemekana kuwa boma hilo ilitobolewa na panya, likabomoka na kusababisha mafuriko makubwa pamoja hasara kubwa sana.

 

Matawi Ya Waarabu

Maulamaa wa historia wamewagawa waarabu katika mafungu matatu;

Fungu la mwanzo wameliita; ‘Al-‘Arab Al-Baaidah’, na hawa ni waarabu wa mwanzo kama vile  ‘Aad na Thamuud na Twasam na Jadis na Umlaaq na wengine wa mfano wao ambao si rahisi kupatikana maelezo ya zaidi juu yao.

Fungu la pili wakaliita; ‘Al-‘Arab Al-‘Aaribah’, na hawa ni waarabu wanaotokana na Yuarub bin Yashjab bin Qahtwaan wanaojulikana kwa jina la ‘Al-Qahtwaaniyiin’ au ‘Al-Qahtwaaniyah’.

Ama fungu la tatu kama walivyogawa wataalamu wa historia, wamelipa jina la ‘Al-‘Arab Al-Musta’arabah’, ambao ni vizazi vya Ismaa’iyl, na hawa wanaitwa ‘Al-‘‘Adnaaniyah’.

 

Kundi linaloitwa ‘Al-‘Arab Al-‘Aaribah’, ambao asili yao inatokana na Yuarub bin Yashjab bin Qahtwaan, hawa ni watu wa Yemen ambako asili ya waarabu wote inatoka huko, na kutokana na Yuarab huyu yamepatikana makabila mengi ya Kiarabu.

Yaliyokuwa mashuhuri zaidi ni makabila ya Hamyar na Kahlaan, na kutokana na kabila la Hamyar yakapatikana makabila yafuatayo:

Zaydul Jamhur, Qadha’ah na As-Sakaasik.

Na kutokana na Kahlaan yakapatikana makabila yafuatayo:

Hamadan, Anmar, Watiy, Madhhaj, Kindah, Lakham, Judhaam, Al-‘Azd, Al-‘Aws, Al-Khazraj na watoto wa Jufnah waliokuwa wafalme wa Shaam.

 

Ama kundi la tatu walolipa jina la Al-‘Arab Al-Musta’arabah, hawa asili yao inatokana na Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) aliyetoka mji unaoitwa Aar uliopo kandokando ya mto wa Furaat (Euphrates) katika mji wa Al Kufa huko Iraq.

Anasema Al-Mubaarakpuri katika kitabu chake ‘Ar-Rahiyq Al-Makhtuum’:

“Wataalamu wa jiografia waliokwenda kuchimba katika sehemu hizo walifanikiwa kupata athari nyingi sana zinazoelezea juu ya ustaarabu uliokuwepo wakati wa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam), na juu ya Dini zao na mambo mengi yanayohusu jamii zao.

Inajulikana kuwa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) aliuhama mji huo na kuishi sehemu iliyokuwa ikiitwa Haraan na hatimaye akahamia nchi ya Palastina na huko ndiko alikofanya makao yake ya kuufikisha ujumbe aliopewa na Mola wake.”

 

Nabii Ibraahiym Awasili Makkah

Wakati Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) alipokwenda kutembelea nchi ya Misri akiwa amefuatana na mkewe, Firauni (mfalme wa Misri) aliwapokea na kuwaweka ndani ya qasri yake, na usiku ulipoingia Firauni alijaribu kumdhuru Bibi Sarah mke wa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam), lakini Allaah Alimkinga na shari hiyo kwa kuufanya mkono wa mfalme upooze kila anapojaribu kumsogelea.

 

Alipoona dalili za qudra ya Allaah inayomlinda Bibi huyo, Firauni aliacha vitimbi vyake, na badala yake akaamua kumpa Sarah zawadi, na zawadi yenyewe ilikuwa binti yake aitwae Haajar, na Sarah akaikubali zawadi hiyo na akamuozesha binti huyo mumewe Ibraahiym (‘Alayhis Salaam).[2]

 

Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) akarudi kwao akiwa amefuatana na wake zake wawili, Bibi Sarah na Bibi Haajar, na kutokana na mke mpya Allaah Akamruzuku mtoto wa kiume waliyempa jina la Ismaa’iyl, jambo lililomfanya Bibi Sarah awe na wivu mkubwa juu ya mke mwenzake na baada ya kuamrishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa), Nabii Ibraahiym akamchukua Bibi Haajar pamoja na mwanawe Ismaa’iyl na kufunga nao safari ndefu kutoka Palastina hadi nchi ya Hijaazi (Saudia hivi sasa).

 

Alipowasili mji wa Makkah penye bonde baina ya Swafa na Marwa mahali kilipo kisima cha maji ya zamzam hivi sasa, na wakati huo hapakuwa na mtu yeyote anayeishi hapo, na nyumba ya Allaah (Al-Ka’abah) ilikuwa mfano wa mnyanyuko tu uliokuwa ukishambuliwa na upepo mkali pamoja na mikondo ya maji ya mvua iliyokuwa ikizikwanguwa pembe nne za nyumba hiyo.

 

Hapakuwa na mtu anayeishi mahali hapo wala nyumba wala maji isipokuwa mti mmoja tu ambao chini yake aliwaacha mkewe na mwanawe. Aliwawekea birika la maji pamoja na chombo alichowatilia tende ndani yake, kisha akageuka na kuianza safari ndefu ya kurudi Palastina.

 

Bibi Haajar mama yake Ismaa’iyl alipomuona mumewe akirudi na kuwaacha mahali hapo walipopafikia baada ya safari ndefu iliyowachukua siku nyingi njiani, mahali pasipo na mji wala kijiji, wala hata dalili ya mtu karibu na hapo, akamfuata mumewe na kumuuliza:

“Unatuachia nani mahali hapa pasipo na mtu yeyote?”

Alimuuliza hivyo mara nyingi lakini Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) hakumjibu, na alipomuuliza:

“Allaah ndiye aliyekuamrisha?”

Nabii Ibraahiym akajibu:

“Naam, ndiyo.”

Kwa imani iliyothibiti, na kwa utiifu mkubwa na moyo uliosalimu amri mbele ya maamrisho ya Allaah, Bibi Haajar akamwambia:

“Kwa hivyo Hatotupoteza”.

 

Kisha Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) akageuka na kuianza safari ndefu ya kurudi Palastina akiwaacha nyuma mkewe na mwanawe wa mwanzo na wa pekee wakati ule, na baada ya kutembea muda kidogo, akasimama mahali ambapo mkewe hakuweza kumuona, kisha aligeuka nyuma na kuomba dua ifuatayo:

رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُواْ الصَّلاَةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ

“Mola wetu! Hakika mimi nimewaweka (nimewakalisha baadhi ya kizazi changu (mwanangu Ismaa’iyli na mama yake Haajar) katika bonde (hili la Makkah) lisilokuwa na mimea yoyote; katika nyumba yako takatifu (ya Al-Ka’abah utakayotwambia tuijenge).

Mola wetu! Wajaalie wasimamishe Swala. Na ujaalie nyoyo za watu zieleke kwao (wapende kuja kukaa hapa ili pawe mji) na uwaruzuku matunda ili wapate kushukuru.”

Ibraahiym – 37

 

Nabii Ibraahiym alikuwa mara kwa mara akija Makkah kuwazuru mkewe na mwanawe, na hapana anayejua uhakika wa idadi ya ziara hizo, isipokuwa wanahistoria wameelezea juu ya ziara nne maarufu.

Ya mwanzo ni pale alipooteshwa kumchinja mwanawe wa pekee Ismaa’iyl (‘Alayhis Salaam) na mwanawe akakubali kutii amri aliyopewa baba yake ndani ya ndoto (na ndoto za Mitume ni wahyi), na alipomlaza mwanawe kifudifudi akijitayarisha kumchinja, Allaah Akamfunulia kuwa asimchinje mwanawe na badala yake akamkomboa kwa kondoo.

 

Kisa hicho kimeelezwa ndani ya kitabu cha Allaah Aliposema:

فَلَمَّا أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ. وَنَادَيْنَاهُ أَنْ يَا إِبْرَاهِيمُ. قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا إِنَّا كَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ. إِنَّ هَذَا لَهُوَ الْبَلَاء الْمُبِينُ. وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ

“Basi wote wawili walipojisalimisha (kwa Allaah), na akamlaza kifudifudi (amchinje).

Pale pale tulimwita; “Ewe Ibraahiym; Umekwishasadikisha ndoto. (Usimchinje mwanao).” Kwa yakini hivi ndivyo tunavyowalipa watendao mema.

Bila shaka (jambo) hili ni jaribio lililo dhahiri, (mtihani ulio dhahiri).

Basi tukamkomboa kwa mnyama wa kuchinjwa mtukufu.”

Asw-Swaaffaat – 103-107

 

Tutazitaja ziara tatu nyingine kila tunapoendelea mbele.

 

 

Haajar Na Kisima Cha Zamzam

Baada ya Nabi Ibraahiym kuondoka na kumuacha Bibi Haajar chini ya mtu ule, akawa anakula tende na kumnyonyesha mwanawe Ismaa’iyl, na haukupita muda mrefu maji yakaanza kupungua na hatimaye yakamalizika, na baada ya kumuona mwanawe akiteseka kwa kiu, akaanza kuhangaika huku na kule kutafuta maji.

Akaliendea jabali lililokuwa karibu yake ‘Jabal Swafaa’, akalipanda na kutazama huku na kule asione kitu.

 

Kisha akateremka na kutembea penye bonde baina ya Swafa na Marwa. Akawa anatembea taratibu, na alipofika katikati ya bonde akaanza kukimbia kidogo kidogo huku akiliendea jabali lililokabiliana nalo ‘Jabal Marwa’, akalipanda na kutazama huku na kule, na huko pia hakuona kitu.

Anasema Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Hiyo ndiyo Sa'ayi mnayotembea baina ya Swafaa na Marwa.”

 

Aliendelea kufanya hivyo mara saba, na alipokuwa akiliendea jabali Marwa alisikia sauti ngeni ikimsemesha, akasimama kimya apate kuiskia vizuri huku akitazama mahali alipo mwanawe, akamuona Malaika amesimama (mahali kilipo kisima cha Zamzam hivi sasa) huku akichimba kwa ubawa wake mpaka maji yalipopanda, na hapo ndipo mama yake Ismaa’iyl  alipoyaendea na kuanza kuyazuia kwa mikono yake huku akiyachota.

Imepokelewa kuwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Allaah amrehemu mama yake Ismaa’iyl, lau angeyaacha maji ya zamzam yaendelee basi yangegeuka kuwa chemchem.”

 

Mama yake Ismaa’iyl akaanza kumnywesha mwanawe maji hayo na yeye mwenyewe akawa anakunywa, na Malaika akamwambia:

“Usiogope hutopotea, kwani hapa ndipo ilipo nyumba ya Allaah itakayojengwa na mtoto huyu pamoja na baba yake.”

 

Haajar na Ismaa’iyl waliendelea kuishi hapo peke yao muda mrefu mpaka ulipopita msafara wa watu wa kabila la Jurhum uliopiga kambi sehemu ya chini ya mji wa Makkah, mbali na alipo mama yake Ismaa’iyl. Watu wa Jurhum walipomuona ndege akiruka sehemu ya mbali, mahali alipo mama yake Ismaa’iyl wakasema:

“Bila shaka ndege yule kule alipo ameona maji”, na kwa vile inajulikana kuwa sehemu zile si kawaida kupatikana maji, Jurhum waliamua kutuma mtumishi mmoja au wawili wakachunguze sehemu aliyoonekana ndege yule, watumishi wakakiona kisima cha maji ya Zamzam, na wakarudi kuwajulisha watu wao walioamua kuelekea huko haraka sana, na walipomuona mama yake Ismaa’iyl yuko pale wakamuomba wakae naye mahali hapo wakamwambia:

“Utaturuhusu tukae pamoja na wewe mahali hapa?”

Mama yake Ismaa’iyl akawaambia:

“Nitakuruhusuni, lakini maji haya ni yangu.”

Wakasema:

“Tumekubali.”

Anasema Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Jambo hilo lilimfurahisha sana mama yake Ismaa’iyl, kwa sababu alikuwa mwenye kupenda watu.”

 

Wengine wakashuka na wengine wakarudi kuwaita wenzao, na Ismaa’iyl akaishi pamoja nao, akajifundisha kwao lugha ya Kiarabu, akajifundisha kuwinda, na alipokuwa mkubwa wakamuozesha mmoja katika binti zao.

Baada ya kuishi muda walioishi, mama yake Ismaa’iyl akafariki dunia, na Ismaa’iyl akaendelea kuishi mahali hapo pamoja na watu wa kabila hilo la Jurhum

 

Nabii Ibraahiym alikuja kumtembelea mwanawe Ismaa’iyl katika ziara yake ya pili lakini bahati mbaya safari hii Ismaa’iyl hakuwepo nyumbani na alimkuta mkewe. Alipouliza mahali alipo Ismaa’iyl akamwambia:

“Ametoka kwenda kutafuta rizki.”

Nabi Ibraahiym akamuuliza mke wa Ismaa’iyl juu ya hali zao, akamjibu:

“Sisi ni wanadamu na hali zetu ni za dhiki na shida.”

Akaendela kumshitakia hali zao, na Nabi Ibraahiym alipokuwa akiondoka kurudi Palastina akamwambia:

“Akirudi mumeo msalimie kisha mwambie abadilishe kizingiti cha nyumba.”

Baada ya kupita siku nyingi, Ismaa’iyl (‘Alayhis Salaam) alirudi kutoka safari yake na alihisi kuwa jambo fulani limetokea nyumbani, akamuuliza mkewe:

“Alikuja mtu hapa?”

Mkewe akajibu:

“Ndiyo, alikuja mzee mmoja na wasfu wake ni hivi na hivi akauliza juu yako, na mimi nikamwambia ulipo, akaniuliza juu ya hali zetu, nikamwambia kuwa sisi ni wanadamu na kwamba hali zetu ni za dhiki na shida.”

Ismaa’iyl akamuuliza:

“Alikuachia salamu au maagizo yoyote?”

Akajibu:

“Ndiyo, aliniambia ukija nikusalimie kisha nikwambie ubadilishe kizingiti cha nyumba.”

Akamwambia:

“Yule alikuwa baba yangu na ameniamrisha nifarikiane na wewe, kwa hivyo rudi kwa wazee wako.”

 

Nabii Ismaa’iyl (‘Alayhis Salaam) aliowa mke mwingine, na inasemekana kuwa alikuwa binti wa Mudhaadh bin ‘Amru aliyekuwa mkuu wa kabila la Jurhum.

 

Baada ya miaka mingi kupita Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) alikuja tena kumtembelea mwanawe katika ziara ya tatu, na safari hii pia asimkute mwanawe, na alipomuuliza mkewe akamwambia:

“Amekwenda kutuletea mahitaji yetu.”

Ismaa’iyl alikuwa mwindaji anayesafiri sehemu za mbali kwa ajili ya kazi yake hiyo na huchukua muda mrefu safarini.

Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) akamuuliza:

“Vipi hali zenu?”

Akajibu:

“AlhamduliLlaah, tumo katika kheri kubwa.”

 Akawa anasema hivyo huku akimshukuru Allaah.

Nabii Ibraahiym akamuuliza:

“Mnakula chakula gani?”

 Akajibu:

“Nyama.”

Akamuuliza:

“Mnakunywa nini?”

Akajibu:

“Maji.”

Akamwambia:

“Mola wangu vibariki nyama na maji.”

Anasema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) :

“Na siku hiyo hawakuwa na chochote nyumbani kwao.”

Nabii Ibraahiym akamwambia:

“Akirudi mumeo mpe salam zangu, na umwambie akidhibiti vizuri kizingiti cha nyumba.”

Aliporudi Ismaa’iyl kama kawaida yake akauliza:

“Alikuja mtu leo?”

Akajibu:

“Alikuja mzee mmoja mwenye umbo zuri, akataka kujua habari zako, nikamjulisha, akaniuliza juu ya hali zetu nikamwambia kuwa tupo katika kheri.”

Akamuuliza:

“Alikuusia jambo lolote?”

Akamwambia:

“Ndiyo, yeye anakupa salamu nyingi na anakwambia ukidhibiti vizuri kizingiti cha nyumba yako.”

Akamwambia:

“Yule alikuwa baba yangu, na ananiamrisha nikamatane na wewe.”

 

Nguzo Za Al-Ka’abah

Baada ya kupita muda mrefu, Nabii Ibraahiym alikuja tena katika ziara yake ya nne ya kumtembelea mwanwe, na safari hii Ismaa’iyl alikuwepo nje ya nyumba yake chini ya mti karibu na kisima cha maji ya Zamzam akichonga mshale wake, na alipomuona baba yake alimnyanyukia kwa heshima kubwa, akamwamkia kama mtoto anavyoamuamkia baba yake kisha Nabii Ibraahiym akasema:

“Allaah Amenipa amri.”

Ismaa’iyl akamuuliza:

“Fanya kama ulivyoamrishwa na Mola wako.”

Akamwambia:

“Na wewe unisaidie.”

Akamwambia:

“Nitakusaidia.”

Akamwambia:

“Allaah Ameniamrisha nijenge nyumba mahali hapa….”

Akamuonesha sehemu ile ya ardhi iliyoinuka karibu na kisima cha maji ya Zamzam, kisha wote kwa pamoja wakaanza kufanya kazi ya kuzinyanyua nguzo za nyumba, na Ismaa’iyl akawa anamsogezea baba yake mawe huku Ibraahiym akijenga, mpaka nyumba ilipokamilika. Walikuwa wakijenga huku wakiomba dua ifuatayo:

“Ee Mola Wetu! Tutakabalie (tutakabalie amali yetu hii ya kujenga huu Msikiti.”

Allaah Anasema:

وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ

“Na Ibraahiymu alipoinua kuta za nyumba (hii ya Al-Ka’abah) na Ismaa’iyli (pia) (wakaomba wakasema) “Ee Mola Wetu! Tutakabalie (tutakabalie amali yetu hii ya kujenga huu Msikiti. Hakika wewe ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.”

Ibraahiym – 127

 

Na Akasema:

رَبَّنَا وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولاً مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِكَ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُزَكِّيهِمْ إِنَّكَ أَنتَ العَزِيزُ الحَكِيمُ

“Ee Mola Wetu! Waletee Mtume anayetokana na wao awasomee Aya Zako, na kuwafundisha Kitabu (chako) na hikima (nyingine) na awafundishe kujitakasa (na kila mabaya) hakika Wewe ndiye Mwenye, nguvu na ndiye Mwenye hikima.”

Al-Baqarah-129

 

Na hii ndiyo tafsiri ya hadithi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoulizwa juu ya mwanzo wa amri yake akasema:

“Mimi ni du’aa ya baba yangu Ibraahiym na bishara ya ndugu yangu ‘Iysa (‘Alayhis salaam).”[3]

 

Anasema Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa baada ya kukamilisha ujenzi wa nyumba ya Al-Ka’abah, Allaah Alimuamrisha Nabii Ibraahiym awatangazie watu waje kuhiji. Nabii Ibraahiym akasema:

“Ee Mola wangu vipi itawafikia sauti yangu.”

Akamwambia:

“Juu yako ni kutangaza na juu Yangu kuifikisha,” ndipo Nabii Ibraahiym alipotangaza:

“Enyi watu mumefaridhishiwa Hijjah katika nyumba kongwe.”

Anasema Al-Mubaarakpuri:

“Tangazo hilo likamfikia kila kiumbe baina ya mbingu na ardhi. Hamuoni kuwa watu wanauitikia mwito huo kutoka katika kila pembe ya dunia? Na katika riwaya: “Na watu wa mwanzo kuitikia mwito huo ni watu wa Yemen.[4]

 

Watoto Wa Ismaa’iyl

Allaah Alimruzuku Ismaa’iyl watoto kumi na mbili kupitia kwa mkewe binti wa Mudhaadh, na wote walikuwa watoto wa kiume na majina yao ni; Nabit au Banalut, Qaiydaar, Adbail, Mubsham, Mishma-a, Duma, Misha, Hadad, Yitma, Yatur, Nafiys, Qaydam, na kutokana na watoto hao yakapatikana makabila kumi na mbili yaliyoishi katika mji wa Makkah, na njia yao ya kujipatia riziki ilikuwa ni kufanya biashara na nchi za Yemen, Shaam na Misri.

Makabila hayo yalitawanyika sehemu mbali mbali za bara Arabu na hatimaye nje ya bara hilo na baada ya karne nyingi kupita mengi ya makabila hayo yalitoweka isipokuwa kabila la watoto wa Nabit na Qaydaar.

Kabila la watoto wa Nabit lilikuwa na shani kubwa sana katika nchi ya Hijjahz wakaweza kutawala nchi ya Hijjahz pamoja na nchi zilizo karibu yake na mji mkuu wao ulikuwa Batraa. Walieendelea kutawala kwa muda wa miaka mingi mpaka walipokuja kushindwa na Waroma.

Qaydaar na wanawe, wao waliendelea kuishi mji wa Makkah na waliendelea kuzaliana hapo mpaka alipozaliwa ‘Adnaan aliyemzaa Muad, na kutokana na wawili hao inapatikana nasaba ya waarabu wenye asili ya ‘Adnaaniyin.

 

Utawala Wa Makkah

Nabii Ismaa’iyl (‘Alayhis Salaam) aliishi miaka 137, na muda wote huo yeye ndiye aliyekuwa mkuu wa mji wa Makkah, na baada ya kufa kwake walitawala wanawe wawili Nabit kisha Qaydaar, na riwaya nyingine zinasema kinyume cha hivyo, yaani kwanza Qaydaar kisha Nabit, kisha akatawala babu yao Mudhaadh Al-Jurhumiy, na kutoka hapo utawala wa Makkah ukaingia mikononi mwa watu wa kabila la Jurhum.

Watoto wa Nabii Ismaa’iyl waliendelea kuwa na heshima kubwa sana hapo Makkah, lakini mambo yote ya kuhukumu nchi yalikuwa mikononi mwa Jurhum, walioendela kutawala miaka mingi huku wakitumia vibaya mali iliyokuwa ikipatikana kutokana na Al-Ka’abah, jambo lililojenga chuki kubwa baina yao na baina ya ‘‘Adnaaniyiin walioamua kushirikiana na watu wa kabila la Khuzaa na kulipiga vita kabila la Jurhum. Jurhum walishindwa na kutolewa nje ya Makkah, na hatimaye wakarudi Yemen.

 

Walipokuwa wakihama, watu wa Jurhum walikifukia kisima cha maji ya Zamzam kisiweze kujulikana tena, wakaondoa alama zote za karibu yake ili kuwanyima watu wa Khuzaa heshima ya kukimiliki kisima hicho, na wakazika ndani yake jiwe jeusi pamoja na panga na dhahabu nyingi.

Anasema Al-Mubaarakpuri katika ‘Ar-Rahiyq Al-Makhtuum’; “Inakadiriwa kuwa zama za Nabii Ismaa’iyl ni karne ishirini kabla ya kuzaliwa kwa Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) na kwa ajili hiyo inakisiwa kuwa Jurhum waliishi Makkah muda wa karibu karne ishirini na moja na walitawala muda wa karibu karne ishirini, kisha utawala ukashikwa na watu wa kabila la Khuzaa.”

 

Yemen

Watu wa kabila la Saba-a wanajulikana kuwa ni katika makabila ya zamani sana waliotawala nchi ya Yemen tokea mwaka 650 kabla ya kuzaliwa kwa Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam), isipokuwa katika mwaka wa 115 kabla ya kuzaliwa kwa Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) hadi mwaka 300 baada ya Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) kulitokea mapambano mengi ya wenyewe kwa wenyewe na mapinduzi mengi katika nchi ya Yemen, na utawala ukawa unabadilika mara kwa mara ukitoka mikononi mwa watu wa kabila la Hamyar na kurudi tena katika mikono ya Saba-a nk. jambo lililowafanya wawe chambo chepesi kwa Mataifa mengine, yaani vita vya panzi neema ya kunguru.

 

Katika mwaka 340 baada ya Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) Wahabashi wakaitumia fursa hiyo ya kupigana watu wa Yemen wenyewe kwa wenyewe kwa kuivamia kwa mara ya mwanzo nchi ya Yemen baada ya kusaidiwa na Warumi waliotangulia kuuteka mji wa Aden.

Wahabashi wakaendelea kuitawala nchi ya Yemen mpaka mwaka 378 baada ya Nabii ‘Iysa walipopata uhuru wao

Katika mwaka wa 523 baada ya Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) Myahudi mmoja aitwae Nuwaas aliwapiga vita watu wa Najran[5] na kuwalazimisha kuiacha Dini waliyokuwa wakiifuata ya Nabii ‘Iysa na kuingia Dini ya Kiyahudi, na walipokataa akachimba mahandaki makubwa na kuwasha moto ndani yake kisha akawa anawatupa ndani ya moto huo kila aliyekataa kufuata Dini yake, na hii ndiyo tafsiri ya kauli ya Allaah Aliposema:

 

“Wameangamizwa watu waliowaadhibu Waislamu katika mahandaki.

Yenye moto wenye kuni (nyingi).”

Suratul Buruuj – 4-5

 

Kutoka siku hizo Warumi walianzisha kampeni kubwa ya kuziteka nchi za Kiarabu huku wakiwasaidia Wahabashi katika kutayarisha jeshi kubwa,  wakawasaidia pia kuunda merikebu za vita, na katika mwaka wa 525 baada ya Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) Wahabashi wakafanikiwa kuiteka nchi ya Yemen kwa mara ya pili chini ya uongozi wa Irbat, na mfalme wa Uhabashi akampa Irbat ugavana wa Yemen na akatawala mpaka alipouliwa na Abraha Mhabashi aliyekuwa mmoja katika majemadari wa jeshi la Uhabashi, na Abraha huyu ndiye aliyepeleka jeshi lake Makkah likiongozwa na tembo kwa nia ya kuibomoa Al-Ka’abah, waliokuja kujulikana kwa jina la ‘Asw-haabul Fiyl’.

Baada Wahabashi kujaribu kuibomoa Al-Ka’abah, watu wa Yemen walighadhibika sana, kwa sababu waarabu wote walikuwa wakiiheshimu sana nyumba hiyo ya Allaah, na kwa ajili hiyo wakaomba msaada kutoka nchi ya Faris (Uajemi), na kwa pamoja wakafanikiwa kuwashinda Wahabashi na kuwatoa nje ya Yemen, wakawa huru chini ya uongozi wa Muad bin Yukrab bin Sayf bin Dhiy Yazin Al Hamyariy aliyejitangazia ufalme wa nchi hiyo, huku wakiwa chini ya himaya ya Waajemi mpaka nchi ya Yemen yote ilipoingia katika Uislamu mwaka 638 baada ya Nabii ‘Iysa.

 

Shaam na Iraq

Utawala katika nchi za Sham na Iraq ulikuwa ukiogelea ndani ya mkondo ule ule waliokuwa wakiogelea ndani yake watu wa Yemen na watu wote wa zama hizo katika kupigana vita, mara wenyewe kwa wenyewe na mara nyingine wakipigana dhidi ya Waajemi na mara nyingine wakipigna na Waroma.

Utawala wa nchi hizo ulikuwa ukibadilika mara kwa mara ukitegemea nguvu za mtawala. Mara ulikuwa chini ya ufalme wa Waajemi na mara nyingine chini ya makabila ya Kiarabu, na mara nyingine chini ya Waroma, isipokuwa nchi ya Hijaazi ilikuwa na shani kubwa mbele ya waarabu waliokuwa wakiitukuza sana na kuiheshimu kwa sababu ya kuwepo kwa nyumba ya Allaah ‘Al-Ka’abah’ katika ardhi yake, lakini watawala wa nchi hiyo hawakuwa na uwezo wa kupambana na majeshi makubwa kama ilivyokuwa pale Abraha alipokuja na jeshi lake kutaka kuibomoa Al-Ka’abah.

 

 

Dini Za Waarabu Kabla Ya Uislamu

Waarabu waliuitikia mwito wa Nabii Ismaa’iyl (‘Alayhis Salaam) alipowalingania katika Dini ya baba yake Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) wakawa wanakwenda kuhiji Makkah baada ya kutangaziwa na Nabi Ibraahiym.

Allaah Anasema:

وَأَذِّن فِي النَّاسِ بِالْحَجِّ يَأْتُوكَ رِجَالا وَعَلَى كُلِّ ضَامِرٍ يَأْتِينَ مِن كُلِّ فَجٍّ عَمِيقٍ

“Na (tukamwambia) “Utangaze kwa watu habari za Hijjah, watakujia (wengine) kwa miguu na (wengine) juu ya kila mnyama aliyekonda (kwa machofu ya njiani) wakija kutoka katika kila njia ya mbali.”

Al-Hajj – 27

 

Waarabu walikamatana na itikadi ya Tawhid, na maana yake ni kumpwekesha Allaah kwa kutomshirikisha na yeyote kati ya viumbe vyake katika ibada.

Na asili yake ni kauli aliyotamka Nabi Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) pale aliposema:

قُلْ إِنَّ صَلاَتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ. لاَ شَرِيكَ لَهُ وَبِذَلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَاْ أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ

“Sema; ‘Hakika Swalah yangu, na ibada zangu (zote nyingine) na uzima wangu, na kufa kwangu; (zote) ni kwa Allaah. Mwumba wa walimwengu wote.

Hana mshirika. Na haya ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa waliojielimisha (kwa Allaah).”

Al-An’aam-162 - 163

 

Waarabu waliendelea kuifuata itikadi hii sahihi kupitia karne nyingi, lakini vizazi vipya vilipozaliwa, itikadi hii ikaanza kusahaulika na ushirikina ukaanza kujitokeza.

 

Anasema Shaykh Abu Bakr Al-Jazaairiy katika kitabu chake ‘Haadhal Habiyb’:

“Jambo lisiloshaka ni kuwa Haajar mama yake Ismaa’iyl (‘Alayhis Salaam) alikuwa Muislamu na kwamba mwanawe Ismaa’iyl alikuwa Muislamu pia, kama alivyokuwa baba yake Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) na kwamba hao wawili ni Mitume ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) waliowalingania watu wao na watu wa kabila la Jurhum Dini ya Allaah na wao wakaingia katika Dini hiyo na kwa muda mrefu usiojulikana uhakika wake watu wa bara Arabu walikuwa wakimuabudu Allaah mmoja Asiye na mshirika.

Nabii Ismaa’iyl alipofariki dunia, watoto wake waliendelea katika hali hiyo mpaka zilipopita karne nyingi tokea kukatika kwa wahyi na kusahau yale waliyokuwa wakikumbushwa, watu wakaanza kubadilisha kidogo kidogo na kuingiza ushirikina katika Dini ya Allaah.”

 

 

Wa Mwanzo Kufanya Shirk

Wa mwanzo kuanzisha ushirikina walikuwa watoto waliofuatilia wa Nabii Ismaa’iyl waliokuwa wakichukua mawe ya Msikiti wa Al-Ka’abah kila wanapotoka kwa ajili ya kutafuta rizki au wanaposafiri. Walikuwa kila wanapowasili mahali wakiyaweka mawe hayo juu ya ardhi na kuanza kutufu kwa kuyazunguka mawe hayo kama walivyokuwa wakitufu kuizunguka Al-Ka’abah huku wakimuomba Allaah, na kuanzia wakati huo kizazi kipya kikazuka kilichokuwa kikimshirikisha Allaah kwa ujahili wao wakidhani kuwa huko ndiko kujikurubisha,[6] isipokuwa waarabu waliendelea kuzikamata baadhi ya ibada alizokuja nazo Nabi Ibraahiym (‘Alayhis Salaam).

 

Ama wa mwanzo kuyaingiza masanamu ndani ya Msikiti wa Al-Ka’abah alikuwa ‘Amru bin Luhay mkuu wa kabila la Khuzaa waliotawala Makkah baada ya kuwapiga vita Jurhum na kuwashinda.

Mtu huyu alikuwa mchaji Allaah sana aliyekuwa akiheshimika baina ya watu wake, akipenda kuwasaidia masikini na kuwaendea mbio watu wa kabila lake, na kwa ajili hiyo wakampenda na kumdhania kuwa ni mtu mwenye elimu kubwa katika Dini na kwa ajili hiyo hapana aliyethubutu kulirudisha neno lake.

 

Aliposafiri kwenda nchi ya Shaam, ‘Amru bin Luhay aliwaona watu wa huko wakiyaangukia na kuyaabudu masanamu, jambo lililomfurahisha sana hasa kwa vile Mitume wengi wametokea huko, na vitabu vingi vimeteremshiwa huko, akadhani kuwa watu hawa wako katika haki.

Akawauliza: “Ni kitu gani haya masanamu mnayoyaabudu?”

Wakamuambia: “Tukiyaomba mvua yanatuletea na tukipigana vita yanatuletea ushindi.”

Akawaambia: “Namimi nipeni mmoja nimpeleke kwa waarabu na wao wapate kuwaabudu.”

Akapewa sanamu anayeitwa Hubal, akarudi naye Makkah na kumuingiza ndani ya Al-Ka’abah, na kuwafundisha watu wa Makkah namna ya kumuabudu kama alivyowaona watu wa Shaam na watu wa Makkah wakamtii, na haukupita muda mferu watu wa Hijaaz nao wakaingia katika mkumbo huo.

Nabii Ibraahiym aliwafundisha watu wake kuwa pale wanapotufu wawe wakisema:

“Labbayka Llaahumma Labbayk, Labbayka Laa Shariyka Laka Labbayka, Inna L’hamda Wanni’mata Laka Wal Mulk Laa Shariyka Laka ,” na maana yake ni:

“Nakuitikia Ee Mola wangu nakuitikia, nakuitikia Ee uso mshirika nakuitikia. Hakika shukrani zote na neema zote ni zako pamoja na ufalme (wote ni wako pia) ewe uso mshirika.”

 

Baada ya kuyaingiza masanamu ndani ya Al-Ka’abah, ‘Amru bin Luhay akawataka watu wake wawe wakiongeza kwa kusema:

“Labbayka la shariyka laka illa sharikan huwa laka tamlikuhu wama malaka.”

Na maana yake:

“Nakuitikia ewe uso mshirika isipokuwa mshirika kiumbe chako unayemmiliki na yeye hajamiliki.”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Nilioneshwa ‘Amru bin Luhay akiwa motoni huku akiburura matumbo yake, yeye ni wa mwanzo kuibadilisha Dini ya Allaah.”[7]

 

‘Amru bin Luhay akauendeleza uzushi wake huo kwa kuyataka makabila na Mataifa mbali mbali ya Kiarabu kila mmoja awe na sanamu lake, na alipotambua kuwa watu wa Nabi Nuuh (‘Alayhis Salaam) walikuwa wakiyaabudu masanamu ya Wadda na Suwa’a na Yaghuutha na Ya’uqa na Nasra, akawa kila Taifa na kabila linalokuja Makkah akiwapa sanamu lao na kuwataka waliabudu wao na watu wao.

Ushirikina ukazidi na masanamu yakaongezeka na kugawiwa kama ifuatavyo:

Hubal - watu wa Makkah

Lata na Umyani - watu wa Twaaif

‘Uzza – watu wa bonde la Nakhla

(Na haya ni masanamu matatu makubwa kupita yote)

Kabila la Hudhayl – Suwa-a na wengine wakapewa Wadda na Ya’uqa na Yaghuutha na ‘Wadda’, na ‘Yaghuutha’.

Nasra - watu wa Yemen

Manaata – watu wa makabila ya ‘Aws na Khazraj.

Hivi ndivyo ilivyokuwa mpaka ikawa katika kila kabila na katika kila nyumba mna sanamu linaloabudiwa kinyume na amri ya Allaah na kila kabila na Taifa lilikuwa na sanamu lake ndani ya Al-Ka’abah, na Msikiti ukajaa masanamu na siku ile Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipouteka mji wa Makkah alikuta masamu yapatayo mia tatu na sitini ndani ya Msikiti, akawa anaisukuma na kuyagonganisha huku yakianguka na kuvunjika, kisha akatoa amri ya kuyatoa nje ya Msikiti.

Namna hi ushirikina ulienea bara ya Arabu yote wakati wa ujahilia baada ya kusahau mafundisho aliyookuja nayo Nabi Ibraahiym (‘Alayhis Salaam).

 

 

Dini Ya Kiyahudi

Mayahudi waliwasili bara Arabu kutoka nchi ya wa Palastina kwa mara ya mwanzo katika mwaka wa 578 kabla ya kuzaliwa Nabii ‘Iysa, na hii ilikuwa baada ya Bukhtinassar kuiteka nchi yao na kubomoa hekalu lao na kuwateka watu wao, na baadhi yao wakafanikiwa kukimbilia chi ya Hijaazi (Saudia sasa).

 

Katika mwaka wa 70 baada ya kuzaliwa kwa Nabii ‘Iysa kundi lingine la Mayahudi lilihamia nchi ya Hijaazi baada ya nchi  yao kutekwa na Warumi na wengi wao kuuliwa, na hekalu lao kubomolewa.

Walifikia mji wa Madiynah na wakati huo ulikuwa ukiitwa Yathrib, wakafanikiwa kuyaingiza baadhi chache ya makabila ya Kiarabu katika Dini yao.

 

Walipowasili Madiynah walijenga ngome zao, na iliyo mashuhuri kupita zote ni ile ngome ya Khaybar iliyobomolewa na majeshi ya Kiislamu katika vita vya kuuteka mji huo.

Dini ya kiyahudi iliingia na kuenea katika nchi ya Yemen kupitia mfalme wao Tuban aliyeingia Dini ya Kiyahudi alipokwenda Yathrib kwa ajili ya kupigana nao vita, lakini Mayahudi wa kabila la bani Quraydhwah walifanikiwa kumkinaisha aingie katika Dini yao, akaondoka hapo na kurudi Yemen akifuatana na maulamaa wawili wa kiyahudi kwa ajili ya kuwafunza watu wake Dini yake hiyo mpya”.

 

Tuban alipofariki dunia alimtawaza mwanawe Yuusuf bin Nuwaas aliyetaka kuwalazimisha watu wa Najran kuingia katika Dini ya kiyahudi, na walipokataa akaamrisha handaki kubwa lichimbwe na moto mkali uwashwe ndani yake kisha akwaamrisha maaskari wake kuwaingiza ndani humo kila aliyekataa kufuata amri yake,

Inakisiwa kuwa idadi ya waliouliwa siku hiyo ni baina ya elfu ishirini hadi elfu arubaini watoto kwa wakubwa, wanawake kwa wanaume, na kisa hiki kama tulivyotangulia kueleza kuwa kimetajwa katika Qur-aan tukufu.

 

 

Dini Ya Kinasara

Ama Dini ya kinasara iliingia bara Arabu kupitia utawala wa Warumi wakisaidiana na Wahabashi baada ya kufanikiwa kuitawala nchi ya Yemen katika mwaka 340 baada ya Nabii ‘Iysa, na ikaendelea kusitawi na kuenea pembe zote za Yemen, na katika nchi ya Sham na Iraq Dini hiyo iliingia kupitia kwa washambulizi wa Kirumi.

 

 

Majusi

Dini ya Majusi ilikuwa na wafuasi wachache miongoni mwa Waarabu, wengi wao wakiwa wale walioishi sehemu zilizopakana na nchi ya Iran kama vila Iraq na Bahrain na Al Hassa na sehemu nyingine chache zilizo kando kando ya Ghuba ya waarabu na katika nchi ya Yemen pia wakati ilipotawaliwa Waajemi.

 

Sabaiya

Anasema Al-Mubaarakpuri katika Ar-‘Rahiyq Al-Makhtuum’ kuwa uchimbaji wa ardhi uliofanyika katika nchi ya Iraq umegunduwa kuwa watu wake walikuwa wafuasi wa Dini ya Sabaiya na hii ni Dini Iliyokuwa ikifuatwa na watu wa Nabi Ibraahiym wa kabila la Kaldani na inajulikana pia kuwa wengi katika watu wa Sham na Yemen waliingia katika Dini hii lakini baada ya kuingia kwa Dini ya Kinasara na ya Kiyahudi, wafuasi wa Dini ya Sabaiya walianza kufifia na hatimae wakatoweka.

 

 

Dini Za Waarabu

Hizo ndizo Dini zilizokuwa zikifuatwa katika bara ya Arabu kabla ya kuja kwa Dini ya Kiislamu, na wote walikuwa katika upotofu kwa kuacha mafundisho waliyopewa na Mitume yao na kufuata matamanio ya nafsi zao kwa kuzusha na kuongeza kile walichodhania kuwa kitawafaa na kwa kuacha na kukikataa kile wasichopendezewa nacho.

 

Washirikina waliokuwa wakijigamba kuwa wanafuata Dini ya Nabi Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) waliacha mafundisho sahihi ya Tawhiyd waloletewa na Mtume wao na badala yake wakawa wanamshirikisha Allaah kwa kuzusha kila aina ya bida’h na ushirikina.

 

Wakaachana na tabia na mwenendo mwema aliokuja nao Mtume wao na badala yake wakafuata matamanio ya nafsi kwa kupenda mali, utukufu, na uluwa.

Ama Mayahudi, wao walikuwa na viongozi wenye kupenda ufalme, wenye kupenda kutoa hukmu baina yao na kujigeuza mfano wa miungu mingine wasiokuwa Allaah bila kujali mafundisho ya Dini yao.

 

Masihi (Wakristo) nao wakavumbua fikra ya muungano baina ya mwanadamu na Allaah jambo lililopunguza taathira katika nyoyo za wacha Allaah wa Kiarabu wakashindwa kufahamu vizuri na wengi wakaiacha Dini hiyo na kwa ajili hiyo wengi wao wakarudi kuabudu masanamu.

 

 

Walikuwepo Waongofu

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Allaah Aliwatazama watu waliopo ardhini akawachukia waarabu na wasio waarabu isipokuwa wachache katika watu walioteremshiwa kitabu...”[8]

 

Na hi ni kwa sababu katika bara Arabu yote hapakuwa na waongofu waliokuwa wakimuabudu Allaah peke yake wakati huo isipokuwa wawili tu na majina yao ni Zayd bin Amru bin Nofeil na Qus bin Saaidah ambaye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoulizwa juu yao alisema:

“Atafufuliwa siku ya Qiyaamah (mmoja) peke yake akiwa (sawa na) umma.”[9]

‘Amru bin Nawfal alikuwa bila uoga akikanusha matendo ya kijahilia mbele ya washirikina na alikuwa akisema:

“Naapa kwa yule ambaye nafsi ya ‘Amru imo mikononi mwake, hapana yeyote kati yenu anayefuata Dini ya Ibraahiym isipokuwa mimi.”[10]

Alifariki kabla ya kuja kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na huyu anaingia katika kundi lililotajwa katika hadithi iliyotanguliwa isemayo:

“Allaah Aliwatazama watu waliopo ardhini akawachukia waarabu na wasio waarabu isipokuwa wachache katika watu walioteremshiwa Kitabu...”[11]

 

Ama Qussa bin Sa’idah, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema juu yake:

“Allaah Amrehemu Qussa” na alipoulizwa:

“Ewe Mtume wa Allaah unamuombea rehema Qussa?”

Akajibu:

“Hakika yeye alikuwa katika Dini ya baba yangu Ismaa’iyl mwana wa Ibraahiym.”[12]

 

Na kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema:

“Ulikuja ujumbe wa Bani Qays kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza:

“Yupi kati yenu mwenye kumjua Al Quss bin Saaidah Al Ayadi?”

Wakasema:

“Sote.”

Akauliza tena:

“Yuwapi?”

Wakajibu:

“Keshakufa.”

Akasema:

“Siwezi kumsahau hata siku moja siku ile alipokuwa katika soko la Akadha juu ya ngamia wake akisema:

“Enyi watu! Anayeishi atakufa, na atakayekufa keshapita, na kila linalokuja litakuja, hakika mbinguni yapo matarajio na katika ardhi yapo mazingatio, ardhi iliyotandazwa na sakafu zilizonyanyuliwa na kusambazwa na nyota zinazoangaza na maji ya bahari yasiyopunguzwa’ – Kisha Quss akaapa kiapo akasema: ‘Hakika Allaah anayo Dini anayoipenda kuliko hiyo yenu mliyokuwa nayo. Mbona naona watu wanakwenda wala hawarudi? Waliridhika wakabaki au waliachwa wakalala na kurudi hawataki.”[13]

 

Quss huyu alifariki dunia kabla ya kupewa utume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Ama Mayahudi na Manasara wao walibaki wachache sana waliokuwa wakimuabudu Allaah sawa kama walivyoamrishwa na Nabi Musa na ‘Iysa (‘Alayhis Salaam), na kutokana uchache wao hawakuweza kupata wafuasi.

Mmoja wao alikuwa Waraqah bin Nawfal aliyekuwa akifuata Dini ya Kinasara na alifariki dunia kabla ya kupewa utume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  na Waraqah huyu aliwahi kumwambia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) :

"Yareti ningeliishi mpaka siku ile watu wako watakapokutoa katika nchi yako".

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza;

“Hivyo watakuja kunitoa?”

Waraqah akasema:

“Ndiyo, hapana aliyekuja na haya ulokuja nayo wewe isipokuwa lazima atafanyiwa uadui, na nikijaaliwa kuishi mpaka siku hiyo, basi nitakusaidia mpaka utakapopata ushindi”.

 

Waraqah alifariki dunia siku chache baada ya kupewa Utume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Mwengine alikuwa ‘Abdullaah bin Jahsh bin Rithab aliyesilimu kisha akarudi katika Dini ya Kinasara mara baada ya kuwasili Uhabashi baada ya kuhajir yeye pamoja na Waislamu katika hijra ya mwanzo akamwacha mkewe Ummu Habiybah binti Abi Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘anha)) aliyeolewa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Tabia Nzuri Tabia Za Waarabu Kabla Ya Kuja Kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Kabla ya kuja kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), waarabu walikuwa na tabia zao njema na mbaya.

Miongoni mwa tabia njema ni kama ifuatavyo:

              Kusema kweli, na hii ni tabia waliyokuwa nayo waarabu hata kabla ya kuja kwa Dini ya Kiislamu, na ulipokuja Uislamu uliitilia nguvu.

              Kumkirimu mgeni, na ulipokuja Uislamu ukaitilia nguvu tabia hiyo aliposema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) :

“Mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Akhera amkirimu mgeni wake.”[14]

 

              Kutimiza ahadi. Hata iwe thamani yake kubwa namna gani mtu alikuwa hana budi kuitimiza ahadi yake na Uislamu ukautilia nguvu mwenendo huu.

              Kumheshimu jirani

              Subira na ustahamilivu

              Ushujaa

              Kuoga wanapokuwa na janaba

              Kuhiji na kufanya ‘Umrah

Hizi kwa ujumla ni baadhi ya tabia na mwenendo mwema waliokuwa nazo waarabu, juu ya kuwa si wote waliokuwa wakizifuata, lakini wengi wao walikuwa na tabia hizo.

 

 

Tabia Mbaya

Walikuwa wakipenda kufuata matamanio ya nafsi zao bila kujali matokeo yake.

Kufru ilienea, na kuikanusha Siku ya Qiyaamah lilikuwa ni jambo la kawaida. Walikuwa wakisema:

“Ni matumbo tu yanatoa na ardhi inameza.”

 

Allaah Aliwatolea hoja mbali mbali ndani ya Qur-aan tukufu, na hapa tutataja mfano mmoja:

Katika Suratu Qaaf Allaah Anasema:

فَقَالَ الْكَافِرُونَ هَذَا شَيْءٌ عَجِيبٌ . أَئِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا ذَلِكَ رَجْعٌ بَعِيدٌ. قَدْ عَلِمْنَا مَا تَنقُصُ الْأَرْضُ مِنْهُمْ وَعِندَنَا كِتَابٌ حَفِيظٌ

“Na wakasema makafiri; ‘Hili ni jambo la ajabu.

Kuwa tutakapokufa na tukawa udongo kuwa tutafufuliwa? Marejeo hayo ni ya mbali kabisa (hayawezi kuwa).”

(Allaah Akawajibu;)

“Kwa hakika tunajua kiasi cha kila kinachopunguzwa na ardhi katika miili yao) wakati wanapooza huko makaburini). Na kwetu kiko Kitabu kinachohifadhi (kila kitu).”[15]

Qaaf - 2-4

 

Kutakabari, na kuikanusha haki, mfano wa kauli ya Amru bin Hishaam (Abu Jahl) alipokuwa akiukanusha ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

“Tulichuana na watu wa kabila la ‘Abdu Manaaf (kabila la Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika heshima kama farasi wanavyochuana katika mashindano, sasa wanatuambia: “Katika kabila letu tunaye Mtume anayefunuliwa wahyi.” WaLlaahi hatumuamini wala hatumfuati abadan, ila kama na sisi tutafunuliwa wahyi kama anavyofunuliwa yeye.”

 

Waliyd bin Mughiyrah naye pia aliwahi kumwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) maneno yafuatayo:

“Kama ni utume kweli, basi mimi ndiye ninayestahiki zaidi kuliko wewe, kwa sababu mimi ni mkubwa wako kwa umri na nina mali kukupita.”

 

Walikuwa wakipenda kucheza kamari, na Allaah Akaiharamisha aliposema katika Suratul Maidah:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالأَنصَابُ وَالأَزْلاَمُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

“Enyi mlioamini! Bila shaka ulevi na kamari na kuabudiwa (na kuombwa) asiyekuwa Allaah na kutazamia kwa mishare ya kupiga ramli ni uchafu katika kazi ya Shaytwaan. Basi jiepusheni navyo ili mpate kufaulu.[16]

Al-Maaidah - 90

 

        Kulewa, kuua watoto wa kike wangali wachanga eti wakihofia wasije wakaleta aibu pale watakapokuwa.

        Kuua hata na watoto wa kiume umasikini unapozidi.

        Kutoka wanawake huku wakionyesha mapambo yao wakipita mbele ya wanaume kwa maringo.

        Kuweka wanawake kinyumba

        Kuweka bendera nyekundu nje ya nyumba za wanawake wanaouza miili yao

        Chuki za kikabila na kushambuliana na kupigana vita mara kwa mara baina yao na kutekana mali zao, na vita mashuhuri ni vile vilivyojulikana kwa jina la ‘Da’is na Ghabraa’ vilivyopiganwa kwa muda wa miaka arubaini[17], na vita vingine vilivyodumu miaka mingi ni vita vinavyojulikana kwa jina la ‘Harbul fujaar’ na ‘Harb Bu’ath’[18]

 

Hii ndiyo hali waliyokuwa ndani yake kabla ya kuja kwa Mtume wa Allaah Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), waarabu walikuwa katika ukingo wa kuporomoka.

Allaah Anasema:

وَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ لَوْ أَنفَقْتَ مَا فِي الأَرْضِ جَمِيعاً مَّا أَلَّفَتْ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ وَلَـكِنَّ اللّهَ أَلَّفَ بَيْنَهُمْ إِنَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Na akaziunga nyoyo zao (wote hao Maswahaba wako); hata kama ungalitoa vyote vilivyomo ardhini usingaliweza kuziunga nyoyo zao, lakini Allaah ndiye aliyewaunganisha. Hakika Yeye ni Mbora na Mwenye hikima.”[19]

Al-Anfaal – 63

 

Na akasema katika Surat Aali Imran:

وَاعْتَصِمُواْ بِحَبْلِ اللّهِ جَمِيعًا وَلاَ تَفَرَّقُواْ وَاذْكُرُواْ نِعْمَةَ اللّهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنتُمْ أَعْدَاء فَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَأَصْبَحْتُم بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا وَكُنتُمْ عَلَىَ شَفَا حُفْرَةٍ مِّنَ النَّارِ فَأَنقَذَكُم مِّنْهَا كَذَلِكَ يُبَيِّنُ اللّهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ

“Na shikamaneni kwa kamba (Dini) ya Allaah nyote, wala msiachane.  Na kumbukeni neema ya Allaah iliyo juu yenu (Zamani) mlikuwa maadui; naye akaziunganisha nyoyo zenu hivyo, kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la moto (wa Jahannam) naye akakuokoni nalo. Namna hivi Allaah anakubainishieni Aya zake ili mpate kuongoka.”[20]

Aali-‘Imraan – 103

 

 

Nasaba Yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

Anasema Al-Mubaarakpuri katika kitabu chake ‘Ar-Rahiyq Al-Makhtuum;

Nasaba ya Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) imegawika sehemu tatu tutakazozitaja hapo chini:

 

Sehemu ya mwanzo inayomalizikia kwa ‘Adnaan inakubaliwa kuwa ni sahihi na maulamaa wote wa Siyrah na wale wanaodurusu nasaba za watu mashuhuri.

Sehemu ya pili inayoanzia kwa ‘Adnaan na kumalizikia kwa Nabi Ibraahiym (‘Alayhis Salaam), wapo katika wanavyuoni wanaoikubali kuwa yote ni sahihi, na wapo wanaoutilia shaka usahihi wa baadhi yake.

Ama sehemu ya tatu, inayoanzia kwa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) na kumalizikia kwa Adam (‘Alayhis Salaam), hii maulamaa wote takriban wanautilia shaka usahihi wake.

 

Sehemu ya kwanza ya nasaba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka kufikia kwa ‘Adnaan (inayokubaliwa na maulamaa wote kuwa ni sahihi) ni kama ifuatavyo:

1.           Muhammad bin ‘Abdillaah bin ‘Abdil-Muttwallib (aliyekuwa maarufu kwa jina Shaybatul Hamd) bin Haashim (jina lake hasa ni ‘Amru) bin ‘Abdu Manaaf (akijulikana pia kwa jina la Al-Mughiyrah) bin Qusay (jina lake ni Zayd) bin Kilaab bin Murrah bin Ka’ab bin Luay bin Ghaalib bin Fihr (na huyu ndiye aliyekuwa akijulikana kwa jina la Quraysh na asili ya watu wote wa Kabila la Quraysh inatokana na huyu) bin Maalik bin Nadhar (jina lake hasa ni Qays) bin Kinaanah bin Khuzaymah bin Mudrikatah (na jina lake hasa ni ‘Aamir) bin Ilyaas bin Madhar bin Nizar bin Ma-adi bin ‘Adnaan.

 

Sehemu ya pili inayoanzia kwa ‘Adnaan kwenda juu:

2.   ‘Adnaan bin ‘Aadd bin Hamiyj bin Salaamaan bin Iwaas bin Bawz bin Qamwal bin Ubay bin Iwaam bin Nashid bin Hazaa bin Baldaas bin Badlaf bin Tabikh bin Jahim bin Nahish bin Makhiy bin Abadh bin Abqar bin Abiyd bin Ad da-a bin Hamdan bin Saniyr bin Yathribiy bin Yahzan bin Yalhan bin Ar-awiy bin Ais bin Dishan bin Aysar bin Afnad bin Ayham bin Maqsar bin Nahith bin Zarih bin Samiy bin Maziy bin Awadhah bin Iram bin Qaydaar bin Ismaa’iyl bin Ibraahiym (‘alayhima ssalaam).

 

Ama sehemu ya tatu inayoanzia kwa Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) ni kama ifuatavyo:

3.       Ibraahiym bin Tarih (ambaye jina lake hasa ni Aazar) bin Nahur bin Saruh bin Sarugh bin Rauw bin Falikh bin Amir bin Shalikh bin Arafkhashad bin Sam bin Nuuh (‘Alayhis Salaam) bin Lamik bin Mutawashlakh bin Akhnukh (inasemekana kuwa huyu ndiye Nabii Idriys (‘Alayhis Salaam)) bin Yarad bin Mahlayl bin Qaynaan bin Anushah bin Shiyth bin Adam (‘Alayhis Salaam).

 

 

Ukoo Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

Ukoo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) unajulikana kwa jina la Ukoo wa Haashim (Bani Haashim), na Haashim huyu ni babu yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa mtu mkarimu sana mwenye kuheshimika miongoni mwa watu wa kabila lake, na kwa ajili hii alipewa yeye jukumu la kuwanywisha na kuwalisha mahujaji waliokuwa wakija kutufu Al-Ka’abah, na hili lilikuwa ni jukumu adhimu sana analopewa mtu mwenye kuheshimika sana katika watu wa Makkah wakati ule.

 

Haashim alikuwa mtu wa mwanzo kuwalisha mahujaji chakula maarufu kinachoitwa ‘Thariyd’, nacho ni mikate mikavu inayokatwakatwa na kuchanganywa na mchuzi wa nyama. Heshima ya chakula hiki katika kuwakaribisha wageni ni mfano wa heshima ya biriani katika jamii yetu.

Jina lake hasa lilikuwa ni ‘Amru, lakini alipewa jina hili la Haashim kwa sababu yeye mwenyewe ndiye aliyekuwa akiikatakata mikate mikavu kwa ajili ya kutayarisha chakula hicho cha ‘Thariyd’.

Na neno ‘Haashim’ katika lugha ya Kiarabu maana yake ni kitu kikavu kilichokatikakatika.

Allaah Anasema juu ya mimea ya ardhi:

فَأَصْبَحَ هَشِيمًا تَذْرُوهُ الرِّيَاحُ

Fa aswbaha ‘Hashiyman’ tadhruwhu rriyahu” na maana yake (mimea Ikawa majani makavu yaliyokatikatika ambayo upepo huyarusha huku na kule).

Al-Kahf – 45

 

Imepokelewa kuwa Haashim alipokuwa akienda nchi ya Sham katika safari zake za kibiashara alipita Madiynah na alipokuwa hapo alimuoa Bibi mmoja aitwae Salma binti ‘Amru anayetokana na kabila la bani Najjar, akakaa naye muda wa siku chache kabla ya kuendelea na safari yake kwenda Sham na kumuacha Bibi Salma kwa wazee wake akiwa na mimba ya ‘Abdul-Muttwallib bila watu wake waliopo Makkah kujua.

Wakati Haashim alipokuwa safarini, Salma alimzaa ‘Abdul-Muttwallib, lakini Haashim hakuweza kurudi kwani alifariki dunia akiwa Gaza nchi ya Palastina.

 

‘Abdul-Muttwallib alizaliwa katika mwaka wa 497 baada ya Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) na akapewa jina la Shaybatul Hamd kutokana na unywele mmoja wa mvi aliokuwa nao kichwani, kwa sababu neno ‘Shaybah’ katika lugha ya Kiarabu maana yake ni mvi.

Bibi Salma aliyekuwa akiishi nyumbani kwa baba yake huko Madiynah alimlea mwanawe ‘Abdul-Muttwallib malezi bora.

Haashim alikuwa na watoto wa kiume wanne, watatu walikuwa Makkah na mmoja ambaye ni ‘Abdul-Muttwallib aliyekuwa Madiynah kwa mama yake, na majina yao ni; Asad na Abu Sayf na Nadhlah na ‘Abdul-Muttwallib, na alikuwa na watoto wa kike watano nao ni Ash-Shifaa na Khaalidah na Dhaifah na Ruqayyah na Jannah.

 

Jamaa zake walioko Makkah hawakuwa na habari zozote juu ya ndugu yao ‘Abdul-Muttwallib aliyekuwepo Madiynah, lakini habari zilimfikia Al Muttwallib ndugu yake Haashim ambaye ni ami yake ‘Abdul-Muttwallib aliyeifunga safari ya kwenda Madiynah kumchukua mtoto wa ndugu yake.

Al-Muttwallib alilia sana alipomuona ‘Abdul-Muttwallib, akambeba na kumbusu na kumkumbatia huku akilia kwa furaha, kisha akamtaka ende naye Makkah, lakini ‘Abdul-Muttwallib alikataa na kumwambia kuwa hawezi kuondoka bila ya ruhusa ya mama yake.

Mama yake alikubali baada ya kuombwa sana na kushikiliwa, lakini alipotakiwa na yeye afuatane nao Makkah alikataa na akachagua kubaki kwa wazee wake hapo Madiynah.

 

Al-Muttwallib aliingia Makkah akiwa amempakia ‘Abdul-Muttwallib juu ya ngamia na watu walipomuona walikuwa wakisema:

“Huyu hapa ‘Abdul-Muttwallib!”

Al-Muttwallib akawa anasema:

“Ole wenu! Huyu ni mwana wa ndugu yangu Haashim.”

 

Akamlea nyumbani kwake mpaka alipokuwa mkubwa, na Al-Muttwallib alipofariki akiwa safarini katika nchi ya Yemen mji wa Radman, watu wakamchagua ‘Abdul-Muttwallib kuwa kiongozi wao, akawa anatenda yale wazee wake waliyokuwa wakitenda katika heshima ya kuwalisha na kuwanywisha mahujaji. Alikuwa mkarimu sana na watu wake wakampa jina la ‘Al-Fayaadh’ na maana yake ni ‘Mkarimu sana’, akapata heshima kubwa sana asiyowahi kupata yeyote katika wazee wake waliotangulia na watu wake wakampenda sana na kumtukuza.[21]

 

Mambo Adhimu Yaliyotokea Kabla Ya Kuja Kwa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

Bila shaka jambo lolote adhimu hutanguliwa na matukio, dalili na bishara mbali mbali adhimu yakiwa kama ni ishara ya kulikaribisha jambo hilo. Na wanadamu hawajapata kutokewa na jambo adhimu kuliko hili la kuzaliwa kwa Al-Habiyb Al-Mustwafaa (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Kufukuliwa Kisima Cha Zamzam

Anasema Ibn Kathiyr katika ‘Al-Bidaayah wan-Nihaayah’:

“Amesema Ibn Is-haaq; nimehadithiwa na Yaziyd bin Abi Habib Al-Masri kutoka kwa Murthad bin ‘Abdillaah Al-Yazni kutoka kwa ‘Abdullaah bin Zarir al-Ghafiqiy kuwa alimsikia ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) akihadithia hadithi ya Zamzam alipoamrishwa ‘Abdul-Muttwallib kukichimba. Anasema: “Alisema ‘Abdul-Muttwallib:

“Nilipokuwa nimelala chumbani kwangu nikasikia sauti usingizini ikiniambia; ‘Chimba At-Tiyba’.

Akasema:

“Nikauliza; ‘Nini At-Tiyba?’ lakini mtu huyo akatoweka.”

Ulipoingia usiku wa pili yake nikaenda kitandani pangu kulala na mtu yule akanijia tena usingizini, akaniambia:

“Chimba Barrah,’ nikamuuliza:

“Ni nini hii Barrah?” kisha akatoweka tena. Na usiku uliofuata nikaenda kitandani pangu kulala, akanijia akaniambia:

“Chimba Al-Madhnuwnah,” nikamuuliza:

“Nini Al-Madhnuwnah?” akatoweka. Usiku uliofuata nikaenda kitandani kulala, akanijia tena akaniambia:

“Chimba Zamzam,” nikamuuliza:

“Nini Zamzam?”

Akaniambia:

“Hakikauki abadan, wala hayapunguwi maji yake. Kitawanywisha mahujaji na kipo baina ya mavi na damu karibu na mahali atakapodokowa kunguru mwenye miguu meusi penye kichungu cha sisimizi.”

Anasema Ibn Is-haaq:

“Alipojulisha utukufu wake na kufahamishwa mahali kilipo na alipojua kuwa aliyoyasikia ni ya kweli, asubuhi ilipoiniga akachukua jembe lake na kuondoka pamoja na mwanawe Al-Haarith, na wakati huo hakuwa na mtoto mwengine isipokuwa huyo, akaanza kuchimba na alipoyafikia maji akapiga takbir, na Maquraysh watu wa kabila la Bani Umayyah wanaotokana na Bani Abdu Manaf wakajua kuwa keshapata alichokitaka wakamwendea na kumwambia:

“Ewe ‘Abdul-Muttwallib! Hiki ni kisima cha baba yetu Ismaa’iyl, na sisi tuna haki yetu ndani yake kwa hivyo utushirikishe na sisi pia.”

Akasema:

“Sitofanya hivyo, jambo hili nimehusishwa nalo peke yangu na nyinyi hamumo na nimechaguliwa mimi kati yenu nyote.”

Wakamwambia:

“Tupe haki yetu kwani sisi hatutokuacha mpaka tumtafute atakayehukumu baina yetu.”

Akasema:

“Mchagueni mnayemtaka ahukumu baina yetu.”

Wakasema:

“Mpiga ramli mwanamke wa kabila la Bani Sa’ad Hudhaym.”

Akasema:

“Nimekubali.”

Anasema Ibnu Is-haaq:

“Mpiga ramli huyo alikuwa akiishi karibu na nchi ya Shaam, na ‘Abdul-Muttwallib akapanda farasi wake, nao wakapanda farasi wao pia, na kutoka katika kila kabila akatoka mtu mmoja, wakafuatana na kuianza safari ndefu kuelekea Sham., na ardhi yote wakati huo ilikuwa jangwa, walipofika katika sehemu mojawapo ya jangwa hilo iliyopo baina ya Hijjahz na Sham maji ya ‘Abdul-Muttwallib na ya wenzake yakamalizika, wakashikwa na kiu na walipotambua kuwa watakuja kufa kiu, wakawaomba Maquraysh waliofuatana nao, wakakataa wakasema:

“Na sisi tuko jangwani pia, tunajiogopea nafsi zetu yasije yakatukuta yalokukuteni.”

‘Abdul-Muttwallib akawauliza wenzake:

“Mnaonaje?”

Wakasema:

“Tupe rai yako na sisi tuko tayari kukufuata.”

Akasema:

“Mimi naona kwa vile bado tuna nguvu zetu, bora kila mmoja wenu ajichimbie shimo lake na kila atakapokufa mmoja, basi wenzake wamsukume ndani ya shimo lake kisha wamfukie mpaka atakapobaki mmoja tu kati yenu, na akipotea mtu mmoja bora kuliko kupotea kundi zima.”

Wakasema:

“Rai yako ni nzuri sana.”

Wakashuka, na kila mmoja wao akaanza kujichimbia shimo lake kisha wakakaa kila mmoja akisubiri kifo chake.

‘Abdul-Muttwallib akawaambia wenzake”

“WaLlaahi huku kukaa kwetu tukiyangoja mauti ni uvivu, kwa nini tusiendelee na safari, huenda tukabahatika kuufikia mji tukapata maji? Inukeni tuendelee na safari.”

Wakainuka na kumsubiri ‘Abdul-Muttwallib apande farasi wake, na alipokuwa akimpanda farasi wake, pakatokea mpasuko chini ya farasi wake na maji matamu yakaanza kutoka, akawaita makabila yote ya Kiquraysh aliofuatana nao akawaambia:

“Njooni mpate kunywa maji, kwani Allaah ndiye aliyetuletea maji haya, kwa hivyo kunyweni, jazeni viriba vyenu na wapeni farasi wenu pia.”

Wenzake wakasema:

“WaLlaahi Allaah keshatoa uamuzi wake juu ya kisima cha maji ya Zamzam, kwa hivyo hatutoshindana na wewe abadan. Bali yule aliyekuletea maji katika jangwa hili ndiye aliyekuletea kisima cha Zamzam, kwa hivyo rudi katika kisima chako ukiwa mshindi.”

 

Wakarudi wote pamoja na hawakumuendea tena mpiga ramli.[22]

 

 

Kisa Cha Nadhiri aliyoweka ‘Abdul-Mutwallib Ya Kumchinja Mmoja Kati Ya Wanawe

‘Abdullaah, baba yake Mtume wa Allaah Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni mwana wa ‘Abdul-Muttwallib, na mama yake ni Faatwimah bint ‘Amru bin ‘Aid bin ‘Umran ibn Makhzum bin Yaqadhah bin Murrah, na ‘Abdullaah alikuwa ndiye kipenzi cha baba yake ‘Abdul-Muttwallib.

Imeandikwa katika kitabu cha Siyrah ya Ibn Hishaam na katika Al-Bidaayah wan Nihaayah kuwa; ‘Abdul-Muttwallib alipofanikiwa kukifukuwa kisima cha maji ya Zamzam baada ya kufukiwa na watu wa kabila la Jurhum, na kutoa kila kilichofukiwa ndani ya kisima hicho, aliweka nadhiri kuwa akipata watoto kumi atamchinja mmoja wao mbele ya Al-Ka’abah.

Allaah Akamruzuku watoto kumi na majina yao ni; Al-Haarith na Az-Zubayr na Abu Twaalib na ‘Abdullaah na Hamzah na Abu Lahab na Al-Ghaidaq na Al-Maqum na Sifar na Al-‘Abbaas.

‘Abdul-Muttwallib akawajulisha wanawe hao juu ya nadhiri yake, na wote wakakubali, akawataka kila mmoja wao aandike jina lake, akayachukua majina hayo na kwenda nayo mpaka penye sanamu la Hubal na kuyapigia kura mahali hapo.

Kura ikamuangukia kipenzi chake katika wanawe na mdogo wao ‘Abdullaah bin ‘Abdil-Muttwallib – baba yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ‘Abdul-Muttwallib alipomshika mkono mwanawe huyo kumsogeza karibu na mahali pa kuchinja mihanga mbele ya sanamu la Hubal, akambana chini ya miguu yake tayari kisu mkononi, ndugu zake wote wakamkabili na kumuuliza:

“Unataka kufanya nini ewe ‘Abdul-Muttwallib?”

‘Abdul-Muttwallib akasema: “Nataka kumchinja.”

Ndugu zake wote pamoja na jamaa zake waliohudhuria wakasema:

“WaLlaahi humchinji, na ujuwe kuwa utakapoanza wewe mwenendo huo, basi kila mtu atakuwa akija na mwanawe kutaka kumchinja mahali hapa.”

 

Inasemekana kuwa ndugu yake Al-‘Abbaas ndiye aliyemchomoa ‘Abdullaah chini ya miguu ya baba yake, lakini ‘Abdul-Muttwallib hajakubali kuiacha nadhiri yake hiyo bila kuitimiza mpaka walipokubaliana kumuendea mganga maarufu na mpiga ramli anayeishi Hijaaz kumtaka shauri lake, na mpiga ramli huyo akawaambia:

“Pigeni kura baina ya mtoto wenu na ngamia kumi na kama kura itaangukia kwa mtoto ongezeni ngami kumi kisha pigeni kura mara ya pili, na ikimuangukia mtoto wenu tena endeleeni kuongeza ngamia kumi kumi mpaka pale Mola wenu atakaporidhika, kisha muwachinje ngamia wote kwani hapo Mola wenu atakuwa kesharidhika, na mtoto wenu keshaokoka.”

 

Wote wakakubaliana na shauri hilo, wakaondoka na kurudi Makkah, na mara baada ya kuwasili, ‘Abdul-Muttwallib akamuomba Allaah kisha wakamsogeza ‘Abdullaah na kuwasogeza ngamia kumi na kuanza kupiga kura, na kila mara kura ilikuwa ikimuangukia ‘Abdullaah. Wakaongeza ngamia kumi wengine, kura ikamuangukia tena ‘Abdullaah. Wakawa wanaongeza ngamia kumi kumi mpaka walipotimia ngamia mia ndipo kura ilipowaangukia ngamia, wakamwendea ‘Abdul-Muttwallib aliyekuwa amesimama mbele ya sanamu la Hubal huku akimuomba Allaah na kumjulisha juu ya matokeo ya kura.[23]

 

Imepokelewa kutoka kwa Qubaydhah bin Dhaub kuwa mwanamke mmoja aliweka nadhiri kuwa akitenda jambo fulani atamchinja mwanawe mbele ya Al-Ka’abah. Mwanamke huyo akalifanya jambo hilo, kisha akamwendea ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kutaka fatwa, na ‘Abdullaah bin ‘Umar akamwambia:

“Allaah Amekukatazeni kuziuwa nafsi zenu,”

Akamwambia hivyo bila kuongeza neno lolote, kisha mwanamke akamwendea ‘Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kutaka fatwa kutoka kwake, na Ibn ‘Abbaas akamwambia:

“Allaah Ameamrisha kutimiza nadhiri, na nadhiri ni deni, wakati huo huo Allaah Amekukatazeni kuua nafsi zenu, na ‘Abdul-Muttwallib bin Haashim aliweka nadhiri kuwa akipata watoto kumi atamchinja mmoja kati yao, na alipopata watoto kumi akapiga kura kuchagua amchinje yupi kati yao na kura ikamuangukia ‘Abdullaah bin ‘Abdul-Muttwallib, kisha akaleta ngamia mia moja, akapiga kura amchinje ‘Abdullaah au awachinje ngamia mia, na kura ikaangukia kwa ngamia mia.”

Kisha Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamwambia mwanamke huyo:

“Kwa hivyo mimi naona bora uchinje ngamia mia badala ya mwanao.”

Habari zilipomfikia Marwan aliyekuwa gavana wa Madiynah wakati huo akasema:

“Naona kuwa Ibn ‘Umar na Ibn ‘Abbaas wote wamekosea katika fatwa zao, kwa sababu haijuzu nadhiri katika jambo la kumuasi Allaah, bora muombe maghfira Allaah na utubu na utowe sadaka na uzidishe kufanya matendo mema. Lakini kitendo cha kumchinja mwanao ni jambo lililokatazwa na Allaah.”

Fatwa hii ya Marwan iliwafurahisha sana watu, wakaona kuwa imesibu, na wao wakawa wanatoa fatwa ya kutotimiza nadhiri yenye kumuasi Allaah.[24]

 

Kisa Cha Asw-Haabul Fiyl (Watu Wa Ndovu)

Abraha Mhabashi aliyekuwa gavana wa Al Najashi katika nchi ya Yemen iliyokuwa ikitawaliwa na Ethiopia wakati ule alikuwa akiona wivu sana kila anapowaona waarabu wakienda kuhiji Al-Ka’abah, akaamua kujenga kanisa kubwa katika mji wa Sana-a na akawataka waarabu waache kwenda Makkah na badala yake wakahiji penye kanisa lake.

Habari zilipomfikia mmoja katika watu wa kabila la bani Kinaanah, alighadhibika akaingia ndani ya kanisa hilo wakati wa usiku na kukipaka mavi kibla cha kanisa, jambo lililomghadhibisha sana Abraha aliyekusanya jeshi kubwa sana idadi yake askari wapatao elfu sitini pamoja na tembo ishirini na mbili yeye mwenyewe akiwa juu ya tembo mkubwa sana, na kuelekea nalo Makkah kwa ajili ya kuibomoa Al-Ka’abah.

Alipowasili penye bonde la Muhsir baina ya Makkah na Muzdalifa (baina ya Muzdalifa na Mina), tembo alipiga magoti na kukataa kuendelea na safari ya kuelekea Makkah. Wakawa kila wanapomuelekeza kusini au kaskazini anainuka na kutembea, lakini wanapomuelekeza upande wa Makkah anakataa na kupiga magoti.

Wakabaki katika hali hiyo mpaka pale Allaah Alipowapelekea ndege makundi kwa makundi, wakawapiga kwa mawe ya udongo unaounguza.

Allaah Anasema:

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ. أَلَمْ يَجْعَلْ كَيْدَهُمْ فِي تَضْلِيلٍ. وَأَرْسَلَ عَلَيْهِمْ طَيْرًا أَبَابِيلَ. تَرْمِيهِم بِحِجَارَةٍ مِّن سِجِّيلٍ. فَجَعَلَهُمْ كَعَصْفٍ مَّأْكُولٍ

“Je! Huoni jinsi Mola wako Alivyowafanya watu wenye ndovu?

Je! Hakujaalia vitimbi vyao kuharibika.

Na akawapelekea ndege makundi kwa makundi

Wakawapiga kwa mawe ya udongo wa kuchoma.

Akawafanya kama majani yaliyoliwa (yakatapikwa)?”[25]

Suratul Fiyl

 

Ndege walikuwa wakiwajia kwa wingi makundi kwa makundi, mfano wa vijumba mshale au zuwarde, kila mmoja amebeba mawe matatu, moja mdomoni na mawili ameyabana mguuni ukubwa wa dengu, kila anayepigwa na jiwe mwili wake hukatika vipande vipande na kuangamia.

Si wote waliopigwa na mawe hayo, walikuwemo walioachwa wakarudi mbio kuelekea makwao huku wakiangukiana. Lakini Abraha, Allaah Alimsalitishia maradhi yaliyosababisha makucha yake kukatika na kupukutika huku akirudi alikotoka, na alifariki alipowasili Sana-a mwili wake ukiwa mfano wa kuku aliyenyonyoka manyoa.

Maquraysh walikimbilia sehemu mbali mbali mbondeni na juu ya vilele vya majabali wakihofia maisha yao, na hawakurudi majumbani mwao mpaka baada ya kutokea yaliyowatokea majeshi hayo.

Tukio hili lilitokea mwezi wa Muharram karibu siku hamsini au hamsini na tano kabla ya kuzaliwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  muwafaka wa mwisho wa mwezi February au mwanzo wa mwezi wa March mwaka 571 baada ya Nabii ‘Iysa.

 

Katika tafsiri ya Suratul Fiyl anasema Ibn Kathiyr:

“Hii ni mojawapo ya neema za Allaah walizopewa Maquraysh baada ya kuwalinda na shari waliokuja nayo watu wa ndovu waliokuja wakiwa na azma ya kuibomoa Al-Ka’abah na kuiondoa isiwepo tena. Lakini Allaah Aliwaangamiza na kuwalazimisha waliobaki warudi wakiwa wameshindwa, juu ya kuwa walikuwa watu wanaofuata Dini ya Manasara na kwa wakati ule wao walikuwa bora kuliko Maquraysh waliokuwa wakiabudu Masanamu, lakini haya yalikuwa ni matayarisho ya kuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  kwa sababu kauli nyingi zinasema kuwa katika mwaka ule alizaliwa.”

 

Anaendelea kusema Ibn Kathiyr:

“Kama kwamba uhakika wa mambo unasema; ‘Enyi Maquraysh hamkupata nusura hii juu ya Mahabashi kutokana na ubora wenu, bali kwa ajili ya kuilinda nyumba kongwe itakayopata heshima kwa kuzaliwa hivi karibuni kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mwisho wa Manabii.”

 

Habari za tukio hili zilienea kila pembe ya ulimwengu wa wakati ule, na kwa vile Wahabashi walikuwa na uhusiano mzuri na Warumi, Waajemi waliokuwa wakiisubiri fursa nzuri kama hii wakaingia na kuiteka nchi ya Yemen kwa haraka sana, na dola mbili hizi (Persia na Rome) ndizo zilizokuwa dola kubwa za wakati ule, na wakati huo huo tukio hili la kuangamizwa kwa watu wa ndovu liliujulisha ulimwengu juu ya utukufu wa nyumba ile ya Allaah na kwamba Allaah ndiye aliyeitukuza na kuiadhimisha, na kwa ajili hiyo atakapotokea yeyote katika watu wake akasema kuwa yeye ni Mtume, basi tukio hilo linampa nguvu mtu huyo.

Kwa hivyo ndani ya tukio hili mna hekima ya Allaah iliyojificha ya kuwapa ushindi washirikina dhidi ya watu wa imani kwa njia ya kimiujiza.

 

Kuzaliwa Kwake Na Miaka Arubaini Kabla Ya Utume

 

Alama Za Utume

Bibi Amiynah, mama yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

"Nilipoolewa na ‘Abdullaah (baba yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), sijaishi naye zaidi ya siku kumi. Na siku ya kumi na moja alifunga safari kuelekea nchi ya Shaam akifuatana na msafara wa wafanya biashara.

Usiku uliofuata nilipata tabu sana kupata usingizi kutokana na dhiki niliyokuwa nayo moyoni mwangu kwa kumfikiria sana mume wangu, na katika nyakati za alfajiri ulinichukua usingizi kidogo, na ndani yake niliota ndoto ya ajabu sana.  

Nilitamani ‘Abdullaah awe pamoja nami usiku ule nipate kumhadithia habari njema na bishara ile. Nilimhadithia ‘Abdul-Mutwallib aliyeniambia: "Ewe Amiynah, zifiche habari hizi, usimhadithie mtu yeyote."

 

Ummu Ayman, mtumishi wa Bibi Amiynah alikuwa akisema: "Nilikuwa nikizungumza sana na Bibi Amiynah kwa ajili ya kumliwaza baada ya mumewe kusafiri, na siku moja alinitazama sana kisha akaniambia: "Ewe Ummu Ayman, nimehakikisha sasa kuwa mimi ni mja mzito, lakini sioni uzito wowote wala maumivu kama wanavyoona wanawake wengine waja wazito!. Na kila unaponichukua usingizi ananijia usingizini mwenye kuniambia kuwa nimebeba tumboni mwangu bwana wa umati huu.

Sijui lini atarudi ‘Abdullaah? Atarudi lini ewe Ummu Ayman?"

 

Lakini ‘Abdullaah hakurudi tena. Aliumwa alipokuwa safarini, akafariki dunia akiwa katika mji wa Madiynah kwa wajomba zake watu wa kabila la Bani Najjar, na wakati huo alikuwa na umri wa miaka kumi na nane tu, na umri wa Bibi Amiynah ulikuwa miaka kumi na sita!

Ndani ya usiku mmoja wa mbalamwezi (mbaamwezi), Bibi Amiynah aliamka nyakati za alfajiri akiwa mwenye hofu, akamuita mtumishi wake Ummu Ayman na kumuambia: "Ewe Ummu Ayman; ndoto hizi zinaniandama na zote zimefanana, na usiku wa leo alinijia aliyenijia akaniambia: "Wakati wa kuzaa umekaribia, na utamzaa bwana wa umati huu", kisha akanifundisha maneno ya kusema pale nitakapomzaa. Aliniambia niseme:

أعيذه بالواحد، من شر كل حاسد

Ninamkinga kwa aliye Mmoja kutokana na shari ya kila hasidi.

Kisha akaniambia nimpe jina la Muhammad!"

 

Bwana Anazaliwa

Alizaliwa bwana wa Mitume yote Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika nyumba ya Abu Twaalib, mtaa wa Bani Haashim – Makkah, na nyumba hiyo hivi sasa imefanywa kuwa ni Maktaba (Public Library).

Ilikuwa asubuhi ya siku ya Jumatatu tarehe tisa mwezi wa Rabiul Awwal mwaka wa tukio la tembo, na inasemekana pia kuwa ilikuwa tarehe nane na wengine wanasema tarehe kumi na wengi wanasema ilikuwa tarehe kumi na mbili[26] baada ya kupita miaka arubaini ya utawala wa Mfalme Anu Sharwan alipozaliwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam), na hii inawafikiana na tarehe 20 April mwaka 571 baada ya Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam), kama ilivyofanyiwa tahakiki na mwanachuoni mkubwa Muhammad Sulaymaan Al-Mansuurpuriy.

 

Kabla ya kuingia alfajiri ya siku ya Jumatatu Bibi Amiynah alihisi kuwa wakati wa kujifungua (kuzaa) umewadia, na hapakuwa na mtu mwingine nyumbani kwake isipokuwa Ummu Ayman. Ikamuingia hofu moyoni mwake, lakini alipokuwa akiangalia huku na kule, aliona nuru ikizagaa na kung'arisha chumba chake, na akahisi kama kwamba kundi la wanawake waliovaa nguo nyeupe wamekaa juu ya kitanda chake. Bibi Amiynah alidhania kuwa ni wanawake wa kabila lake. Alishangaa huku akijiuliza: "Walizipataje habari za kuwadia kwa wakati wangu wa kujifungua, wakati nina hakika kuwa sijawahi kumhadithia mtu yeyote?"

Na baada ya kujifungua, Bibi Amiynah hakuwaona tena wanawake wale waliokuwa chumbani kwake. Akaelewa kuwa ni Rahma iliyotoka kwa Allaah imeletwa kwa ajili ya kumliwaza na kumuondoshea hofu na uoga wakati wa kumzaa bwana wa umati huu.

 

Baada ya kujifungua, Bibi Amiynah akataka aitiwe ‘Abdul-Mutwallib, apate kumpa bishara njema ya kuzaliwa kwa mjukuu wake, na baada ya kupewa bishara hiyo, babu alimbeba mjukuu wake kwa furaha na kuingia naye ndani ya Msikiti wa Al-Ka’abah, na huko alimuomba Allaah na kumshukuru na inasemekana kuwa yeye ndiye aliyempa jina la Muhammad. Jina hili halikuwa maarufu miongoni mwa waarabu wakati ule, na ilipofika siku ya saba akamtahirisha kama walivyokuwa wakifanya waarabu.

 

Wa mwanzo kumnyonyesha baada ya mama yake ni Thuwaybah aliyekuwa mtumwa aliyeachwa huru na Abu Lahab, aliyemyonyesha ziwa la mwanawe Masrouh, na kabla ya hapo aliwahi kumnyonyesha Hamzah bin ‘Abdul-Muttwallib na kabla yake pia alimnyonyesha Abu Salamah bin Abul Asad Al-Makhzumiy[27], na kwa ajili hiyo wote hao wanakuwa ndugu wa kunyonya wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Asubuhi Njema

Jua lilichomoza kwa furaha asubuhi ile pale Makkah. Bali ulimwengu mzima ulijaa furaha siku ile. Kila kitu kilifurahi kwa sababu mtoto amezaliwa katika mji wa Makkah, na mtoto huyo hakuwa mtoto wa kawaida. Mtoto huyo ni zawadi iliyotoka kwa Allaah kwa ajili ya wanaadamu. Mtoto huyo alikuwa mfano mwema na ruwaza njema iliyokuja kueneza mapenzi na huruma na uadilifu baina ya viumbe. Amezaliwa Mtume aliyekuja kuingiza furaha na tumaini ndani ya nyoyo zilizokwisha kata tamaa, na kuziongoza nyoyo hizo katika uongofu na imani, na kuzitoa katika giza na kuziingiza katika mwangaza.

 

Ilikuwa asubuhi njema kupita zote ulimwenguni. Asubuhi ya furaha na vifijo na vigelegele, aliyozaliwa ndani yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kipenzi cha Allaah na mbora wa viumbe vyote.

 

Hata Malaika waliifurahia siku ile kwa kuzaliwa Mkweli mwaminifu, mpole, mkarimu, shujaa, mchaji Allaah, Rahma kwa walimwengu aliyekuja kuwatoa watu kutoka katika giza la kufru na kuwangiza ndani ya nuru itokayo kwa Allaah.

 

Amezaliwa yule ambaye ulimwengu ulikuwa ukimsubiri. Kiumbe aliyebeba kila sifa njema asizokuwa nazo kiumbe mwingine. Mtume mtukufu, muaminifu, muungwana, mwenye kila sifa ya ubinaadamu, fadhila, ucha Allaah, moyo mkubwa, na tabia njema ya hali ya juu isiyoweza kufananishwa na kiumbe kingine.

 

Bali kila kiumbe kilifurahi. Hata ndege na miti ilifurahi kwa kuwasili kiongozi aliyekuja kuondoa na kuufuta ukafiri, ushirikina na ujinga ulimwenguni.

 

Babu yake ‘Abdul-Mutwallib alifurahi kupita kiasi siku hiyo, akamuambia Bibi Amiynah: "Kipenzi chetu huyu ni urithi wetu huyu kutoka kwa baba yake ‘Abdullaah. Utazame uso wake na macho yake na mdomo wake. Utazame uzuri wake. Kila kitu chake kinafanana na baba yake. Mzuri alioje mtoto huyu kupita watoto wote, aliyewashinda watoto wote kwa uzuri na kupendeza."

 

Alizaliwa yatima Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ambaye baba yake ‘Abdullaah alifariki dunia alipokuwa akirudi Makkah kutoka Shaam alipotamani kupita Madiynah kuwatembelea wajomba zake watu wa kabila la Bani Najjaar wanaoishi huko. Na alipokuwa Madiynah, ‘Abdullaah alipatwa na maradhi, akafariki dunia wakati mwanawe Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) bado angali tumboni mwa mama yake katika mimba ya miezi sita.

 

 

Kwa Bi Haliymah As-Sa’adiyah

Siku moja katika nyakati za asubuhi, ‘Abdul-Mutwallib aliingia ndani ya nyumba ya Bibi Amiynah akiwa pamoja na Bibi wa kibedui wa kabila la Bani Sa’ad na jina lake lilikuwa Haliymah, maarufu kwa jina la Haliymah As-Sa’adiyah.

‘Abdul-Mutwallib akasema: "Ewe Amiynah, huyu ni Bibi wa kibedui anayetokana na watu wakarimu. Nimekuletea ili awe mnyonyeshaji wa mwana wetu Muhammad. Atamchukua mtoto na kwenda naye katika kijiji chake apate malezi ya kibeduwi ambayo ndani yake mna hewa safi na nguvu na ushujaa na utulivu na starehe."

 

Bi Haliymah alimpenda sana Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na alikuwa akisema:

"Nilipokwenda Makkah nikifuatana na wanyonyeshaji wenzangu wengi, kila mmoja alijichagulia mtoto wa kitajiri kumnyonyesha, hapana hata mmoja aliyetaka kumchukua Muhammad kwa sababu alikuwa yatima na masikini.

Walikuwa wakisema:

"Tutafaidika nini na mtoto yatima na mama yake masikini wakati sisi tunataka malipo na kunufaika kwa kunyonyesha?"

Nilipoona wenzangu wote hawamtaki, nikaamuwa kumchukua mimi, nikamuambia mume wangu niliyekuwa nimefuatana naye: "Nitamchukua mimi yatima huyu." Na mume wangu akaniambia: "Mchukue, huenda akawa na kheri nyingi."

Nikamchukua Muhammad na matokeo yake, nyumba yangu ikaingia barka na ikawa na kheri nyingi hata wenzangu wakawa wananihusudu!"

Anaendelea kusema:

“Nilipoondoka kijijini petu nikifuatana na mume wangu na mwanangu mchanga niliyekuwa nikimnyonyesha, tukiwa pamoja na wanawake wengine wa kabila la Bani Sa’ad bin Bakr wakitafuta watoto wa kuwanyonyesha.

 

Ule ulikuwa mwaka wa ukame na hatukuwa na chochote nyumbani kwetu. Nilikuwa nimepanda punda jike rangi ya kijivu na pia tulikuwa tunaye ngamia aliyezeeka - WaLlaahi hakuwa akitoa hata tone la maziwa, na hatukuweza kulala wakati wa usiku kwa sababu ya kelele za mtoto aliyekuwa akilia na njaa.

Kifuani pangu sikuwa na maziwa ya kutosha, wala ngamia yule aliyezeeka hakuwa na maziwa ya kuweza kumnywesha, tukawa tunasafiri huku tukiomba mvua na faraja mpaka tulipowasili Makkah kwa ajili ya kutafuta mtoto wa kumlea.

Kila mwanamke aliyetakiwa amchukue Muhammad alimkataa alipoambiwa kuwa ni yatima, na hii ni kwa sababu kila mmoja wetu alikuwa akitegemea kulipwa chochote na wazee wa mtoto. Tukawa tunasema:

“Yatima! Wataweza kutulipa nini babu na mama wa mtoto huyu?”

Kila mtu alikataa kumchukua, na kila mwanamke niliyefuatana naye alipata mtoto wa kumlea isipokuwa mimi, na tulipokuwa tukijitayarisha kuondoka nikamwambia mume wangu:

“WaLlaahi nitakwenda kumchukua yatima yule.”

Akaniambia:

“Bora ufanye hivyo, huenda Allaah Akatubariki kwa ajili yake.”

Nikaenda kumchukua na hapana kilichonifanya nimchukue isipokuwa kwa sababu sikupata mtoto mwengine. Baada ya kumchukua nikarudi naye kwa mume wangu, lakini nilipomkumbatia tu na kuanza kumyonyesha, nilishangazwa kuona maziwa yangu yamejaa. Alikunywa mtoto yule mpaka akashiba, kisha akanywa mwanangu mpaka akashiba, kisha akalala, na hakuwa akilala tulipokuwa pamoja naye kabla ya siku hiyo.

Mume wangu akaenda kumtazama ngamia wetu aliyezeeka, akashangazwa alipomuona akiwa amejaa maziwa. Akamkamua na sote kwa pamoja tukanywa mpaka tukashiba, na usiku huo tulipata usingizi mzuri sana.

Asubuhi  yake mume wangu akasema:

“Unajua ewe Haliymah! WaLlaahi tumebahatika kupata mtoto mwenye baraka.”

Nikamjibu:

“InshaAllaah iwe hivyo.”

 

Bi Haliymah As-Sa’adiyah anaendelea kusema:

"Tulipokuwa safarini kuelekea Makkah, punda wangu dhaifu alikuwa akienda huku akipepesuka. Nikawa nyuma ya wenzagu ambao wanyama wao walikuwa wepesi wenye siha nzuri. Lakini nilipoondoka Makkah kurudi kijijini kwetu nikiwa nimembeba Muhammad juu ya punda wangu, mambo yaligeuka, na punda wangu kwa uwezo wa Allaah Aligeuka kuwa mwenye siha nzuri, mwenye nguvu, mwepesi, anayekwenda kwa kasi kubwa kama farasi. Alikuwa akienda mbio na kuwapita wenzangu wote waliokuwa katika msafara wetu uliokuwa ukirudi nyumbani ubeduini, hata wenzangu walikuwa wakisema:

"Ana nini punda wa Haliymah. Tulipokuwa tukienda Makkah alikuwa dhaifu anayekwenda huku akipepesuka hata akachelewa njiani siku kadha, na sasa tunamuona anakwenda mbio kama upepo na anatupita sote!"

Nikajua nafsini mwangu kuwa niliyembeba alikuwa mtoto aliyebarikiwa, mwenye siri asiyoijua isipokuwa Allaah.

 

Wenzangu walikuja kuniuliza:

“Ewe binti wa Abu Dhu’ayb, tuambie kweli, huyu si yule yule punda wako uliyempanda tulipokuwa tukija?”

Nikawajibu:

“WaLlaahi ni huyu huyu!”

Wakaniambia:

“WaLlaahi ana maajabu makubwa.”

 

Anasema Bibi Haliymah

“Kisha tukaendelea na safari yetu ya kuelekea katika kijiji cha Bani Sa’ad, na wakati huo hapakuwa na mahali penye ukame kupita kijiji chetu, lakini juu ya hayo, mbuzi wetu wanaporudi kutoka malishoni walikuwa wameshiba na wamejaa maziwa.

Tukawa tunawakamua na kunywa maziwa wakati wenzetu hawakuwa wakipata hata tone la maziwa.

Na watu wetu walikuwa wakiambizana:

“Ole wenu! Kwa nini na nyinyi hampeleki wanyama wenu mahali wanapopelekwa mifugo ya binti wa Abu Dhuayb (yaani Bibi Haliymah)?”

 

Wakawa na wao wanapeleka mifugo yao huko, lakini walikuwa wakirudi nao bila kupata chakula cha kutosha wala kujaa maziwa, wakati mifugo yetu ilikuwa ikipata chakula cha kutosha na walikuwa na maziwa ya kutosha.

 

Tuliendelea na hali hiyo mpaka muda wa kumnyonyesha ulipokamilika, na mtoto kukuwa, na hata kukuwa kwake pia kulikhitalifiana na ukuwaji wa watoto wenzake, tukamrudisha kwa mama yake huku tukitamani aendelee kubaki kwetu kutokana na baraka tulizoziona.

Tukamuambia mama yake:

“Kwa nini humuachi kwetu mpaka awe na nguvu za kutosha? Tunamuogopea asije akapata maradhi ya mjini Makkah.”

Anasema Bibi Haliymah:

“Tukamshikilia mpaka akakubali turudi naye.”[28]

 

Mtoto Wa Ajabu!

Anaendelea kusema Bibi Haliymah:

"Muhammad alikuwa mtoto mzuri wa ajabu. Ilikuwa ninapomlaza juu ya tandiko la sufi, na chini yake nikiweka kipande cha kitambaa cha hariri rangi ya kijani, alikuwa akinukia harufu nzuri sana ya miski.

Uso wake ulikuwa ukitabasamu wakati amelala mfano wa malaika mzuri, na ninapouweka mkono wangu juu ya kifua chake, alikuwa akifungua macho na kuniangalia huku akiendelea kutabasamu, na nuru ilikuwa ikitoka ndani ya macho yake, kisha humbusu juu ya kipaji chake na kumbeba na kumpa ziwa langu la kulia, na maziwa mengi yalikuwa yakitoka ziwani mwangu, naye alikuwa akinywa kiasi anachokitaka."

 

Angelikuwa Yatima...

Bishara ilikuwemo ndani ya vitabu vya Mayahudi kuwa wakati umefika wa kuzaliwa mtume katika mji wa Makkah, na kwamba mtoto huyo atakayezaliwa atakuwa yatima na jina lake litakuwa Muhammad. Mayahudi walianza kuulizia na kutafuta habari za mtoto huyo.

Anasema Bi Haliymah:

“Siku moja tulipokuwa safarini tulikutana na kundi la Mayahudi, nikawahadithia juu ya maajabu ya mtoto wetu na kuwataka waniambie siri yake, nikawasikia wakiambiana: "Tumuuwe mtoto huyu!"

Wakaniuliza kama mtoto yule alikuwa yatima, nikawaambia: "Si yatima. Yule ni baba yake, na mimi ni mama yake."

Nikawasikia wakisema: "Angelikuwa yatima tungelimuua."

 

Kisa Cha Kupasuliwa Kifua

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alibaki katika kijiji cha Bani Sa’ad mpaka alipotimia umri wa miaka mine au mitano wakati kilipotokea kisa cha kupasuliwa kifua.[29]

Imesimuliwa na Muslim kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akicheza na watoto wenzake alijiwa na Jibriyl, akamchukua na kumlaza chini, kisha akampasua kifua chake na kuutoa nje moyo wake na kutoa kutoka ndani ya moyo huo kipande cha damu iliyoganda:

Kisha akamuosha kwa maji ya Zamzam yaliyokuwemo ndani ya chombo cha dhahabu, kisha akaurudisha moyo mahali pake.

Watoto waliokuwa wakicheza pamoja naye walikimbia mpaka nyumbani kwa mnyonyeshaji wake Bibi Haliymah, wakamuambia:

“Muhammad kesha uliwa!”

Walipomrudia walimkuta amekaa, mzima hana chochote isipokuwa rangi ya uso wake ilikuwa imebadilika na kugeuka nyeupe.[30]

 

Anarudi Kwa Mama Yake

Muhammad alibaki kwa mnyonyeshaji wake muda wa miaka miwili, kisha akarudishwa kwa mama yake Bi Amiynah baada ya kumaliza muda wa kunyonya, lakini Bi Amiynah alimuomba Bi Haliymah amrudishe Muhammad ubeduini.

Bi Haliymah alimhadithia Bi Amiynah juu ya maneno aliyoyasikia kutoka kwa Mayahudi, kisha akamuambia: "Mimi namuogopea sana Muhammad."

Bi Amiynah akasema: "Usiogope ewe Haliymah! Allaah Atamuhifadhi na kumlinda. Alipotoka tumboni mwangu mtoto huyu, uso wake ulikuwa umeelekea mbinguni."

Anasema Bi Haliymah:

"Nikarudi na Muhammad ubeduini, na njiani nilikutana na Manasara (Wakristo) kutoka nchi ya Uhabashi walionisimamisha, wakamtazama vizuri mtoto na kumchunguza, kisha wakaniambia: "Tutamchukua mtoto huyu kwa mfalme wetu, kwani anayo shani kubwa sisi ndiyo wenye kuijua."

Nikapiga ukelele mkubwa, na wakati ule nilikuwa karibu na kijiji chetu, na watu wa kabila langu walikuja kuniokowa kwa haraka sana panga mkononi."

Aliporudishwa tena Makkah kwa wazee wake Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na umri wa miaka mitano, na mama yake na babu yake walimpokea kwa furaha kubwa huku wakimbusu na kumkumbatia kutokana na hamu kubwa waliyokuwa nayo juu ya mtoto wao huku wakisema: "Karibu kwako ewe kipenzi chetu. Karibu kwako ewe mtoto wetu mpenzi."

Kisha ‘Abdul-Mutwallib akamgeukia Bi Haliymah na kumuuliza: "Umewahi kuona maajabu yoyote kutoka kwa mtoto huyu ewe Haliymah?"

Bi Haliymah akasema: "Alikuwa na shani kubwa na mambo mengi ya ajabu! Tokea Muhammad alipoingia nyumbani kwangu, baraka na kheri nyingi sana zimeingia. Nilikuwa na mbuzi wachache dhaifu waliokonda wasiokuwa na maziwa ya kutosha, wakageuka kuwa mbuzi walionenepa waliojaa nyama wenye kutoa maziwa mengi sana sijapata kuona mfano wake katika mbuzi wangu!" Bi Haliymah akanyamaza kidogo, akaanza kuwaza na kufikiri, kisha akamuangalia ‘Abdul-Mutwallib akamwambia: "Lakini jambo la ajabu zaidi lilimtokea mtoto huyu siku moja alipokuwa nyumbani kwetu ubeduini lilinifanya niwaze sana na kufikiri usiku na mchana."

‘Abdul-Mutwallib akauliza:

"Ni jambo jambo gani tena hilo ewe Haliymah?"

Bi Haliymah akasema:

"Asubuhi moja alitoka Muhammad kwenda kutembea jangwani akifuatana na watoto wenzake wa kijijini, wakatokea watu watatu wakamkamata Muhammad na kumlaza chini, na wale watoto wengine wakaogopa na kukimbia na wengine walibaki, wakawaendea watu wale na kuwaambia: "Muacheni Muhammad! Muacheni. Huyu ni mtoto wa ‘Abdul-Mutwallib bwana wa Maquraysh." Lakini wale watu watatu hawakuwasemesha, kisha mmoja wao akaunyosha mkono wake na kulipasuwa tumbo la Muhammad, akaelekeza ndani ya tumbo hilo mwangaza mkubwa. Mtu wa pili akapasuwa kifua cha Muhammad na kutoa kipande cha nyama alichokitupa juu ya ardhi.

Na wa tatu alipangusa juu ya kifua cha Muhammad na juu ya tumbo lake, akarudi mzima mwenye afya kama kwamba hapana kilichotendeka juu ya mwili wake. Kisha wakamkumbatia na kumbusu kisha wakatoweka!"

‘Abdul-Mutwallib alipiga ukulele huku akisema:

"Jambo la hatari! Siri kubwa!"

Bi Haliymah akaendelea kusema:

"Nilipopata habari ya kukamatwa kwa Muhammad kutoka kwa watoto wa kijijini niliingiwa na hofu kubwa, nikatoka nikifuatana pamoja na baadhi ya watu wa kijijini kuelekea jangwani kumtafuta. Tukamuona Muhammad akirudi peke yake huku nuru inayong'ara ikitoka usoni na kichwani pake!"

Bi Amiynah, mama yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alionyesha mshangao mkubwa, na babu yake, ‘Abdul-Mutwallib akawa anapiga kelele akisema: "Allaah ni mkubwa! Hao ni Malaika kutoka mbinguni. Bila shaka Muhammad atakuwa na shani kubwa sana!"

 

Ndugu Zake Wa Kunyonya

Ilikuwa kawaida ya waarabu wakati ule kuwapeleka watoto wao nje ya miji katika makabila ya kibedui kwa ajili ya kunyonyeshwa na kujiepusha na maradhi ya mijini na ili wapate kuwa na miili yenye nguvu pamoja na kujifunza ustahamilivu na kujifunza lugha ya Kiarabu asili tokea utotoni.

Kama tulivyoona hapo mwanzo kuwa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alinyonyeshwa na Bibi Haliymah kutoka katika kabila la Bani Sa’ad bin Bakr – na jina lake ni Haliymah bint Abi Dhu’ayb  -   na jina la mumewe ni Al-Haarith bin Abdil-‘‘Uzza – maarufu kwa jina la Abu Kabshah, kutoka kabila hilo hilo (la Bani Sa’ad).

Na ndugu zake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wa kunyonya kutokana na bi Haliymah ni ‘Abdullaah bin Al-Haarith, Aniysah bint Al-Haarith na Hudhafa au Judamah bin Al-Haarith (akijulikana zaidi kwa jina la kubandikwa la Shaymaa).

 

Hamzah bin ‘Abdil-Muttwallib ami yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alinyonya pia kwa watu wa kabila la Bani Sa’ad bin Bakr na kwa ajili hiyo Hamzah anakuwa ndugu wa kunyonya wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mara mbili, kwa sababu hapo mwanzo kama tulivyotangulia kueleza kuwa walinyonya pamoja kwa Thuwaybah aliyekuwa mtumwa aliyeachwa huru na Abu Lahab, aliyemyonyesha ziwa la mwanawe Masruuh.

 

Mama Yake Anafariki

Bi Amiynah, mama yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitamani kwenda Madiynah kulizuru kaburi la mumewe ‘Abdullaah bin ‘Abdul-Mutwallib, baba yake Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Akaifunga safari akifuatana na mwanawe Muhammad pamoja na kijakazi wake ((Barakah)), na katika riwaya nyingine; alifuatana pia na ‘Abdul-Mutwallib.

Walipowasili Madiynah alikwenda kuzuru kaburi la mumewe ‘Abdullaah, kisha akafikia nyumbani kwa watu wake na kubaki hapo muda wa mwezi mzima, kisha wakaifunga safari ya kurudi Makkah.

Walipokuwa njiani mwanzo wa safari yao ya kurudi, Bi Amiynah (mama yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipatwa na homa kali sana na kwa vile walikuwa katikati ya jangwa, hawakuweza kupata dawa na hatimaye akafariki dunia. Alifariki katika mji uitwao Abwa uliopo njiani baina ya Makkah na Madiynah.[31]

 

Bwana Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ) pamoja na aliokuwa nao safarini walilia sana na kukumbatiana kwa majonzi na huzuni nyingi, kisha wakarudi Makkah Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa yatima hana baba wala mama, na wakati huo alikuwa na umri mdogo wa miaka sita tu.

 

‘Abdul-Mutwallib naye alihuzunika sana kwa kifo cha Bi Amiynah kama alivyohuzunika pale mwanzo kwa kifo cha mwanawe ‘Abdullaah. Akamchukua Muhammad nyumbani kwake, akamlea na kumpenda mapenzi yasiyo na mfano. Alikuwa mpole sana juu yake, na mwenye huruma nyingi, na alimpa mapenzi yaliyomfanya Muhammad ahisi kuwa anaye baba na mama na babu. Alimpenda na kumfadhilisha kupita wanawe wote, bali alimpenda kupita kiumbe yeyote ulimwenguni

Alikuwa akimchukua kila anapokwenda Al-Ka’abah, na alikuwa akifuatana naye katika mikutano akimpakata na kucheza naye, na akawa anajulikana kama ni mtoto wa ‘Abdul-Mutwallib.

 

Kwa Babu Yake Mwenye Huruma

‘Abdul-Muttwallib alimlea Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa huruma na mapenzi makubwa sana kupita hata mapenzi aliyokuwa nayo juu ya wanawe. Hakuwa akimuacha peke yake, bali alikuwa akimshughulikia zaidi kuliko anavyowashughulikia wanawe.

Anasema mwandishi wa historia Ibn Hishaam:

“Palikuwa pakitandikwa mkeka penye kivuli cha Al-Ka’abah kwa ajii ya ‘Abdul-Muttwallib, na wanawe walikuwa wakikaa nje ya mkeka huo huku wakiwa wameuznguka, na hawakuwa wakithubutu kuukalia kwa ajili ya kumheshimu baba yao, mpaka pale baba yao anapokuja na kukaa yeye kwanza. Lakini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa bado mdogo wakati huo, anapouona mkeka umeshatandikwa alikuwa akiujia na kuukalia, na ami zake walikuwa wakimuondoa na kumtaka asubiri mpaka akae baba yao kwanza. Lakini ‘Abdul-Muttwallib anapowaona wakifanya hivo alikuwa akiwaambia:

“Mwacheni mwanangu huyu, kwani WaLlaahi atakuwa na shani kubwa.”

Kisha hukaa pamoja naye huku akimpapasa mgongo wake, na alikuwa akifurahishwa na kila anachofanya mtoto huyo.

 

Alipokuwa na umri wa miaka minane na miezi miwili na siku kumi, babu yake ‘Abdul-Muttwallib alifariki dunia na kabla ya kufariki kwake alimkabidhi mjukuu wake huyo ami yake Abu Twaalib ndugu wa baba yake.

 

Kufariki Kwa Babu Yake

Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa na umri wa miaka minane, ‘Abdul-Mutwallib aliumwa sana, na wakati huo babu yake huyo alikuwa na umri uliopindukia miaka themanini. Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawa hambanduki babu yake isipokuwa wakati wa kulala, na alikuwa hatoki nyumbani isipokuwa wakati mchache sana.

Kila maradhi yanapomzidi, ‘Abdul-Mutwallib alikuwa akizidi kupenda kuwa karibu na mjukuu wake Muhammad na akizidi kujikurubisha naye. Alikuwa akimkumbatia na kumbusu na kumweka kifuani pake na kumuonyesha mapenzi na huruma isiyokuwa na mfano.

Siku moja Abu Twaalib alipoingia chumbani kwa baba yake ‘Abdul-Mutwallib akamuona akilia. Akamuuliza:

"Unalia ewe baba yangu wakati wewe ni mtu mzima na mkubwa wa kabila la Quraysh? Ninavyokujua ewe baba yangu kuwa wewe ni mtu shujaa mwenye kuyakabili mambo ukiwa na moyo thaabit. Kipi tena kinachokuliza ewe baba yangu?"

‘Abdul-Mutwallib akasema:

"Namuogopea Muhammad baada yangu!"

Abu Twaalib akasema:

"Ewe baba yangu! Muhammad ni mwanangu, kwa sababu yeye ni mwana wa ndugu yangu ‘Abdullaah, na ‘Abdullaah alikuwa kipenzi chetu sote miongoni mwa ndugu zetu. Tulikuwa tukimpenda kupita hata nafsi zetu. Inakuwaje tena uwe na hofu juu ya Muhammad wakati sisi tuko tayari kumkinga kwa roho zetu na kwa kila tunachokipenda!?"

‘Abdul-Mutwallib akasema:

"Nikaribie ewe Abu Twaalib na usikilize vizuri nitakayokuambia."

Abu Twaalib akasema:

"Nitasikiliza na kutii ewe baba yangu."

‘Abdul-Mutwallib akasema:

"Baada ya kufa kwangu, umchukuwe Muhammad nyumbani kwako, umchanganye na wanao, na umhusishe kwa huruma na mapenzi, na wala asihisi hata chembe kuwa yuko peke yake, na uwe kwake mfano wa babu na baba na mama.

Muhammad atakuwa na shani kubwa sana huyu, na pale Maquraysh watakapomfanyia uadui na kutaka kumshambulia, uwe kwake mfano wa ngao yenye kumkinga, na ngome yenye kumlinda. Na watakapompiga vita, wewe uwe upande wake, umsaidie na uwe pamoja naye. Usije ukamuacha peke yake wala usimuache anyakuliwe na adui zake katika watu wa kabila la Quraysh hata kama nyote mtauliwa kwa ajili hiyo.

Huu ndio usia wangu kwako ewe Abu Twaalib."

 

Alipomaliza kusema maneno yale ‘Abdul-Mutwallib akafumba macho yake na kuisalimisha roho kwa Mola wake, na Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawa yatima asiye na baba wala mama wala babu.

 

Kwa Ami Yake

Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alihamia kwa ami yake Abu Twaalib aliyekuwa mtu fakiri mwenye watoto wengi. Abu Twaalib Alikuwa akimpenda sana Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na alimlea vizuri kwa wema na kwa mapenzi na huruma kupita hata wanawe.

Wakati huo Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na umri wa miaka minane, lakini uso wake ulianza kuonyesha dalili ya ucha Allaah na alama za kutafakari na alama nyingine zenye kudhihirisha kuwa alikuwa mtu mwenye mustakabali mwema na shani kubwa.

 

Kwa vile ami yake alikuwa mtu faqiri, Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimsaidia katika baadhi ya shughuli zake ili aweze kuongeza pato lake litakalomsaidia katika kuwalea wanawe waliokuwa wengi.

 

Alimuomba ami yake amruhusu kumchungia kondoo wake, akakubali na akawa anakwenda nao jangwani penye mabonde na maji mengi na miti. Alijitahidi kuwatafutia mahali penye mimea mizuri ya kula, jambo lilowafanya kondoo hao wanenepe na kujaa maziwa na kusababisha nyumba ya ami yake kuwa na maziwa mengi na jibini (chizi), na hii ikawa mojawapo ya baraka za mtoto huyu mwema ndani ya nyumba ya ami yake.

 

Uso Wa Baraka

Imeelezwa na Ibn ‘Asaakir kutoka kwa Jalhamah bin Arfatah kuwa amesema:

“Nilipowasili Makkah, mji ulikuwa na ukame na mvua ilikuwa haijanyesha muda mrefu sana, na Maquraysh wakamwambia Abu Twaalib:

“Mabonde yamekauka na watoto wana njaa. Twende tukaombe mvua.”

Abu Twaalib akatoka akiwa amembeba Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa bado mdogo wakati ule, huku wingu zito likimfuata mtoto huyo juu yake likimkinga na jua.

Abu Twaalib alisimama na mtoto akiwa ameegemea Al-Ka’abahh akawa anaomba dua ya mvua huku akiushika mkono wa mtoto huyo na kuvishika baadhi ya viungo vyake, na wakati huo hapakuwa na wingu lolote (isipokuwa lile lililokuwa likimkinga na jua), na ghafla! Mawingu yaakaanza kujikusanya kutoka kila upande, na mvua kali sana ikanyesha na ardhi yote ikasharabu maji na mimea ikaanza kuota katika nchi nzima.

 

Kabla Ya Kupewa Utume

Katika ujana wake Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na kila aina ya tabia na mwenenedo mwema. Alikuwa mtu wa aina ya pekee katika mawazo yake, katika kuyapima mambo na katika kutoa uamuzi wenye kusibu.

Walikuwa wakipenda ushauri wake wa hekima na akili zake zenye kubuni na kuanzisha mambo yenye manufaa na yenye malengo mema.

Mara nyingi alikuwa akipenda kujitenga mbali na watu na wakati mwingi alikuwa akipenda kukaa kimya na kutafakari, jambo lililomsaidia sana katika mambo ya kupatanisha watu na kutoa uamuzi bora baina ya watu.

 

Alikuwa akichukizwa sana na ushirikina, na akijitenga na watu wake katika hilo, lakini alikuwa akishirikiana nao katika mambo ya kheri ya kuisaidia jamii nk. ama sivyo alikuwa akipenda kurudi katika kujitenga na kukaa kimya huku akiwaza na kutafakari.

Hakuwa mnywaji wa ulevi kama walivyokuwa wengi wa watu wa Makkah wakati ule, hakuwa akila nyama zilizokuwa zikichinjwa kwa ajili ya masanamu wala hakuwa akihudhuria sikukuu za masanamu yao wala hafla zao, bali tokea utotoni alikuwa akichukizwa na miungu hiyo ya uongo na hapakuwa na kitu kilichokuwa kikimchukiza kupita masanamu hayo, na alikuwa hawezi kustahamili anapomsikia mtu akiapa kwa jina la Lata au ‘Uzza.[32]

 

Bila shaka Allaah ndiye aliyekuwa akimlinda na kila matendo mabaya, na hata alipotaka kujaribu kuziendea starehe za kawaida tu, Allaah Alimlinda na kumhifadhi na kumzuia.

 

Ameelezea Ibn Kathiyr kuwa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

"Sikupata kujaribu kufanya yale waliyokuwa wakifanya watu wa kabila langu wakati wa ujahilia, isipokuwa mara mbili, na mara zote hizo Allaah Alijaalia nisiweze kutenda hayo. Kisha sikujaribu tena mpaka Allaah Aliponikirimu kwa kunipa Utume.

Usiku mmoja nilisema kumwambia mchungaji kondoo mwenzangu nilipokuwa sehemu za juu ya mji wa Makkah:

"Kama utanitazamia kondoo wangu ili nami niweze kwenda Makkah na kukesha kama wanavyokesha vijana wengine, naye akakubali."

Nikaelekea Makkah, na nilipowasili nyumba ya mwanzo katika nyumba za mji wa Makkah iliyo chini ya jabali nikaanza kusikia sauti za ngoma, nikauliza:

"Pana nini hapa?"

Wakaniambia:

"Arusi ya fulani na fulani."

Nikataka kukaa na kusikiliza, lakini Allaah Akaniziba masikio yangu, akaniteremshia usingizi, na sikuweza kusikia lolote mpaka asubuhi ilipoingia, nikaamka nilipohisi joto la jua likinipiga usoni!  Nikarudi asubuhi ile kwa kijana niliyemuachia kondoo wangu, akaniuliza: 'Umefanya nini?' Nikamuambia: 'Sijaona chochote.'

Kisha nikamwambia:

"Nitajaribu tena usiku mwingine.” Na usiku uliofuata nilikwenda tena Makkah, na yakanikuta yale yale yaliyonikuta usiku uliotangulia, na tokea siku hiyo sikujaribu tena.[33]

 

Mchaji Allaah Buhayrah

Alipotimia umri wa miaka kumi na mbili, na inasemekana miaka kumi na mbili na miezi miwili na siku kumi[34], Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuomba ami yake asafiri naye kwenda nchi ya Shaam (Syria), na ami yake alikubali kwa furaha.

Walipokuwa safarini kuelekea Shaam (Syria), katika mji wa Basra mkoa wa Howran mojawapo ya miji ya Kiarabu uliokuwa chini ya utawala wa Warumi, walikutana na mchaji Allaah aliyekuwa akijulikana kwa jina la Buhayrah na jina lake hasa lilikuwa ni Georges, aliyewatokea na kuwapokea, akawakarib   isha na kuwakirimu juu ya kuwa mchaji Allaah huyo hakuwa na kawaida hiyo kabla ya hapo.

Alimjua Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa dalili zake, akasema huku akiushika mkono wake:

“Huyu ni bwana wa ulimwengu. Huyu ataletwa na Allaah akiwa ni Rahma kwa walimwengu.”

Abu Twaalib akamuuliza:

“Nani aliyekuambia hayo?”

Akasema:

“Mimi namjua kutokana na mhuri wa utume uliopo baina ya mabega yake mfano wa tufaa, na haya yote yameandikwa ndani ya vitabu vyetu.”

Kisha akamtaka Abu Twaalib amrudishe mtoto huyo Makkah na asisafiri naye kwenda Syria kwa kumhofia asije akadhuriwa na Mayahudi, na ami yake akafanya hivyo.

 

Alipokuwa Basra, Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliona namna gani masoko ya Shaam yalivyojaa bidhaa, na akajulishwa na wafanya biashara wa hapo na kufundishwa namna ya kufanya biashara nao.

 

Abu Twaalib alianza kuona dalili ya faida kubwa anayoipata katika biashara zake, na kukuwa kwa biashara kwa haraka. Akaona pia kuwa wafanya biashara wenzake wanazidi kumpenda na kwamba kila mmoja anakimbilia kununua bidhaa zake. Akatambuwa kuwa Allaah Amemfungulia yote hayo kwa baraka za mtoto huyu yatima aliyetwahirika.

Maisha yake yakaanza kuwa bora kuliko mwanzo, na rizki ikaongezeka na hali yake ikazidi kuwa nzuri, na watoto wake wakawa na siha nzuri, na Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaendelea kuishi ndani ya nyumba ya ami yake mpaka alipokuwa mtu mzima.

 

Vita Vya Al-Fujaar (Waovu)

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na umri wa miaka kumi na mitano wakati vita vya Al-Fujaar vilipopiganwa, na vita hivi vilikuwa baina ya Maquraysh wakishirikiana na watu wa kabila la Bani Kinaanah dhidi ya kabila la Qas Ailan na kiongozi wa Maquraysh pamoja na Bani Kinaanah alikuwa Harb bin Umayyah na alipewa uongozi huo kutokana na umri wake pamoja na heshima yake.

Vita hivi vilipewa jina la ‘Al-Fujaar’ (waovu) kwa sababu vilipiganwa ndani ya miezi iliyoharamishwa kupigana ndani yake (Ash-huril Hurum).

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alishiriki katika vita hivi akiwa upande wa ami zake, lakini hakupigana, isipokuwa alikuwa akiwasaidia kuokota mishale inayoangukia upande wao na kuwapa ami zake kwa ajili ya kuitumia tena.

 

Muwafaka Wa Al-Fudhuwl

Baada ya vita vya Al-Fujaar kumalizika, watu wa Makkah waliona umuhimu wa kuandikiana muwafaka kwa ajili ya kulinda amani ya mji wao na kuwalinda madhaifu na waliodhulumiwa na kuhakikisha dhulma isitendeke tena katika mji wao.

Kwa ajili hiyo katika mwezi wa Dhul Qa’adah watu wa kabila la Quraysh, wakiwakilishwa na Bani Haashim, Bani Muttwallib na Asad bin ‘Abdul ‘Uzza na Zahra bin Kilaab na Tiym bin Murrah, wote hawa walikutana katika nyumba ya mtu aitwae ‘Abdullaah bin Jadaan Atiymiy kwa sababu ya umri wake na heshima yake, na wakakubaliana kuwa wawe pamoja katika kumuandama dhalimu yeyote mpaka atakapoirudisha haki ya aliyemdhulumu.

Na mwafaka huu ulihudhuriwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na inasemekana kuwa ulifanyika siku chache sana baada ya kupewa utume. Akasema:

“Nilishuhudia katika nyumba ya ‘Abdullaah bin Jadaan muwafaka uliokuwa bora kwangu kuliko kumiliki makundi kwa makundi ya ng’ombe, na hata kama ningeitwa kuhudhuria mkutano kama ule wakati huu baada ya kuja kwa Dini ya Kiislamu, basi ningeuitikia mwito huo”[35]

 

Muwafaka huu ulikuwa mwanzo wa mabadiliko ya nidhamu iliyokuwa ikitendeka wakati wa ujahilia (kabla ya kuja kwa Uislamu), wakati waarabu walipokuwa wakisaidiana kikabila. Mtu alikuwa akimsaidia mtu wa kabila lake, bila kujali kama mtu huyo ndiye aliyedhulumu au aliyedhulumiwa.

Inasemekana kuwa kilichosababisha kuandikwa kwa muafaka huo ni kuwa siku moja mtu kutoka katika kabila la Zubayd alikwenda Makkah kwa ajili ya kuuza bidhaa zake, lakini Al-’Aasw bin Waail as-Sahamiy aliyenunua bidhaa hizo alikataa kata kata kumlipa pesa zake, jambo lilimfanya muuzaji kutaka msaada kutoka kwa Maquraysh lakini hapana hata mmoja aliyekubali kumsaidia.

Mfanya biashara huyo akaamua kupanda juu ya mojawapo ya majabali ya Makkah na kupaza sauti yake huku akisoma mashairi juu ya dhulma aliyotendewa, na Az-Zubayr bin ‘Abdil-Muttwallib aliposikia juu ya uonevu huo akachunguza na baada ya kuhakikisha juu ya uonevu huo, akaitisha mkutano na kumlazimisha Al-’Aasw kumlipa mtu huyo wa kabila la Zubaydy pesa zake.

 

Shughuli Za Mwanzo

Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa na kazi maalum utotoni mwake, na imepolekewa kuwa aliwahi kuchunga kondoo wa Bani Sa’ad[36], na alipokuwa Makkah aliifanya kazi hiyo kwa ujira.

Alipokuwa na umri wa miaka 25 alikwenda Shaam kwa ajili ya kufanya biashara za Bibi Khadiyjah binti Khuwaylid (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyekuwa mfanya biashara maarufu mwenye kuheshimika na mwenye utajiri mkubwa sana.

Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa akiwaajiri wanaume waliokuwa wafanya biashara maarufu na waaminifu kwa ajili ya kumuendeshea biashara zake na alikuwa akiwalipa asilimia maalum katika faida inayopatikana, lakini aliposikia juu ya ukweli na uaminifu mkubwa wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  na juu ya tabia zake njema na upole wake, akamtaka ashughulikie biashara zake na kusafiri nazo nchi ya Shaam huku akimuahidi kumlipa ujira mkubwa kuliko anavyowalipa wafanya biashara wengine, na kwamba atampa mtumishi wake Maysarah afuatane naye, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alilikubali na kuifunga safari ya kwenda Shaam akifuatana na Maysarah.[37]

 

Habari Za Kiwingu

Baadhi ya waliokuwa safarini pamoja naye walisema:

"Nyuso zetu zilikuwa zikiungua kwa joto kali wakati Muhammad alikuwa akizingwa na kiwingu mbinguni kilichokuwa kikimfuata kila anapokwenda na kumkinga na jua kali."

 

Na wengine walisema:

"Tulikiona kijiwingu kwa macho yetu. Kwanza tulidhania ni kijiwingu kilichotokea mara moja kisha kitatoweka kama vijiwingu vyengine vinavyotokea na kutoweka, lakini kiwingu kile kiliendelea kuwepo tulipokuwa tukienda na pia wakati wa kurudi, kama kwamba kimetumwa kumkinga Muhammad peke yake baina ya wasafiri."

 

Habari za kiwingu zilienea mjini Makkah. Wazee, vijana, wake kwa waume, wote walikuwa wakizungumza juu ya habari hizo. Walikuwa wanapokutana panapo Al-Ka’abah wakizungumza juu ya maajabu hayo.

Habari zikamfikia Bi Khadiyjah aliyemuita mtumishi wake Maysarah na kumuuliza:

"Ni kweli habari za kiwingu hiki ewe Maysarah?"

Maysarah akasema:

"Naapa ewe Bibi kuwa kiwingu kilikuwa kikimkinga Muhammad kutokana na jua kali tokea alipoondoka Makkah kuelekea Shaam na tulipokuwa tukirudi. Wingu lilijitandaza juu yake halikuondoka wala kusogea kama kwamba limepigiliwa misumari juu yake, au kama limefungwa na kamba juu ya kichwa chake peke yake mbali na wasafiri wengine."

Maysarah akaendelea:

“Sikupata kuona mtu bora wa kusafiri naye kuliko yeye. Alikuwa mtulivu, hana kiburi, mkarimu na mpole sana. Nilikuwa ninapoumwa akinishughulikia na ninapochoka ananisaidia, na alikuwa akigawana na mimi sawa sawa chakula chake na maji yake. Kwa hakika alikuwa akinitendea kama kwamba ni ndugu yake.

Ni kweli kilikuwepo na kiwingu kilichokuwa kikimfuata wakati wote tokea tulipoondoka mpaka tuliporudi. Kilikuwa kikimfuata na kumkinga na jua kali wala hakuwa akihisi joto hata kidogo wakati wote wa safari.”

“Enhe! Kisha? Endelea.”

Maysarah akaendelea:

“Tulipokuwa tukirudi Makkah, tulisimama mahali muda kidogo kwa ajili ya kujipumzisha, na mimi nikaondoka kwenda kutafuta chakula cha ngamia, na mahali hapo palikuwa na mti mkubwa sana na Muhammad alikaa chini ya mti huo huku akitazama mbinguni kama kawaida yake kama kwamba anatafuta kitu, na karibu na mahali hapo palikuwa na hekalu la mchaji Allaah mmoja aitwae Nastwuur aliyenijia na kuniuliza:

“Nani huyu kijana aliyekaa chini ya mti ule?”

Nikamwambia:

“Huyu ni kijana anayetokana na mabwana wa kabila la Kiquraysh”.

Akaniambia:

“Umeona lolote lisilo la kawaida kutoka kwake?”

Nikamwambia:

“Nimeona kiwingu kikimfuata kikimkinga na jua kali tokea tulipoondoka na wala hakikumuacha abadan.”

Akauliza tena:

“Macho yake yakoje?”

Nikamjibu:

“Meusi makubwa na katika weupe wake umo wekundu khafifu ndani yake.”

Akasema:

“Kijana huyu atakuwa na shani kubwa. Rudi naye Makkah haraka sana, kwani hakupata kukaa chini ya mti huu isipokuwa Nabii”.

 

Anamuoa Bibi Khadiyjah

Kutokana na yote aliyokuwa akiyasikia juu ya Muhammad, Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) akaanza kujishughulisha na kuwaza juu yake (Swalla Laahu ‘alayhi wa sallam).

Alikuwa kila anapokaa, hukumbuka maneno ya Maysarah aliposema:

"Naapa ewe Bibi kuwa kiwingu kilikuwa kikimkinga Muhammad kutokana na jua kali tokea alipoondoka Makkah kuelekea Shaam na tulipokuwa tukirudi. Wingu lilijitandaza juu yake, na halikuondoka wala kusogea kama kwamba limepigiliwa misumari juu yake au kama kimefungwa na kamba juu ya kichwa chake peke yake mbali na wasafiri wengine."

 

Baada ya kusikia hayo na kukumbuka juu ya uaminifu mkubwa wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na baraka iliyoingia ndani ya biashara zake ambayo hajapata kuona mfano wake kabla ya hapo, na baada ya kuziona kila sifa njema za Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) akatambua kuwa huyu ndiye mume aliyekuwa akimsubiri, juu ya kuwa kabla ya hapo wengi miongoni mwa watu wanaoheshimika na wenye uluwa katika watu wa kabila lake walikuja kumposa lakini Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliwakataa.

 

Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) akaamua kumfichulia yaliyo moyoni mwake shoga yake mwaminifu aitwae Bi Nafiysah binti Muniyah ambaye kwa upande wake akamhadithia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumtaka amuoe Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha), na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akalikubali ombi hilo, akawahadithia ami zake waliokwenda kwa ami yake Bi Khadiyjah na kumposea.

 

Arusi ilihudhuriwa na wakubwa wa makabila ya Bani Haashim na Bani Madhar, na haya yalifanyika miezi miwili baada ya Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kurudi kutoka Shaam.

Mahari yalikuwa ngamia 20 na wakati huo Bi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa na umri wa miaka arubaini na alikuwa mzuri na mbora kupita wanawake wote kwa utajiri na kwa akili na kuheshimika.

Alikuwa mwanamke wa mwanzo kuolewa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na hajamuolea mwanamke mwengine mpaka alipofariki dunia.[38]

 

Watoto wote wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wametokana na Bi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) isipokuwa Ibraahiym.

 

Kwanza alimzaa Qaasim na kutokana naye, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa 'kun-yah' umaarufu kwa kuitwa Abul-Qaasim (na maana yake ni baba yake Qaasim). Kisha akazaliwa Zaynab, kisha Ruqayah, kisha Ummu Kulthuum, kisha Faatwimah, kisha ‘Abdullaah, na ‘Abdullaah alikuwa akijulikana pia kwa jina na At-Twaahir (na maana yake ni aliyetwahirika).

Wanawe wa kiume wote walifariki utotoni, na wanawe wa kike wote (Radhiya Allaahu ‘anhunna) waliuwahi Uislamu, wakasilimu na kuhajir kwenda Madiynah, lakini wote walifariki wakati wa uhai wa baba yao (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  isipokuwa Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyefariki miezi sita baada ya kufariki kwa baba yake.[39]

 

Kuijenga Upya Al-Ka’abah

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na umri wa miaka thelathini na tano wakati Maquraysh walipoujenga upya Msikiti wa Al-Ka’abah, kwa sababu miaka mingi ilikwishapita tokea Nabii Ismaa’iyl alipoujenga na hapakuwa na kilichobaki katika jengo hilo isipokuwa rundo la udongo lenye urefu wa kiasi cha dhiraa sita, na halikuwa na kipaa, jambo lililowarahisishia wezi kuingia ndani na kuiba hazina zilizowekwa humo.

Na kwa vile miaka mingi ilikwishapita tokea kujengwa kwake, kanuni za maumbile zilikwishafanya kazi yake. Kuta zilikuwa na nyufa, na miaka mitano kabla ya kupewa utume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yalitokea mafuriko makubwa yaliyosababisha maji kuingia ndani ya Msikiti na kubomoa sehemu kubwa za Msikiti huo, na kwa ajili ya yote hayo Maquraysh wakaona hapana budi kuujenga tena Msikiti.

 

Walikubaliana kuwa zisiingizwe katika ujenzi wa jengo hilo pesa zozote za haramu. Zisiingizwe pesa za mahari ya mzinzi, wala pesa za ribaa, wala pesa alizodhulumiwa mtu.

Mwanzo walikuwa wakiogopa kuubomoa Msikiti, mpaka pale alipotangulia Al-Waliyd bin Mughiyrah na kuianza yeye kazi hiyo, na wenzake walipoona kuwa hapana kilichomsibu, ndipo nao wakaingia kazini. Wakawa wanaendelea kubomoa mpaka walipozifikia nguzo zilizosimamishwa na Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam), kisha wakaanza kuujenga tena, na kila kabila likapewa sehemu yake ya kujenga, na kila kabila lilikuwa likikusanya mawe yake ya ujenzi, na msimamiaji wa ujenzi alikuwa Mrumi aitwae Baqum.

Kazi ilikwenda vizuri mpaka ulipofika wakati wa kulirudisha jiwe jeusi mahali pake ndipo walipokhitalifiana nani anayestahiki kupewa heshima ya kulirudisha jiwe jeusi hilo mahali pake.

Mgogoro uliendelea muda wa siku nne au tano na mambo yakawa magumu, watu wote panga mkononi, walikaribia kupigana vita vikubwa, mpaka pale Abu Umayyah bin Mughiyra Al-Makhzumiy alipotoa rai kuwa; wa mwanzo kuingia Msikitini kupitia mlangoni ndiye atakayeamua baina yao, na wote wakaridhika na rai hiyo.

Allaah Alitaka Mtume wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) awe mtu huyo, na walipomuona tu akiingia, wote kwa pamoja wakapiga ukulele:

"Huyu Muaminifu! Sote tumeridhika naye huyu Muhammad."

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipojulishwa juu ya uamuzi huo akaukubali, na kwa utulivu kabisa akaomba kiletwe kitambaa, akakitandaza na kuliweka jiwe jeusi juu yake, kisha akawataka viongozi wa makabila yote kila mmoja akamate upande wa kitambaa hicho kisha wanyanyuwe kwa pamoja, na walipopafikia mahali pa kuliweka, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akalinyanyua jiwe kwa mikono yake miwili na kuliweka.

Kwa njia hii Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliweza kulitatua tatizo lililokaribia kuleta umwagaji wa damu mkubwa baina ya Makabila ya Kiquraysh, na kila mmoja aliondoka hapo akiwa ameridhika.

 

Pesa za hAli zilipowaishia, kabla ya kazi kukamilika, wakaamua kupunguza kiasi cha dhiraa sita upande wa kaskazini mwa Al-Ka’abah na hii ni ile sehemu inayojulikana kwa jina la Al-Hijr, na Al-Hatiym, na wakaunyanyua mlango kiasi cha dhiraa mbili kutoka juu ya ardhi ili asiweze kuingia isipokuwa wanayemtaka wao tu kuingia, na urefu wa jengo ulipotimia kiasi cha dhiraa kumi na tano wakaiezeka sakafu juu ya nguzo sita, na baada ya kumalizika kazi hiyo, Al-Ka’abah ikawa na umbo la mraba lenye urefu wa mita kumi na tano, na upande wa jiwe jeusi pamoja na upande wa pili yake (mkabala wake) pande zote mbili kila moja ilikuwa na urefu wa mita kumi.

Na jiwe jeusi liliwekwa juu katika uwanja wa tawafu kiasi cha urefu wa mita unusu kutoka juu ya ardhi, na upande wa mlango na upande wa mkabala wake ukawa na urefu wa mita kumi kila mmoja, na mlango ukanyanyuliwa kiasi cha mita mbili kutoka juu ya ardhi na kwa nje yake Al-Ka’abah ikaachwa ikiwa imezungukwa na msingi ulionyanyuka kutoka juu ya ardhi kiasi cha robo mita na upana wa kiasi cha nusu mita.

Na sehemu hii ilikuwa ikiitwa Ash-Shadhirwaan, sehemu ambayo asili yake ilikuwa ndani ya jengo la Al-Ka’abah lakini Maquraysh iliwabidi waiache bila kuijenga.[40]

 

Akihuzunika

Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akihuzunika sana kila anapokwenda penye Al-Ka’abah na kuwaona Maquraysh wakiyatukuza na kuyaangukia na kuyasujudia na kuyaomba masanamu yaliyojaa ndani ya Msikiti huo huku wakiyaita miungu. Akihuzunika anapowaona wakichinja kwa ajili ya masanamu hayo na kuyaomba msaada na kuyaomba maghfira.

 

Alikuwa akihuzunika na kudhikika kila anapowaona watu wake katika hali ile, na mmoja wao alipomuuliza:

"Ewe Muhammad, kwa nini ukishatufu unakaa mbali na sisi na huyatukuzi masanamu yetu na miungu yetu kama sisi tunavyoiadhimisha?"

Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Haya ni mawe yasiyosikia wala kuona. Hata kama utayapiga ngumi kwa mkono wako au kuyapiga mateke au kuyabomoa kwa shoka, basi yatabaki kimya, hayawezi kujitetea."

 

Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiungulika na kuumia pia kila anapowaona vijana wa ki Quraysh wakizama katika starehe za kidunia. Walikuwa wakinywa pombe na kucheza kamari. Wakila ribaa na hawakuona tabu kufanya kitendo chochote katika matendo maovu. Kwa ajili hiyo alikuwa kila akishatufu Al-Ka’abah akiondoka na kurudi nyumbani.

 

Chini Ya Kivuli Cha Utume

 

Ndani Ya Pango La Hiraa

Umri wake ulipokaribia miaka arubaini, na wakati huo kuwaza kwake kwingi pamoja na kutafakari kwake kwingi kulizidisha pengo lililokuwepo baina yake na baina ya watu wa qawm yake, jambo lililomfanya apende kuwa mbali nao. Akawa anachukua 'Sawik', (uji wa shayiri) pamoja na maji, na kwenda katika pango linaloitwa 'Ghari Hira-a' juu ya jabali linaloitwa 'Jabal Nuur' lililopo umbali wa kiasi cha maili mbili kutoka Makkah.

Pango lilikuwa dogo lenye urefu wa kiasi cha dhiraa mbili kasorobo. Alikuwa (mara nyingi) akichukua baadhi ya jamaa zake na kukaa huko siku nyingi, na hasa katika mwezi wa Ramadhaan alikuwa akibaki huko mwezi mzima na alikuwa akiwalisha masikini pamoja na watu wanaokuja kumtembelea, na alikuwa akiutumia wakati wake wote katika ibada na katika kutafakari juu ya kuumbwa kwa dunia na juu ya nguvu kubwa isiyoonekana yenye uwezo huu usio na kifani.

Wakati huo huo moyo wake ulikuwa hauna raha kila anapowaona watu wake wamezama katika maasi na katika kuyaabudu na kuyasujudia masanamu, na moyo wake ulikuwa ukihuzunika zaidi kwa sababu hakuwa na njia yoyote ya kuwatoa katika upotofu ule wala mwongozo maalum anaoweza kuufikia utakaoweza kuutuliza moyo wake na kuridhika nao.[41]

 

Uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) ndio uliomfanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam apende kujitenga mbali na qawm yake, kwa ajili ya kumtayarisha na ujumbe mtukufu sana. Na nafsi yoyote inayotakiwa kuubeba ujumbe mtukufu kama huu lazima uwe umebeba sifa mbili hizi:

Sifa ya mwenendo na tabia njema, na sifa ya kujitenga mbali na mambo ya kidunia, na matamanio yake, pamoja na;

sifa ya kutafakari na kuwaza.

Hivi ndivyo Allaah Alivyomtayarisha Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya kumebebesha amana kubwa itakayoubadilisha ulimwengu wote, na kuibadilisha historia.

Alimtayarisha kwa kumfanya ajitenge mbali na watu muda wa miaka mitatu kabla ya kumpa jukumu la Utume.

Katika miaka mitatu hiyo, alikuwa mara nyingine akijitenga muda wa karibu mwezi mzima huku akitafakari na kuwaza. Alikuwa akijiuliza:

'Nani mwenye nguvu zote hizi na uwezo wote huu aliyeiumba dunia hii na kuwepo huku?' Alikuwa akipenda kukaa kimya huku akitazama juu mbinguni na kuziangalia nyota na sayari, jua na mawingu, mvua na upepo, kisha akijiuliza:

“Nani aliyevitengeneza vyote hivi? Bila shaka ipo nguvu kubwa yenye uwezo wa kuumba uhai pamoja na kuvitengeneza.”

 

Aliendelea katika hali hiyo mpaka pale Allaah Alipotoa idhini Yake.

 

Mpe Hongera Muhammad

Siku moja Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Bi Khadiyjah (Radhiya Llah ‘anha) kuwa anahisi moyoni mwake kama kwamba anatakiwa aende penye pango la Hiraa.

Bi Khadiyjah (Radhiya Llah ‘anha) akamwambia:

“Haya nenda, lakini kwa vile pango liko nje ya mji, mimi nakuogopea kubaki huko peke yako”.

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

“Usiogope Khadiyjah, kwani Allaah yuko pamoja nami”.

Lakini siku hiyo Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alirudi nyumbani akiwa mwenye hofu kubwa, na Bibi Khadiyjah alipomuuliza:

“Una nini ewe Muhammad?”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

“Ewe Khadiyjah! Nilipokuwa nikitembea huku na kule juu ya jabali, ghafla niliona nuru iking’ara juu yangu kisha nikasikia sauti ikiniita:

“Ewe Muhammad, ewe Muhammad!”

Bibi Khadiyjah akamuuliza:

“Na umeweza kujua sauti hiyo inatokea wapi?”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

“Sikuweza kujua ewe Khadiyjah, na nilikuwa kila ninapoisikia sauti ninageuka huku na kule kumtafuta mwenye sauti hiyo wala simuoni. Nikaingiwa na hofu na kuamua kurudi nyumbani”.

 

Bibi Khadiyjah alimuendea bin ami yake Waraqah bin Nawfal aliyekuwa aalim mwenye kufuata Dini ya Manasara (Dini ya Kikristo) na kumhadithia yote aliyohadithiwa na Muhammad, na Waraqah akamwambia:

“Ewe binti ami yangu, hizi ni bishara njema kutoka mbinguni. Mpe hongera zangu Muhammad na mwambie awe mvumilivu.”

Waraqah aliiingia katika Dini ya Kinasara tokea wakati wa Ujahilia, na alikuwa akijua kuandika lugha ya Ki-Ibrania (Kiyahudi), na aliwahi kuandika Injili katika lugha ya Kiyahudi kile alichojaaliwa na Allaah kukiandika na alikuwa mtu mzima sana (mzee sana) kipofu.

 

Jibriyl Anateremsha Wahyi

Alipotimia umri wa miaka 40, na huu ndio umri uliokamilika (na inasemekana kuwa Mitume yote ‘alayhimus Salaam hupewa utume wakiwa na umri huu), hapo ndipo athari za unabii zilipoanza kuonekana na kudhihirika juu yake, na alama hizo ni ndoto za kweli.

Alikuwa kila anachokiota usingizini hutokea kweli mfano wa asubuhi inavyopambazuka. Akaendelea katika hali hiyo muda wa karibu miezi sita, na muda wa utume wake ulikuwa miaka ishirini na tatu, na ndoto hizo za kweli ni sehemu mojawapo ya sehemu arubaini za utume.

Katika Ramadhaan ya mwaka wa tatu tokea alipoanza kujitenga mbali na watu na kukaa peke yake katika pango la Hiraa, Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) akataka kuuteremshia ulimwengu Rahma Yake na kuukirimu kwa Utume kwa kumteremshia Jibriyl (‘Alayhis Salaam) pamoja na aya za Qur-aan.[42]

 

Anasema Al-Mubaarakpuri:

“Baada ya kuchunguza na kuzitazama dalili zote zenye kuaminika, tunaweza kusema kuwa; Ulikuwa usiku wa Jumatatu – Ramadhaan ya 21 muwafaka na tarehe 10 August mwaka 610 (kalenda ya Gregorian), na wakati huo umri wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ulikuwa ushatimia miaka 40 meizi 6 na siku 12 kwa kalenda ya mwezi (lunar calendar). Na miaka 39 miezi 3 na siku 22 kalenda ya Gregorian.

Ipo khitilafu baina ya Maulamaa juu ya mwezi gani alipewa utume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuteremshiwa wahyi. Maulamaa wengi wanasema kuwa alipewa katika mwezi wa Rabi’ul Awwal, na wengine wakasema kuwa ulikuwa mwezi wa Ramadhaan, na wapo pia wanaosema kuwa ilikuwa katika mwezi wa Rajab, lakini sisi tunaona kuwa rai ya pili ndiyo iliyo sawa, nakusudia katika mwezi wa Ramadhaan, na hii inatokana na kauli Yake (Subhaanahu wa Ta’alaa) Aliposema:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ

"Ni mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa katika mwezi huo hii Qur-aan."

Al-Baqarah – 185

Na inajulikana kuwa Laylatul Qadr imo katika mwezi wa Ramadhaan.

Na pia kutokana na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kupenda kuliendea pango la Hiraa katika mwezi wa Ramadhaan, na ikawa kama inavyojulikana kuwa Jibriyl alimteremkia akiwa penye pango hilo.”

Mwisho wa maneno ya Al-Mubaarakpuri

Ar-Rahiyq Al-Makhtuum ukurasa wa 56

 

Tumsikilize Bibi ‘Aaishah binti Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anha) akituhadithia kisa hicho namna kilivyotokea, kisa kilichoanzisha cheche iliyokuja kuwasha mwanga mkubwa uliomurika ulimwengu mzima huku ukieneza nuru ya Allaah katika kila pembe yake, na huku ikiwatoa watu kutoka katika kiza cha kufru na kuwaingiza katika nuru ya Uislamu. Nuru iliyokuja kuibadilisha nidhamu yote ya ulimwengu na kuibadilisha historia, na kuuongoza uliwengu katika njia mpya na mabadiliko mepya.

Anasema Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha):

“Mwanzo wake alikuwa akiota ndoto njema, na alikuwa kila anachokiota hutokea kweli mfano wa asubuhi inavyopambazuka, kisha akawa anapenda kujitenga mbali na watu na alikuwa akipenda kukaa peke yake kwa muda wa siku nyingi katika pango la Hiraa akifanya ibada, kisha hurudi nyumbani kwa Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) na kukaa naye muda wa siku chache kisha hurudi tena katika pango la Hiraa na kuendelea na ibada zake, mpaka siku ile wahyi wa Allaah ulipomteremkia akiwa pangoni hapo.”

 

Anasema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

“Nilikuwa nimekaa pangoni, na ghafla nikaona nuru juu yangu ikipita kama umeme, kisha nikamuona mtu anateremka kutoka mbinguni huku akinikaribia. Nikaingiwa na khofu, lakini mtu huyo aliniambia:

"Mimi ni Jibriyl, na wewe ni Mtume wa Allaah kwa umati huu."

Kisha Jibriyl akaninyanyua na kunibana kwa nguvu kifuani pake kisha akaniacha, kisha akaniambia:

Iqra-a - Soma!”

Nikamwambia:

Maa – ana biqaarii – (Mimi sijui kusoma)”

"Kisha akanichukua tena na kunibana mpaka nikaishiwa na nguvu, kisha akaniacha na kuniambia; ' Iqra-a!"

Nikamwambia:

Maa – ana biqaarii – (Mimi sijui kusoma).”

Kisha akanikusanya tena na kunibana mpaka nikaishiwa na nguvu, kisha akaniacha na kuniambia:

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ.  خَلَقَ الاِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ. اقْرَأْ وَرَبُّكَ الاَكْرَمُ. الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ. عَلَّمَ الاِنسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ

"Soma kwa jina la Mola wako Aliyeumba.

Amemuumba mwanaadamu kwa pande la damu.

Soma, na Mola wako ni Karimu sana.

Ambaye amefundisha (mwanadamu ilimu zote hizi) kwa msaada wa kalamu.

Amemfundisha mwanaadamu (chungu ya) mambo aliyokuwa hayajui."

Suratul ‘Alaq – 1 – 5

 

Zammiluuniy Zammiluuniy

Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alirudi nyumbani akiwa anatetemeka kwa hofu huku meno yakigongana. Akamuambia mkewe:

Zammiluuniy zammiluuniy" (nifunikeni, nifunikeni), Bibi Khadiyjah akamlaza mumewe kitandani kisha akamfunika huku akimpangusa jasho lililokuwa likimtoka kwa wingi kichwani, huku akimwambia maneno ya kumtuliza mpaka usingizi ulipomchukua.

Aliamka akiwa bado uoga unaonekana usoni pake na Bibi Khadiyjah akamuuliza:

“Una nini ewe Muhammad?”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamhadithia yaliyotokea pangoni, na maneno hayo yalimshitua sana Bibi Khadiyjah, aliyemtaka avae nguo haraka na afuatane naye mpaka kwa

Waraqah bin Nawfal bin Asad bin ‘Abdu-l ‘Uzzah, ambaye ni bin ami yake Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha).

Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) akamwambia Waraqah:

"Ewe mwana wa ami yangu! Hebu msikilize mwana wa ndugu yako huyu."

Waraqah akamuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) :

"Ewe bin ami yangu, kitu gani unachokiona?"

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuhadithia yote aliyoyaona, na Waraqah akamuambia:

"Malaika huyu ndiye yule yule aliyemteremsha Allaah kwa Muusa. Huyu ndiye Malaika mkubwa ‘Jibriyl’ ambaye Allaah Aliwateremshia Muusa na ‘Iysa, na wewe ndiye utakayekuwa Nabii wa umati huu. Yareti ningelikuwa kijana, yareti ningelikuwa hai pale watu wako watakapokutoa."

Mtume wa Allaah Akasema:

"Kwani wao watanitoa?"

Akasema:

"Ndiyo, hajapata mtu anayekuja na kile ulichokuja nacho wewe isipokuwa atafanyiwa uadui, na kama nitaishi mpaka siku hiyo, nitakusaidia kwa nguvu zangu zote."

Haukupita muda mrefu Waraqah alifariki dunia.[43]

 

Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa akimpooza na kumliwaza Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kila anapomuona na hofu.

Alikuwa akimuambia:

"Allaah Hawezi kukufedhehesha hata siku moja, kwa sababu wewe unawaendea na kuwashughulikia watu wako, na unasaidia na kuziendea mbio shida za watu, na unawapa watu kile ambacho kwengine hawawezi kukipata, na unawakirimu wageni, na unachukua juhudi katika kuidhihirisha haki."

 

Wewe Ndiye Mtume Wa Umati Huu

Imesimuliwa na Attabariy kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam alisema:

“Nilipofika kwa Khadiyjah nilikaa karibu yake mwili wangu ukiwa umegandana na wake huku nikimuegemea, akaniambia:

"Ewe Abal Qaasim! Ulikuwa wapi? Kwani WaLlaahi niliwatuma watu wakutafute wakarudi Makkah bila kukuona."

Kisha nikamuhadithia yote yaliyonikuta, akaniambia:

“Ni bishara njema ewe mwana wa ami yangu, tulia usiwe na wasi wasi, Naapa kwa yule ambaye nafsi ya Khadiyjah imo mikononi mwake, nataraji kuwa wewe ndiye Mtume wa umati huu.”[44]

 

Riwaya inaendelea kusema kuwa; Bibi akaondoka na kuelekea moja kwa moja mpaka kwa Waraqah bin Nawfal ambaye baada ya kusikia kisa hicho akasema:

"Qudduus Qudduus, (aliyetakasika aliyetakasika). Naapa kwa yule ambaye nafsi ya Waraqah imo mikononi mwake amejiwa na Malaika mkubwa aliyekuwa akimjia Muusa, na huyu ndiye Nabii wa umati huu. Mwambie apoe asiwe na wasi wasi."

 

Jibriyl ('Alayhis Salaam) aliendela kumshukia Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumfundisha Dini mpya inayowalingania watu katika kumuabudu Allaah Mmoja asiye na mshirika, aliyeumba mbingu na ardhi na kila kilicho ndani yake na baina yake. Mola Mwenye kuuendesha na kuusimama ulimwengu, Mwenye kusimamia kila kubwa na dogo.

Aliendelea kumteremshia aya za Qur-aan tukufu na mafundisho mbali mbali

 

Kutoka siku ile Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawa ndiye Mtume wa Allaah na Nabii wa umati wake na kwa walimwengu wote, aliyeletwa kuwaongoza watu katika njia ya haki na kuwatoa katika giza na kuwaingiza katika nuru.

 

Mafunzo

Katika darsa iliyotangulia tunapata mafunzo juu ya mke mwema ambaye ni mama yetu Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyesimama imara kumsaidia mumewe na kumtii na kumpa moyo, na pia tunapata fundisho namna mke anavyotakiwa kumpokea vizuri mumewe anayerudi nyumbani akiwa amedhikika na matatizo mbali mbali, na kumfanya ahisi kuwa yuko pamoja naye katika matatizo yake yote na kumnusuru na kumsaidia katika kila kubwa na dogo linalomtatiza.

Bibi Khadiyjah alikuwa akimuogopea mumewe (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na alikuwa akijaribu kumpooza na kumtuliza kila anapomuona kuwa anahitaji kutulizwa, kwani alikuwa na uhakika kuwa mumewe yupo juu ya njia ya haki na kwamba mtu mwenye khulqa kama za mumewe kamwe hawezi kupotea wala kupotoka, bali kinyume na hayo, mtu wa aina hiyo lazima atakirimiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa).

 

Kusimama Kwa Wahyi

Imesimuliwa na Ibn Sa’ad kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa zilipita siku nyingi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa akipata wahyi. Na wakati wote huo alikuwa mwingi wa huzuni na masikitiko pamoja na mwingi wa kushangaa.

Amesema Swafiyur Rahmaan Al-Mubaarakpuri katika ‘Ar-Rahiyq Al-Makhtuum’:

“Kwa hakika muda wa kusimama kwa wahyi kama ulivyoelezwa na Ibn Mas’uud kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhum) ulikuwa ni siku nyingi (na siyo miaka mingi), na hili ndilo linalopaswa kukubalika baada ya kupitia malezo yote yanayohusu maudhui haya.

Ama zile habari zilizoenea kuwa kusimama huko kulichukua muda wa miaka mitatu au miwili unusu hayo si sahihi, na hapa si mahali pa kuyasherehesha maudhui haya, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mwingi wa huzuni na masikitiko wakati wote huo.”

Ar-Rahiyq Al-Makhtuum – uk.79-80

 

Jibriyl Anateremka Tena

Anasema Ibn Hajar:

"Na muda wa kukatika Wahyi ulikuwa kwa ajili ya kuiondoa hofu aliyokuwa nayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuacha awe na hamu ya kupokea wahyi mwengine. Na baada ya kutoweka vivuli vya mshangao, na uhakika kuthibiti, na Mtume wa Allaah kuwa na uhakika kuwa yeye kweli ni Mtume wa Allaah Aliyetukuka, na kwamba yule aliyemjia alikuwa mjumbe aliyetoka kwa Allaah akimletea habari kutoka mbinguni.

Kwa ajili hiyo kusubiri kwake kwa hamu kubwa ya kuteremshiwa wahyi kulimfanya awe na msimamo madhubuti na asiwe na uoga atakapojiwa tena.”

 

Jibriyl alimjia tena kwa mara ya pili, na imepokelewa na Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa alimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akihadithia juu ya wakati wahyi ulipokatika, akasema:

"Nilipokuwa nikitembea nilisikia sauti kutoka mbinguni, nikanyanyua macho yangu kuyaelekeza mbinguni, nikamuona Malaika yule aliyenijia Hiraa akiwa amekaa juu ya kiti baina ya mbingu na ardhi, nikamuogopa sana na kuanguka, nikarudi nyumbani na kumwambia mke wangu;

"Zammiluuniy zammiluuniy. (Nifunikeni nifunikeni)" Ndipo Allaah Alipoteremsha kauli Yake:

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ. قُمْ فَأَنذِرْ. وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ. وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ. وَالرُّجْزَ فَاهْجُرْ.

"Ewe uliyejifunika maguo

Simama uonye (viumbe)

Na Mola wako umtukuze

Na nguo zako uzisafishe.

Na Mabaya yapuuze (endelea kuyapuuza)".[45]

 

Kuanzia siku hiyo wahyi ukawa unamteremkia kila mara na kila wakati.[46]

 

Kulingania Kwa Siri

Katika muda wa miaka mitatu ya mwanzo tokea kupewa utume, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alianza kwa kuwalingania watu kwa siri. Alikuwa akiwaita wale tu aliokuwa na uhakika kuwa watamsikiliza na kumfuata au wataificha siri yake hata kama hawatomfuata.

Alianza kwa kumlingania mkewe Bi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyekuwa wa mwanzo kusilimu upande wa wanawake.

Kisha akamlingania sahibu yake Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akimuamini na ambaye hakurudi nyuma, akawa wa mwanzo kuulingania Uislamu, kwani mara baada ya kusilimu kwake, Abu Bakr alianza kufanya kazi ya kuwalingania watu, na siku ya pili yake tu aliweza kuwasilimisha ‘Uthmaan bin ‘Affaan na Az-Zubayr bin ‘Awwaam na ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf na Sa’ad bin Abi Waqaas mjomba wake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  na Twalha bin ‘Ubaydullaah na wote hawa (Radhiya Allaahu ‘anhum) ni katika wale kumi waliobashiriwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa wataingia Peponi.

 

Walioanza Kusilimu

Wa mwanzo kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika wanaume alikuwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa sahibu yake wa utotoni, na ambaye wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoanza kuteremshiwa wahyi, yeye alikuwa safarini Sham kwa ajili ya biashara.

Alipokuwa akirudi Makkah, wa mwanzo kukutana naye njiani alikuwa Abu Jahl (‘Amr ibn Hishaam) aliyemsogelea na kumvamia kwa masuali:

"Umesikia juu ya sahibu yako Muhammad ewe ‘Atiyq?" (‘Atiyq lilikuwa jina la kubandikwa la Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Abu Bakr akauliza: "Amepatwa na jambo lolote?"

Abu Jahl akasema: Eti anadai kuwa yeye ni Mtume anayepata habari kutoka mbinguni."

Abu Bakr: "Nani anayemletea habari hizo?"

Abu Jahl: "Anasema eti Malaika aitwaye Jibriyl."

Abu Bakr: "Yeye mwenyewe amesema hivyo?"

Abu Jahl: "Ndiyo! nimemsikia kwa sikio langu."

Abu Bakr: "Ikiwa yeye mwenyewe amesema hivyo, basi mimi namsadiki."

Abu Bakr akaenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), akagonga mlango na alipofunguliwa akaanza kumuliza:

"Ni kweli haya wanayosema juu yako?"

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: "Wanasema nini?"

Abu Bakr: "Wanasema kwamba wewe unasema kuwa umepata Utume, na kwamba unapata habari kutoka mbinguni."

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Na wewe uliwajibu nini?"

Abu Bakr: "Nimewaambia kuwa; Ikiwa wewe mwenyewe umesema hivyo basi mimi nasadiki."

Kwa furaha isiyo na kifani huku machozi yakimlenga, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimkumbatia sahibu yake huku akimbusu kipaji cha uso wake, kisha akakaa naye na kuanza kumhadithia namna alivyojiwa na Jibriyl katika Pango la Hiraa na jinsi alivyobanwa na Malaika huyo na kumtaka asome aya tano za mwanzo za Surat Al-‘Alaq.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akiyasikiliza yote hayo kwa utulivu mkubwa, alitazama chini kwa khushuu, kisha akatamka:

"Ash- hadu al laa ilaaha Illa Allaah wa ash-hadu annaka Rasuulu Llaah."

(Nashuhudia kuwa hapana mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allaah na nashuhudia kuwa wewe ni Mtume wa Allaah).

 

Kusilimu Kwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa na umri wa miaka minane na zipo kauli zinazosema kuwa alikuwa na umri wa miaka kumi pale wahyi ulipoanza kuteremka. Na siku ile alipomuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiswali, alimuuliza:

"Unafanya nini?"

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

"Ninaswali".

"Unamswalia nani?"

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Mola wa ulimwengu wote".

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu):

"Nani huyu Mola wa ulimwengu wote?"

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

"Ni Allaah mmoja asiye na mshirika, aliyeumba kila kitu, na mikononi mwake imo amri ya kila kitu, Naye ni Mweza wa kila kitu".

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) hapo hapo akazitamka shahada mbili na kuwa mtoto wa mwanzo kusilimu, na akawa miongoni mwa watu wa mwanzo waliokuwa wakihudhuria darsa za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika nyumba ya Al-Arqam bin Abil Arqam pamoja na Maswahaba wenye umri mkubwa kupita yeye kama vile Abu Bakr na ‘Uthmaan na Az-Zubayr na Twalha na ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf na Sa’ad bin Abi Waqqaas na wengine (Radhiya Allaahu ‘anhum).

 

Miongoni Mwa Waliotangulia

Siku ya pili baada ya kusilimu kwake, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwasilimisha watano katika mabwana wa kabila la Quraysh, nao ni ‘Uthmaan bin ‘Affaan, Az-Zubayr bin ‘Awwaam, Abdurahman bin ‘Awf, Sa’ad bin Abiy Waqaas na Twalha bin ‘Ubaydullaah; akaja nao mpaka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na wote hawa kama tulivyotangulia kueleza ni katika wale kumi waliobashiriwa kuingia Peponi.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alifanikiwa kuwasilimisha watu kwa urahisi na kwa haraka sana kwa sababu alikuwa mtu mwenye kupendeza mbele ya watu, mwepesi kuingiliana nao na mwenye tabia njema. Wengi walikuwa wakimpenda na kumheshimu na mara kwa mara walikuwa wakimuendea kutaka ushauri wake juu ya biashara zao, na pia kutaka rai yake katika mambo yao mbali mbali, na hii inatokana na hekima kubwa aliyonayo pamoja na fahamu nzuri juu hali za watu na makabila ya Kiarabu na tabia na mwenendo wao pamoja na Siyrah zao.

 

Siku iliyofuata baada kuwasilimisha ‘Uthmaan na wenzake, Abu Bakr aliweza kuwasilimisha wanne wengine na kuja nao kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  nao ni ‘Uthmaan bin Madh’uun, na huyu ni ndugu wa kunyonya wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  na wa mwanzo kuhajir kwenda Madiynah na alifariki Madiynah, na anajulikana kuwa hakuwa mnywaji wa pombe hata wakati wa ujahilia (kabla ya kuja kwa Uislamu), na alikuwa akisema: “Sitokunywa kinywaji chenye kuipoteza akili yangu akanicheka aliye duni, na wakati huo huo kinaweza kunifanya nikamuingilia hata dada yangu bila kujua.[47]

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimsilimisha pia Abu ‘Ubaydah ‘‘Aamir bin Al-Jarraah (Mwaminifu wa umma huu), Abu Salama na Al-Arqam bin Abi Al-Arqam na jina lake hasa ni ‘Abdul-Manaaf bin Asad Al-Qurashiy.

 

Kisha akasilimu Ja’afar bin Abi Twaalib na mkewe Asmaa binti Umays na ‘Ammaar bin Yaasir na Suhayb bin Sinaan (Mrumi) (Radhiya Allaahu ‘anhum). Na wakati wote huo watu walikuwa wakilinganiwa kwa siri kwa kuendewa kila mtu nyumbani kwake au kazini au shambani pake nk.

 

 

Kusilimu Kwa ‘Uthmaan Bin ‘Affaan

Aliposilimu ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu), watu wake walikasirika sana, na ami yake alimkamata na kumfunga kwa minyororo ndani ya chumba cha kiza, akamuambia:

"Hutoki humo mpaka uiache Dini ya Muhammad na kurudi katika Dini yetu."

‘Uthmaan akamuambia ami yake: "WaLlaahi ewe ami yangu, sitoiacha Dini ya Kiislamu hata siku moja! Hii ndiyo nuru iliyokuja kukiondoa kiza. Sitoiacha Dini ya Muhammad kamwe, hata kama nitakufa ndani ya minyororo hii."

Ami yake alipoona kuwa ameshikilia na hataki kuiacha Dini yake, akaamua kumfungua na kumuacha huru.

 

Sa’ad Bin Abiy Waqaas

Anasema Sa’ad bin Abiy Waqaas:

"Niliposilimu na kuamini Muhammad kuwa ni Mtume wa Allaah na mjumbe wake, mama yangu alikasirika sana akaapa kuwa hatokula chakula chochote mpaka nitoke katika Uislamu. Akagoma kula chakula muda wa wiki nzima, na siha yake ikaanza kuwa dhaifu. Nikamuambia: "Ewe mama yangu! Fanya utakavyo, lakini mimi sitoiacha Dini hii hata siku moja. Vipi unataka nikutii wewe mama yangu na kumuasi Allaah?'

 

Bilaal Bin Rabaah

Miongoni mwa waliopata tabu sana na kuadhibishwa vibaya kwa sababu ya kusilimu kwao alikuwa Bilaal bin Rabaah (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Anasema Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu):

"Bilaal alikuwa mtumwa aliyemilikiwa na mmoja katika makafiri wa Makkah, na aliposilimu, bwana wake huyo akaanza kuMu’aadhibu adhabu iumizayo. Alikuwa akimuacha jangwani mchana kutwa na jua kali likimuunguza. Na mara nyingine alikuwa akimfunga kamba na kuwakabidhi watoto wadogo wamburure na kupita naye mitaani huku wakimpiga mpaka damu ikitoka shingoni. Na mara nyingine alikuwa akimvua nguo zote na kumuacha juu ya mchanga umoto wa jangwani, kisha akiweka jiwe zito kifuani pake huku akimuambia: "Utabaki hivyo hivyo mpaka uiache Dini ya Muhammad na kurudi kuabudu masanamu kama sisi."

 

Lakini Bilaal alihiari kuikabili adhabu nzito na maumivu makali kuliko kuiacha Dini yake, mpaka alipokuja Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), akamnunua kutoka kwa bwana wake, kisha akamuacha huru, na kwa njia hii alimkomboa kutokana na adhabu ile, na Bilaal alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuingia katika Dini ya Kiislamu, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimchagua kuwa ni Mu’aadhini wake.

 

Zayd Bin Haarithah

Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhu) pia ni katika watu wa mwanzo kusilimu. Naye alikuwa mtumwa wa Bi Khadiyjah, akampa zawadi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  akamuacha huru, lakini Zayd alipenda kubaki kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  alikuwa akimpenda sana hata akawa akijulikana kwa jina la ‘Kipenzi cha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ’

 

Nyumba Ya Al-Arqam

Katika vitabu vya Siyrah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  Siyrah ya Ibn Hishaam, Mukhtaswar ya Shaykh An Najd, Ibn Kathiyr, Ibn Taymiyah, Ibn Al-Jawziy, Maimam Al-Bukhaariy, Muslim, Atw-Twabariy, Atw-Twabaraaniy, Abu Bakr Al-Jazaairiy katika ‘Haadhal Habiyb’, Al-Mubarakpuri katika ‘Ar-Rahiyq’ na wengi wengineo wameandika kuwa;

Siku za mwanzo wakati Waislamu walipokuwa wachache sana, makafiri wa Makkah walikuwa kila wanapopata habari juu ya mtu aliyesilimu walikuwa wakimuandama na kumtendea kila aina ya udhia na mateso. Kwa ajili hiyo Waislamu wakawa wanakutana kwa siri katika nyumba ya Al-Arqam bin Abil Arqam Al-Makhzuumiy na kujifunza Dini yao huko.

Wakati huo Waislamu walikuwa kiasi cha watu wasiozidi arubaini, wakiwemo; Bibi Khadiyjah, Binti zake, Abu Bakr Asw-Swiddiyq, ‘Aliy bin Abi Twaalib, na wakati huo ‘Aliy alikuwa na umri wa kiasi cha miaka kumi au minane kama zinavyosema riwaya nyingine.

‘Uthmaan bin ‘Affaan, Bibi ‘Aaishah na Asmaa mabinti wa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Bibi ‘Aaishah alisilimu akiwa mtoto mdogo sana), Zayd bin Haarithah, Az-Zubayr bin ‘Awwaam, ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf, Sa’ad bin Abi Waqaas, Abu ‘Ubaydah, Abu Salamah, Al-Arqam bin Abil Arqam, ‘Uthmaan bin Madh’uun, ‘Ubaydah bin Al-Haarith, Sa’iyd bin Zayd, Khabaab bin Al-Arat, ‘Abdullaah bin Mas’uud, ‘Umayr   bin Abi Waqaas, na wengine (Radhiya Allaahu ‘anhum).

Na hapa tunapata dalili kuwa; wapo wanawake wengi waliokuwa miongoni mwa waliotangulia kuingia katika Dini hii tukufu.

Ukiwatoa wachache hawa, watu wote waliobaki ulimwenguni wakati ule walikuwa wakiabudu masanamu, na wengine wakiabudu miungu wanadamu, miti, mizimu nk.

Allaah Anasema:

وَاذْكُرُواْ إِذْ أَنتُمْ قَلِيلٌ مُّسْتَضْعَفُونَ فِي الأَرْضِ تَخَافُونَ أَن يَتَخَطَّفَكُمُ النَّاسُ فَآوَاكُمْ وَأَيَّدَكُم بِنَصْرِهِ وَرَزَقَكُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

"Na kumbukeni (enyi Waislamu) mlipokuwa wachache, mkionekana madhaifu katika ardhi; mkawa mnaogopa watu wasikunyakueni, Akakupeni mahala pazuri pa kukaa, na Akakutieni nguvu kwa nusura Yake, na Akakupeni riziki nzuri ili mupate kushukuru."

Al-Anfaal-26

 

Waislamu wachache hawa walizungukwa na maelfu ya makafiri washirikina wa Makkah, waliokuwa wakiwasaka na kuwatafuta na kumtesa kila waliyepata habari kuwa ameingia katika Dini hii mpya.

Na mahali pa pekee walipoweza kukutana kwa siri na kujifunza Dini yao palikuwa ndani ya nyumba hiyo ya Al-Arqam ibn Abil Arqam (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

Anasema Al-Mubaarakpuri:

“Ilipita miaka mitatu na watu walikuwa wakilinganiwa kwa siri au kwa kuendewa mtu mmoja mmoja, na ndani ya kipindi hiki likapatikana kundi la Waumini waliokuwa wakishirikiana na kupendana huku wakifanya kazi ya kuufikisha ujumbe kwa watu kwa siri na tahadhari, mpaka pale ilipotolewa amri ya kumtaka Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  kuwalingania watu kwa dhahir bila kuficha.”

 

Anasema Shaykh Abu Bakr Al-Jazaairy:

“Idadi ya Waislamu iliongezeka kila siku juu ya kuwa watu walikuwa wakilinganiwa kwa siri, kwa sababu idadi hii haitoshi kuweza kupambana na makafiri kama watataka kuwadhuru. Lakini sababu kubwa ya kulingania kwa siri si uhaba wao, bali ni kwa kuwa Allaah bado Hakumuamrisha Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wafuasi wake kulingania kwa jahara, na lau kama wangeliamrishwa basi wangelifanya hivyo juu ya uchache wao na juu ya kuelewa fika kuwa watapambana na mateso na adhabu za kila aina, na hii ni kwa sababu walikuwa pamoja na Allaah, na atakayekuwa pamoja na Allaah, basi huyo ni kipenzi chake.”

Haadhal Habiyb – uk.97

 

Hijra Ya Uhabashi

Katika mwezi wa Rajab mwaka wa tano tokea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuanza kuwalingania watu, idadi ya Waislamu iliongezeka na kufikia watu themanini. Hata hivyo idadi hii haikuwa ya kutosha kuwa na nguvu za uwezo wa kusimama mbele ya jeuri na udhia na mateso ya Maquraysh waliozidisha jeuri yao kila wanapoona idadi ya Waislamu ikiongezeka.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawanasihi watu wake wauhame mji wa Makkah kwenda Uhabashi (Ethiopia), akawaambia:

“Itakuwa bora kama baadhi yenu mtaondoka na kuhamia nchi ya Uhabashi, maana huko yuko mfalme ambaye hakubali mtu kudhulumiwa ndani ya nchi yake, na ni nchi ya ukweli. Kwa hivyo hamieni huko mpaka pale Allaah Atakapoleta faraja Yake."

Wakaondoka Makkah watu wapatao kumi wakiwemo Ja’afar na mkewe na ‘Uthmaan bin ‘Affaan na mkewe pamoja na Ruqayyah bint wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  na Waislamu wengine na kuanza safari ndefu ya kuhamia nchi ya Uhabashi katika Hijra ya mwanzo. Kisha idadi yao ikaongezeka na kufikia watu themanini na tatu, na walipowasili huko walipokelewa vizuri na An-Najaashiy mfalme wa Uhabashi.

Jambo hilo liliwakera sana Maquraysh walioamua kutuma ujumbe kwa mfalme wa Uhabashi ukiongozwa na ‘Amru bin Al-’Aasw (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye wakati huo alikuwa bado hajasilimu.

Anasema Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha):

“Tulipowasili nchi ya Uhabashi tulipata mapokezi mazuri kutoka kwa An-Najaashiy na wakatupa himaya na kuturuhusu kuendelea na Dini yetu pamoja na ibada yetu ya kumuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) bila kuudhiwa wala kukirihishwa na jambo lolote.

Habari hizi zilipowafikia Maquraysh ziliwakera sana wakaamua kutuma ujumbe wa watu wawili wenye nguvu na wanaoaminika pamoja na kuwabebesha zawadi nyingi za thamani kubwa zilizokuwa zikipendwa na watu wa Uhabashi wakati ule kwa ajili ya mfalme na maaskofu wake wote, wakausiwa wajumbe wawili hao kuwapa zawadi hizo kwanza maaskofu kabla ya kumpa mfalme wao, na wahakikishe kuwa kila askofu anapata zawadi yake."

Ujumbe huo ulikuwa wa watu wawili maarufu sana kwa uhodari wa kujadiliana, nao ni ‘Amru bin Al-’Aasw na ‘Abdullaah bin Abi Rabiy’ah.

Walipowasili nchi ya Uhabashi wakaenda moja kwa moja kwanza kwa maaskofu wa mfalme na kumpa kila mmoja zawadi yake kisha wakawaambia:

“Wamekimbilia nchini kwenu watoto katika watu duni miongoni mwetu walioiacha Dini yao na Dini ya baba zao na babu zao na wakaleta mfarakano baina ya watu wao. Kwa hivyo pale sisi tutakapomhadithia mfalme wenu juu ya watu wetu hao, nyinyi mpeni ishara kuwa atukabidhi sisi watu hao bila hata kuwauliza juu ya Dini yao, kwani sisi kwa vile ni watu tunaoheshimika katika makabila yao tunawaelewa zaidi na tunaijua zaidi itikadi yao."

Maaskofu wakaitika:

“Sawa”.

Kisha wakamwendea An-Najaashiy na kumpa zawadi anazozipenda sana naye akafurahi nazo, kisha wakamsemesha na kumwambia:

“Ewe mfalme, kwa hakika wamekimbilia nchini kwako watu waovu miongoni mwa watoto wetu, na wamekuja na Dini tusiyoijua sisi wala nyinyi, wakaiacha Dini yetu na wala hawakuingia katika Dini yenu.

Kwa ajili hiyo tumeletwa kwako sisi watu tunaoheshimika katika watu wa makabila yao kutoka kwa baba zao na ami zao na jamaa zao ili utukabidhi watu hao tuarudishe makwao, na wao wanaelewa zaidi juu ya uzushi na fitna waliyoileta.”

Anaendelea kusema Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha):

“An-Najaashiy akawatazama maaskofu wake kama kwamba anataka ushauri wao. Wakamwambia:

“Ewe mfalme, hakika watu wao wanaelewa zaidi na wanajua zaidi juu ya yale waliyotenda, kwa hivyo warudishe makwao wapate kuamua wenyewe juu yao”.

Mfalme akaghadhibika sana kwa maneno ya maaskofu wake akasema:

“Sivyo WaLlaahi! Sitowarudisha kwa mtu yeyote mpaka niwaite wao kwanza kisha niwaulize juu ya yale waliyonasibishwa nayo, na ikiwa maneno waliyosema watu wawili hawa ni kweli, hapo nitawarudisha. Ama ikiwa kinyume na hivyo, basi nitawalinda na nitawapa ukaribisho mwema ikiwa wanataka kuwa chini ya ulinzi wangu”.

Anaendela kusema Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha):

“Kisha An-Najaashiy akatuita na tukamchagua Ja’afar bin Abi Twaalib awe msemaji wetu. Tukaenda kwa An-Najaashiy tuliyemkuta amekaa pamoja na maaskofu wake waliokuwa wamevaa nguo zao za kanisani na kofia zao huku vitabu vyao vikiwa vimetandazwa mbele yao wakiwa kuliani na kushotoni pake. Na tukawaona pia ‘Amru bin Al-’Aasw na ‘Abdullaah bin Abi Rabiy’ah wakiwa pamoja naye.

Baada ya sote kukaa na kutulia katika majlis hiyo, An-Najaashiy akaanza kusema huku akitutazama:

“Ni Dini gani hii mliyoizusha, Dini ambayo kwa ajili yake mkaiacha Dini ya qaumu yenu na wala hamkuingia katika Dini yangu wala katika Dini yoyote nyingine miongoni mwa Dini zilizokuwepo?”

Akainuka Ja’afar bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu), na kwa ushujaa na haiba na ufasaha akaanza kusema maneno ya hekima aliyoyagawa katika mafungu matano. Alikuwa akisema huku akimtazama mfalme huyo kwa jicho la mapenzi na Rahma kutokana na mapenzi na Rahma aliyowaonyesha wageni wake hao katika muda wote waliokaa katika nchi yake. Akasema:

 “Ewe Mfalme!  Tulikuwa watu majahili (wajinga), tukiabudu masanamu, tukila nyamafu, tukifanya matendo machafu, tukiwapiga pande ndugu na jamaa, na majirani hatuwapi haki zao, na mwenye nguvu kati yetu alikuwa akimla dhaifu.

Mpaka Allaah Alipotuletea Mtume katika sisi, tunayemjua yeye na nasabu yake na ukweli wake na uaminifu wake, na kutakasika kwake.

Akatutaka tumpwekeshe na kumwabudu Allaah mmoja Peke Yake na tuache kuabudu yale tuliyokuwa tukiabudu sisi na baba zetu katika mawe na masanamu. Akatuamrisha kusema kweli, kuwa waaminifu, kuunganisha uhusiano baina ya ndugu na jamaa, na akatufundisha juu ya ujirani mwema na akatuamrisha kuacha yale yaliyoharamishwa pamoja na kuacha kumwaga damu baina yetu, akatukataza pia kufanya matendo machafu, na kusema uongo, na kula mali ya yatima, na kuwasingizia uongo wanawake walioolewa.

Tukamsadiki na kumuamini, na tukayafuata yale aliyokuja nayo kutoka kwa Mola wake, tukamuabudu Allaah peke Yake na wala hatukumshirikisha na yeyote na tukayaharamisha yale Aliyotuharamishia, na tukayahAlisha yale AliyotuhAlishia.

Watu wetu wakatugeukia na kuanza kututesa kwa ajili ya Dini yetu ili waturudishe katika kuabudu masanamu na kurudia yale maovu tuliyokuwa tukiyatenda. Na baada ya kutuadhibisha na kutudhulumu na kutudhiki na kutuzuia tusiifuate Dini yetu, tukatoka na kukimbilia katika nchi yako, na tukachagua kuwa chini ya ulinzi wako na tukatamani tusidhulumiwe tukiwa kwako.”

 

An-Najaashiy akamtazama Ja’afar muda kidogo kisha akamuuliza:

“Unaweza kunisomea chochote katika yale aliyoteremshiwa Mtume wenu?”

Ja’afar akamsomea Surat Maryam kuanzia:

كهيعص. ذِكْرُ رَحْمَةِ رَبِّكَ عَبْدَهُ زَكَرِيَّا. إِذْ نَادَى رَبَّهُ نِدَاء خَفِيًّا. قَالَ رَبِّ إِنِّي وَهَنَ الْعَظْمُ مِنِّي وَاشْتَعَلَ الرَّأْسُ شَيْبًا وَلَمْ أَكُن بِدُعَائِكَ رَبِّ شَقِيًّا

“Kaaaaaaf Ha Ya ‘Aaaaaaayn Swaaaaaad.

(Huu ni) Ukumbusho wa rehema ya Mola wako (kumrehemu) mja Wake Zakaria.

Aliomlingania Mola wake kwa mlingano wa siri.

Akasema: “Mola wangu. Bila shaka mifupa yangu imekuwa dhaifu na kichwa kinawaka kwa mvi, wala sikuwa mwenye bahati mbaya. Mola wangu kwa kukuomba wewe…”

 

Akaendela kuisoma Surat Maryam kwa khushuu na utulivu, jambo lililomfanya An-Najaashiy alie mpaka ndevu zake zikarowa machozi, na maaskofu wake wote wakawa wanalia.”

Kisha An-Najaashiy akasema:

“Haya aliyokuja nayo Mtume wenu na aliyokuja nayo ‘Iysa yanatokana na nuru moja”.

Kisha akamgeukia ‘Amru na sahibu yake akawaambia:

“Rudini, kwani WaLlaahi sitokupeni kabisa muondoke nao.”

 

Walipokuwa wakitoka, ‘Amru na mwenzake walitoa ahadi kuwa lazima wataondoka nasi, akamwambia mwenzake:

“WaLlaahi tutakuja kwa mfalme kesho na tutamulezea mambo yatakayomjaza chuki juu yenu kifuani pake ili akung’oeni mpaka mizizi yenu”.

Mwenzake akamwambia:

“Usifanye hivyo ewe ‘Amru, kwani hawa ni jamaa zetu juu ya kuwa wamekwenda kinyume nasi.”

‘Amru akasema:

“Achana na maneno yako, WaLlaahi nitamwambia mambo yatakayoitetemesha miguu ya mfalme, nitamwambia kuwa wao wanasema kuwa ‘Iysa bin Maryam ni mtumwa”.

Siku ya pili yake ‘Amru akaingia kwa An-Najaashiy na kumwambia:

“Ewe mfalme, hawa uliowapokea na kuwapa himaya yako wanasema juu ya ‘Iysa mwana wa Maryam maneno mabaya sana”.

An-Najaashiy akawaita tena na kutaka kujua nini kauli yao juu ya ‘Iysa bin Maryam.

Anasema Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha):

“Tulipojua kuwa tunaitiwa jambo hilo, tukaingiwa na wasiwasi na khofu wala hatukupata kuingiwa na hofu namna hiyo. Lakini tukaamua kuwa hatutomwambia isipokuwa yale tu aliyosema Allaah juu ya Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) bila kuzidisha wala kupunguza.

Na tuliposimama mbele ya An-Najaashiy akatuuliza:

“Mnasemaje juu ya ‘Iysa bin Maryam?”

Ja’afar akainuka na kusema:

“Sisi tunasema juu yake yale aliyokuja nayo Mtume wetu”.

Akasema An-Najaashiy:

“Na nini hayo alokuja nayo Mtume wenu?”

Ja’afar akajibu:

“Anasema kuwa yeye ni mja wa Allaah na Mtume wake na roho iliyotoka kwake na Tamko Lake alilompelekea Maryam Al-Batuul”.

Alipoyasikia hayo An-Najaashiy akaupiga mkono wake juu ya ardhi, akaokota kijiti, kisha akakinyanyua, akasema:

“WaLlaahi ‘Iysa hajakivuka kijiti hiki kwa hayo unayoyasema”. (yaani hayo uliyosema juu ya ‘Iysa ni sawa na wala hujaongeza wala kuzidisha chochote juu yake).

Maaskofu wakakohoa kuonyesha kutoridhika kwao na maneno hayo. An-Najaashiy akasema:

“Hata kama mtakohoa WaLlaahi”, kisha akatugeukia na kutuambia:

“Nendeni, nanyi mko katika amani, na yeyote atakayekutukaneni atakulipeni fidia na atakayekushambulieni atatiwa adabu, WaLlaahi sitopenda niwe na dhahabu ukubwa wa jabali kisha mmoja wenu limsibu jambo lolote lile baya.”

Kisha akamgeukia ‘Amru na mwenzake na kuwaambia:

“Warudishieni watu wawili hawa zawadi zao, sina haja nazo mimi.”

Wakarudishiwa zawadi zao na kuondoka kurudi Makkah huku wakiwa wamehizika.

“Amma sisi”, anaendelea kusema Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha), “Tukabaki hapo na tulikirimiwa vizuri na mtu mwema huyo”.

 

Kusilimu Kwa Hamzah

Siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amekaa juu ya mlima wa Swafaa, na Abu Jahl alipomuona alianza kumtukana matusi machafu na kumwambia maneno ya kumdharau na kuidharau amri aliyokuja nayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakumjibu wala hakumsemesha, lakini Bibi mmoja aliyesikia maneno hayo alimhadithia Hamzah (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa wakati huo akipita njia akitoka safari ya kuwinda huku akiwa amebeba upinde na mishale.

Baada ya kuhadithiwa namna Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyotukanwa na Abu Jahl, Hamzah hakutazama huku wala kule, aliondoka moja kwa moja mpaka kwa Abu Jahl aliyekuwa amekaa barazani pamoja na sahibu zake, akampiga usoni kwa upinde aliokuwa ameubeba na damu zikamtoka, kisha akamuambia:

"Unamtukana wakati mimi nafuata Dini yake na nasema yale anayosema? Nipige na wewe basi kama unaweza."

Wakainuka baadhi ya watu wa kabila la Bani Makhzuum kutaka kumsaidia Abu Jahl, lakini akawaambia:

"Muacheni. Kweli mimi nilimtukana mtoto wa ndugu yake matusi mabaya."

Hamzah akasilimu kama alivyosema, jambo lililowafurahisha sana Waislamu kwani Hamzah alikuwa akijulikana kuwa ni kijana hodari na shujaa miongoni mwa vijana wa Kiquraysh.

 

Kusilimu Kwa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Adhuhuri moja katika mwaka wa sita tokea kupewa utume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alitoka nyumbani panga mkononi akielekea nyumba ya Al-Arqam bin Abil Arqam ili amuue Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Hii ilikuwa siku ya tatu tokea kusilimu Hamzah (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Wakati huo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa keshaomba dua aliposema:

"Mola wangu upe nguvu Uislamu kwa kusilimu mmoja katika ‘Umar wawili."

Mtu mmoja alipomuona ‘Umar katika hali ile akamuuliza:

"Unaelekea wapi ewe ‘Umar?"

‘Umar akasema: "Nakwenda kwa huyu anayewabadilisha watu na kuwatenganisha Maquraysh na kuitukana Dini yao pamoja na miungu yao. Nakwenda kumuua".

Yule mtu akamwambia:

"Uelekeaji mbaya unaoelekea na mwendo mbaya unaokwenda."

‘Umar akadhani kuwa huyu naye keshasilimu, akamuuliza:

"Isiwe na wewe wamekubadilisha pia? Ikiwa ni hivyo basi bora nikuanze wewe."

Huku akiwa na hofu yule mtu akamwambia:

"‘Umar, Jua ya kuwa dada yako keshasilimu pamoja na mumewe Sa’iyd bin Zayd na wamekwisha iacha Dini yako".

 

‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akageuza njia na kuelekea nyumbani kwa dada yake Faatwimah bint Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyekuwa wakati huo yuko pamoja na mumewe na Swahaba mwengine aitwae Khabbaab bin Al-Arat (RadhiyaLlaahu ‘anhum), na wote walikuwa wakisoma na kuidurusu Qur-aan tukufu.

‘Umar akagonga mlango kwa kishindo kikubwa.

"Nani?"
"Mimi ‘Umar!"

Khabbaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliruka na kujificha chini ya kitanda. Faatwimah dada yake ‘Umar, aliwahi kuzificha karatasi zilizoandikwa Qur-aan tukufu. Wakamfungulia mlango na kumkaribisha.

‘Umar akawauliza:

"Ni yepi haya maneno niliyoyasikia mkiyasoma?"

Wakajibu:

"Si kitu ni mazungumzo na hadithi tu."

‘Umar:

"Nasikia nanyi pia mumebadilisha Dini yenu?"

Sa’iyd:

"‘Umar! unaonaje ikiwa ukweli upo katika Dini nyingine….?"

‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakumuacha amalize maneno yake, akamrukia kwa nguvu za ajabu na kumwangusha chini kwa kishindo kisha akamkalia juu ya kifua chake, na dada yake alipojaribu kumsaidia mumewe, alipigwa kofi la nguvu usoni na damu zikaanza kumtoka, jambo lililomfanya apige ukelele mfano wa baragumu au radi huku akimkabili ‘Umar na kumwambia:

"Ewe adui wa Allaah! Unanipiga kwa sababu nimemuamini Allaah mmoja? Basi fanya utakavyo mimi natamka:

"Ash-hadu al-laa ilaaha illa Llaah wa anna Muhammadan Rasuulu Llaah!"

 

‘Umar akainuka juu ya kifua cha Sa’iyd (Radhiya Allaahu ‘anhu), na alipoziona zile karatasi alozificha dada yake akamwambia:

"Nipe hizo karatasi."

Dada yake akamwambia:

"Hawazigusi hizi isipokuwa waliotwaharikia. Nenda kaoge kwanza upate kutwaharika."

‘Umar akaenda kuoga kisha akarudi haraka huku ndevu zake zikiwa bado zinatiririka maji, akazichukua karatasi kutoka kwa dada yake na kuanza kuzisoma, na ndani yake ilikuwa imeandikwa Surat Twaahaa - kuanzia aya ya mwanzo hadi ya kumi na sita, na baada ya kumaliza kusoma ‘Umar akasema:

"Haipaswi kwa mwenye aya kama hizi kuwa na mshirika anayeabudiwa pamoja naye, - Nipelekeni kwa Muhammad!"

 

Hapo ndipo Khabbaab aliyekuwa amejificha chini ya kitanda alipojitokeza na kusema:

"Bishara njema ewe ‘Umar, WaLlaahi Allaah Ameikubali dua ya Mtume Wake."

‘Umar akatoka na kuelekea nyumba ya Al-Arqam, na Hamzah aliyekuwa ndani humo pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomuona ‘Umar akija na uso mkunjufu, akasema:

"Huyo anakuja. Ikiwa Allaah Anamtakia kheri basi atasilimu, ama iwapo hamtakii hivyo, basi kifo chake kitakuwa mikononi mwetu leo."

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuendea ‘Umar, akamkabili na kumuambia:

"Hivyo utangoja ewe ‘Umar mpaka Allaah Atakapoteremsha aya juu yako zikikulaani kama alivyoteremshiwa Al-Waliyd bin Mughiyrah?

Mola wangu, huyu ‘Umar bin Al-Khattwaab! Allaah Ipe nguvu Dini kwa kumuingiza ‘Umar katika Dini yako."

‘Umar akazitamka shahada mbili:

"Ash-hadu al-laa ilaaha illa Llaah wa ash-hadu annaka Rasuulu Llaah."

Kwa kauli hii, ushujaa na nguvu zake alizokuwa akizitumia katika kuupiga vita Uislamu akavigeuza na kuvitumia katika kuulinda na kuuendeleza Uislamu.

 

Alisilimu akiwa na umri wa miaka ishirini na sita. Anasema Al-Mubaarakpuri katika Ar-Rahiyq Al-Makhtuum:

"Na wakati huo walikuwa wamekwishasilimu watu thelathini na tisa na yeye akawa wa arubaini."

 

Siku ya pili yake ‘Umar alimwendea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuuliza:

"Sisi si tuko katika haki katika kuishi kwetu na kufa kwetu ewe Mtume wa Allaah?"

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Ndiyo ewe ‘Umar. Naapa kwa Yule ambaye nafsi zetu zimo mikononi Mwake, nyinyi mumo katika haki katika maisha yenu na katika kufa kwenu".

‘Umar ((Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:

"Kwa nini basi tunajificha? Naapa kwa Yule aliyekuleta kwa haki, utoke, na sisi tutoke pamoja na wewe."

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akalikubali ombi la ‘Umar.

Anasema ‘Umar bin Al-Khattwaab:

"Tukatoka na tukawa tunatembea katika barabara za Makkah mistari miwili. Msitari mmoja ukiongozwa na Hamzah na mwengine ukiongozwa na mimi mpaka tulipoingia Msikitini (Al-Ka’abah) huku makafiri wakituangalia tu wakiwa wamepigwa na bumbuwazi. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliponibandika jina la 'Al-Faruuq'. (mwenye kuiweka sawa haki mbele ya batil).

(Tariykh ‘Umar bin Al-Khattwaab cha Ibn Al-Jawziy)

 

Aila Yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

Baada ya idadi ya Waislamu kufikia kiasi cha watu arubaini na zaidi kidogo wakiwemo wanawake wachache, na baada ya kusilimu kwa Hamzah na ‘Umar, nguvu ya Waislamu ikaongezeka, na Allaah Akamuamrisha Mtume wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aanze kuwalingania watu wa nyumba yake bila kificho.

Allaah Alisema:

وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الأَقْرَبِينَ

Na uwaonye jamaa zako walio karibu (nawe)

Ash-Shu’araa- 214

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaita watu wa nyumba yake, kisha akapanda juu ya jabali Swafaa ambalo hivi sasa limo ndani ya Msikiti wa Makkah, akawaambia:

"Enyi watu wa kabila la Quraysh, kama nitawaambieni kuwa wapanda farasi wapo nyuma ya jabali hili wakijitayarisha kukushambulieni, mtanisadiki?"

Wote kwa pamoja wakamuambia:

"Bila shaka tutakusadiki, kwa sababu hatujapata kusikia kutoka kwako isipokuwa maneno ya kweli."

Akasema: "Basi mimi ni muonyaji kwenu juu ya adhabu kali iliyo mbele yenu. Okoeni nafsi zenu kutokana na moto…"

Akainuka Abu Lahab na kusema:

"Tabban laka (umeangamia wewe) hivyo umetukusanya na huna la kutuambia isipokuwa maneno haya?"

Allaah Akateremsha Surat Al-Masad:

تبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ. مَا أَغْنَى عَنْهُ مَالُهُ وَمَا كَسَبَ.  سَيَصْلَى نَارًا ذَاتَ لَهَبٍ. وَامْرَأَتُهُ حَمَّالَةَ الْحَطَبِ. فِي جِيدِهَا حَبْلٌ مِّن مَّسَدٍ.

“Imeangamia mikono ya Abu Lahab, na yeye pia ameangamia. Hayatamfaa mali yake, wala alivyovichuma. Atauingia Moto wenye mwako. Na mkewe, mchukuzi wa kuni. Shingoni mwake iko kamba iliyosokotwa.”

Surat Al-Masad

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwalingania watu kwa siri muda wa miaka mitatu, na baada ya hapo, na kwa muda wa zaidi ya miaka ishirini iliyofuata aliwalingania watu kwa jahari na hajapata tena raha yoyote wala wakati mwingi kwa ajili ya nafsi yake wala kwa wake zake wala watoto wake.

Aliupokea mwito wa Mola wake tokea alipoambiwa:

Simama uonye (viumbe)

Na Mola wako umtukuze

Alisimama kidete katika kuwaonya watu na kuwaita katika njia ya Allaah, na katika kumtukuza Mola wake. Aliubeba mzigo aliopewa kwa mikono miwili, akapambana na kila aina ya tabu na adhabu na mateso na uadui.

Aliipigania Dini kwa juhudi yake yote, akasimama imara dhidi ya kila adui dhaalim aliyejaribu kumzuia asiisimamishe Dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa).

 

Kulingania Kwa Jahara

Tunaweza kuzigawa sehemu za kulingania watu katika awamu mbili:

1.    Awamu ya Makkah – nayo ni miaka kumi.

2.    Awamu ya Madiynah – karibu miaka kumi na mitatu.

 

Tunaweza pia kuigawa awamu ya Makkah katika sehemu mbili:

Sehemu ya kulingania kwa siri – nayo ni miaka mitatu.

Sehemu ya kulingania kwa jahari hapo Makkah – kuanzia mwaka wa nne tokea kupata utume hadi mwisho wa mwaka wa kumi.

Sehemu ya kulingania watu nje ya Makkah na kuenea kwake – kuanzia mwaka wa kumi mpaka alipohamia Madiynah

 

Baada ya kusilimu kwa Hamzah na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhum), watu wengi waliokuwa wakiuficha Uislamu wao wakaanza kuudhihirisha, na katika wakati huo huo Allaah Akaitermsha aya isemayo:

فَاصْدَعْ بِمَا تُؤْمَرُ وَأَعْرِضْ عَنِ الْمُشْرِكِينَ

Basi wewe yatangaze uliyoamrishwa, na jitenge na washirikina

Al-Hijr- 94

 

Hapo ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoanza kuutangaza Uislamu wazi wazi bila kuficha. Akawa anawaendea watu na kuwaambia juu ya ujinga wa kuyaabudu masanamu na kuyasujudia, na kwamba masanamu hayo hayana uwezo wa kunufaisha wala kudhuru, bali hayana uwezo hata wa kujikinga yenyewe na madhara. Akawataka wamuabudu Allaah mmoja aliyeumba ulimwengu wote na kila kilicho juu yake.

 

Maquraysh walikasirishwa sana waliposikia kwa mara ya mwanzo sauti ikinyanyuka na kuwatukana miungu yao kwa kuwaambia kuwa haina uwezo wa kudhuru wala kunufanisha, wakaanza kuwamiminia Waislamu hasa wale madhaifu wasiokuwa na makabila makubwa ya kuwalinda na kuwahami, waliwatesa na kuwaadhibu na kuwanyanganya mali zao nk.

 

Mateso Mbali Mbali

Utumbo Wa Ngamia

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa; siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ndani ya Al-Ka’abah akiswali, na Abu Jahl na sahibu zake walikuwa wamekaa. Wakawa wanasemezana: ‘Nani kati yenu atakayeleta utumbo wa ngamia (aliyechinjwa) na watu wa kabila fulani na kuuweka utumbo huo juu ya mgongo wa Muhammad wakati amesujudu?’

Anaendela kuhadithia ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu); “Akainuka muovu wao, akauleta, akasubiri mpaka pale Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposujudu, akauweka (utumbo huo) juu ya mgongo wake baina ya mabega yake mawili, na mimi nikawa ninaangalia tu sina uwezo wa kufanya lolote kwa sababu sina nguvu za kupigana nao (au sina kabila la kunihami.)” Akasema: “Wakawa wanacheka kwa furaha huku wakiegemeana na kuashiriana, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa bado amesujudu. Hakuinua uso wake, mpaka alipokuja Faatwimah akauondoa utumbo juu ya mgongo wake, ndipo alipounyanyua uso wake kisha akasema: ((Mola wangu waangamize (makafiri) wa Quraysh)). (Alisema hivyo) mara tatu jambo lilowafanya Maquraysh waone uzito nyoyoni mwao kwa dua hiyo kwa sababu walikuwa wakiamini kuwa dua katika mji ule inakubaliwa. Kisha akaomba dua kwa kutaja majina. Akasema: ((Mola wangu muangamize Abu Jahl na muangamize ‘Utbah bin Rabiy’ah na Shaybah bin Rabiy’ah na Al-Waliyd bin ‘Utbah na Umayyah bin Khalaf na ‘Uqbah bin Abi Mu’iyt)). Akamtaja na mtu wa saba lakini nimemsahau.” Akasema (Ibn Mas’uud): “Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake; Niliwaona wale waliotajwa majina yao na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakiwa miongoni mwa waliouliwa na kutupwa ndani ya kisima cha Qulayb siku ya vita vya Badr.”

Al-Bukhaariy, Muslim na wengine

 

Nitamkanyaga Shingo Yake

Siku moja Abu Jahl aliinuka akasema kwa sauti kubwa: "Enyi watu! Muhammad anasujudu na kuuweka uso wake juu ya ardhi mbele yenu?” wakasema: “Ndiyo.” Akasema: “Naapa kwa Lata na ‘Uzza kuwa nitakapomuona akifanya hivyo nitamkanyaga shingo yake na nitausugua uso wake juu ya ardhi!"

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaja Msikitini akawa anaswali na Abu Jahl alipomkaribia kujaribu kumkanyaga alirudi nyuma haraka huku akijikinga kwa mikono yake. Wakamuuliza: "Una nini ewe Abal Hakam?"

Akasema: "Baina yangu na yeye pana handaki la moto na mnyama mkubwa wa kutisha sana mwenye mbawa.” Alisema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Angelinisogelea zaidi angelinyakuliwa na Malaika vipande vipande.))

Muslim na wengine

 

Oh! Mtamuua?

Kutoka kwa Urwa bin Zubayr alisema: “Nilimuuliza mwana wa ‘Amru bin Al-’Aasw anihadithie juu ya kitendo kiovu sana alichowahi kutendewa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia:

“Siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali penye Al-Ka’abah, akamtokelea ‘Uqbah bin Abi Mu’iyt na kumshika mabega yake, kisha akamzungushia nguo shingoni pake, akamkaba nayo roho kwa nguvu sana, akawa anashindwa kuvuta pumzi. Akatokea Abu Bakr na kumshika mabega ‘Uqbah akamsukuma mbali na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kisha akasema:

أَتَقْتُلُونَ رَجُلاا أَن يَقُولَ رَبِّيَ اللَّهُ

“Oh! Mtamuua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Allaah?”

Al-Bukhaariy

 

Rudi Kwenu Ukawalinganie

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) akihadithia juu ya kisa cha kusilimu kwa Abu Dhar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia ((Rudi kwa watu wa kabila lako na uwajulishe (baki huko) mpaka itakapokuja amri kutoka kwangu.)) Akasema: “Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake, nitaulingania Uislamu kwa sauti kubwa mbele yao (makafiri).” Akatoka na kuelekea moja kwa moja mpaka penye Al-Ka’abah akapaza sauti yake akisema: “Nashuhudia kuwa hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume Wake.” Wakainuka watu wakaanza kumpiga na kumuumiza. Akaja Al-’Abbaas na kumkinga kisha akasema: “Ole wenu! Kwani hamuelewi kuwa huyu anatokana na kabila la Ghufar, na kwao ndiyo njia yenu mnayopitia katika biashara zenu?” Akamuokoa nao. Na siku iliyofuata alifanya hivyo hivyo na Al-’Abbaas akamkinga tena.”

Al-Bukhaariy

 

Wa Mwanzo Kuudhihirisha Uislamu

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Wa mwanzo kuudhirihirisha Uislamu wao walikuwa saba; Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr, ‘Ammaar na mama yake Sumayyah, na Suhayb na Bilaal na Al-Miqdaad. Ama Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Allaah Alimjaalia ami yake Abu Twaalib awe kama kinga yake, na Abu Bakr Allaah Alimkinga kutokana na ukoo wake, lakini waliobaki walichukuliwa na makafiri, wakavishwa ngao za chuma na kuwekwa juani huku wakiteswa. Hapana hata mmoja kati yao aliyeweza kustahamili mateso hayo, wakawakubalia kwa wanayoyataka isipokuwa Bilaal, yeye hakuithamini nafsi yake mbele ya Allaah na watu wake hawakuweza kumsaidia.”

 

‘Ammaar bin Yaasir alikuwa akimilikiwa na watu wa kabila la Bani Makhzuum, na alisilimu yeye pamoja na baba yake na mama yake (Radhiya Allaahu ‘anhum). Abu Jahl akishirikiana na washirikina wenzake walikuwa wakiwachukua jangwani wakati wa jua kali na kuwavisha ngao za chuma (wapate kuungua vizuri), kisha wanawaadhibu na kuwatesa.  Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipita na kuwaona wanavyoadhibishwa, akawa anawaambia: “Vumilieni enyi watu wa nyumba ya Yaasir, hakika zawadi yenu ni Pepo.” Yaasir alifariki kutokana na adhabu kali, na mkewe Sumayyah (mama yake Yaasir) aliuliwa na Abu Jahl kwa kupigwa kisu cha moyo na Bibi huyu ni mtu wa mwanzo kufa shahiyd katika Uislamu.

‘Ammaar aliendelea kuteswa kwa kuwekewa mawe ya moto kifuani au kuzamishwa uso wake ndani ya maji huku akiambiwa: “Hatukuachi mpaka umtukane Muhammad au uwasifie miungu yetu Lata na ‘Uzza.” Akawatii katika hayo kwa kulazimishwa baada ya kuteswa sana, ndipo walipomuacha, akaenda moja kwa moja mpaka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa analia huku akimuomba msamaha. Ndipo ilipoteremshwa aya isemayo:

مَن كَفَرَ بِاللّهِ مِن بَعْدِ إيمَانِهِ إِلاَّ مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالإِيمَانِ

Anayemkataa Allaah baada ya kuamini kwake - isipokuwa aliyelazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetua juu ya Imani

An-Nahl - 106

Siyrah Ibn Hishaam na Ibn Maajah

 

Mafunzo

Hii ni mifano michache ya mashambulizi na mateso aliyotendewa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na sahibu zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) ikisadikisha kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Aliposema:

أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لا يُفْتَنُونَ

“Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe?”

Surat al-‘Ankabuut- 1

 

Na Akasema:

أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُواْ الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَأْتِكُم مَّثَلُ الَّذِينَ خَلَوْاْ مِن قَبْلِكُم مَّسَّتْهُمُ الْبَأْسَاء وَالضَّرَّاء وَزُلْزِلُواْ حَتَّى يَقُولَ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُواْ مَعَهُ مَتَى نَصْرُ اللّهِ أَلا إِنَّ نَصْرَ اللّهِ قَرِيبٌ

“Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, bila ya kukujieni kama yaliyowajia wale waliopita kabla yenu? Iliwapata shida na madhara na wakatikiswa hata Mtume na walioamini pamoja naye wakasema: Lini nusura ya Allaah itakuja? Jueni kuwa nusura ya Allaah ipo karibu.”

Al-Baqarah-214

 

Imepokelewa kuwa siku moja Khubaab bin Al-Arat alimuendea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: “Ewe Mtume wa Allaah, makafiri wanatutesa sana, si bora ungelimuomba Allaah atusaidie?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa chini kwanza huku uso wake ukiwa mwekundu kisha akasema: “Waliokuja kabla yenu, mtu alikuwa akichunwa nyama yake au mishipa iliyo juu ya mafupa yake kwa msumeno wa chuma, na mateso hayo hayakuweza kumtoa katika Dini yake. Kisha akiwekewa msumeno juu ya kichwa chake na kukatwa pande mbili na hayakumtoa hayo katika Dini yake. Allaah Ataitimiza (ataipa ushindi) Dini hii, na itafika siku mtu ataweza kusafiri kutoka Swan’aa (Yemen) hadi Hadhramawt bila ya kuhofia chochote isipokuwa Allaah.”

Al-Bukhaariy na Ahmad

 

Kutokana na aya hizi pamoja na mateso yale, tunaelewa kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Hampi mja wake ushindi mpaka kwanza Ampambanishe na mithihani na majaribio.

Na kutokana na yaliyotangulia, tunapata pia fundisho kuwa Allaah Alimpa ushindi Mtume wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) dhidi ya adui zake waliokuwa wakimfanyia isthizai na kumkejeli na kumtesa kwa kuuliwa makafiri hao na kutupwa ndani ya kisima.

Allaah Anasema:

إِنَّا كَفَيْنَاكَ الْمُسْتَهْزِئِينَ

Hakika Sisi tunatosha kukukinga na wanao kejeli.

Al-Hijr - 95

 

Wanasema Maulamaa pia kuwa katika darsa iliyotangulia tunapata fundisho kuwa mtu anatakiwa kuwalingania watu wa karibu yake kwanza, ndugu na jamaa zake kabla hajawaendea watu wa mbali. Kwani si jambo la busara kwa mtu kuwaita watu wa mbali katika tabia njema kwa mfano wakati watoto wake na watu wa nyumba yake wako katika upotovu (upotevu). Isitoshe mlinganiaji anahitajia watu wa kumhami na kumlinda na kumsaidia, na bila shaka watu wake watakapomfuata watakuwa msitari wa mbele katika kumhami mlinganiaji kupita watu wa mbali. Ndiyo maana watu wa mwanzo kusilimu walikuwa mkewe Bibi Khadiyjah na Zayd na ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhum) waliokuwa wakiishi nyumbani kwake, na pia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa sahibu yake.

 

Tunapata fundisho pia kuwa kule kusimama imara Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya mateso yote yale ni dalili ya imani yao ya kweli isiyotetereka, na kwamba walikuwa wakishirikiana na kupendana, na walikuwa tayari kujitolea kwa roho zao na nafsi zao na mali zao kwa ajili ya kuisimamisha Dini ya Allaah, na walikuwa wakitegemea kutoka kwa Allaah zawadi tukufu zaidi kupita adhabu ile iumizayo waliokuwa wakiipata hapa duniani kutoka kwa makafiri wa Makkah.

 

Starehe na natija na faida inayomtawala na kumridhisha mtu aliyeamini kikweli inakuwa ya kiroho na siyo kimwili. Maswahaba kwa mfano (Radhiya Allaahu ‘anhum) utawakuta siku zote nafsi zao zikiridhika na mateso ya kimwili kama vile njaa na usingizi na adhabu na kufukuzwa na kukimbizwa na adhabu nyingine za kimwili, kwa kutegemea kupata kilicho kitukufu zaidi, nacho ni radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa).

Kwa njia hii azma ilipata ushindi na uhuru wa kweli ulipatikana, na kwa njia hii waliweza kufanikiwa kuwatoa watu katika giza na kuwaingiza katika nuru.

 

Mbinu Mbali Mbali

Makafiri walipoona kuwa mateso mbali mbali na ukatili waliokuwa wakimfanyia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Sahibu zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) hayakuweza kuivunja nguvu Dini hii mpya, wakaamua kutumia mbinu nyingine za kuwachukiza watu nayo. Wakaanza kwa kusema kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni mwendawazimu, kisha wakasema kuwa ni muongo, wakamtuhumu kuwa ni mchawi, na kwamba Qur-aan ni visa vya watu wa zamani, wapotovu na mambo mengi mengine, ikawa kama Allaah Alivyosema:

إِنَّ الَّذِينَ أَجْرَمُوا كَانُواْ مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا يَضْحَكُونَ. وَإِذَا مَرُّواْ بِهِمْ يَتَغَامَزُونَ. وَإِذَا انقَلَبُواْ إِلَى أَهْلِهِمُ انقَلَبُواْ فَكِهِينَ. وَإِذَا رَأَوْهُمْ قَالُوا إِنَّ هَؤُلَاء لَضَالُّونَ. وَمَا أُرْسِلُوا عَلَيْهِمْ حَافِظِينَ

Kwa hakika wale waliokuwa wakosefu walikuwa wakiwacheka walioamini. Na wanapopita karibu yao wakikonyezana. Na wanaporudi kwa watu wao hurudi nao wamefurahi. Na wanapowaona husema: Hakika hawa ndio khasa waliopotea. Na wao hawakutumwa wawe walinzi juu yao.

Al-Mutwaffifiyn – 29-33

 

Unaonaje Tukaabudu Unachoabudu

Imepokelewa kuwa siku moja wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akitufu Al-Ka’abah, alisimamishwa na Al Aswad bin ‘Abdul-Mutwallib bin Asad na ‘Abdul’Uzza na Al Waliyd bin Mughiyra na Umayya bin Khalaf na makafiri wengine, wakamuambia: “Ewe Muhammad! Unaonaje sisi tukaabudu unachokiabudu na wewe pia uabudu tunachokiabudu sisi na tushirikiane sisi na wewe katika jambo hili. Ikiwa unachokiabudu wewe kina Kheri kuliko chetu na sisi tutapata kufaidika pia, na kama tunachoabudu sisi kina Kheri zaidi kuliko unachoabudu wewe, na wewe pia utapata kufaidika. Kutokana na kauli yao hiyo, ndipo Allaah Alipoiteremsha Suratul Kaafirun:

قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ. لا أَعْبُدُ مَا تَعْبُدُونَ. وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ. وَلا أَنَا عَابِدٌ مَّا عَبَدتُّمْ. وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ. لَكُمْ دِينُكُمْ وَلِيَ دِينِ.

Sema: Enyi makafiri!. Siabudu mnachokiabudu.  Wala nyinyi. hamuabudu ninayemuabudu. Wala sitaabudu mnachoabudu. Wala nyinyi hamuabudu ninayemuabudu.  Nyinyi mna dini yenu, nami nina Dini yangu. 

Suratul Kaafiruun

 

Akitaka Mali Tutampa

Baada ya kushindwa na njia zote za kuizuia Dini hii mpya, na baada ya kuona idadi ya Waislamu ikizidi kuongezeka, hofu ikaanza kuingia ndani ya nyoyo za washirikina wa Makkah wakihofia wafuasi wa Muhammad wasije kuwa na nguvu za kuwashinda. Wakaamua kuitisha mkutano wa kutafuta ufumbuzi.

Abu Jahl aliyehudhuria mkutano huo alihutubia akasema:

"Enyi watu wa kabila la Quraysh, kama mnavyoona idadi ya wafuasi wa Muhammad inaongezeka kila siku, kwani kila siku watu wanaingia katika Dini ya Uislamu, na kama tutalinyamazia jambo hili, idadi ya wafuasi wake itaongezeka na idadi yetu itapungua, na dini yetu na dini ya baba zetu itapotea! Kwa hivyo twendeni tukamuue Muhammad tupate kujipumzisha na balaa lake na tupate kuiokoa miungu yetu kutokana na uovu wa Waislamu!"

Mmoja wao akasema: "Vipi tutaweza kumuua Muhammad wakati ami yake Abu Twaalib ndiye mlezi wake na mlinzi wake?"

 

Mwengine akasema: "Lakini Abu Twaalib hakuingia katika Dini ya Kiislamu, kwa hivyo bado yumo katika dini yetu, na bila shaka atapenda kuwalinda masanamu ambayo ni dini yake na dini ya baba na babu yake ‘Abdul-Mutwallib."

 

Wa tatu akasema: "Bora tumuendee ami yake Abu Twaalib tuzungumze naye juu ya jambo hili."

 

Ukatoka ujumbe wakubwa wa kabila la Quraysh kuelekea nyumbani kwa Abu Twaalib wakamuambia:

"Ewe Abu Twaalib, sisi hatukuja kwa ajili ya kukuembelea, bali kwa ajili ya mtoto wa ndugu yako Muhammad aliyetuletea Dini mpya inayokwenda kinyume na dini yetu na dini ya baba zetu. Na wengi kati ya watu wa kabila la Quraysh wamemfuata na kuingia katika Dini hiyo, na kwa ajili hiyo dini yetu imekuwa katika hatari ya kutoweka kwa kukosa wafuasi.

Ikiwa Muhammad anawaita watu katika Dini yake kwa ajili ya kutaka mali, basi sisi tutampa mali aitakayo. Na kama anataka ukubwa, basi tuko tayari kumfanya yeye awe kiongozi wetu. Kwa hivyo mwambie ewe Abu Twaalib asiendelee na amri yake hii, na umnasihi kwa sababu hana budi kusikiliza nasaha zako, kwani wewe ni ami yake, hatoweza kukataa kufuata amri yako."

 

Abu Twaalib akaingia katika mtihani mkubwa baina ya matakwa ya watu wa kabila lake la Quraysh na makatakwa ya mtoto wa ndugu yake; Muhammad!

Akaamua kumuita na kumuambia:

"Watu wa kabila la Quraysh wamekasirika sana juu ya amri yako hii, na wanakuambia kuwa watakupa mali kama unataka mali, na watakupa ukubwa kama unataka ukubwa, lakini wanakutaka uache kuwaita watu katika Dini yako hii mpya, na urudi kama ulivyokuwa hapo mwanzo. Na jua ewe Muhammad kuwa sisi hatuwezi kuwafanyia uadui Quraysh kwani wao kwanza ni watu wetu na kabila letu ni moja, kisha jambo la pili ni kuwa idadi yao ni kubwa kupita sisi  wanao uwezo na nguvu na mali kupita sisi, usinibebeshe mzigo nisiouweza."

 

Muhammad alisikiliza vizuri maneno ya ami yake Abu Twaalib ambaye hakuwa ameingia katika Dini ya Kiislamu, akaona uchungu mkubwa sana, akasema nafsini mwake: "Huyu kweli ni ami yangu aliyeusiwa juu yangu na babu yangu ‘Abdul-Mutwallib? Alitoa ahadi mbele ya ami yangu kuwa atanilinda kwa hali na mali na kwa kila anachomiliki."

Akaendelea kuisemesha nafsi yake: "Kipi kilichojiri leo? Anadhani ami yangu kuwa mimi ninataka manufaa yoyote ya kidunia ya pesa na ufalme? Hapana WaLlaahi!"

Kisha akamkabili ami yake na kumuambia:

"Ewe ami yangu! WaLlaahi lau kama wataliweka jua mkono wangu wa kulia na mwezi mkono wangu wa kushoto ili niiache Dini hii, basi sitoiacha mpaka Allaah Atakapoipa ushindi, au nife kwa ajili yake!"

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ’Aliyatamka maneno haya matukufu yaliyotoka moyoni mwake kwa nguvu zake zote na kwa hamasa kubwa, na ami yake alishtushwa na ujasiri ule, akatahayari kwa nini alitamka maneno yale ya kumkataza Muhammad asiwaite watu katika Dini yake. Moyo wake uliathirika sana, akawa anamuangalia mtoto wa ndugu yake kwa mapenzi na heshima kubwa, kisha akamuambia:

"Ewe mwana wa ndugu yangu! Waite watu katika Dini yako kama unavyopenda, na WaLlaahi sitokuacha peke yako mbele ya adui wako kamwe wakati bado niko hai."

 

Makubaliano Ya Bani Haashim Na Bani Muttwallib

Baada ya kuona hatari ya kushambuliwa na Quraysh ikiwakaribia, na baada ya majaribio mbali mbali yaliyofanywa kujaribu kumuua mtoto wa ami yake Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  Abu Twaalib aliamua kuwaita watu wa ukoo wake, ukoo wa Bani Haashim na Bani Muttwallib watoto wa Abdu Manaaf, Waislamu na wasiokuwa Waislamu na kuwajulisha juu ya hatari hiyo. Akawataka wakubaliane kumlinda kwa hali na mali na washirikiane katika kuzuia njama za Quraysh za kutaka kumuua, na wote kwa pamoja wakakubaliana kumlinda, wengine kwa sababu ya Uislamu wao na wengine juu ya kuwa bado ni washirikina lakini walikubali kwa sababu ya uhusiano wao wa ukoo, isipokuwa Abu Lahab aliyejitenga nao na kujiunga na Quraysh.

Ar-Rahiyqul Makhtuum 95-96

 

Kupigwa Pande

Anasema Al-Mubaarakpuri:

“Katika muda wa wiki nne mambo manne makuu yaliyokea kwa mfululizo, na mambo yote hayo hayakuwapendeza washirikina. Kusilimu kwa Hamzah na kusilimu kwa ‘Umar, kisha Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuyakataa maombi ya Quraysh, kisha makubaliano baina ya Bani Haashim na Bani Muttwallib ya kumlinda Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Washirikina walielewa kuwa baada ya makubaliano hayo damu nyingi itamwagika iwapo watajaribu kumuua.

 

Makubaliano Ya Dhulma Na Uadui

Maquraysh nao wakakutana mahali panapoitwa Khiyf ya Bani Kinaanah na kuandikiana mkataba dhidi ya watu wa ‘ailah ya Bani Haashim na Bani Muttwallib, na katika mkataba huo walikubaliana kuwa wasioane nao, wasikubaliane nao kwa lolote, wasikae nao, wasishirikiane nao, wasiingie majumbani mwao, wasiwasemeshe, wasiwauzie kitu wala wasinunue kutoka kwao, na wakakubaliana pia kutowaonea huruma mpaka wakubali kumkamata Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwakabidhi wao wapate kumuua. Baada ya kumaliza kuandika mkataba huo ndani ya sahifa, wakautundika ndani ya Al-Ka’abah.

 

Kutokana na mkataba huo, Waislamu wakiwa pamoja na watu wa ‘ailah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Waislamu na wasiokuwa Waislamu, wote walihamia katika bonde la Abu Twaalib, na hapo wakapigwa pande kwa muda wa miaka mitatu. Waligomewa kuuziwa kitu chochote, na inapokuja misafara kutoka nje walikuwa wanapotaka kununua chochote kutoka kwao, Quraysh walikuwa wakiongeza bei na kununua wao kwa bei ya juu zaidi ili Waislamu wasiipate.

 

Wakawa katika hali hiyo muda wa miaka mitatu ambayo ndani yake walipata tabu kubwa sana. Ulipita wakati Waislamu walikula majani ya miti na magamba yake kwa sababu ya kushindwa kupata chakula. Sauti za wanawake na watoto waliokuwa wakilia kwa njaa na kuugua kwa maumivu zilikuwa zikisikilizana. Hapana kilichoweza kuwafikia isipokuwa mara chache sana tena katika nyakati za usiku kwa njia za siri kupitia kwa Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyekuwa akiletewa bidhaa na mtoto wa ndugu yake aitwae Haakim bin Hizaam, au kwa njia ya Hishaam bin ‘Amru aliyekuwa akiwaplekea Bani Haashim chakula kwa kificho nyakati za usiku. Na walikuwa hawatoki kwenda kununua mahitajio yao isipokuwa katika miezi iliyoharamishwa (Ash huril hurum).

Ar-Rahiyqul Makhtuum – 97-98

 

Kuvunjika Kwa Mkataba

Katika mwaka wa kumi tokea Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kupewa utume, ndani ya mwezi wa Muharram na baada ya kupita miaka mitatu tokea walipohamia katika bonde la Abu Twaalib, mmoja katika watu wa kabila la Quraysh aitwae Hishaam bin ‘Amru bin Rabiy’ah alimwendea Mut’am bin ‘Uday na baadhi ya washirikina wa kabila la Quraysh na kuwaomba washirikiane naye katika kuufuta mkataba wenye kuwadhulumu ndugu na jamaa zao kwa kuwaweka na njaa muda wa miaka mitatu wakati wao wanakula na kushiba.

Wakati huo huo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwajulisha aliokuwa nao kuwa Allaah Amewatuma mchwa wakaila sahifa ile ya dhulma, na hawakubakisha katika maneno yaliyomo ndani ya sahifa ile isipokuwa jina la Allaah “Bismika Allaahumma”.  Abu Twaalib akawaendea Quraysh na kuwajulisha juu ya utabiri wa mtoto wa Ndugu yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya sahifa yao, na washirikiana wakiongozwa na Abu Jahl walipohakikisha juu ya ukweli wa utabiri ule baada ya kuiona sahifa yao imeliwa yote isipokuwa jina la Allaah, waliogopa wakakubali kuuvunja mkataba.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na aliokuwa nao wakatoka katika bonde na kuendelea na maisha yao kama kawaida.

 

Funzo

Bila shaka sababu kubwa zinazoleta ushindi ni imani na uongozi bora. Wafuasi wanapokuwa na imani iliyo thaabit, kisha wakawa na kiongozi mkweli, mwenye kuwatakia kheri na hana tamaa ya kidunia wala ya nafsi yake, wanakuwa tayari kupoteza mali zao na maisha yao kwa ajli ya kile walichokiamini kupitia kiongozi wao huyo.

Anasema Ibn Kathiyr: “Khubayb (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipokuwa akisulubiwa na makafiri aliulizwa: (Unaonaje Muhammad akawa mahali pako?) alijibu: (Hapana. Naapa kwa Allaah Mtukufu kuwa, sikubali hata kama atachomwa na mwiba ili mimi niokoke.)

 

Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) walielewa kuwa ikiwa wataregeza kamba na kusalimu amri mbele ya mateso ya adhabu na dhulma za makafiri wa Makkah, basi hawatoweza kuieneza Dini ya Allaah ulimwenguni na kuwatoa watu kutoka katika giza la kufru na kuwaingiza katika nuru ya Uislamu.

Anasema Swafiyur-Rahmaan Al-Mubaarakpuri:

“Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wakilijua vizuri jukumu lao kubwa juu ya wanaadamu, na kwamba haiwezekani kulikimbia wala kulikwepa. Walielewa kuwa matokeo ya kulikimbia jukumu lao na natija yake ni mbaya  sana na kubwa zaidi kuliko adhabu wanayoipata ya kuteswa na kuwekwa na njaa na kuadhibishwa na kudhulumiwa nk. Walielewa pia kuwa hasara watakayoipata wao na watakayoipata watu wote ulimwenguni ikiwa watalikimbia jukumu lao hilo, ni kubwa zaidi isiyostahamilika na isiyolingana na adhabu wanayopambana nayo.

Ar-Rahiyqul Makhtuum - 143

 

 

Kufariki Kwa Abu Twaalib Na Bi Khadiyjah

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliendelea kulingania, na watu wengi walimfuata, na ami yake Abu Twaalib alimsaidia sana kwa kumpa himaya na ulinzi aliokuwa akiuhitajia sana wakati ule, akaweza kuifanya kazi yake kwa usalama bila ya kushambuliwa wala kudhuriwa na Maquraysh waliokasirishwa sana na mafanikio yake makubwa.

Miezi sita baada ya kumalizika mgomo waliofanyiwa na Quraysh katika bonde la Abu Twaalib, ami yake alifariki dunia, na kifo chake kilikuwa katika mwezi wa Rajab mwaka wa kumi tokea kupewa utume, na inasemekana pia kuwa alifariki katika mwezi wa Ramadhaan, miezi mitatu kabla ya Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) naye pia kufariki dunia.

Ar-Rahiyqul Makhtuum - 103

 

Imepokelewa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia chumbani kwa ami yake Abu Twaalib wakati alipokuwa akikata roho, na wakati huo Abu Jahl alikuwa ubavuni mwake. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: “Ewe ami yangu; sema: ‘Laa ilaaha illa Llaah’, neno ambalo kwalo nitaweza kukutetea mbele ya Allaah.”

Abu Jahl na ‘Abdullaah bin Abi Umayah wakasema: “Ewe Abu Twaalib, unaiacha dini ya ‘Abdul-Mutwallib?” Wakaendelea kumsemesha mpaka mwisho akasema: “Nakufa katika dini ya ‘Abdul-Mutwallib.”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Nitakuombea maghfira ikiwa sitokatazwa.” Ndipo ilipoteremka kauli ya Allaah isemayo:

مَا كَانَ لِلنَّبِيِّ وَالَّذِينَ آمَنُواْ أَن يَسْتَغْفِرُواْ لِلْمُشْرِكِينَ وَلَوْ كَانُواْ أُوْلِي قُرْبَى

“Haimpasii Nabii na wale walio amini kuwatakia msamaha washirikina, ijapo kuwa ni jamaa zao.”

At-Tawbah – 113

 

Kisha ikateremka aya:

إِنَّكَ لا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ

“Kwa hakika wewe humwongoi umpendaye.”

Al-Qaswas – 56

 

 

Na Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) alifariki dunia miezi miwili au mitatu baada ya Abu Twaalib.

 

Bi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa akimsaidia sana Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa hali na mali na kwa kumpa nasaha na moyo kila anapopatwa na masaibu au mitihani.

Ami yake pia alikuwa akimpenda na kumhami kutokana na adui zake na akimlinda na kila aliyejaribu kumdhuru katika washirikina wa Makkah ambao wengi wao walitokana na kabila la Quraysh.

Kwa ajili hiyo vifo viwili hivi vilimhuzunisha sana Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyeona kuwa msaada wa hali na mali na kupewa moyo na nasaha alokuwa akivipata kutoka kwa mkewe, na himaya aliyokuwa akiipata kutoka kwa ami yake, vyote vimetoweka. Na mwaka huu uliitwa “Mwaka wa huzuni.”

 

Quraysh walifurahi sana kwa vifo vile na kwa msiba ule mkubwa uliompata Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), wakawa wanasema:

"Keshakufa Abu Twaalib mlinzi wa Muhammad, kwa hivyo sasa tunaweza kumuondoa kwa wepesi sana!"

 

 

Safari Ya Twaaif

Baada ya misiba miwili iliyofululiza, Quraysh walizidisha jeuri, wakawa wanamtukana Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumdhalilisha kila wanapomuona na wakati mwingine walikuwa wakimrushia michanga ya uso na juu ya kichwa chake kitukufu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Na wafuasi wake nao pia waliadhibiwa vikali sana na kuteswa hasa wale madhaifu na watumwa na wale wasiokuwa na makabila makubwa ya kuwakinga au kuwatetea.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaamua kwenda Twaaif, mji ulio mbali na Makkah kiasi cha maili sitini, akifuatana na Zayd bin Haarithah (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa mtumwa wake aliyemuacha huru.

Huko alijaribu kutafuta msaada na himaya kutoka kwa watu wa kabila la Thaqiyf na alijaribu kuwaita watu wa kabila hilo katika Dini aliyokuja nayo kutoka kwa Allaah.

 

Watu wa Twaaif wakiongozwa na wakuu wa makabila yao walikataa kumfuata, wakamuambia: “Kama Allaah amekutuma wewe basi bora tuichane nguo ya Al-Ka’abah.” Na wengine wakamuambia: “Hivyo Allaah hajapata wa kumtuma isipokuwa wewe?” Na wengine wakamuambia: “Ama miye sitokusemesha tena wewe.”

Yote hayo hayakumvunja moyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyebaki Twaaif muda wa siku kumi akiwaendea wakubwa wa makabila mbali mbali ya huko na kuwaita katika Dini ya Uislamu, lakini wakubwa hao walikataa kumfuata na badala yake waliwatuma watoto wadogo na wenda wazimu na watumwa wao wamfukuze. Wakawa wanamuandama huku wakimtukana na kumpiga mawe mpaka damu ikaanza kumtoka (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  na viatu vyake vikarowa damu, na wakati wote huo Zayd bin Haarithah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akijaribu kumkinga kwa mwili wake, lakini yeye pia alipigwa mawe ya kichwa mpaka kipaji chake kikachanika.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaondoka Twaaif huku akiandamwa kwa mawe na matusi, akakimbilia mahali penye shamba la ‘Utbah na Shaybah wana wa Abu Rabiy’ah liliopo kiasi cha umbali wa maili tatu kutoka Twaaif, na hapo ndipo walipoondoka na kumuacha.

 

Watoto wa Rabiy’ah walimuonea huruma walipomuona katika hali ile, wakamtuma mtumishi wao Udaas ampelekee tawi la zabibu. Udaas alikuwa akifuata dini ya Nasara (Ukristo), wakamwambia: “Chukua zabibu hizi nenda kampe mtu yule.” Alipomuwekea mbele yake, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaunyosha mkono kuzichukua huku akisema: “BismiLlaah”, kisha akala.

Udaas akashangazwa na kitendo kile, akamuuliza: “Maneno haya hayasemwi na watu wa mji huu.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: “Kwani wewe unatokea mji upi? Na dini yako ni ipi” Udaas akasema: “Mimi natoka mji wa Naynawa.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Unatoka mji wa Mtume mwema Yuunus bin Matta?” Akamuuliza: “Unamjuaje Yuunus bin Matta?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: “Yule ni ndugu yangu. Alikuwa Nabii na mimi ni Nabii.” Udaas akaanza kukibusu kichwa cha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na mikono yake, na watoto wa Rabiy’ah walipomuona mtumishi wao akifanya vile wakasemezana: “Keshamharibu kijana wako.” Na aliporudi wakamwambia: “Ole wako! Nini kile ulichokuwa ukifanya?” Akasema: “Ewe bwana wangu, hapana juu ya ardhi hii aliye bora kuliko mtu yule. Ameniambia neno asiloweza kulijua mwengine isipokuwa Nabii.” Wakamwambia: “Ole wako ewe Udaas, asije akakutoa katika dini yako, kwani dini yako ni bora kuliko yake.”

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliondoka Twaaif na kurudi Makkah akiwa mwenye huzuni kubwa sana, na alipowasili mji wa Qarnul Manaazil akajiwa na Jibriyl akiwa pamoja na Malaika wa Majabali, wakamuuliza iwapo anataka yaangushwe majabali mawili na kuwaangamiza watu wa Makkah.

 

Anasema Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha): “Nilimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) iwapo aliwahi kupata tabu kama ile aliyoipata siku ya vita vya Uhud? Akanijibu: ((Nilipata tabu sana kwa watu wako kiasi nilichopata, na katika tabu kubwa niliyoipata ilikuwa siku ya ‘Aqabah (Twaaif) nilipojijulisha kwa mwana wa Abdu Aliyl (mkubwa wa makabila ya Twaaif), na hakunikubalia kwa yale niliyotaka. Nikaondoka huku nikiona dhiki mpaka nilipowasili mahali panapoitwa Qarnu Thaalib niliponyanyua kichwa changu kutazama juu nikaona kiwingu kikinikinga kutokana na jua, nikaangalia nikamuona Jibriyl, akaniita akaniambia: ‘Allaah Ameyasikia maneno ya watu wako dhidi yako na waliyokutendea, na Allaah Amemtuma kwako Malaika wa jabali anayesubiri umpe amri awafanye unavyotaka.’ Akaniita Malaika wa jabali akanisalimia kisha akaniambia: ‘Ewe Muhammad, unataka niwaangushie majabali mawili juu yao?’ Nikasema: ((Bali nataraji Allaah atowe katika migongo yao mwenye kumuabudu Allaah peke Yake bila ya kumshirikisha na chochote.))

Al-Bukhaariy na Muslim

 

Funzo

Hapa ndipo anapojulikana kiongozi mwema mwenye busara. Kiongozi mwenye hekima, mpole, mwenye tabia njema asiyependa kulipa kisasi kwa ajili ya nafsi yake. Kiongozi wa kweli hawi na kinyongo juu ya wafuasi wake. Haipendi nafsi yake kuliko anavyowapendelea watu wake.

Na kwa nini asiwe hivyo wakati huyu ndiye Muhammad Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Amesema juu yake:

وَإِنَّكَ لَعَلى خُلُقٍ عَظِيمٍ

Na bila shaka una tabia njema kabisa

Al-Qalam – 4

 

Nafsi yake iliridhika na Malaika waliomjia, na furaha kubwa iliingia moyoni mwake na kuiondoa ile huzuni iliyojengeka baada ya kuteswa na watu wake, kisha akafukuzwa na kupigwa mawe na watu wa Twaaif.

Huku akiwa na matumaini makubwa, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaianza safari ya kurudi Makkah, na alipoulizwa na Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhu): “Kwa nini unarudi Makkah baada ya kufukuzwa?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: “Ewe Zayd, Allaah Ataleta faraja Yake na kututoa katika masaibu haya, na Allaah Atainusuru Dini Yake na kumpa ushindi Mtume Wake.”

 

Alipowasili Makkah, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa himaya na Al-Mut’im bin Uday, akaenda moja kwa moja mpaka Msikitini, akaswali rakaa mbili, kisha akaelekea nyumbani kwake.

 

Israa Na Mi’iraaj

Baada ya misiba miwili mikubwa ya kufiwa na mkewe na kufiwa na ami yake, na baada ya kupata mateso ya watu wa Makkah na ya watu wa Twaaif, Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Alitaka kumliwaza na kumfariji Mtume wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kumpa zawadi adhimu ya kumpandisha juu ya mbingu saba katika safari ya Israa na Mi’iraaj.

 

Israa ni safari aliyopelekwa katika usiku mmoja kutoka Makkah hadi Baytul Maqdis (Jerusalem), alipowaswalisha Mitume yote yeye akiwa Imaam wao. Na kutoka hapo ndipo alipopandishwa mbinguni.

Kupelekwa kwake kutoka Makkah hadi Baytul Maqdis katika usiku mmoja kulikuwa ni dalili kwa makafiri ikiwathibitishia ukweli wake.

Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Alimpandisha kwa ajili ya kumtayarisha na jukumu kubwa la kuitangaza Dini Yake na kuieneza Ulimwenguni kote.

Maulamaa wamekhitilafiana juu ya lini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda safari hii ya Israa na Mi’iraaj lakini uhakika ni kuwa ilikuwa baada ya vifo vya Abu Twaalib na Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha).

 

Ndani ya usiku mmoja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisafiri kutoka Msikiti wa Makkah hadi Msikiti wa Baytul Maqdis kisha akapandishwa hadi Sidratul Muntaha kwa roho na mwili akifuatana na Jibriyl (‘Alayhis Salaam) akiwa amepanda mnyama aitwae Buraaq.

 

Alipowasili Baytul Maqdis aliwaswalisha Mitume yote (‘alayhimus Salaam) kisha katika usiku huo huyo akapandishwa mbinguni, na alipowasili mbingu ya mwanzo Jibriyl aliomba afunguliwe mlango, ukafunguliwa na hapo alimuona Aadam (‘Alayhis Salaam) akamsalimia, na Aadam (‘Alayhis Salaam) akaitikia salam yake, kisha akamkaribisha, kisha akapandishwa mbingu ya pili akafunguliwa mlango, na hapo aliwaona Yahya mwana wa Zakariya na ‘Iysa mwana wa Maryam (‘alayhimus Salaam), akawasalimia, nao wakaitikia salaam yake, wakamkaribisha, kisha akapandishwa mbingu ya tatu, na huko pia alifunguliwa mlango, akamuona Yuusuf (‘Alayhis Salaam), akamsalimia naye akaitikia salaam yake, akamkaribisha, kisha akapandishwa mbingu ya nne, na huko akamuona Idriys (‘Alayhis Salaam), akamsalimia, naye akaitikia salaam yake, kisha akapandishwa mbingu ya tano, na hapo akamuona Haaruun (‘Alayhis Salaam), akamsalimia, naye akaitikia salaam yake na kumkaribisha, kisha akapandishwa mbingu ya sita, na hapo alimuona Muusa mwana wa ‘Imraan (‘Alayhis Salaam), akamsalimia, naye akaitikia salaam yake, akamkaribisha, kisha akapandishwa mbingu ya saba, na huko alimuona Ibraahiym (‘Alayhis Salaam), akamsalimia, naye akaitikia salaam yake kisha akamkaribisha, kisha akapandishwa mpaka Sidratul Muntaha, kisha akapandishwa Baytul Ma’amuur, kisha akapandishwa kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa), akamkaribia, akawa kama baina ya mipinde miwili, au karibu zaidi, (Allaah) Akamfunulia mja Wake Alichomfunulia, akafaridhishiwa Swalah tano.

Anasema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Kisha Akanifunulia (Wahyi) Allaah kile Alichonifunulia akanifaridhishia Swalah khamsini kila siku mchana na usiku. Nikashuka mpaka kwa Muusa (‘Alayhis Salaam) akaniuliza: “Amekufaridhishia nini Mola wako?” Nikamuambia: “Swalah khamsini.” Akasema: “Rudi kwa Mola wako muombe akupunguzie, kwa sababu umati wako hawatoziweza kwani mimi niliwajaribu Wana wa Israili na nimewajua vizuri.” Akasema: “Nikarudi kwa Mola wangu nikamuambia: “Ee Mola wangu wapunguzie umati wangu.” Akanipunguzia tano. Nikarudi kwa Musa nikamuambia: “Amenipunguzia tano.” Akasema: “Hakika umati wako hawatoziweza hizo. Rudi kwa Mola wako umuombe akupunguzie.” Akasema: “Nikawa nakwenda nikirudi baina ya Mola wangu aliyetukuka na Muusa (‘Alayhis Salaam) mpaka Aliposema: “Ewe Muhammad! Hizi ni Swalah tano kila usiku na mchana, na kila Swala moja kwa kumi, kwa hivyo ni sawa na khamsini. Na anayekusudia kutenda dhambi kisha asiitende, hatoandikiwa kitu. Na akiifanya ataandikiwa dhambi moja.

Akasema: “Kisha nikashuka mpaka kwa Musa (‘Alayhis Salaam) nikamhadithia, akasema: “Rudi kwa Mola wako umuombe akupunguzie.” Akasema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Nikamuambia: ‘Nisharudi sana kwa Mola wangu mpaka nikamuonea hayaa.”[48]

 

Anasema Ibnul Qayyim: Maswahaba wamekhitalifiana iwapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amemuona Mola wake usiku ule au hakumuona. Na imesihi kutoka kwa Ibn ‘Abbaas kuwa kuwa ‘Alimuona Mola wake.’ Na imesihi pia kutoka kwa Ibn ‘Abbaas kuwa alisema: ‘Alimuona kwa moyo wake.”[49]

Na imepokelewa kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) na Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa wamekanusha hayo wakasema kuwa aliyekusudiwa ni Jibriyl (‘Alayhis Salaam) katika ile kauli ya Allaah Aliposema:

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَى. عِندَ سِدْرَةِ الْمُنْتَهَى

“Na akamuona mara nyingine (kwa sura ile yake ya katika usiku wa Mi’iraaj). Penye Mkunazi wa kumalizikia (mambo yote).”

An-Najm 13-14

 

Na imepokelewa katika hadithi sahihi kutoka kwa Abi Dhar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa alimuuliza: “Ulimuona Mola wako.?” Akasema: “Nuru vipi nitaweza kuiona.” Na maana yake ni kuwa baina yake na baina ya Mola wake ilikuwepo Nuru iliyomzuia kuweza kumuona. Na katika riwaya nyingine imepokelewa kuwa alisema: “Niliona Nuru.”[50]

 

Kupelekwa kwake kutoka Makkah hadi Baytul Maqdis katika usiku mmoja kulikuwa ni dalili kwa makafiri ikiwathibitishia ukweli wake, kwa sababu makafiri walimkadhibisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kisha wakamuuliza maswali kwa ajili ya kuhakikisha ukweli wake.

Walimtaka awaelezee wasfu wa Baytul Maqdis, wakiwa wanaelewa kuwa yeye hajapata kuuona Msikiti huo. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaelezea Msikiti ulivyo, na akawaelezea juu ya kila pembe yake.

Kisha wakamuuliza juu ya msafara wa jamaa zao waliokuwa wakiusubiri (ukitokea huko Quds), na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaeleza mahali msafara huo ulipo kwa wakati huo, idadi ya watu waliokuwemo ndani yake msafara huo, kabila zao, aina ya ngamia waliokuwa nao, na akawaelezea hata wasfu wa ngamia anayeutangulia msafara huo na nini amebeba ngamia huyo, na akawaelezea wakati gani utawasili msafara huo, na ukawasili wakati ule ule alowatajia.

Haya yote yakawa ni ushahidi wa kupelekwa kwake Baytul Maqdis (Israa), na kwa ajili hiyo unakuwa pia ni ushahidi wa kupandishwa kwake mbinguni (Mi’iraaj).

Allaah Anasema:

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَى بِعَبْدِهِ لَيْلاً مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ

"Utukufu ni wake Yeye ambaye aliyempeleka mja Wake usiku mmoja tu kutoka Msikiti mtukufu wa (Makkah) mpaka Msikiti wa mbali wa (Baytul Maqdis-Palastina) ambao Tumeubariki na (tumevibariki) vilivyoko pembezoni mwake."

Suratul Israa (Bani Israaiyl ) -1

 

Tunamuomba Allaah Autwaharishe Msikiti huo kwa kuwaondoa Mayahudi wanaochafua Msikiti huo, na tunamuomba Aijaalie bendera ya Uislamu ipepee tena juu ya ardhi yake, na Atustareheshe kwa kuufikia Msikiti huo na kuswali ndani yake baada ya kutwaharishwa kutokana na Mayahudi waovu kama alivyoutwaharisha Swalaahud-Diyn Al-Ayyuubiy (Allaah Amrehemu). Na katika khutbah ya Ijumaa ya mwanzo baada ya kukombolewa Baytul Maqdis Imaam wa Msikiti alianza khutbah yake kwa kusema:

فَقُطِعَ دَابِرُ الْقَوْمِ الَّذِينَ ظَلَمُواْ وَالْحَمْدُ لِلّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Ikakatwa mizizi ya watu waliodhulumu Na sifa zote njema ni za Allaah Muumba wa walimwengu (wote).”

Al-An’aam – 45

 

Kwa hivyo tunamuomba Allaah kama Alivyoikata mizizi ya madhalimu wale, aikate pia mizizi ya madhwaalim hawa – Aamiyn.[51]

 

Kuhusu dalili ya Mi’iraaj (kupandishwa mbinguni), Allaah Anasema:

أَفَتُمَارُونَهُ عَلَى مَا يَرَى. وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَى. عِندَ سِدْرَةِ الْمُنْتَهَى. عِندَهَا جَنَّةُ الْمَأْوَى. إِذْ يَغْشَى السِّدْرَةَ مَا يَغْشَى. مَا زَاغَ الْبَصَرُ وَمَا طَغَى. لَقَدْ رَأَى مِنْ آيَاتِ رَبِّهِ الْكُبْرَى

"Jee! Mnabishana naye juu ya yale anayoyaona (daima)?

Na Mtume akamuona (Jibriyl) mara nyengine (kwa sura ile ile ya Kimalaika katika usiku wa Mi’iraaj). Penye mkunazi wa kumalizikia (mambo yote). Karibu yake kuna hiyo Bustani, (Pepo) itakayokaliwa maisha (na hao watu wema). Kilipowafunika mkunazi huo Kilichowafunika (katika mambo ya kiajabu ya kimbinguni). Jicho halikuhangaika wala halikuruka mpaka huo (uliowekwa). Kwa yakini aliona (Nabii Muhammad) Mambo makubwa kabisa katika alama, (Qudra) za Mola wake".

An-Najm 12-18.

 

Pepo na Moto ni katika miujiza ya Allaah Aliyoiona.

Hakika Israa na Mi’iraaj ni miongoni wa ubadilishaji wa nidhamu Alizoziumba Allaah na Akazijaalia kuwa ni ushahidi wa kuthibitisha ukweli wa Mtume wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Anasema Shaykh Ahmad Fariyd katika kitabu chake ‘Waqafaat Tarbawiyah’:

“Amesema Al-Qaadhi ‘Iyaadh na wengi sana katika Maulamaa wetu, kuwa safari ya Mi’iraaj ilikuwa kimwili na kiroho. Al-Qaadhi ‘Iyaadh ameendelea kusema: “Na iliyo sahihi Insha Allaah, ni kuwa amepelekwa safari yote hiyo kwa roho na mwili akiwa yupo macho kama zinavyotujulisha aya na hadithi sahihi, na hakiwezi kutuondoa ndani ya uhakika huo isipokuwa kama jambo hilo haliwezekani.

Angelipelekwa akiwa amelala, basi Allaah Angelisema: “"Utukufu ni wake Yeye aliyeipeleka (roho ya mja Wake).” Na Asingesema: "Aliyempeleka mja Wake.”

 

Fungamano La Mwanzo La ‘Aqabah

Hijra ilitanguliwa na matukio mawili muhimu na maarufu sana nayo ni:

'Bay-atul ‘Aqabatul Uwlaa' - (Fungamano la ‘Aqabah la mwanzo), - na 'Bay-atul ‘Aqabatu Thaaniyah' - (Fungamano la ‘Aqabah la pili).

‘Aqabah ni lile Jamaraat iliyopo Minaa, linalojulikana kama ni 'Shaytwaan mkubwa' linalopigwa mawe pekee siku ya Hijjah, siku ya Sikukuu mosi.

Katika mwaka wa kumi na mbili baada ya kupewa Utume, watu kumi na mbili walikuja Makkah kwa siri kutoka Madiynah kwa ajili ya kufungamana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alahyi wa sallam).

Watu hao waliokutana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alahyi wa sallam) katika msimu wa Hijjah hapo Minaa penye Jamaraat kubwa, ni matunda ya kusilimu kabla yao kwa watu sita waliokuja kutoka huko Madiynah katika msimu wa kabla yake na kumuahidi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alahyi wa sallam) kuufikisha ujumbe wake kwa watu wao.

Msimu wa Hijjah uliofuata, waliwasili kutoka Madiynah watu kumi na mbili wakiwemo watano katika wale watu sita wa mwanzo, na mmoja wao hakuweza kuhudhuria. Kumi kati yao walikuwa watu wa kabila la Khazraj na wawili wa kabila la ‘Aws.

Imesimuliwa na Al-Bukhaariy kuwa, imepokelewa kutoka kwa ‘Ubaadah bin Swaamit (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa; katika fungamano hilo la mwanzo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alahyi wa sallam) alipokutana na watu hao aliwaambia:

"Fungamaneni nami kuwa hamtomshirikisha Allaah na chochote, wala hamutoiba, wala hamutozini, wala hamutouwa watoto wenu, wala hamutosema uwongo kwa midomo yenu wala nyoyoni mwenu na wala hamtoniasi katika wema. Atakayetimiza (ahadi hii) kati yenu, basi ujira wake upo kwa Allaah, lakini atakayetenda chochote katika hayo kisha akalipwa na Mola wake hapa hapa duniani, basi atakuwa keshalipwa badala ya kosa lake, na atakayetenda lolote katika hayo kisha Allaah Akamsitiri, basi hukumu yake iko kwa Allaah, Akitaka AtaMu’aadhibu na Akitaka Atamsamehe."

Wote waliohudhuria wakafungamana naye kwa ahadi hiyo.”[52]

 

Baada ya fungamano hilo na msimu wa Hijjah kumalizika, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alahyi wa sallam) alimchagua kijana mmoja katika Maswahaba wake waliotangulia kusilimu aitwae Musw’ab bin ‘Umayr  (Radhiya Allaahu ‘anhu), aende nao Madiynah kuwafundisha Qur-aan pamoja na mafundisho mengine ya Dini na asaidie katika kuieneza Dini ya Kiislamu.

 

Mafanikio ya Musw’ab

Alipokuwa Madiynah, Musw’ab bin ‘Umayr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alifikia katika nyumba ya As’ad bin Ziraarah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye ni miongoni mwa watu wa mwanzo wa Madiynah kusilimu, na watu wawili hao wakawa wanawalingania watu katika Dini hii mpya.

Katika mojawapo ya mafanikio yake Musw’ab ni yale yaliyoelezwa na Ibn Hishaam (Mwandishi maarufu wa Siyrah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alahyi wa sallam), katika kitabu chake kiitwacho Siyrah ya Ibn Hishaam.

Anasema Ibn Hishaam:

"Siku moja walitoka watu wawili hao 'Musw’ab na As’ad (Radhiya Allaahu ‘anhum), na kuuendea mji unaokaliwa na watu wa kabila la Bani Dhafar, ambao kiongozi wao alikuwa ni Sa’ad bin Mu’aadh. Walipowasili walikaa juu ya kisima kiitwacho Bi-ir Muriyq wakiwa wamezungukwa na baadhi ya wenzao waliokwishatangulia kusilimu katika watu wa Madiynah. Wakati huo Sa’ad bin Mu’aadh na Usayd bin Hadhiyr waliokuwa viongozi wa kabila lao walikuwa bado hawakusilimu, na walikuwa wamekaa mahala wanapokutana siku zote kwa ajili ya mazungumzo.

Sa’ad alipowaona Waislamu hao katika hali ile, akamwambia Usayd:

"Nenda ukawatetemeshe hawa waliokuja kuwapoteza watu wetu na uwakataze, waambie wasizisogelee nyumba zetu, kwani angelikuwa As’ad bin Ziraarah si mtoto wa Khali yangu, basi mimi mwenyewe ningeliwaendea."

Usayd akachukua mkuki wake na kuwaendea.

As’ad (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipomuona akija, akamwambia Musw’ab (Radhiya Allaahu ‘anhu):

"Huyu anayekuja ni mkubwa wa kabila lake, mjulishe juu ya ukweli uliotoka kwa Allaah."

Musw’ab (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:

"Akikubali kukaa nitamsemesha."

Usayd akaja na kusimama mbele yao huku akiwashutumu kwa kuwaambia:

"Kitu gani kilichokuleteni hapa, mnataka kuwapotosha watu wetu? Ondokeni ikiwa bado mnazihitajiya nafsi zenu".

Musw’ab (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:

"Kwa nini hukai na kutusikiliza. Ukiridhika utafuata, usiporidhika tutayaacha usiyopendezewa nayo."

Akasema:

"Sawa ulivyosema."

Akauchomeka mkuki wake ardhini na kukaa. Musw’ab (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamsemesha juu ya Uislamu na kumsomea aya za Qur-aan mpaka uso wake ukaanza kubadilika.

Wakasema:

"WaLlaahi tukauona Uislamu usoni pake kabla hata hajautamka."

Kisha Usayd akasema:

"Mtu akitaka kuingia katika Dini hii afanye nini?"

Wakamwambia:

"Ukoge, utwaharishe nguo zako kisha utamke shahada ya haki, kisha uswali rakaa mbili."

Akainuka, akaoga na kuzitwaharisha nguo zake kisha akaswali rakaa mbili, kisha akasema:

"Kuna mtu mmoja nyuma yangu, ikiwa atakufuateni mtu huyu, basi hakuna hata mmoja katika watu wake atakayebaki nyuma (wote nao watakufuateni) nitamwongoza aje kwenu sasa hivi, mtu wenyewe ni Sa’ad bin Mu’aadh".

Akauchomoa mkuki wake, akauchukua na kuondoka akielekea kwa Sa’ad bin Mu’aadh aliyekuwa pamoja na watu wa kabila lake waliokaa mahali pao pa siku zote wanapokutana kwa ajili ya mazungumzo.

Sa’ad alipomuona Usayd akielekea kwake, akasema:

"WaLlaahi uso wake umebadilika, sivyo hivi alivyokuwa pale mwanzo pamoja nasi."

Aliposimama mbele yao, Sa’ad akamuuliza:

"Umefanya nini?"

Akamjibu:

"Nimewasemesha watu wale wawili, lakini sikuona kama wana ubaya wowote ule na nilipowakataza hawakubisha, wakasema:

"Sawa, tutafanya kama utakavyo."

Sa’ad akauchukua mkuki wake na kuwaendea watu wawili hao. Alipowafikia na kusimama mbele yao, akamwambia As’ad bin Ziraarah (Radhiya Allaahu ‘anhu):

"WaLlaahi ingelikuwa hatuhusiana mimi na wewe, basi ningekupiga nao huu. Mnakuja katika nyumba zetu na kutuenezea yale yanayotuchukiza?"

Kabla ya hapo, pale alipokuwa Sa’ad bin Mu’aadh akija, As’ad (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimnong'oneza Musw’ab (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kumwambia:

"Huyu ndiye bwana wa kabila lake, WaLlaahi akikufuata huyu, basi hakuna hata mmoja katika qawm yake atakayethubutu kwenda kinyume naye."

Musw’ab (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema kumwambia Sa’ad bin Mu’aadh:

"Kwa nini hukai ukatusikiliza? Ukiridhika utafuata, usiporidhika tutaacha usiyopendezewa nayo."

Sa’ad akasema:

"Sawa ulivyosema."

Akuchomeka mkuki wake ardhini na kukaa kitako. Musw’ab (Radhiya Allaahu ‘anhu) akaanza kumsemesha juu ya Uislamu na kumsomea aya za Qur-aan, wakasema:

"WaLlaahi tukauona Uislamu usoni pake kabla hata hajautamka."

Kisha Sa’ad akasema:

"Mtu akitaka kuingia katika Dini hii afanye nini?"

Wakamwambia:

"Ukoge, utahirishe nguo zako kisha utamke shahada ya haki, kisha uswali raka-a mbili."

Akafanya kama alivyoambiwa, kisha akauchukua mkuki wake na kuwaendea watu wa kabila lake na kuwaita. Walipomuona tu, wakasema:

"WaLlaahi tunaapa kuwa uso wake si kama pale alipoondoka, amebadilika kabisa."

Walipokusanyika mbele yake akawaambia:

"Enyi watu wa Bani Ash’hal, mnanijua vipi mimi?"

Wakasema:

"Bwana wetu, mwenye rai bora kupita sote, na kiongozi wetu."

Akasema:

"Kwa hivyo kuanzia leo haramu juu yangu mimi kumsemesha yeyote kati yenu, mwanamume au mwanamke mpaka kwanza mumuamini Allaah kuwa ni Mola wenu na Muhammad kuwa ni Mtume wenu."

Haukuingia usiku wa siku hiyo isipokuwa watu wote wa kabila lake wanaume kwa wanawake waliingia katika Uislamu isipokuwa mtu mmoja aitwae Asiyram aliyechelewa kuingia katika Uislamu mpaka siku ya vita vya Uhud. Alisilimu siku hiyo akapigana vita na akauliwa na wala hakuwahi kumsujudia Allaah hata siku moja.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alahyi wa sallam) akasema juu yake:

"Matendo aliyofanya ni kidogo, lakini ujira alioupata ni mkubwa,"

 

Balozi Wa Uislamu Madiynah

Musw’ab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alibaki Madiynah akiwa kama balozi wa Uislamu hapo, akiwalingania watu katika Dini ya Allaah na kwa jitihada yake alifanikiwa kuiingiza Dini hii katika kila nyumba ya mji huo.

Kabla ya kuingia msimu wa Hijjah wa Mwaka uliofuata (mwaka wa kumi na tatu) Musw’ab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alirudi Makkah akiwa na habari njema kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya ushindi wake huo, na juu ya makabila ya mji wa Madiynah, nguvu zao, Imani yao na azma yao.

 

Funzo

Katika mlango huu tumejifunza juu ya fadhila za Musw’ab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipokuwa Madiynah, na mafanikio yake katika kuzifungua nyoyo za watu na nyumba zao, akaweza kuwaingiza watu wa nyumba zile katika Dini ya Uislamu baada ya kuteuliwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuifanya kazi hiyo, na athari ya mafaniko yake yalionekana katika muda wa mwaka mmoja tu, akaweza kuwaingiza karibu watu wote wa Madiynah katika Dini ya Uislamu.

Na hii ni dalili ya fadhila za Maswahaba kwa ujumla na fadhila za Musw’ab namna alivyoweza kuitambua njia ya kuyaingiza mapenzi ya Uislamu ndani ya nyoyo za watu wale, na pia fadhila za As’ad bin Ziraarah namna alivyokuwa akimnasihi Musw’ab alipomuambia: "Huyu ndiye bwana wa kabila lake, WaLlaahi akikufuata huyu, basi hapana hata mmoja katika qawm yake atakayethubutu kwenda kinyume naye."

Kutokana na nasaha za As’ad na hekima ya Musw’ab (Radhiya Allaahu ‘anhum) wakasilimu Sa’ad pamoja na qawm yake (Radhiya Allaahu ‘anhum).

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atakayelingania katika uongofu atapata ujira wa kila atakayemfuata bila kupungua katika ujira wa aliyefuata hata chembe.”[53]

 

Katika mlango huu tunapata pia fadhila za watu wa Madiynah, uhodari na ushujaa wao kwa kuukubali ukweli mara wanapouona, na kuwa kwao tayari kuitetea haki kwa hali na mali zao, na namna walivyokuwa  tayari kuitetea Dini hii na kumlinda na kumsaidia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Fungamano La ‘Aqabah La Pili

Pamoja na watu wengi waliokuwa bado wamo katika ushirikina waliowasili Makkah kutoka Madiynah katika msimu wa Hijjah ya mwaka wa kumi na tatu tokea kupewa utume Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  walikuwemo pia watu wapatao sabini na tano waliokwishasilimu waliokuja kukutana na kufungamana kwa siri na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Walipofika Makkah watu sabini na tano hao, walifanya mawasiliano ya siri baina yao na baina ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wakakubaliana wakutane hapo Minaa kwenye kijiji karibu na Jamaraat la mwanzo, na kwamba mkutano huo uwe wa siri ya hali ya juu kabisa na ufanyike usiku wa manane.

Hebu tumsilikilize Ka’ab bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) akituhadithia juu ya mkutano huo wa kihistoria uliofanyika katika siku za mapambano ya kimya baina ya Uislamu na Ushirikina.

Anasema Kaab (Radhiya Allaahu ‘anhu):

"Tulitoka kwa ajili ya Hijjah na tukaahidiana na Mtume wa Allaah kukutana ‘Aqabah katika siku za Hijjah, na tulikuwa na ‘Abdullaah bin ‘Amru bin Hiraam, mkubwa wa kabila letu na mwema katika wema wetu aliyekuwa bado yumo katika ushirikina. Tulimchukua juu ya kuwa hatukuwaambia washirikina wengine waliokuwa pamoja nasi, lakini yeye tulimsemesha na kumwambia:

"Ewe Aba Jaabir, wewe ni bwana katika mabwana wa kabila letu, na mwema miongoni mwetu, na sisi kwa heshima hii uliyonayo hatupendi uwe kuni katika kuni za Motoni kesho."

Kisha tukamtaka aingie katika Dini ya Uislamu, na tukamjulisha juu ya miadi tuliyonayo ya kukutana na Mtume wa Allaah katika ‘Aqabah. Akasilimu na akaja pamoja nasi penye ‘Aqabah, akachaguliwa kuwa miongoni mwa viongozi wetu".

Anaendelea kusema Ka’ab (Radhiya Allaahu ‘anhu):

"Tulilala siku hiyo sisi na wenzetu juu ya migongo ya wanyama wetu, mpaka ilipoingia thuluthi ya usiku, tukatoka na kwenda pale tulipoagana kukutana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huku tukinyemelea na kujificha mpaka tukawasili penye ‘Aqabah. Na tulikuwa idadi yetu siku hiyo wanaume sabini na tatu na wanawake wawili na majina yao ni; Nusaybah bint Ka’ab kutoka katika kabila la Bani Najjaar na Asmaa binti ‘Amru kutoka katika kabila la Bani Salamah. Wote tulikutana mahali hapo tukawa tunamsubiri Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka alipowasili akiwa na ami yake Al-’Abbaas bin ‘Abdil-Muttwallib ambaye wakati huo alikuwa bado yupo katika dini ya qawm yake (ya ushirikina), isipokuwa alipenda naye awepo ili awe na uhakika juu ya usalama wa mtoto wa ndugu yake na yeye ndiye aliyekuwa wa mwanzo kuzungumza."

Al-’Abbaas alianza kwa kuwakumbusha watu wa Madiynah juu ya hatari itakayowakabili iwapo watataka kumnusuru Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kwamba wao ami zake hawakushindwa kumhami mtoto wa ndugu yao, isipokuwa Mtume mwenyewe (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye aliyeshikilia kutaka kuhamia Madiynah. Kwa hivyo iwapo wanaweza kulichukua jukumu hilo basi na waendelee, ama iwapo hawawezi basi na waseme kutoka sasa kwani Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hana matatizo yoyote na yupo baina ya qawm yake na watu wake.

 

Watu wa Madiynah walimtaka Mtume mwenyewe (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) azungumze, na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaanza kwa kusoma aya za Qur-aan na kumuomba Allaah, kisha akawapendezesha juu ya Uislamu, kisha akasema:

"Nafungamana nanyi kwa masharti yafuatayo; Munipe himaya kama mnayowapa watu wenu, na mufuate amri na kutii na kutoa katika dhiki na faraja, na katika kuamrisha mema na kukataza mabaya na muisimamie kazi ya Allaah bila ya kuogopa lawama za watakaolaumu."

Kisha mtu mmoja aitwae Al-Bara-a bin Maaraf akauchukua mkono wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kusema:

"Ndiyo. Naapa kwa yule aliyekuleta kwa haki uwe Mtume, kuwa tutakulinda kama tunavyowalinda watu wetu."

Anasema Ka’ab bin Maalik:

"Tukafungamana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kwani WaLlaahi sisi ni watu wa vita. Tumeurithi ushujaa kutoka kwa mababu na mababu."

Abul Haytham akasema:

"Ewe Mtume wa Allaah, uhusiano wetu na hawa jamaa tutauvunja (Mayahudi wa Madiynah), tusije tukafanya hivyo kisha wewe ukabadilisha niyah yako na kurudi kwa watu wako na kutuacha".

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akatabasamu na kusema:

"Bali damu kwa damu, mauti kwa mauti, mimi ni wenu na nyinyi ni wangu, tutampiga vita anayekupigeni vita na tutampa amani anayekupeni amani."

 

Mmoja kati ya wale waliosilimu msimu uliotangulia aliwajulisha na kuwatahadharisha wenzake kuwa kabla ya kufungamana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) lazima waielewe vizuri hatari itakayowakabili na kuwajulisha athari ya fungamano hilo, ili wasije baadaye watakapoona watu wao wanauliwa na mali zao zinapotea wakageuka na kumwendea kinyume Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Watu wa Madiynah wakasema:

"Ikiwa sisi tutakuwa nawe pale tunapopata masaibu katika mali zetu na pale watakapouliwa wakubwa wetu, tutalipwa nini ewe Mtume wa Allaah?"

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Pepo".

Wakasema:

"Unyoshe mkono wako."

Akaunyosha mkono wake na wote wakafungamana naye.

Watu wote walifungamana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kumpa mkono isipokuwa wale wanawake wawili walifungamana naye kwa kauli tu, kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hajawahi hata siku moja kupeana mkono na mwanamke anayeweza kumuoa.[54]

 

Viongozi Kumi Na Mbili

Baada ya kufungamana nao, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwataka wachague viongozi kumi na mbili watakaochukua jukumu la kufuatilia kutimizwa masharti ya Fungamano hilo. Wakachaguliwa watu tisa kutoka katika kabila la Khazraj na watatu kutoka ‘Aws.

Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akachukua kutoka kwa viongozi hao ahadi nyingine wakiwa wao kama ni viongozi wa qawm yao kuwataka wawe mfano mwema na walezi wema kwa watu wao.

Watu wa Madiynah walimwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

"Tunaapa kwa yule aliyekuleta kwa haki, ukitaka (hata) kesho tutawashambulia washirikina waliopo (hapa) Minaa kwa panga zetu."

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:

"Sikupewa amri hiyo bado, lakini rudini katika msafara wenu."

Wakarudi na kulala mpaka asubuhi.

 

Quraysh Wanapeleka Malalamiko

Zilipoanza kuwafikia fununu juu ya fungamano hilo, watu wa kabila la Quraysh walipata msituko mkubwa, kwa sababu walielewa vizuri juu ya hatari inayoweza kuwakabili iwapo kweli jambo hilo limetokea. Walielewa vizuri kuwa roho zao na mali pamoja na ufalme wao utaingia hatarini.

Ukatoka ujumbe mkubwa wa Quraysh kelekea katika kambi ya watu wa Madiynah waliopo Minaa kuwafikishia malalamiko yao makubwa kuhusu tukio hili.

Kwa vile washirikina wa Madiynah hawakuwa na habari yoyote juu ya fungamano hilo, na kwa sababu lilifanywa kwa siri katika kiza cha usiku, washirikina waliapa kuwa jambo hilo haliwezekani kabisa kutokea.

Quraysh wakawaendea wakubwa wao mmoja baada ya mwengine mpaka walipomfikia ‘Abdullaah bin Ubay bin Saluul, aliyesema:

"Hii si haki, haiwezekani ikawa hivi, haiwezekani watu wangu wakadanganyika na jambo kama hili. Ningelikuwa nipo Yathrib, watu wangu wasingeweza kufanya hivi."

Lakini Waislamu, wao walikuwa wakitazamana wao kwa wao na kukaa kimya, hawajakubali wala kukanusha.

Quraysh wakawasadiki washirikina na kurudi makwao.

 

Quraysh Wanapata Uhakika

Quraysh walirudi kambini mwao wakiwa na shaka kubwa juu ya kukanusha kwa watu wa Madiynah. Wakaanza kufanya upelelezi mwingi na kuulizia mpaka walipopata uhakika kuwa fungamano hilo lilifanyika kweli. Lakini hii ilikuwa baada ya Mahujaji kuanza kurudi makwao.

 

Wakaanza kuifukuzia misafara wakijaribu kumkamata yeyote aliyechelewa njiani, na walifanikiwa kuwakaribia watu wawili katika watu wa Madiynah, nao ni Sa’ad bin ‘Ubaadah na Al-Mundhir bin ‘Amru (Radhiya Allaahu ‘anhum). Walifanikiwa kumkamata Sa’ad, lakini Al-Mundhir aliwashinda na akaweza kuwakimbia.

Walipomkamata Sa’ad bin ‘Ubaadah (Radhiya Allaahu ‘anhu), walimfunga mikono pamoja na shingo yake na kumpiga na kumtesa huku wakimburura kwa nywele zake mpaka wakamuingiza Makkah. Akatokea Al-Mut’im bin Uday bin Al-Haarith na kumuokoa na adhabu hiyo, na hii ni kwa sababu Sa’ad alikuwa akishughulikia misafara ya Mut’im inayopita Madiynah kutoka nchi za mbali.

Huko nyuma watu wa Madiynah walikubaliana kurudi Makkah kumuokoa Sa’ad, na walipokuwa wakijitayarisha, wakamuona Sa’ad akirudi, wakafuatana na kurudi pamoja Madiynah.

 

Anasema Al-Mubaarakpuri katika kitabu chake cha Ar-Rahiyqul Makhtuum:

"Hili ndilo fungamano la ‘Aqabah la Pili lililotimizwa katika hali ya mapenzi na utiifu wa hali ya juu kabisa baina ya Waislamu wa pande mbili. Fungamano lilobeba kila maana ya tumaini, kuaminiana, ushujaa, pamoja na kusaidiana baina ya Waislamu wa Makkah na wa Madiynah. Waislamu wa Makkah waliokuwa wakikabiliwa na vitisho na kukandamizwa na washirikina, na wenzao wa Madiynah wakiwaonea huruma na kughadhibika kwa maonevu hayo, hata wakaifunga safari hiyo iliyozungukwa na kila aina ya hatari hadi Minaa kwa ajili ya kufungamna na Mtume wao (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuahidiana naye kuwa roho zao, watu wao na mali zao, zote hizo hazina thamani yoyote mbele ya kuilinda Dini hii na kuwasaidia wenzao.

Na hisia hizi hazikuja hivi hivi tu, bali ni matokeo ya imani ya kweli ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na ya kitabu Chake. Imani isiyotetereka mbele ya nguvu yoyote ile ya dhulma na uadui. Imani ambayo upepo wake ukivuma, unakuja na maajabu katika itikadi na matendo. Kwa imani hii Waislamu waliweza kutenda matendo yasiyosahaulika milele na kuacha athari isiyo na mfano katika zama zao, zama zetu na zama zijazo."[55]

 

Funzo

Mtu anaweza kujiuliza; kwa nini watu wa Madiynah walikuja Makkah kufungamana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakati watu wake wa Makkah walikuwa wakimkanusha? Bali kwa nini watu wa Madiynah walikuwa tayari usiku ule ule kuingia vitani dhidi ya washirikina wa Makkah walipomuambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

"Tunaapa kwa yule aliyekuleta kwa haki, ukitaka (hata) kesho tutawashambulia washirikina waliopo (hapa) Minaa kwa panga zetu."

Lakini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaambia:

"Sikupewa amri hiyo bado."

 

Yote haya hayakutokea kwa sudfa, bali Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) kwa miaka mingi alikuwa akiwatayarisha watu wa Madiynah kwa ajili ya tukio hili.

 

Inajulikana kuwa Mayahudi wengi waliishi Madiynah pamoja na Waarabu waliokuwa washirikina wakati ule. Waarabu wa Madiynah walikuwa makabila mawili makubwa, nayo ni ‘Aws na Khazraj.

Mayahudi kama kawaida yao walijishughulisha na kuingiza mizizi ya fitna na chuki baina ya Waarabu ili waweze kuwagawa na kuwatumilia kwa maslahi yao. Vita baina ya makabila mawili makubwa hayo ya ‘Aws na Khazraj vilikuwa havisiti, na Mayahudi wa kabila la Bani Quraydhwah waliungana na ‘Aws, na Mayahudi wa makabila ya Bani Nadhiyr na Bani Qaynuqaa wakajiunga na Khazraj, na vita visivyokwisha viliendelea baina yao muda wa miaka mingi.

Ilikuwa kila vinapotokea vita baina ya Mayahudi na Waarabu, Mayahudi huwatisha Waarabu wa Madiynah kwa kuwaambia: “Wakati wa kuja kwa Mtume mpya kutoka kwa Allaah ushafika. Na akija Mtume huyo tutamfuata, na tukiwa pamoja naye tutakupigeni vita na tutakuuweni kama walivyouliwa watu wa ‘Aad na Iram.”

Kwa sababu hii watu wa Madiynah nao wakawa wanamsubiri kwa hamu kubwa Mtume huyo atokae wa Allaah huku wakijenga tumaini kuwa huenda kupitia kwake Mtume huyo ikapatikana sulhu na muungano baina ya makabila yao na kurudi tena kuwa Taifa kubwa lenye nguvu. Ndiyo maana waliposikia juu ya Mtume mpya aliyejitokeza huko Makkah, wakasema: “Mnajua enyi watu! Huyu ndiye Nabii ambaye Mayahudi walikuwa wakitutisha naye, kwa hivyo wasitutangulie kumuamini, fanyeni haraka kuujibu mwito wake.”

 

Mwanzo Wa Hijra

Baada ya kukamilika kwa fungamano la pili la ‘Aqabah, Waislamu walifanikiwa kupata ardhi ya kuanzisha dola yao katikati ya jangwa lililozungukwa na kila aina ya ujahili na ushirikina. Mafanikio haya yalikuwa ya hatari sana, kwa sababu yalimaanisha kuanza kwa mfumo mpya. Mfumo mwingine kabisa wa kuilingania Dini ya Allaah. Mfumo wa mapambano marefu baina ya Ujahili ulioenea ulimwengu mzima wakati huo, na baina ya Waislamu wachache waliohama kutoka Makkah na wale wenzao waliosilimu katika watu wa Madiynah.

Mara baada ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwataka wahamie katika nchi yao hiyo mpya, Waislamu walianza kuondoka mmoja mmoja na mara nyingine kwa makundi. Wengi waliondoka nyakati za usiku wakati makafiri wakiwa wamelala wasije wakawazuia au kuwatia katika dhiki.

 

Wa Mwanzo Kuhajir

Ummu Salamah  Radhiya Allaahu ‘Anha)

Miongoni mwa watu wa mwanzo kuhama (kuhajir) alikuwa Abu Salamah, ambaye wakwe zake walimzuia mkewe (Ummu Salamah) pamoja na mwanawe mchanga wasiondoke kwenda Madiynah.

Walimchukua mtoto wao mchanga kwa nguvu. Ikawa kila mmoja (upande wa mume na upande wa mke) anavuta mkono wa mtoto mchanga upande wake mpaka mkono mmoja ulipokatika, ndipo watu wa baba walipofanikiwa kumchukua mtoto huyo.

Abu Salamah ilimbidi aondoke peke yake, na kuwaacha mkewe Ummu Salamah na mwanawe.

Baada ya Abu Salamah kuondoka, Ummu Salamah akawa kila siku asubuhi anatoka na kukaa nje akilia mpaka inapoingia magharibi. Akaendelea katika hali hiyo kiasi cha mwaka, mpaka mmoja katika watu wake alipomuonea huruma na kuwataka jamaa zake wamruhusu aondoke kumfuata mumewe Madiynah.

Akawaambia:

"Hamumwachi masikini huyu aondoke?"

Ndipo walipomruhusu na kumwambia:

"Nenda kwa mumeo ukitaka".

Baada ya kufanikiwa kumpata mwanawe, Ummu Salamah akaianza safari ndefu ya umbali wa kilomita zipatazo mia tano kuelekea Madiynah, na alipowasili mahala panapoitwa Tan’iym, mji uliopo nje kidogo ya Makkah, alikutana na mtu mmoja aitwae ‘Uthmaan bin Twalhah, aliyekubali kufuatana naye mpaka Madiynah, na alipowasili mji wa Qubaa uliopo nje kidogo ya Madiynah, akamwacha hapo na kumwambia:

"Mumeo yupo katika mji huu, ingia umtafute kwa baraka za Allaah".

Kisha Twalhah akarudi Makkah.

(Haya yameandiwa katika Siyrah ya Ibn Hishaam)

 

Suhayb Mrumi (Radhiya Allaahu ‘anhu)

Suhayb (Mrumi) pia ni miongini mwa watu waliopata tabu katika kuhama kwao. Maquraysh walipomuona akijitayarisha walimwendea na kumwambia:

"Ulipokuja kutoka kwenu ulikuwa masikini huna chochote, mali yote hii umeichuma hapa kwetu, sasa leo unataka kutoka na mali yako pamoja na nafsi yako? WaLlaahi hiyo haiwezekani kabisa."

Suhayb akawaambia:

"Mnaonaje nikikuachieni mali yangu yote, je! Mtaniacha niondoke?"

Wakamwambia:

"Ndio, tutakuacha".

Suhayb akasema:

"Basi mimi nakuachieni mali yangu yote".

Zilipomfikia habari hizo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Amefuzu Suhayb. Amefuzu Suhayb".

 

‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alihama kwa njia yake pekee.

Anasema ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu):

“Wote waliohama kutoka Makkah kwenda Madiynah walihama kwa kificho isipokuwa ‘Umar bin Al-Khattwaab. Yeye alipotaka kuhama alivaa upanga wake na kubeba ngao yake, akachukua mikuki mkononi mwake na kwenda moja kwa moja mpaka Al-Ka’abah mbele ya watu wengi waliojaa hapo. Akatufu mara saba mbele yao, kisha akaelekea Maqamu Ibraahiym akaswali rakaa mbili, kisha akaanza kuyaendea makundi yaliyosimama hapo moja baada ya lingine na kuwaambia:

‘Zimedhalilika nyuso zenu, zimedhalilika nyuso zenu. Yeyote kati yenu anayetaka mama yake ampoteze na wanawe wawe mayatima na mkewe awe kizuka, basi na akutane nami nyuma ya bonde hili”.

Anasema Sayiduna ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu):

“Hapana hata mmoja aliyethubutu kumfuata isipokuwa baadhi ya watu wachache waliokuwa wakionewa, hao ndio waliomfuata, pamoja na watu wawili walioagana kuondoka naye, nao ni; ‘Iyaash bin Abi Rabiy’ah na Hishaam bin Al-’Aasw.”

 

Alipowasili Madiynah na kabla hawajapumzika vizuri, ‘Umar na wenzake waligongewa mlango na Abu Jahl akiwa pamoja na ndugu yake Al-Haarith waliotaka kuzungumza na ‘Iyaash ambaye ni ndugu yao kwa mama. ‘Iyaash alipowatokea wakamwambia:

"Ewe ‘Iyaash, mama yako ameapa kuwa hatochana nywele wala hatojificha chini ya kivuli cha jua mpaka utakapokubali kurudi Makkah akuone."

‘Iyaash akaingiwa na huruma akakubali kufuatana nao, lakini ‘Umar akamwambia:

"Ewe ‘Iyaash, WaLlaahi hawa wanataka uwafuate kisha wakukamate na kukutesa tu. Mimi namjua vizuri mama yako. Chawa mmoja akimuudhi hatoweza kustahamili na lazima atazichana nywele zake, na jua la Makkah likimuunguza basi lazima ataondoka juani ajifiche chini ya kivuli."

Lakini ‘Iyaash alishikilia kuwa lazima arudi nao kwa mama yake ili amwondoe katika kiapo chake.

‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipoona ‘Iyaash ameshikilia akamwambia:

"Chukua ngamia wangu huyu anakwenda mbio sana. Wakijaribu kukuendea kinyume, basi mpande uwakimbie."

Wakaondoka pamoja mpaka walipofika nusu ya njia, Abu Jahl akamwambia ‘Iyaash:

"Ewe ndugu yangu, ngamia wangu ananipa tabu kidogo huyu, kwanini hatubadilishani umpande wangu na mimi nimpande wako?"

Waliposhuka wote wawili juu ya ngamia, wakamvamia na kumkamata, kisha wakamfunga kamba na kuingia naye Makkah wakati wa mchana huku wakisema:

"Enyi watu wa Makkah, hivi ndivyo muwafanyie wajinga wenu kama tulivyomfanyia mjinga wetu huyu."

 

Hii ni mifano mitatu katika mifano mingi ya mateso na kujitolea mhanga yaliyowakuta Waislamu waliohajir baada ya kupewa amri na Mtume wao (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Waliobaki Makkah

Baada ya kupita miezi miwili tokea lilipofanyika Fungamano la ‘Aqabah la pili, hawakubaki Makkah isipokuwa Waislamu wachache sana wakiwemo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr na ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhum) kwa amri ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na wachache miongoni mwa Waislamu waliozuiliwa au kufungwa na washirikina wa hapo Makkah.

Wakati huo huo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akijitayarisha kuhama huku akisubiri amri ya kuhama kutoka kwa Mola wake (Subhaanahu wa Ta’alaa),

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) naye pia alikuwa akijitayarisha kuhama.

Imepokelewa katika Sahiyh Al-Bukhaariy  kuwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema:

"Abu Bakr alipokuwa akijitayarisha kuhama, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:

"Usiwe na haraka, kwani mimi nasubiri amri."

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:

"Na unategemea (kuruhusiwa), nakufidia kwa baba yangu na mama yangu?"

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Ndiyo."

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akawa anamsubiri Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Mkutano Wa Halmashauri Ya Maquraysh

Walipoona watu wanauhama mji makundi kwa makundi pamoja na watoto wao na kila walichoweza kukibeba, hofu iliingia nyoyoni mwa Maquraysh wa Makkah, kwa sababu walikuwa wakiiona mbele yao hatari itakayoweza kuwakabili iwapo haya yataachwa kuendelea. Walikuwa wakimjua vizuri Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na waliufahamu vizuri uwezo wake wa kuwakinaisha watu kumfuata, kuwaongoza, na taathira anayoweza kusababisha iwapo naye pia atahama kwenda Madiynah.

Washirikina hao pia walikuwa wakiiona azima waliyokuwa nayo Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na wakiwaona namna gani walivyokuwa tayari kumfuata Mtume wao (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kila anachowaamrisha, pamoja na kuwa tayari kwao kupoteza mali zao, roho zao na kila kilichokuwa ghali kwao kwa ajili ya kuisimamisha Dini yao hii mpya.

Wakati huo huo walikuwa wakiwajua vizuri watu wa Madiynah, hasa makabila ya ‘Aws na Khazraj. Walizijua vizuri nguvu walizokuwa nazo na hekima ya viongozi wao pamoja na uwezo wao wa kupigana vita. Kwani miaka yote ya nyuma makabali haya mawili hayakuwa na shughuli nyingine isipokuwa kupigana vita tu baina yao.

Walikuwa wakiujua pia umuhimu wa mji wa Madiynah kutokana na mahali ulipo, kwani mji huo upo baina ya Makkah na Shaam, mahala inapopita misafara yote ya biashara inayobeba dhahabu nguo na mahitaji mengi ya watu wa Makkah itokayo na inayokwenda Shaam.

Kutokana na yote hayo Maquraysh waliiona mbele yao hatari itakayowakabili iwapo mji wa Madiynah utakuwa makao ya Waislamu na iwapo Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) atafanikiwa kuwaingiza katika Dini hii makabila ya Madiynah na yale yaliyo karibu na mji huo.

Kwa vile kiini cha hatari yote hiyo ni mtu mmoja tu. Mtu huyu aliyeibeba bendera hiyo ya hatari, ambaye bado yupo katika mji wao, ambaye ni Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), wakaona ni bora wakutane ili watoe uamuzi wa kuukata mzizi huo wa hatari inayowakabili kabla mti kumea vizuri.

Siku ya Alkhamisi mwaka wa kumi na nne tokea alipopewa utume, kiasi cha miezi miwili baada ya Fungamano la ‘Aqabah la pili, halmashauri kuu ya Makkah ilikutana ili kutoa uamuzi wa hatari katika historia yao. Mkutano huo ulihudhuriwa na watu wote muhimu wa makabila ya Makkah na vitongoji vyake.

Anasema Al-Mubaarakpuri kuwa miongoni mwa watu muhimu waliohudhuria mkutano huo walikuwa wafuatao:

Abu Jahl (Kiongozi wa kabila la Quraysh)

Jubayr bin Mut’am na Twaima bin Uday na An-Nadhiyr bin Haarith (kabila la Bani Nawfil bin ‘Abdu Manaaf)

Shabih na ‘Utaybah na Abu Sufyaan bin Harb (Viongozi wa kabila la Bani ‘Abdush-Shams).

An-Nadhiyr bin Haarith (Kiongozi wa kabila la Abdud-Daar).

Abul Bakhtari bin Hishaam na Zam’ah na Haakim bin Hizaam (Viongozi wa kabila la Ba Asad).

Nabih na Manbah wana wa Al-Hajjaaj (Viongozi wa kabila la Saham) na

Umayyah bin Khalaf (Kiongozi wa kabila la Bani Jamh)

Katika mkutano huo kila mmoja akatoa rai yake. Wengine wakasema kuwa ni bora Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) afukuzwe na kupelekwa mbali sana na miji yao ili wapumzike naye.

Wengine wakasema bora afungiwe ndani ya jela ya vyuma asiweze kutoka na abaki humo mpaka afe.

Abu Jahl akasema:

"WaLlaahi mimi nina rai nyingine kabisa, kinyume na mnavyoona nyinyi".

Wakamuuliza:

"Nini rai yako ewe Abul Hakam?"

(Makafiri walikuwa wakimwita 'Abul Hakam" na maana yake ni Baba wa Hikma, lakini Waislamu walimwita 'Abu Jahl', na maana yake ni Baba wa Ujinga).

Akasema:

"Mimi naona ni bora atoke kutoka katika kila kabila kijana mmoja madhubuti mwenye nguvu, na tumpe kila mmoja wao upanga mkali sana, kisha wamwendee na kumvamia kwa pamoja, wampige pigo la mtu mmoja na kumuua. Hapo ndipo tutakapopumzika naye. Kwani tukifanya hivyo, damu yake itagawanyika baina ya makabila kumi, na watu wake Banu Abdi Manaaf hawatoweza kupigana na makabila yote hayo na wataridhika na fidia tutakayowapa.”

Wakakubaliana wote na rai hiyo.

Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Ameuelezea mkutano huo katika Kitabu Chake kitufu pale Aliposema:

وَإِذْ يَمْكُرُ بِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِيُثْبِتُوكَ أَوْ يَقْتُلُوكَ أَوْ يُخْرِجُوكَ ۚ وَيَمْكُرُونَ وَيَمْكُرُ اللَّـهُ ۖ وَاللَّـهُ خَيْرُ الْمَاكِرِينَ

"Na (kumbuka Ee Nabii Muhammad) walipokufanyia hila wale waliokufuru ili wakufunge au wakuue au wakutoe (kwa hali mbaya katika Makkah); na wakafanya hila (zao barabara). Na Allaah Akazipindua hila hizo. Na Allaah ni mbora wa kupindua hila (za watu wabaya)".

Al-Anfaal - 30

 

Kuhama Kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

Wakati Maquraysh wanaendela na mkutano wao, Jibriyl (‘Alayhis Salaam) alimteremkia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumjulisha juu ya hila zao, akamwambia:

"Usiku wa leo usilale juu ya kitanda chako."

Kisha akamjulisha juu ya wakati anaotakiwa aondoke kuelekea Madiynah.

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaenda moja kwa moja mpaka kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) ili wapange vizuri safari yao.

Anasema Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha):

"Akaja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuomba ruhusa ya kuingia ndani, na baada ya kupewa ruhusa, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia Abu Bakr:

"Watoe wote waliokuwemo ndani."

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:

"Hawa wote ni watu wako pia."

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

"Nimekwishapewa amri ya kuondoka."

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:

"Tutakuwa pamoja katika safari ewe Mtume wa Allaah."

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Ndiyo."

Baada ya kupanga, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akarudi nyumbani na kuusubiri usiku uingie.

 

Anaendelea kusema Bibi ‘Aaishah bint Abi Bakr (Radhiya Allaahu ‘anha):

"Nilimuona baba yangu akilia kwa furaha, sijapata kumuona mtu kabla ya hapo akilia kwa furaha mpaka nilipomuona Abu Bakr. Nikamsikia akimuambia Mtume wa Allaah: "Ewe Mtume wa Allaah, hawa ni ngamia wawili niliowatayarisha kwa ajili ya safari hii. Ninakufidia kwa baba yangu na mama yangu, mchukue mmoja kati ya ngamia hawa wawili."

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"(Lakini) Kwa thamani yake".

 

Nyumba Inazungukwa

Mchana wote Maquraysh walikuwa wakipanga mpango madhubuti wa kumshambulia na kumuua Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na usiku ulipoingia wakajikusanya nje ya mlango wake wakimsubiri ale ili wamvamie mvamio wa mtu mmoja na kumuua.

Walikuwa na uhakika kuwa watamuua, kiasi ambapo Abu Jahl alisimama akiwahutubia makafiri wenzake kwa istihzai, akisema:

"Hakika Muhammad anadai kuwa eti mkimfuata katika Dini yake mtakuwa wafalme wa waarabu na wasiokuwa waarabu. Kisha eti baada ya kufa kwenu mtafufuliwa na kuingizwa katika bustani za Peponi mfano wa bustani zilizopo katika nchi ya Jordan na kwamba msipomfuata basi mtauliwa na mtafufuliwa baada ya kufa kwenu na kuingizwa katika moto utakaokuunguzeni."

Maquraysh wakabaki hapo wakingoja usiku uingie ili waikamilishe kazi yao.

 

Anaondoka Nyumbani

Kabla ya kuondoka nyumbani kwake, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu):

"Lala juu ya kitanda changu na ujifunike na guo langu hili na wala usiogope kwa sababu hapana chochote kitakachoweza kukudhuru au hata kukugusa."

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapolala akijifunika na guo lake hilo.

Kisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akatoka nje ya nyumba na kupita mbele ya makafiri waliokuwa wakimsubiri mlangoni, akawa anawanyunyizia mchanga juu ya vichwa vyao, huku akisoma:

وَجَعَلْنَا مِن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ سَدًّا وَمِنْ خَلْفِهِمْ سَدًّا فَأَغْشَيْنَاهُمْ فَهُمْ لا يُبْصِرُونَ

"Na (kama kwamba). Tumeweka kizuizi mbele yao na kizuizi nyuma yao na Tumewafunika (macho yao), kwa hivyo hawaoni.”

Yaasiyn - 9

 

Kisha akenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), na baada ya kumgongea mlango, akatoka na wakafuatana pamoja kuelekea Madiynah wakipitia njia inayoelekea Yemen, mpaka walipofika katika pango la Ghaar Thawr.

 

Huku nyuma Maquraysh walibaki mlangoni wakisubiri Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ale wapate kuifanya shughuli yao, na hawakujua nini kilichotendeka mpaka mpita njia aliyekuwa hana habari juu ya mpango huo alipowaona katika hali ile, akawawaamsha na kuwauliza:

"Mnamsubiri nani hapa?"

Wakasema:

"Muhammad."

Akawaambia:

"WaLlaahi mumekula hasara, kwa sababu Muhammad kapita hapa mbele yenu na kukuwekeeni mchanga juu ya vichwa vyenu kisha akenda alikokwenda."

Wakasema:

"WaLlaahi hatukumuona."

Wakainuka huku wakijipangusa michanga vichwani mwao, wakachungulia ndani ya nyumba ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuona ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) akiwa amelala juu ya kitanda chake. Wakamuuliza: "Yuwapi Muhammad?"

Akawajibu: "Sijui."

Na kweli hakuwa akijua wakati huo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yuko wapi.

 

Kutoka Nyumbani Kuelekea Pangoni

Katika kitabu chake kiitwacho Ar-Rahiyqul Makhtuum, anasema Al-Mubaarakpuri:

"Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliondoka nyumbani kwake usiku wa tarehe 27 mwezi wa Swafar mwaka wa kumi na nne tokea alipopewa utume, na kuelekea nyumba ya Sahibu yake na mwaminifu wake Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), kisha wakaondoka pamoja kupitia mlango wa nyuma na kuihama Makkah kabla Alfajiri haijaingia.

Kwa vile walielewa vizuri kuwa Maquraysh mara baada ya kuzindukana wataanza kumsaka na kumtafuta, na kwamba njia ya mwanzo watayoifikira kuifuata ni ile ya kawaida ya kwenda Madiynah, kwa hivyo badala ya kuitumia njia hiyo wakabadilisha na kuitumia njia nyingine, nayo ni ile ya kusini ya Makkah inayoelekea Yemen. Wakaifuata njia hiyo kiasi cha maili tano, kisha wakageuza tena na kulielekea jabali liitwalo Jabal Thawr, na jabali hili ni refu na njia yake ni mbaya yenye hatari sana, lakini juu ya yote hayo, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na sahibu yake (Radhiya Allaahu ‘anhu) walifanikiwa kulipanda na kulifikia pango lililopo juu ya jabali hilo lililokuja kujulikana baadaye kwa jina la (Ghaar Thawr), na kujificha humo.

Walipolifikia pango, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimtaka ruhusa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aingie yeye mwanzo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa hapana hatari yoyote ndani inayoweza kumdhuru Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Alipoingia na kuyaona matundu yaliyojaa ndani ya pango akaanza kuchana baadhi ya nguo zake na kuziba tundu, kwa ajili ya kudhamini hatari yoyote isitokee kupitia humo, kwani kwa kawaida majabali huwa yamejaa nyoka, nnge na vijidudu vyengine vya hatari vinavyodhuru na vilivyojaa simu.

 

Alipoona limebaki tundu moja tu na hakuwa tena na kitu cha kuzibia, akauweka mguu wake hapo na kuliziba tundu hilo ili dhara yoyote itatokea hapo, basi ni bora adhurike yeye kuliko kudhurika Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), akauweka uso wake mtukufu juu ya paja la Sahibu yake (Radhiya Allaahu ‘anhu) ili ajipumzishe kidogo, kwa sababu hapakuwa na nafasi ya kukaa vizuri. Na kabla hawajapumzika vizuri wakaanza kusikia sauti za Maquraysh zikikaribia.

 

Imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhaariy hadithi iliyosimuliwa na Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa alimsikia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akisema:

"Nilikuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pangoni nikanyanyua kichwa changu (kutazama) nikaiona miguu ya watu (ikitusogelea), Nikamwambia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

"Mmoja wao akitazama chini (kidogo tu) atatuona".

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia:

"Nyamaza ewe Abu Bakr, (sisi) wawili wa tatu wetu ni Allaah)".

Na katika riwaya nyingine:

"Unaonaje juu ya wawili, Allaah wa tatu wao?"

Allaah Anasema:

إِلأ تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّـهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لأ تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا ۖ فَأَنزَلَ اللَّـهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ لَّمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُوا السُّفْلَىٰ ۗ وَكَلِمَةُ اللَّـهِ هِيَ الْعُلْيَا ۗ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

"Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Allaah Alikwishamnusuru walipomtoa waliokufuru, naye ni wapili katika wawili walipokuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake: Usihuzunike. Hakika Allaah yu pamoja nasi. Allaah Akamteremshia utulivu Wake, na akamuunga mkono kwa majeshi msiyoyaona, na akalifanya neno la waliokufuru kuwa chini, na Neno la Allaah kuwa ndilo juu. Na Allaah Ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima."

At-Tawbah - 40

Allaah Akamnusuru Mtume wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kwani maadui hao walirudi makwao bila kuwaona.

 

‘Aliy Na Hafswah (Radhiya Allaahu ‘Anhum) Wanaadhibiwa

Walibaki hapo muda wa siku tatu. Usiku wa Ijumaa, siku ya Jumamosi na usiku wa Jumapili, na ‘Abdullaah bin Abi Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akija nyakati za usiku na kulala pamoja nao.

Anasema Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha), kuwa ‘Abdullaah alikuwa kijana mwepesi na hodari. Alikuwa akilala pamoja nao na asubuhi akiingia Makkah kama siye, na alikuwa akipeleleza habari za Makkah na kuwajulisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) juu ya harakati zao na ‘Amr bin Fuhayrah aliyekuwa mchunga kondoo wa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akiwapitisha kondoo wake juu ya alama za miguu ya ‘Abdullaah bin Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa ajili ya kuwapoteza Maquraysh

.

Maquraysh walipata wazimu walipotambua kuwa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) keshawaponyoka na jambo la mwanzo walilofanya ni kumchukua ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kumfunga kamba kisha wakamchukua mpaka mbele ya Al-Ka’abah na kumfunga hapo muda wa saa huku wakimuuliza wakitaka kujua juu ya habari za Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Baada ya kumtesa bila ya mafanikio, wakaamua kwenda nyumbani kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kugonga mlango. Asmaa bint Abi Bakr (Radhiya Allaahu ‘anha) alipofungua mlango, wakamuuliza:

"Yu wapi baba yako?"

Akawajibu:

"Sijui."

Abu Jahl kwa ukhabithi wake akampiga kofi la nguvu usoni mpaka hereni yake ikakatika na kuanguka. Baada ya kutofanikiwa hapo pia, Maquraysh wakaanza kuchukua hatua kali za kuzilinda njia zote zitokazo Makkah kwenda Madiynah na wakatangaza kuwa atakayeweza kumkamata yeyote kati ya wawili hao na kuwaleta mbele ya Maquraysh wakiwa hai au wamekwishakufa, atapata zawadi ya ngamia mia moja kwa kila mmoja wao.

Baada ya tangazo hilo, wasakaji maarufu wakaanza kazi yao itakayowaletea utajiri wa haraka, na kuenea katika sehemu zote za majabali na za jangwa kuwatafuta.

Baadhi yao walifika mpaka kwenye pango hilo, lakini hawakuweza kuwaona.

 

Njiani Kuelekea Madiynah

Baada ya joto la msako kupungua na baada ya kusubiri pangoni kwa muda wa siku tatu, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na sahibu yake Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu) waliamua kuondoka na kuianza safari yao ya kwenda Madiynah.

Walimuajiri ‘Abdullaah bin ‘Urayqah awe akiwaongoza njia, kwani yeye alikuwa akizijua vizuri njia za ndani, na ‘Abdullaah huyu hakuwa Muislamu, alikuwa akifuata Dini ya Maquraysh, lakini juu ya hivyo ilibidi wamuaminishe kwa sababu ya umahiri wake wa kuzijua njia hizo. Wakapanga kuonana naye penye pango la Thawr usiku wa Jumatatu tarehe mosi mwezi wa Rabiy’ul Awwal.

Wakaondoka pamoja na ‘Abdullaah bin ‘Urayqah, wakamchukua na ‘Aamir bin Fuhayrah na kuianza safari ndefu ya kwenda Madiynah.

Ili kuwababaisha Maquraysh, waliianza safari yao kwa kupitia njia ya Kusini inayoelekea nchi ya Yemen, kisha wakageuza njia na kuelekea Mashariki kupitia njia ya pwani pwani, mpaka walipoifikia njia isiyotumiwa na watu isipokuwa kwa nadra, njia iliyopo kando kando ya bahari nyekundu (Red Sea).

Hebu tumsikilize Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu) akituelezea juu ya safari yao hiyo;

Imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhaariy kuwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema:

"Tuliondoka usiku ule tukawa tunakwenda mpaka adhuhuri ya siku ya pili ikatuingilia, tukaifuata njia isiyotumiwa na watu, mbele yetu tukaona jabali kubwa na chini yake pana kivuli, tukashuka hapo na kwa mikono yangu nikamsafishia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mahala ili apate kulala, nikamtandikia shuka kisha nikambwambia:

"Lala ewe Mtume wa Allaah".

Akalala na mimi nikaondoka hapo na kutembea huku na huko ili nichunguze iwapo pana hatari yoyote karibu yetu. Nikamuona kijana mmoja akichunga kondoo, nikamuuliza ni mchungaji wa nani wewe?

Akanijibu:

"Mmoja katika watu wa Madiynah (au Makkah)".

Nikamuuliza:

"Kondoo wako wana maziwa?"

Akanijibu:

"Ndiyo".

Nikamuuliza:

"Utaweza kutukamulia?"

Akasema:

"Ndiyo"

Akanikamulia maziwa na mimi nilikuwa na chombo cha kuyatilia maziwa hayo, nikampelekea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa bado amelala, nikaona uzito kumuamsha, nikamuacha alale mpaka alipoamka, nikampa maziwa anywe, akanywa mpaka nikaridhika kuwa ametosheka, kisha akaniuliza:

"Unaonaje si umefika wakati wa kuondoka?"

Nikamwambia:

"Sawa".

Tukaondoka.

Anasema Al-Mubaarakpuri:

"Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akipenda kuwa nyuma ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na alikuwa ni mtu maarufu na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa maarufu, kwa hivyo mtu yeyote wanayekutana naye njiani alikuwa akimsalimia Abu Bakr na kumuuliza; Nani huyu uliyefuatana naye?"

Na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akijibu:

"Huyu ni kiongozi ananiongoza njia."

Muulizaji hudhani kuwa anamuongoza njia ya safari, wakati Abu Bakr hukusudia njia ya kheri iliyonyooka."

 

Suraaqah Na Bangili Za Mfalme Kisraa

Mtu mmoja aitwae Suraaqah bin Maalik alikuwa akiwafuata kwa mbali. Anasema Suraaqah:

"Nilipokuwa nimekaa katika majlis mojawapo ya kabila letu, akaingia mmoja katika jamaa yetu na kusema:

"Ewe Suraaqah, mimi kabla ya kidogo niliona watu wakitembea njia ya pwani pwani, na sidhani kama ni wengine isipokuwa ni Muhammad na Sahibu yake."

Nikajua kuwa ni wao, lakini nikamwambia:

"Sidhani kama ni wao, labda hao ni fulani na fulani."

 

Nikabaki katika majlis hiyo kiasi cha saa, kisha nikaondoka taratibu kwenda nyumbani kwangu na kumwambia mtumishi wangu:

"Nitayarishie farasi wangu", nikampanda na kuuchukua mkuki wangu, kisha nikatoka kwa mlango wa nyuma ili mtu asinione, na kuianza safari ya kuwafuatia mpaka nilipowakaribia, nikawa namsikia Mtume Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisoma lakini hakuwa akigeuka geuka, lakini Abu Bakr alikuwa mwingi wa kugeuka. Nilipowakaribia zaidi miguu ya mbele ya farasi wangu ikaanza kuzama mpaka mapaja yake, nikashuka juu ya farasi wangu na kujaribu kumtoa miguu yake iliyozama kwa nguvu mpaka nikafanikiwa. Nikampanda tena na kila nilipojaribu kuwasogelea yakawa yananitokea yale yale, mwisho nikawaita na kuwaomba wanisubiri kwani nilikuwa nataka kufanya amani nao. Nilipowaona na kukumbuka yale yaliyonikuta katika kuzama farasi wangu nikatambua kuwa utabainika utukufu wa Mtume huyu wa Allaah. Nikamwambia:

"Watu wako wametangaza kuwa atakayekukamata atapata zawadi”. Kisha nikawataka wachukue chakula nilichokuwa nacho, hawakunishughulikia wala kuchukua, isipokuwa waliniambia:

"Usitufuate."

"Nikamtaka aniandikie mkataba wa amani, akamuamrisha ‘Amru aandike na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akatia saini (sahihi) yake kisha akaendelea na safari."

 

Katika riwaya nyingine anasema Shaykh Abu Bakr Al-Jazaairiy katika kitabu chake Haadhal Habiyb:

"Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia Abu Bakr mwambie: "Hatuna haja ya ngamia wake." Na Suraaqah alipokuwa akirudi, Mtume akamwambia:

"Utakuwaje ewe Suraaqah siku ile utakapovaa bangili za Kisraa mfalme wa Wafursi?"

Suraaqah akauliza: "Kisraa bin Hurmuz?"

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu: "Ndiye"

Suraaqah alipokuwa akirudi Makkah alikuwa kila anayemkuta njiani akimwambia: "Msihangaike inatosha tena mpaka hapa mlipofika."

Subhana Allaah! Asubuhi alikuwa adui wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na usiku wake alikuwa mlinzi wake.

((Bishara aliyopewa Suraaqah ya kuvaa bangili za mfalme Kisraa ilitimia wakati wa utawala wa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) baada ya kutekwa nchi ya Fursi)).

 

Ummu Ma’abad Al-Khuza’iyah

Walipokuwa njiani walipita penye hema la Ummu Ma’abad Al-Khuza’iyah aliyekuwa mwanamke hodari, mwenye nguvu anayeishi ndani ya hema lake na alikuwa akipenda kuwasaidia wasafiri wapitao hapo kwa kuwapa maziwa au maji ya kunywa. Wakamuuliza iwapo ana chochote cha kuwanywisha. Ummu Ma’abad akawaambia:

"WaLlaahi ningelikuwa na chochote kile nisingesubiri mpaka muniombe, na kondoo wangu amekonda hana maziwa na huu ni mwaka wa ukame."

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamtazama kondooo yule aliyefungwa pempezoni mwa hema, kisha akamuuliza:

"Hana maziwa hata kidogo?"

Akasema:

"Kama unavyomuona, amekauka hana chochote."

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza:

"Utaniruhusu nimkamue?"

Akamwambia:

"Kama unadhani utapata maziwa yoyote ndani yake, basi huyo hapo mkamue."

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaunyosha mkono wake mtukufu na kumshika chuchu zake mbuzi yule, kisha akapiga BismiLlaah na kuanza kumuomba Allaah huku akisoma na kuomba dua. Chuchu zikaanza kujaa, na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamtaka Ummu Ma’abad alete chombo cha kukamulia maziwa, chombo kikaletwa, na baada ya kujazwa maziwa chombo hicho akampa Ummu Ma’abad mwenyewe aanze kunywa, na baada ya kushiba akajaza tena na kuwapa Sahibu zake, baada ya kunywa Sahibu zake akanywa mwenyewe. Baada ya kushiba akakijaza chombo hicho tena na kukiacha hapo, kisha wakaondoka na kuendelea na safari yao.

 

Haujapita muda mrefu, mumewe Ummu Ma’abad akarudi nyumbani na kushangazwa kumuona mbuzi yule aliyemwacha akiwa amekondeana sasa amejaa maziwa na chombo cha kukamulia pia kimejaa maziwa. Akamuuliza mkewe:

"Umepata wapi haya?"

Ummu Ma’abad akamwambia:

"Alipita hapa mtu mwenye baraka na maneno yake yalikuwa ya namna hivi na vile." Kisha akaanza kumuelezea baadhi ya sifa zake

Mumewe akasema:

"Huyu si mwingine ila ni yule Mquraysh wanayezungumza juu yake, ningelimuona ningemfuata, na nitakapopata fursa ya kumuona basi nitamfuata."

 

Kusilimu kwa Abu Buraydah

Walipokuwa wakiendelea na safari yao walikutana na Abu Buraydah aliyekuwa akimtafuta Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amkamate na kumrudisha Makkah ili apate wale ngamia mia moja waliotolewa zawadi kwa yoyote atakayeweza kumkamata Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Sahibu yake Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Alipokutana naye, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimsemesha na akasilimu hapo hapo yeye pamoja na watu sabini aliokuwa nao, kisha akavua kilemba chake na kukifunga juu ya mkuki wake ikiwa ni dalili kuwa Mfalme wa Amani na Usalama amewasili ili kuujaza ulimwengu uadilifu na haki.

Walipokuwa njiani walikutana pia na Az-Zubayr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akiwa pamoja na Waislamu wenzake wakitoka Shaam katika msafara wa biashara. Az-Zubayr aliwapa zawadi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) nguo yenye rangi nyeupe.

 

Wanawasili Qubaa

Siku ya Jumatatu tarehe nane mwezi wa Rabiy’ul Awwal mwaka wa kumi na nne tokea apewe utume, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwasili mji wa Qubaa uliopo kiasi cha maili tatu mbali na mji wa Madiynah.

Imesimuliwa na Urwa bin Zubayr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa watu wa Madiynah walipata habari kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) keshaondoka Makkah kuelekea Madiynah, wakawa kila siku wakati wa asubuhi wanatoka nje wakimsubiri mpaka linapoanza joto la adhuhuri walikuwa wakirudi majumbani mwao.

Siku moja baada ya kusubiri sana na kurudi majumbani mwao, Myahudi mmoja aliyekuwa juu ya paa la nyumba yake akamuona Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akija, na hakuweza kuimiliki nafsi yake, akaanza kupiga kelele akisema:

"Enyi waarabu (babu yenu) Mtume wenu huyo anakuja."

 

Watu wa Madiynah wakatoka wakikabbir na kuimba na kupiga vigelegele. Wote walitoka kumpokea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na haikupata kutokea siku ya furaha katika mji wa Madiynah kupita siku hiyo.

Watu wakawa wanazidi kumiminika wakiwa wamebeba matawi ya miti na kila walichoweza kukibeba ili kuionesha furaha yao hiyo.

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Sahibu yake wakakaa chini ya kivuli cha mtende wakipumzika, na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitulia kimya huku watu wakija kuwasalimia yeye na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) na wengine wale wasiopata kumuona hawakuwa na uhakika yupi kati yao alikuwa Mtume, na hii ni kwa sababu umri wao ulikuwa unakaribiana.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipotambua hayo, akaitoa nguo yake ya juu na kumkinga nayo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na jua lililoanza kumfikia, na hapo ndipo walipohakikisha.

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifikia nyumba ya Kulthuum bin Hidaam, na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alifikia nyumba ya Khubayb bin Isaaf.

 

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu) Naye Anawasili Madiynah

‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) alibaki Makkah muda wa siku tatu kwa ajili ya kurudisha  amana za watu zilizowekwa kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kisha akasafiri kwa miguu hadi Qubaa, na aliwasili hapo siku tatu baada ya kuwasili kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomtaka aende kwake, alishindwa kwa sababu miguu yake ilikuwa inamuuma na imevimba sana. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwendea na kumkumbatia, kisha akambusu huku akilia kwa kumuonea huruma, kisha akatema mate mkononi pake na kumpangusia miguuni huku akimsomea na kumuomba Allaah, mpaka akapona. Na tokea siku hiyo mpaka kufa kwake, ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakupata tena kuumwa miguu.

 

Anasema Dkt. Mustafa As-Siba’iy:

"Askari mkweli mtiifu mwenye niyah ya kweli ya kutaka mabadiliko mema. Siku zote ana hiyari afe yeye iwapo kiongozi atakayeleta mabadiliko atasalimika. Kwani kiongozi akiangamia, mwito anaoulingania nao pia utatoweka. aliyofanya ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) siku ya Al Hijra, pale alipokubali kulala mahali pa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alijitolea mhanga maisha yake kwa ajili ya usalama wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Kwani ingewezekana kwa wale majahili kumi wa Kiquraysh kukivamia kitanda hicho na kumshambulia kwa panga zao zilizonolewa vizuri wakidhani kuwa yule aliyelala ni Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Wangeweza hata kumvamia kwa ghadhabu tu, kwa ajili ya kulipa kisasi baada ya kutomuona Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kwa sababu yeye ndiye alisababisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuondoka kwa urahisi. Lakini ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakujali yote hayo, kwa sababu alichokuwa akitaka ni usalama wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)".

 

Kusilimu Kwa Salmaan Al-Faarisy (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alibaki Qubaa muda wa siku nne, akajenga Msikiti wa Qubaa uliotajwa katika Qur-aan katika kauli Yake (Subhaanahu wa Ta’alaa), Aliposema:

لَّمَسْجِدٌ أُسِّسَ عَلَى التَّقْوَىٰ مِنْ أَوَّلِ يَوْمٍ أَحَقُّ أَن تَقُومَ فِيهِ ۚ فِيهِ رِجَالٌ يُحِبُّونَ أَن يَتَطَهَّرُوا ۚ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُطَّهِّرِينَ

"Msikiti uliojengwa juu ya msingi wa kuMchaji Allaah tangu siku ya mwanzo unastahiki zaidi wewe usimame (uswali) humo..."

At-Tawbah - 108

 

Akiwa bado yupo Qubaa, alikuja kwake Salmaan Al-Faarisy aliyekuwa akimsubiri kwa hamu kubwa sana. Alikuja na mfuko wa tende na kumwambia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

"Hii ni sadaka nimekuletea."

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

"Sisi hatupokei sadaka." Kisha akamtaka awape watu wengine sadaka hiyo.

Siku iliyofuata Salmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) akaja na tende nyingine akampa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huku akimwambia:

"Hii ni zawadi kutoka kwangu."

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaikubali zawadi hiyo.

Ndipo Salmaan aliposilimu na kuzitamka shahada ya haki:

"أشهد أن لا إله إلا الله وأشهد أن محمدا رسول الله"

"Ash- hadu allaa ilaaha illa Llaah wa ash-hadu anna Muhammadan Rasuulu Llaah".

 

Na hii ni kwa sababu Salmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisoma kwa watu wa Ahlul Kitaab na pia ndani ya vitabu vilivyotangulia kuwa miongoni mwa sifa za Mtume mpya atakayekuja huwa anakubali zawadi lakini hakubali sadaka.

 

Kuhama Kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Na Kwa ‘Umar Bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

"Inaweza kumpitikia mtu kutaka kufananisha baina ya kuhama kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuhama kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Rahdiya Llaahu ‘anhu), akajiuliza:

"Kwa nini ‘Umar alihama mchana, tena mbele ya watu bila kuogopa, huku akiwabishia makafiri pale alipowaendea na kuwaambia:

‘Zimedhalilika nyuso zenu, zimedhalilika nyuso zenu, yeyote kati yenu anayetaka mama yake ampoteze na wanawe wawe mayatima na mkewe awe kizuka, basi na akutane nami nyuma ya bonde hili.”

Wakati Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alihama kwa kificho bila kumjulisha mtu. Mtu anaweza kujiuliza:

"Hivyo ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) anaweza kuwa shujaa kuliko Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)?"

 

Kuelekea Madiynah

Siku ya Alkhamis baada ya kukamilisha kazi za ujenzi wa Msikiti wa Qubaa, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaita watu wa kabila la Bani Najjaar (wajomba zake), wakaja wakiwa kiasi cha watu mia moja na panga zao mkononi, akaondoka nao akifuatana na Sahibu zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) kuelekea Madiynah.

Ijumaa iliwaingilia wakiwa njiani katika kijiji cha Bani Saalim bin ‘Awf, wakakusanyika penye Msikiti uliojengwa bondeni na kuswali hapo.

 

Kuingia Madiynah

Ansema Al-Mubaarakpuri:

“Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliiingia Madiynah, mji uliokuwa ukiitwa Yathrib, siku ya Ijumaa tarehe 12 Rabiy’ul Awwal, muwafaka na tarehe 27 Septemba mwaka 622 kalenda ya Gregori).”

Aliswali Ijumaa katika kijiji cha Bani Saalim bin ‘Awf, na tokea siku hiyo mji huo ukaitwa Madiynat Rasuuli Llaah na ukawa kwa ufupi unaitwa Madiynah.

 

Hii ilikuwa siku ya historia isiyosahaulika, kwani kutoka majumbani, barabarani na kutoka kila sehemu, sauti za Takbiyr na Tahmiyd zilisikika.

Wanaume kwa wanawake pamoja na watoto wadogo, wote walitoka nje kumpokea mgeni wao mtukufu. Wengine walisimama juu ya paa za nyumba wengine juu ya miti na wengine walimzunguka Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huku wakizishika hatamu za ngamia wake na kumwambia:

"Njoo kwetu, karibu nyumbani kwetu ewe Mtume wa Allaah".

Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwaambia:

"Mwacheni huyo, kwani ameamrishwa".

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawa anaendela kwenda katikati ya makundi hayo ya watu, ambayo Anas bin Malik alipoielezea furaha ya siku hiyo alisema:

"Nilikuwepo siku ile Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoingia Madiynah, na nilikuwepo pia siku ile alipofariki dunia, sikupata kuona siku adhimu kuliko siku mbili hizo."

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuacha ngamia wake aende mwenyewe mpaka akasimama alipofika mahala ulipo Msikiti wake siku hizi, akapiga magoti mahala hapo palipokuwa na shamba, na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akashuka. Kwa bahati mahala hapo palikuwa pa Bani Najjaar (wajomba zake), na yeye alipenda kufikia kwa wajomba zake.

Watu wakawa wanamwendea, kila mmoja akimtaka afikie kwake. Abu Ayyuub Al-Answaariy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alifanikiwa kuwatangulia wenzake na kuishika hatamu ya ngamia na kumuingiza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ndani ya nyumba yake.

Riwaya nyingine iliyotolewa na Al-Bukhaariy inasema:

(Ngamia alipopiga magoti) Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza:

"Nyumba ya nani ipo karibu zaidi?"

Abu Ayyuub (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:

"Nyumba yangu, na huu mlango wangu."

Akazishika hatamu za ngamia wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumkaribisha ndani.

Baada ya siku chache akawasili Madiynah mkewe Bi Sawdah na binti zake wawili Faatwimah na Ummu Kulthuum na wakawasili pia Usaamah bin Zayd na Ummu Ayman na ‘Abdullaah bin Abi Bakr pamoja na watoto wadogo wa Abu Bakr pamoja Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu nhum).

 

Mafunzo Juu Ya Hijra 

 

"Kutokana na Hijra hii Mtume wetu mtukufu (Swalah Llaahu ‘alayhi wa sallam) atakuwa ametimiza Sunnah ya Mitume wenzake waliomtangulia, kwani Mitume yote (‘Alayhimus Salaam) kuanzia Nabii Ibraahiym mpaka kufikia kwa Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam), wote waliihama miji yao waliyozaliwa, waliteseka na kusubiri ili wawe mfano mwema kwa watu wao".

 

Anasema Shaykh Ahmad Fariyd:

"Na hii ndiyo maana Waraqah bin Nawfal alimwambia Mtume wa Allaah (Swalah Llaahu ‘alayhi wa sallam):

"Yareti ningeliishi mpaka siku ile watu wako watakapokutoa katika nchi yako".

 

Allaah Anasema:

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِرُسُلِهِمْ لَنُخْرِجَنَّكُم مِّنْ أَرْضِنَا أَوْ لَتَعُودُنَّ فِي مِلَّتِنَا 

"Na wale waliokufuru wakawaambia Mitume yao "Tutakutoeni katika nchi yetu au lazima murudi katika mila yetu."

Ibraahiym - 13

 

Ujenzi Wa Msikiti Wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

Baada ya kuingia nyumbani kwa Abu Ayyuub Al-Answaariy (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kumpumzika, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akatoka nje tena kwa ajili ya kutaka kumjua mwenye kuimiliki ile ardhi aliyopiga magoti ngamia wake. Akasema:

"Enyi watu wa Madiynah, nijulisheni thamani ya ardhi hii iliyozungukwa na ukuta ili niinunue na kujenga Msikiti."

Mahali hapo palikuwa na shamba la mitende, milki ya ndugu wawili vijana mayatima.

Mu’aadh bin Afraa akasema:

"Hii ni ya mayatima wangu wawili na majina yao ni Sahal na Suhayl bin ‘Amru na wao wataridhika."

Mayatima hao wakaja mbele ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuambia:

"Ewe Mtume wa Allaah, sisi tunakupa ardhi yetu bila malipo yoyote ili ujenge Msikiti juu yake."

Lakini Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakukubali akawalipa thamani yake.

 

Akaanza kupasafisha mahala hapo, na kukata magugu pamoja na kuiweka ardhi sawa, na kwa vile mahala hapo palikuwa na makaburi ya washirikina, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaamrisha yafukuliwe na kutolewa mizoga yao ipate kuzikwa mahali pengine, na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawa anafanya kazi pamoja nao akibeba matofali huku akiimba:

اللَّهُمّ َلأ عَيْشَ إِلأ عَيْشُ ‏ ‏الْآخِرَهْ ‏َأَكْرِمْ ‏ ‏الْأَنْصَارَ ‏ ‏وَالْمُهَاجِرَهْ

"Mola wangu hapana maisha (bora) isipokuwa maisha ya Akhera, kwa hivyo wakirimu Answaar (watu wa Madiynah) na Muhajiriyn (watu wa Makkah)."

 

Magogo ya mitende yakafanywa kuwa nguzo za Msikiti, na makuti yake kuwa mapaa na ardhi ya Msikiti ikatandazwa mchanga na kokoto laini na ikajengewa milango mitatu.

Waislamu wakati huo walikuwa wakielekea Baytul Maqdis, na katika mwezi wa Sha’abaan, mwaka wa pili baada ya Hijra iliteremshwa amri ya kubadilisha Qiblah kutoka Baytul Maqdis kuelekea Msikiti wa Makkah.

Karibu ya Msikiti vikajengwa vyumba vya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wake zake (Radhiya Allaahu ‘anhunna) na kuambatanishwa na Msikiti huo.

Msikiti haukuwa mahali pa kuswali tu, bali ulikuwa shule wanayokutana Waislamu na mwalimu wao Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), aliyekuwa akiwafunza, akiwalea na kuwapatanisha pale wanapokoseana. Na wakati huo huo ilikuwa nyumba ya kufikia wale waliohama kutoka Makkah wasiokuwa na mahala wala watu wa kufikia kwao.

Anasema Dkt. Ahmad Fariyd katika kitabu chake 'Waqafaat Tarbawiyah':

"Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ulikuwa ni chuo kikuu kilichotoa Maswahaba shujaa waliofungua nchi nyingi pamoja na nyoyo nyingi, kwani Msikiti haukuwa mahali pa kuswali tu, bali ulikuwa mahali walipokuwa wakifunzwa Maswahaba hao (Radhiya Allaahu ‘anhum) namna ya kuondoa kiburi na namna ya kumnyenyekea Mola wao. Msikiti ulikuwa mfano wa kile chombo kinachopuliza moto unaosafisha uchafu wa chuma na kwa ajili hiyo uliweza kuzisafisha nyoyo za Maswahaba na kuwafanya wawe wacha Allaah, wawe na nyoyo za huruma wakihurumiana wao kwa wao, na wawe wenye elimu kupita watu wote na wawe na nyoyo thaabit mbele ya makafiri."

Allaah Anasema:

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ ۖ تَرَاهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا ۖ سِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِم مِّنْ أَثَرِ السُّجُودِ ۚ ذَٰلِكَ مَثَلُهُمْ فِي التَّوْرَاةِ ۚ وَمَثَلُهُمْ فِي الْإِنجِيلِ كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ فَآزَرَهُ فَاسْتَغْلَظَ فَاسْتَوَىٰ عَلَىٰ سُوقِهِ يُعْجِبُ الزُّرَّاعَ لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ ۗ وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِنْهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا ﴿٢٩﴾

Muhammad ni Mtume wa Allaah. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Allaah. Alama zao zi katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu. Huu ndio mfano wao katika Taurati. Na mfano wao katika Injili ni kama mmea ulio toa chipukizi lake, kisha ukalitia nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa juu ya ubuwa wake, ukawafurahisha wakulima, ili kuwakasirisha kwa ajili yao makafiri. Allaah Amewaahidi walioamini na wakatenda mema katika wao msamaha na ujira mkubwa.

Al-Fat-h - 29

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Akiwa Madiynah

Anasema Abu Bakr Al-Jazaairiy:

"Hakika ya miaka yote kumi na tatu aliyoishi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pale Makkah tokea alipopewa utume mpaka siku ile aliyohama kwenda Madiynah, yote ilikuwa ni maumivu na machozi na huzuni. Hakupata kufurahi hata kwa muda wa saa moja au kustarehe angalau kwa siku moja.

Na miaka kumi aloishi Madiynah, yote ilikuwa ni miaka ya Jihaad iliyofuatana. Hakupata hata siku moja kukaa bure wala kustarehe. Hata maisha, kwake yalikuwa magumu, kwani hakupata hata siku moja kushiba mkate au tende au kula vizuri mara mbili katika siku moja.

Naam, ingawaje kwa Mtume siku alizoishi Madiynah zilikuwa ni siku za kuchomoza nuru, lakini siku nyingi katika hizo zilikuwa ni za kuunguza."

 

Kuijenga Jamii Ya Madiynah

Baada ya ujenzi wa Msikiti kumalizika, Waislamu kwa mara ya mwanzo wakawa na mambo mawili muhimu, nayo ni kuwa pamoja, wakati hapo mwanzo wengine walikuwa Makkah wakisakwa na kufukuzwa na wengine wako Madiynah. Jambo la pili ni nguvu baada ya wote kuwepo Madiynah juu ya ardhi moja pamoja na kiongozi wao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Msikiti ukawa ndio makao yao makuu ya kukutana kwa ajili ya kufanya ibada, kupanga mipango na kupata elimu mbali mbali kutoka kwa Mtume wao (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyeletwa kuwafundisha kitabu na hekima na kujenga jamii ya Kiislamu itakayoishi kwa amani baina yao wenyewe kwa wenyewe na pia baina yao na wasiokuwa Waislamu.

Allaah Anasema:

هُوَ الَّذِي بَعَثَ فِي الأمِّيِّينَ رَسُولأ مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ

“Yeye ndiye Aliyempeleka Mtume kwenye watu wasiojua kusoma, awasomee Aya Zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima.”

Al-Jumua’h - 2

 

Na Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) ambao kule Makkah hawakuweza kuipata fursa kama hiyo, walikuwa wakimuelekea Mtume wao (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakimsikiliza kwa makini na kumfuata na kuyapokea mafudisho yake kwa masikio yaliyo wazi, huku imani yao ikizidi kuongezeka.

Allaah Anasema:

وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا

“Na wanapo somewa Aya Zake huwazidisha Imani”

Al-Anfaal – 2

 

Walikuwa wakiishi Madiynah watu wa aina tatu nao ni:

1.   Waislamu, watu wa Makkah na Madiynah.

2.   Washirikina, ambao ni baadhi ya watu wanaotokana na makabila ya Kiarabu, waliokuwa bado kusilimu, hawa hawakuwa na uadui mkubwa kwa Waislamu isipokuwa wachache, akiwemo kiongozi wao ‘Abdullaah bin Ubay bin Saluul aliyekuwa tayari anataka kuvalishwa taji la ufalme muda mdogo kabla ya Uislamu kuingia Madiynah, na baada ya kuingia Uislamu wengi wakampuuza na kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  jambo lililomkera sana, lakini  hatimaye aliingia katika Uislamu huku akificha uadui wake mkubwa dhidi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na wengi kati ya washirikina wa Madiynah hawakuchukua muda mrefu walisilimu.

3.   Mayahudi, nao walikuwa makabila matatu, Bani Qaynuqaa, Bani An-Nadhiyr na Bani Quraydhwah. Waliwasili katika nchi ya Hijaazi (Saudia hivi sasa) mwaka wa 578 kabla ya kuzaliwa Nabii ‘Iysa baada ya kupigwa vibaya na kuteswa na Warumi na Bukhtinassar, na Mayahudi hawa ambao asili yao ni Waibrani (Hebrews), walipowasili nchi ya Hijaazi (Saudia hivi sasa) walichanganyika na Waarabu waliowapokea vizuri, wakajaribu kugeuza tabia zao na kujifanya kama  ni katika wao. Walikuwa wafanya biashara maarufu pale Madiynah wakijishughulisha na biashara za tende na nafaka na nguo, lakini walikuwa maarufu kwa kupenda kula ribaa. Wakiwakopesha mali Waarabu kwa njia ya ribaa wapate kuwadhoofisha wawe siku zote chini ya amri yao katika mahitaji ya kimaisha. Walikuwa pia watu wa fitna na kupanga mipango ya kugombanisha makabila ya Kiarabu kwa kuwafitinisha bila wenyewe kujua, na vita vikali vinapozuka baina ya Waarabu, wao huwapa mikopo mikubwa kwa ajili ya kununua silaha na mahitaji ya vita kisha hukaa mbali kama si wao wakifurahia mafanikio yao ya kuwafarikisha Waarabu wapate kuendelea kuwepo na ya kuiendeleza riba.

 

Bila shaka kuja kwa Uislamu, Dini inayokataza kuua bila ya sababu, kula ribaa, kudhulumu, kula mali ya haramu na kupigana vita wenyewe kwa wenyewe, Dini yenye kuwaita watu katika mwenendo na tabia njema na kuwaunganisha watu wote, Waarabu na Wasiokuwa Waarabu kuwa wote ni sawa mbele ya Allaah, jambo hilo halikuwapendeza Mayahudi waliokuwa wakijiona kuwa wao ni Taifa bora kupita walimwengu wote.

Haya kwa ujumla ni matatizo yaliyomkabili Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika kujenga Taifa la mwanzo la Kiislamu akiwa kama ni Mtume, Kiongozi na Imaam.

Mengi ya matatizo yaliondoka baada ya watu wa Madiynah kuuona upole na Rahma aliyokuwa nayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na hekima yake katika kutatua matatizo yao, haukupita muda mrefu karibu Waarabu wote wa Madiynah waliingia katika Dini ya Uislamu.

 

Kufungisha Undugu

Ili hali ya maisha na jamii iweze kustawi pale Madiynah na kuondoa uwezekano wa kutokea machafuko na kuendeana kinyume na Mayahudi, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akachukua hatua mbili muhimu sana, nazo ni kuwaunganisha undugu watu wa Makkah na wa Madiynah na kuweka mkataba wa masikilizano baina ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwafungisha undugu Muhaajirin (Watu wa Makkah) na Answaar (Watu wa Madiynah) ili wapate kushikamana zaidi na kuwa na nguvu inayoweza kujilinda wakati inapohitajika, kuuzatiti ushirikiano baina yao na ili kuwapoza nyoyo Muhaajirin walioihama nchi yao na kuacha watu wao na mali zao na nyumba zao kwa ajili ya Uislamu kwa kupata ndugu wepya katika imani.

Aliwafungisha wapate kuishi kindugu na wenzi wao watu wa Madiynah na kujimakinisha vizuri kwa ajili ya kuujenga umoja wao na kuisimamisha dola yao na kuipigania Dini yao kwa roho moja na nguvu moja.

Allaah Anasema:

وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِن قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ ولا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِّمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ 

“Na wale waliofanya maskani yao hapa (yaani Madiynah) na wakautakasa Uislamu (wao barabara) kabla ya kuja hao (Muhajiriyn huko Madiynah) na wakawapenda hao waliohamia kwao, wala hawapati (hawaoni) dhiki nyoyoni mwao kwa hayo waliyopewa (hao Muhajiriyn), na wanawapendelea kuliko nafsi zao ingawa wenyewe wana hali ndogo.”

Al-Hashr - 9

 

Aliwafungisha undugu watu tisini. Wawili wawili, mmoja kutoka Muhaajiriyn na mwengine kutoka Answaar. Arubaini na tano watu wa Makkah na arubaini na tano wa Madiynah.

Zipo hitilafu katika riwaya kuhusu undugu huo uliofungwa katika nyumba ya Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kama ulikuwa baada ya ujenzi wa Msikiti au kabla yake.

Anasema Shaykh Ahmad Fariyd kuwa Dkt. Akram Dhiyaa Al-‘Umary ameandika katika kitabu chake ’Al-Mujtama’a al-Madani’: “Masharti ya undugu yalikuwa ni katika kunasihiana, kutembeleana, kupendana, kuwa pamoja na kusaidiana kwa hali na mali katika shida mbali mbali za kimaisha na hata kurithiana kwa ndugu hao wawili tu pasina kuwaingiza ndugu zao kwa damu.”

Waqafaat Tarbawiyah Uk.167

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa watu wa Madiynah walisema: “Tutagawa mitende yetu (nusu kwa nusu) baina yetu na ndugu zetu: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hapana.” Wakasema: “(Basi) Mtatusaidia kutia maji na kuisimamia kisha tutagawana mazao.” Wakasema: “Tumesikia na kutii.”

Al-Bukhaariy.

 

Kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Alipowasili ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimfungisha undugu na Sa’ad bin Ar-Rabiy’ah Al-Answaariy, akamtaka wagawane nusu kwa nusu wake zake na mali yake, akasema ‘Abdur-Rahmaan: “Allaah Akubariki katika wake zako na mali yako. Nionyeshe mahali soko lilipo.” Akafanya biashara ya maziwa na samli, na baada ya kupita siku chache Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona njiani akiwa na alama ya manjano nguoni mwake (amepaka mafuta mazuri), akamuuliza: “Umeipata wapi?” Akasema: “Nimeoa mwanamke wa Answaar (watu wa Madiynah).” Akamuuliza: “Umempa mahari kiasi gani?” Akasema: “Dhahabu yenye uzito wa kiasi cha kokwa ya tende.” Na tafsiri ya neno ‘Nuwat’ ilotumika katika hadithi hii inaleta maana pia kuwa ni (Kiasi cha thamani ya Dirham tatu za dhahabu). Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: “Fanya waliymah (chakula cha harusi) uchinje angalau mbuzi mdogo.”

Al-Bukhaariy mlango wa kufungisha undugu, na At-Tirmidhiy na wengine

 

Mkataba Wa Maridhiano Baina Ya Waislamu

Ili dola mpya iweze kusimama juu ya msingi madhubuti, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya jambo lingine muhimu sana likiwa ni dalili kuwa alikuwa Kiongozi mwenye hekima na umahiri wa hali ya juu.

 

Baada ya kumaliza shughuli ya kufungisha undugu baina ya watu wa Makkah na wa Madiynah, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliandika mikataba miwili. Mmoja wa Maridhiano baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe, na mwengine baina ya Waislamu na Mayahudi, ili uwe dira ya kuiongoza dola hii mpya na kujenga uhusiano mwema baina ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu, katika wakati ambao ulimwengu haukuwa ukijua isipokuwa kuuana na kutekana na kuuzana.

 

Yafuatayo ni mafungu muhimu yaliyokuwemo ndani ya mkataba huo:

Huu ni mkataba ulioandikwa na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baina ya Waislamu, Maquraysh na watu wa Yathrib (Madiynah) pamoja na walioungana nao na kupigana jihada pamoja nao:

1.   Wao ni umma mmoja mbali na watu wengine.

2.  Muhaajiriyn wa Quraysh watashirikiana wao kwa wao katika kulipa fidia na katika kuwatendea wema wafungwa wao. Makabila yote ya Answaar (Watu wa Madiynah) watarudi kuwa pamoja kama walivyokuwa hapo mwanzo, na kila kabila litashirikiana wao kwa wao katika kulipa fidia ya kumkomboa mfungwa wake.

3.   Waislamu wasimuache mwenzao akiwa na shida au dhiki bila ya kumsaidia au kumkomboa.

4.   Waislamu wacha Allaah wote kwa pamoja watashirikiana katika kumpiga vita mwenye kuwashambulia Waislamu au mwenye kueneza fitna baina ya Waislamu au haini (msaliti), hata kama ni mwanawe.

5.   Waislamu wasiuane wenyewe kwa wenyewe kwa ajili ya kafiri, wala wasiungane na kafiri dhidi ya Muislamu.

6.   Himaya ya Allaah ni moja na inamuenea kila mmoja hata aliye mnyonge kupita Waislamu wote.

7.   Atakeyetufuata miongoni mwa Mayahudi atalindwa na kusaidiwa, wala hatofanyiwa uadui.

8.   Usalama wa Waislamu ni mmoja. Pasifanyike sulhu tofauti wakati Waislamu wanapigana Jihaad kwa ajili ya Allaah, Masharti yawe yanayokubalika na wote na yenye uadilifu baina yao.

9.   Haijuzu kwa Muislamu kumnusuru mzushi au kumpa ulinzi, na atakayemnusuru au kumpa ulinzi basi Laana ya Allaah na ghadhabu Zake zitakuwa juu yake siku ya Qiyaamah na wala hawatapa ulinzi wowote.

10. Nanyi mtakapokhitalifiana katika lolote, basi marudio yenu yawe kwa Allaah Azzza wa Jalla (Qur-aan) na kwa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) (Mafundisho yake).

 

Mkataba Na Mayahudi

Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliandika mkataba baina ya Waislamu na Mayahudi, na yafuatayo ni baadhi ya mafungu muhimu yaliyokuwemo ndani yake:

1.   Mayahudi wa kabila la Bani ‘Awf ni Taifa moja pamoja na Waislamu. Mayahudi wana Dini yao na Waislamu wana Dini yao.

2.   Mayahudi watakuwa na jukumu lao wenyewe katika matumizi yao, na Waislamu watakuwa na matumizi yao.

3.   Waliotia sahihi mkataba huu wanawajibika kusaidiana watakaposhambuliwa na kundi kutoka nje yao.

4.   Pande zote mbili zinawajibika kushauriana na kunasihiana. Uhusiano uwe kwa wema na usiwe katika maovu.

5.   Pande zote zisitendeane maovu.

6.   Aliyedhulimiwa asaidiwe.

7.   Mayahudi watashirikiana katika malipo ya vita watakapokuwa wanapigana upande mmoja na Waislamu.

8.   Mji wa Madiynah utakuwa mtukufu kwa wote waliotia sahihi mkataba huu.

9.  Pakitokea kutokuelewana baina ya waliotia sahihi mkataba huu, marejeo yake yatakuwa kwa Allaah na kwa Muhammad Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

10. Waliotia sahihi mkataba wasifanye biashara na Maquraysh na wanaowaunga mkono.

11. Wote watashirikiana katika kuulinda mji wa Madiynah kama utashambuliwa kutoka nje.

12. Mkataba huu usiwe kizuizi kwa upande wowote kutafuta haki zake kisheria.

 

Anasema Al-Mubaarakpuri:

“Baada ya mkataba huu kukamilika, mji wa Madiynah na vitongoji vyake ungeweza kuitwa kama tunavyoita hivi sasa kuwa; Ni Dola iliyojengeka kwa mkataba na makubaliano na maridhiano, na mji mkuu wake ukawa Madiynah mjini, na Rais wake, kama itakuwa sawa kuitwa hivi; ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na wenye nguvu na walio wengi katika dola hiyo ni Waislamu, na kwa ajili hiyo mji wa Madiynah ukawa hakika ni mji mkuu wa Waislamu.”[56]

 

Kusilimu Kwa ‘Abdullaah Bin Salaam (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Anasema Imaam Al-Bukhaariy katika 'Kitabu cha Mitume' kuwa; mara baada ya kupata habari za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwasili Madiynah, ‘Abdullaah bin Salaam (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikwenda kwake na kumuuliza masuali ambayo hawezi kuyajibu isipokuwa Mtume aliyeletwa na Allaah. Na baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuyajibu maswali yake ‘Abdullaah aliyekuwa ‘aalim mkubwa katika Maulamaa wa Kiyahudi alisema:

"Nashuhudia kuwa hapana anayepaswa kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba wewe ni Mtume wa Allaah na kwamba uliyokuja nayo ni haki. Ewe Mtume wa Allaah, Mayahudi ni watu waongo, wanajua kuwa mimi ni bwana wao na mwana wa bwana wao na wanajua pia kuwa mimi ni ‘aalim wao na mwana wa ‘aalim wao, kwa hivyo nakuomba (uniache nijifiche, kisha) uwaite na uwaulize juu yangu kabla ya kuwajulisha juu ya kusilimu kwangu, kwani wakijua kuwa nimesilimu watasema juu yangu yale nisiyokuwa nayo".

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaita Mayahudi, na walipohudhuria akawaambia:

"Enyi Mayahudi! Adhabu kali itakufikieni, mcheni Allaah, Naapa kwa yule ambaye hapana anayepaswa kuabudiwa isipokuwa Yeye, kuwa mnajua vizuri kwamba mimi ni Mtume wa kweli wa Allaah na kwamba niliyokuja nayo ni haki, kwa hivyo ingieni katika Dini ya Kiislamu".

Wakasema mara tatu:

"Sisi hatujui".

Kisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza:

"Ana daraja gani kwenu ‘Abdullaah bin Salaam?"

Wakasema:

"Yule ni bwana wetu na mwana wa bwana wetu, na ‘aalim kutupita sote na mwana wa ‘aalim kutupita sote".

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza:

"Mnaonaje akisilimu?"

Wakasema:

"Haiwezekani hata siku moja akasilimu".

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza hivyo mara tatu, kisha akasema:

"Ewe ‘Abdullaah bin Salaam, watokee".

Akawatokea na kusema:

"Enyi Mayahudi, mcheni Allaah kwani naapa kwa yule ambaye hapana anayepaswa kuabudiwa isipokuwa Yeye, mnajua vizuri kuwa huyu ni Mtume wa Allaah na kwamba amekuja na haki".

Wakasema:

"Muongo! wewe si bwana wetu wala si ‘aalim wetu".

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaamrisha watolewe nje.

Al-Bukhaariy

 

Kujenga Mwenendo Na Tabia Njema

Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaanza kazi kubwa ya kuwafundisha Waislamu waliojikuta katika hali hii mpya ya kuwa wenye nguvu na wako pamoja, akaanza kuwafunza mwenendo na Tabia njema na huruma kama ni msingi wa mafundisho ya Dini.

Mtu mmoja anapomuuliza: “Uislamu upi ulio bora?”

Alikuwa akisema: “Kuwalisha watu, na kumtolea salam unayemjua na usiyemjua.”[57]

Na alikuwa akisema: “Haingii peponi asiyemuepusha jirani yake na shari zake.”[58]

Alisema pia: “Muislamu (wa kweli) ni yule atakayewaepusha Waislamu wenzake na ulimi wake.”[59]

Akasema pia: “Hawi Muislamu wa kweli mpaka awe mwenye kumpendelea ndugu yake kila anachokipendelea nafsi yake.”[60]

Alisema pia: “Waislamu ni mfano wa majengo, kila mmoja linalizuia jingine lisianguke.”[61]

Na akasema: “Msichukiane, wala msihusudiane, wala msiendeane kinyume, na kuweni waja wa Allaah nyote ndugu, na si halali kwa Muislamu asimsemeshe ndugu yake zaidi ya siku tatu.”[62]

Alikuwa akiwafundisha pia kuwa: “Muislamu ni ndugu ya Muislamu, asimdhulumu, asimuendee kinyume, na mwenye kumsaidia ndugu yake na Allaah Atamsaidia, na atakayemuondolea Muislamu dhiki zake na Allaah Atamuondolea katika dhiki zake za siku ya Qiyaamah, na atakayemsitiri Muislamu na Allaah Atamsitiri siku ya Qiyaamah.”[63]

Na akisema: “Mukimrehemu aliye juu ya ardhi, Atakurehemuni aliye mbinguni.”[64]

Akasema pia: “Hawi Muislamu wa kweli mwenye kushiba wakati jirani yake ana njaa.”

Al-Bayhaqiy

 

Na akasema: “Kumtukana Muislamu ni dhambi kubwa na kupigana naye vita ni kufru.”

Al-Bukhaariy

 

Alikuwa akiwafundisha kuwa kuondoa udhia njiani, (miba, vigae, uchafu nk.) ni sawa na kutoa sadaka, na akasema kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya Imani.

Alikuwa akiwahimiza sana katika kuwasaidia wasiojiweza kwa chakula na nguo nk.

Alikuwa akisema: “Muislamu yeyote atakayemvisha nguo Muislamu asiyekuwa na nguo na Allaah Atamvisha katika mavazi ya kijani ya Peponi. Na Muislamu yeyote atakayemlisha Muislamu mwenzake mwenye njaa, na Allaah Atamlisha katika vyakula vya Peponi. Na Muislamu yeyote atakayemnywesha maji Muislamu mwenye kiu, na Allaah Atamnywesha katika vinywaji vizuri vya Peponi vilivyofungwa kwa vizibo madhubuti.”

Abu Daawuud na At-Tirmidhiy

 

Alikuwa pia akiwaambia: “Jiepusheni na moto hata kwa (kutoa sadaka) kwa nusu ya tende, na kama hamkupata basi kwa neno jema.”

Al-Bukhaariy

 

Alikuwa kila tendo jema akiliunganisha na Wahyi kutoka mbinguni akiwafundisha namna gani Allaah Anavyopenda matendo mema.

Alikuwa akiwaambia: “Nimeletwa ili kukamilisha mwenendo na tabia njema.”

 

Kwa mafundisho ya namna hii alifanikiwa kuingiza ndani ya nyoyo zao, ucha Allaah na mapenzi ya hali ya juu baina yao, na kuingiza katika jamii tabia njema, na akaweza kuwafanya Waislamu wawe wenye kukimbilia kufanya mema na kuwasaidia wasiojiweza wakawa wenye kujitegemea wenyewe kwa wenyewe kindugu, kiukoo, kijamii na wote kwa pamoja kama Waislamu, wakaweza kuwa umati bora kuliko umati wowote uliowahi kuteremshiwa watu.

 

Mwaka Wa Mwanzo Wa Hijra

Yafuatayo ni baadhi ya matukio mbali mbali yaliyotokea katika mwaka wa mwanzo wa Hijra:

1- Katika mwaka wa mwanzo tokea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhamia Madiynah, Waislamu waliruhusiwa kupigana vita, wakati hapo mwanzo hawakuwa na ruhusa hiyo.

Waislamu waliokuwa wakipigwa na kuteswa na kufukuzwa na kunyang’anywa mali zao kutokana na udhaifu waliokuwa nao huko Makkah, walistahamili miaka mingi mateso hayo, lakini hivi sasa baada ya kuhamia Madiynah na kuungana na ndugu zao wa hapo, wakawa na nguvu za kutosha za kuweza kujilinda, na kuurudisha uadui wa Quraysh, walipewa ruhusa na Allaah ya kupigana.

Allaah Amesema:

أذِنَ لِلَّذِينَ يُقَاتَلُونَ بِأَنَّهُمْ ظُلِمُوا ۚ وَإِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ نَصْرِهِمْ لَقَدِيرٌ

“Wameruhusiwa kupigana wale wanao pigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa - na kwa yakini Allaah ni Muweza wa kuwasaidia.”

Al-Hajj – 39

 

2-  Katika mwaka huo alifariki dunia As’ad bin Ziraarah (Radhiya Allaahu ‘anhu), na huyu alikuwa miongoni mwa viongozi kumi na mbili waliochaguliwa baada ya Fungamano la ‘Aqabah la pili, naye ni mtu wa mwanzo kufungamana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) siku ile.

3-  Alifariki dunia katika mwaka wa mwanzo pia ‘Uthmaan bin Madh’uun (Radhiya Allaahu ‘anhu), na huyu ni ndugu wa kunyonya wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye alikuwa mtu wa mwanzo kuzikwa katika makaburi ya Al-Baqiy’.

4-  Na katika washirikina wa Makkah aliyefariki mwaka ule alikuwa Al-Waliyd bin Mughiyrah na huyu ni baba yake Khaalid bin Waliyd.

5-  Alizaliwa katika mwaka huu mtoto wa mwanzo wa Kiislamu tokea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhamia Madiynah, naye ni ‘Abdullaah bin Az-Zubayr, aliyekuwa mchaji Allaah na shujaa na mama yake ni Asmaa binti Abi Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhum). Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mtu wa mwanzo kumlisha tende baada ya kuilainisha kwa kinywa chake kitukufu.

6-  Katika watu wa Madiynah (Answaar) waliozaliwa mwaka huu An-Nu’umaan bin Bashiyr (Radhiya Allaahu ‘anhu).

7-  Na katika mwaka huu Waislamu walitakiwa waelekee Makkah badala ya Baytul Maqdis wakati wa kuswali.

 

Mwaka Wa Pili Wa Hijra

Ndani ya mwezi wa Sha’abaan mwaka wa pili wa Hijra Allaah Aliteremsha amri ya kuwajibisha kufunga mwezi wa Ramadhaan, wakati hapo mwanzo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifunga siku tatu katika kila mwezi. Na katika mwaka huu pia ilifaridhishwa Zakaah ya mali na Zakaatul Fitwr kwa ajili ya kuwasidia ndugu zao walio maskini na mafakiri na wasiojiweza.

 

Anasema Imaam Muslim katika mlango wa Fadhila za Sa’ad bin Abi Waqaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa; Usiku mmoja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikawia kulala kwa sababu ya kuwapokea wageni waliokuja Madiynah, akasema: “Nataka mtu mwema katika Swahaba zangu anilinde usiku huu.” Anasema: “Tulipokuwa katika hali ile tukasikia sauti ya silaha, akauliza: “Nani huyu?” Akasema: “Mimi Sa’ad bin Abi Waqaas.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza: “Kipi kilichokuleta?” Akasema: “Nilikuogopea nikaona bora nije kukulinda.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea dua kisha akalala.”

Muslim 2/280

 

Anasema Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha): “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akilindwa nyakati za usiku mpaka ilipoteremsha aya isemayo:

وَاللَّـهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ

Na Allaah Atakulinda na watu

Al-Maaidah – 67

Baada ya kuteremka aya hii, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akautoa uso wake nje ya hema na kuwaambia Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum), “Enyi watu, nendeni zenu, kwa sababu Allaah keshanikinga.

 

Barua Ya Quraysh Kwa ‘Abdullaah Bin Ubay

Washirikina wa Makkah hawakuwaacha Waislamu waishi kwa amani pale Madiynah, bali chuki iliwazidi na nyoyo zao kuungulika, na jambo la mwanzo walilofanya ni kumuandikia barua ‘Abdullaah bin Ubay bin Saluul wakimuambia: “Nyinyi munampa ulinzi sahibu yetu, na sisi tunaapa kuwa utampiga vita huyo na kumtoa, ama sivyo tutakuja sisi wenyewe, tena sote kwa pamoja kuwaua askari wenu na kuwateka wanawake wenu.”

Abu Daawuud

 

Baada ya kuipata barua hii ‘Abdullaah bin Saluul aliondoka moja kwa moja akifuatana na washirikina wenzake watu wa Madiynah waliokuwa bado hawajasilimu, kwenda kupambana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokutana nao akawaambia: “Inaelekea vitisho vya Quraysh vimekutisheni sana. Munakata kupigana vita na watoto wenu na ndugu zenu?” Kusikia hivyo wakaondoka na kila mmoja akaenda njia yake.

Al-Bukhaariy

 

Vita Vya Badr

Badr ni mji ulio kiasi cha Kilomita mia na hamsini mbali na Madiynah, na mahali hapo hapakuwa na chochote isipokuwa bonde tu na kisima kilichokuwa milki ya mtu mmoja aitwae Badr, na kwa ajili hiyo mahala hapo pakaitwa ‘Badr’, na vita vilivyopiganwa hapo vikaitwa vita vya Badr.

Vita hivyo vilitokea asubuhi ya siku ya Ijumaa, Ramadhaan ya kumi na saba mwaka wa pili baada ya Hijra. (baada ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhamia Madiynah).

 

Sababu Za Vita

Chanzo cha vita hivi kilikuwa ni msafara wa biashara wa makafiri ukiongozwa na Abu Sufyaan uliokuwa ukitoka nchi ya Shaam ukirudi Makkah ukiwa na watu wasiozidi arubaini. Msafara ulikuwa umebeba mali nyingi sana ya watu wa Makkah, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaona hii ni fursa nzuri ya kuipiga dola hiyo ya kikafiri kiuchumi, kijeshi na kisiasa, na pia kulipiza kisasi, hasa kwa vile Waislamu walipohama Makkah kwenda Madiynah, Makafiri waliwalazimisha kuziacha mali zao zote huko, na kuondoka bila chochote isipokuwa nguo na mnyama wa kumpanda, bali wengine walinyang’anywa hata wanyama wao, ikawabidi kutembea kwa miguu hadi Madiynah na wengine waliviziwa njiani na kuuliwa.

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia Waislamu:

“Msafara huu wa Maquraysh umejaa mali zao, uendeeni, huenda Allaah Akatulipa (haki zetu walizotunyang’anya) kwa kutuwezesha kuuteka.”

 

Jeshi Dogo

Si watu wengi waliojitolea kwenda, na hii ni kwa sababu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  hakutilia mkazo sana kutoka huko, hakumlazimisha mtu kwenda naye na wala hakumlaumu yeyote asiyetoka pamoja naye, bali alimwacha kila mmoja ajiamulie mwenyewe ikiwa anataka kwenda au hataki kwa sababu kutoka kwao kulikuwa kuuteka msafara mdogo tu wa Abu Sufyaan. Na kwa ajili hiyo Maswahaba wachache walimfuata.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliondoka akiwa na watu wapatao mia tatu na kidogo tu hivi. Inasemekana walikuwa mia tatu na kumi na tatu au kumi na nne na riwaya nyengine zinasema kuwa walikuwa mia tatu na kumi na saba. Themanini na sita kati yao ni Muhajiriyn, na mia mbili thelathini na moja ni watu wa pale pale Madiynah.

Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhu) hawakujua kuwa msafara huu utageuka kuwa ni moja katika mapambano makubwa baina ya Haki na Batwil, walidhania kuwa yatakuwa yale mapambano ya kawaida baina ya Makundi ya wapiganaji wa Kiislamu na misafara midogo midogo ya makafiri iliyokwisha tokea mara nyingi kabla ya hapo.

Waliondoka wakiwa na farasi wawili tu, mmoja wa Az-Zubayr bin ‘Awwaam na mwengine wa Miqdaqd bin Al-Aswad Al-Kindiy (Radhiya Allaahu ‘anhum), na walikuwa na ngamia sabini wakipokezana katika kuwapanda.

 

Jeshi Linaondoka Kuelekea Badr

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaondoka Madiynah pamoja na Swahaba zake kuufuatia msafara huo wa Abu Sufyan, akamchagua Ibn Ummi Maktuum (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa gavana wa Madiynah badala yake, lakini alipofika nje kidogo ya Madiynah, mahali panapoitwa Ar-Rawha, akamrudisha Swahaba mmoja anayeita Abu Lubaabah (Radhiya Allaahu ‘anhu), na kumtaka yeye awe gavana badala ya Ibn Ummi Maktuum (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Katika msafara huo, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamchagua Musw’ab bin ‘Umayr  (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa ni mshika bendera, na bendera yenyewe ilikuwa ya rangi nyeupe.

Akaligawa jeshi makundi mawili:

1.   Kikosi cha Muhajiriyn (watu wa Makkah) na akampa bendera yao ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu).

2.   Kikosi cha watu wa Madiynah, na akampa bendera yao Sa’ad bin Mu’aadh (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaondoka na jeshi lake hilo akiifuata njia ya Makkah, na alipofika mji uanoitwa Ar-Rawha akapumzika, na baada ya kupumzika akaondoka kuelekea mji wa Badr akiiacha njia ya Makkah kushotoni kwake na kuendelea na safari mpaka alipolifikia bonde la Rahiqan na baada ya kuendelea mbele kidogo, akawatuma Maswahaba Basis bin ‘Umar na Uday bin Az-Zaghbah (Radhiya Allaahu ‘anhum) watangulie kwa ajili ya kupeleleza habari za msafara waliokusudia kuuteka.

 

Msafara Wa Abu Sufyaan

Abu Sufyaan aliyekuwa kiongozi wa msafara wa biashara ya makafiri wa Makkah, alikuwa mtu mwenye kuchukua hadhari sana. Alijua kuwa njia ya Makkah ina hatari nyingi, na kwa ajili hiyo kila mara alikuwa akitanguliza wapelelezi wamletee habari za mbele ya safari, na wakati huo huo alikuwa akimuuliza kila anayekutana naye njiani iwapo huko alikotoka ameona chochote kile kisichokuwa cha kawaida.

Katika kuuliza uliza kwake akamuuliza mtu mmoja anayeitwa Majd bin ‘Amru iwapo ameona jeshi kutoka mji wa Madiynah, akasema:

“Mimi sikuona majeshi, lakini niliona kundi kubwa la watu waliopumzisha ngamia wao mahali hapa.”

 

Abu Sufyaan akaenda kupafanyia uchunguzi mahali pale alipoambiwa kuwa watu walipumzisha ngamia wao, na baada ya kuchambua kinyesi cha ngamia waliopumzishwa mahali hapo na kuona kokwa za tende ndani yake, akasema:

“Kwa vile choo chao kimejaa kokwa za tende, hapana shaka yeyote kuwa hawa ni ngamia wa watu wa Madiynah.”

 

Akajua kuwa anaviziwa, akageuza njia na kumtuma mtu mmoja aitwae Dhamdham bin ‘Amru Al-Ghafariy atangulie mbio sana, ende kuwazindua watu wa Makkah juu ya hatari inayoukabili msafara wao wenye vitu vya thamani kubwa sana.

Watu wa Makkah waliposikia hayo, wakasema:

“Muhammad anadhania kuwa atauteka msafara huu kwa urahisi kama alivyouteka msafara wa ‘Amru bin Al Hadhramiy? Haitokuwa hivyo kabisa! WaLlaahi atakiona chake Muhammad safari hii.”

 

Jeshi La Quraysh

Maquraysh mara baada ya kujulishwa juu ya hatari hiyo, wakakusanya jeshi la watu wapatao elfu moja na mia tatu, farasi wapatao mia moja na ngamia wengi sana, wakaondoka wakiongozwa na Abu Jahl bin Hishaam pamoja na vigogo vya Maquraysh.

Walisafiri kwa kasi kubwa sana kuelekea kaskazini mahali uliopo mji wa Badr. Walipofika mji uitwao Al Juhufa, wakapata salam kutoka kwa Abu Sufyaan kuwa; Msafara wake umekwishasalimika na hatari ya kutekwa, na akawataka warudi Makkah, na hii ni kwa sababu mara Abu Sufyan alipotambua kuwa anafuatwa, alibadilisha njia na kupita njia ya pwani pwani badala ya kupitia njia ya mji wa Badr.

Abu Jahl akasema:

“WaLlaahi haturudi, mpaka tufike Badr, tukae hapo siku tatu, tuchinje wanyama wetu, tunywe pombe yetu na waimbaji waimbe mpaka habari zetu ziwafikie waarabu wote ili wapate kutujua ni nani sisi na ili watuogope.”

 

Jeshi La Waislamu

Waislamu walipata habari za kuwaponyoka kwa msafara wa Abu Sufyaan na wakati huo huo wakapata habari za jeshi kubwa la watu wa Makkah lililowakabili lililoazimia kwenda mji wa Badr.

Baadhi yao wakaingiwa na hofu, na wengine wakatoa wazo la kurudi Madiynah kwa sababu walikuwa wachache, na hawana silaha za kutosha kwani hawakutoka kivita.

Juu ya yote hayo iliwabidi kulikabili tatizo hilo kwa ushujaa mkubwa kabisa kwani iwapo watakimbia na kuliacha jeshi la makafiri litambe hapo Badr, mji ulio katika eneo la karibu na mji wa Madiynah, huko kutawapa nguvu na kichwa kikubwa makafiri, jambo ambalo halitakuwa na mwisho mwema. Wakati huo huo haiba ya jeshi la Waislamu itaondoka.

 

Mwanachuoni mkubwa Al-Mubaarakpuri anasema katika kitabu chake Ar-Rahiyqul Makhtuum:

“Jeshi la Waislamu lingekuwa mfano wa mwili bila ya roho, na makafiri wangepata moyo wa kujaribu kuushambulia mji wao wa Madiynah bila ya hofu yoyote.”

Allaah Anasema:

كَمَا أَخْرَجَكَ رَبُّكَ مِن بَيْتِكَ بِالْحَقِّ وَإِنَّ فَرِيقًا مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ لَكَارِهُونَ ﴿٥﴾ يُجَادِلُونَكَ فِي الْحَقِّ بَعْدَ مَا تَبَيَّنَ كَأَنَّمَا يُسَاقُونَ إِلَى الْمَوْتِ وَهُمْ يَنظُرُونَ ﴿٦﴾ وَإِذْ يَعِدُكُمُ اللَّـهُ إِحْدَى الطَّائِفَتَيْنِ أَنَّهَا لَكُمْ وَتَوَدُّونَ أَنَّ غَيْرَ ذَاتِ الشَّوْكَةِ تَكُونُ لَكُمْ وَيُرِيدُ اللَّـهُ أَن يُحِقَّ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ وَيَقْطَعَ دَابِرَ الْكَافِرِينَ ﴿٧﴾ لِيُحِقَّ الْحَقَّ وَيُبْطِلَ الْبَاطِلَ وَلَوْ كَرِهَ الْمُجْرِمُونَ

“(Atakunusuru) kama alivyokutoa Mola wako katika nyumba yako kwa haki, na kundi moja la walioamini halipendi (utoke).

Wakabishana nawe katika haki baada ya kubainika kwenda huko kama kwamba wanasukumwa katika mauti na huku wanaona.

Na Allaah Alipo kuahidini kuwa moja katika makundi mawili ni lenu. Nanyi mkapenda lisilo na nguvu ndio liwe lenu; na Allaah anapenda ahakikishe Haki kwa maneno yake, na aikate mizizi ya makafiri.

Ili ahakikishe Haki na auvunje upotovu na wangechukia wakosefu.”

Al-Anfaal – 5-8

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Aitisha Mkutano

Kutokana na mabadiliko haya ya ghafla na ya hatari, ilimbidi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aitishe mkutano wa mashauriano na wakuu wa jeshi lake.

Aliinuka Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akatoa khutbah nzuri ya kumuunga mkono Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu kulazimika kwao kupigana na makafiri.

Kisha akainuka ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kutoa khotbah nzuri vile vile.

Kisha akainuka Al-Miqdaad bin ‘Amru (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:

“Ewe Mtume wa Allaah, nenda kama Atakavyokuonyesha Allaah, na sisi tuko nyuma yako. WaLlaahi hatukuambii kama walivyomuambia wana wa Israili Mtume wao Muusa; ‘Nenda wewe na Mola wako mkapigane vita sisi tutakaa hapa (tunangoja)’, bali tunakwambia; ‘Nenda wewe na Mola wako ukapigane na sisi pamoja nanyi tutapigana …”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

“Vyema”

Kisha akamuombea dua.

 

Watatu hawa wote walikuwa katika Muhajiriyn ‘Watu wa Makkah’, ambao ni wachache katika jeshi hilo, na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akapenda kujua rai ya viongozi wa watu wa Madiynah waliokuwa wengi katika jeshi hilo, akasema:

“Nipeni shauri lenu enyi watu.”

Akikusudia watu wa Madiynah. Sa’ad bin Mu’aadh (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa mmoja wa viongozi wa watu wa Madiynah akatambua hayo, akasema:

“WaLlaahi kama kwamba unatukusudia sisi ewe Mtume wa Allaah?”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

“Ndiyo.”

Sa’ad (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:

“Sisi tumekuamini na kukusadiki, na tukashuhudia kuwa uliyokuja nayo ndiyo haki, na tukakupa ahadi zetu na neno letu kuwa tutakusikiliza na kukutii, kwa hivyo endelea tu kama unavyotaka kwani WaLlaahi kama utatutaka tuivuke bahari hii, ukaivuka, basi tutaivuka pamoja nawe na hapana hata mmoja kati yetu atakayebaki nyuma, sisi hatuogopi kupambana na adui kesho, sisi ni watu wenye kusubiri katika vita na wakweli katika mapambano, na InshaAllaah Allaah Atakuonyesha ndani yetu yale yatakayokufurahisha macho yako, kwa hivyo tuongoze kwa baraka za Allaah.”

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifurahishwa sana na maneno ya Sa’ad (Radhiya Allaahu ‘anhu), akasema:

“Nendeni na nakupeni bishara njema, Allaah Ameniahidi moja wapo ya makundi mawili. WaLlaahi kama kwamba ninaona wapi wataanguka kila mmoja kati ya maadui.”

 

Majeshi Ya Kiislamu Yanafanya Uchunguzi

Walipowasili mahali panapoitwa Addiya, karibu na Badr, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Sahibu yake wa pangoni Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu), walitoka na kuanza kufanya uchunguzi nje ya kambi yao, na katika kutembea kwao walikutana na mzee mmoja wa Kiarabu wakamuuliza juu ya habari za jeshi la Maquraysh na juu ya habari za jeshi la Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ili asiweze kutambua ni katika kundi gani wao.

Yule mtu akawaambia:

“Kabla sijakujibuni, niambieni kwanza nyinyi mnatokea wapi?”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

“Ukituambia na sisi tutakuambia.”

Yule mtu akasema:

“Nimesikia kuwa jeshi la Muhammad na Sahibu zake lilitoka siku kadha wa kadhaa, ikiwa habari hizo ni sahihi, basi leo watakuwa washafika mahali kadhaa.”

Akapataja mahali lilipo jeshi la watu wa Madiynah.

“Na nimesikia kuwa Maquraysh wametoka siku kadhaa wa kadhaa, na ikiwa maneno niliyoambiwa ni kweli, basi leo watakuwa washafika mahali kadhaa wa kadhaa.”

Akapataja mahali lilipo jeshi la Maquraysh.

Baada ya kumaliza kusema, akawauliza:

“Nyinyi mnatokea wapi?”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia:

“Sisi tunatokana na maji.”

Kisha akaondoka.

Yule mtu akawa anajiuliza:

“Hawa wanatoka katika maji ya Iraq au maji gani?”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakusema uongo, kwani viumbe vyote vinatokana na maji.

Allaah Anasema:

وَجَعَلْنَا مِنَ الْمَاءِ كُلَّ شَيْءٍ حَيٍّ

“Na tukafanya kwa maji kila kitu kilicho hai.”

Al-Anbiyaa-30

 

Habari Muhimu Kuhusu Jeshi La Quraysh

Mchana wake siku hiyo, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwatuma watu watatu kwenda kupeleleza juu ya habari za jeshi la Maquraysh panapo kisima cha Badr, nao ni; ‘Aliy bin Abi Twaalib, Az-Zubayr bin ‘Awwaam na Sa’ad bin Abi Waqaas (Radhiya Allaahu ‘anhum). Waliwakuta vijana watatu wadogo wakichota maji kwa ajili ya kuwapelekea jeshi la Maquraysh, wakawateka na kwenda nao kambini ili kuwauliza masuali.

Walipofika nao kambini Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali, kwa hivyo wao wakaanza kuwauliza mateka wao.

Vijana hao wakasema kuwa wametumwa na Maquraysh kuwachotea maji. Maswahaba walikasirishwa na jibu hilo, kwani walitamani wawe watu wa msafara wa Abu Sufyaan. Wakawapiga sana mpaka wakasema kuwa wao ni watu wa Abu Sufyaan na si watu wa jeshi la Maquraysh. Baada ya kutamka hayo, wakawaachilia.

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumaliza kuswali akawaambia:

“Waliposema kweli mliwapiga, na walipokudanganyeni mkawachilia, walisema kweli WaLlaahi, kwani wao ni watu wa jeshi la Maquraysh.”

Kisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawuliza wale vijana:

“Nipeni habari za Maquraysh.”

Wakasema:

“Wapo katika ng’ambo ya bonde lile la mbali.”

Akawauliza;

“Wako wangapi?”

Wakasema:

“Wengi.”

Akawauliza;

“Idadi yao ngapi?”

Wakasema:

“Hatujui.”

Akawauliza;

“Wanachinja wanyama wangapi kila siku?”

Wakasema:

“Siku nyingine wanachinja ngamia tisa na siku nyingine kumi.”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kuwaambia Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhu):

“Idadi yao ni baina ya watu mia tisa na elfu.”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza tena wale vijana:

“Nani katika vigogo vya Maquraysh wamo miongoni mwao?”

Wakasema:

“‘Utbah na Shaybah watoto wa Rabiy’ah, Abu Al-Bakhtariy bin Hishaam, Haakim bin Hizaam, Nawfal bin Khuwaylid, Al-Haarith, Taymah, An-Nadhr bin Haarith, Za’amah bin Aswad, Abu Jahl bin Hishaam, na Umayyah bin Khalaf.”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kuwaambia Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum):

“Makkah imekutupieni (imekuleteeni) vipande vya maini yao.” (vigogo vyao na vipenzi vyao).

 

Kuteremka Mvua

Waislamu wakasogea mbele kidogo mpaka wakakaribia bonde la karibu na mahali yalipopiga kambi majeshi ya Maquraysh.

Allaah Aliwateremshia Waislamu utulivu wakalala vizuri, hata wengine wakaota na kuamka wakiwa na janaba.

Kwa vile mahali hapo hapakuwa na maji ya kuogea ili wapate kujitwaharisha na wala ya kunywa, Shaytwaan akaanza kuwatia wasi wasi;

“Vipi mtapigana kesho wakati miili yenu haina twahara, vipi mtapigana kesho mkiwa na kiu…?”

Allaah Akawateremshia mvua, na kutokana nayo wakaweza kujitwaharisha, kuondoa uchafu wa Shaytwaan, na kuzipa nguvu nyoyo zao, Na maji ya mvua pia yakawasaidia kuufanya mchanga chini yao uwe mgumu wakaweza kutembea vizuri bila ya kuteleza wakati wa mapambano.

Allaah Anasema:

إِذْ يُغَشِّيكُمُ النُّعَاسَ أَمَنَةً مِّنْهُ وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّنَ السَّمَاءِ مَاءً لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ وَيُذْهِبَ عَنكُمْ رِجْزَ الشَّيْطَانِ وَلِيَرْبِطَ عَلَىٰ قُلُوبِكُمْ وَيُثَبِّتَ بِهِ الْأَقْدَامَ

“Alipokufunikeni kwa usingizi uwe ni uaminisho kutoka Kwake, na Akakuteremshieni maji kutoka mbinguni ili kukusafisheni kwayo na kukuondoleeni uchafu wa Shaytwaan, na kuzipa nguvu nyoyo zenu, na kuitia imara miguu yenu.”

Al-Anfaal – 11

 

 

Jeshi La Waislamu Linashika Sehemu Muhimu

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaliamrisha jeshi lake liondoke pale walipo haraka ili wawahi kusogea mbele karibu na mahali yalipo maji ya mji wa Badr, wakasogea mpaka wakafika mwanzo wa visima vya maji ya Badr na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawawaamrisha kupiga kambi hapo.

Mmoja katika Maswahaba, Al-Khabaab bin Mundhir (Radhiya Allaahu ‘anhu), akamuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

“Ewe Mtume wa Allaah, mahala hapa tuliposimama, Allaah Amekuamrisha na hatuna haki ya kusonga mbele zaidi au ni katika hila za kivita tu na rai yako mwenyewe?”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwabia:

“Bali ni hila za kivita na rai yangu mwenyewe.”

Akasema:

“Ewe Mtume wa Allaah, mimi naona kuwa hapa si makazi mazuri, bora tusogee mbele mpaka mwisho wa visima vya maji ya Badr, tuvizunguke kisha tujenge mahodhi, tuyajaze maji, kisha tupambane nao, sisi tutakuwa tunakunywa na wao wasipate kunywa.”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

“Rai uliyotoa ni nzuri.”

Wakaondoka na kusogea sehemu ya juu ya mahali yalipo maji, na usiku wakaanza kutengeneza mahodhi na kuyajaza maji.

 

Makao Makuu Ya Jeshi

Baada ya kumaliza kazi hiyo, Sa’ad bin Mu’aadh (Radhiya Allaahu ‘anhu) akatoa rai pajengwe mahali patakapokuwa makao makuu ya jeshi lao ili waweze kujitayarisha na kuikabili hali ya hatari yoyote itakayotokea iwapo jeshi lao litashindwa katika vita hivyo.

Akasema:

“Ewe Mtume wa Allaah, unaonaje tukakujengea kipaa mfano wa hema (Ariysh), kisha tukakuwekea tayari wanyama wa kupanda, kisha sisi tutapambana na adui, ikiwa Allaah Atatujaalia tukawashinda, hayo ndiyo tunayoyapenda, ama ikiwa kinyume na hivyo, basi wewe utapanda wanyama wako na utakwenda kujiunga na wenzetu tuliowaacha nyuma, kwani hao tuliowaacha nyuma mapenzi yao juu yako ni makubwa pia kama sisi. Wangelijua kuwa utapambana na adui, basi wasingerudi nyuma na wangepigana Jihaad pamoja nawe.”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea kila la kheri kwa rai yake hiyo, na Waislamu wakajenga mfano wa hema juu ya kilima, sehemu ya Kaskazini ya uwanja wa mapambano, sehemu ambayo mtu anaweza kuviona vita vikiendelea bila ya tabu.

 

Usiku Kabla Ya Mapambano

Usiku kabla ya mapambano, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwapanga vizuri askari wake, kisha akawa anatembea huku akiwaonyesha Swahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum), mahali watakapokufa maadui mbali mbali, kabla hata vita havijaanza. Alikuwa akisema:

“Hapa ataanguka fulani, hapa atauliwa fulani …”

Alipokuwa akiwapanga watu wake, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipita mbele ya Sawaad bin ‘Aziya (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamgonga kwa nguvu tumboni pake kwa bapa la mkuki na kumwambia:

“Simama vizuri ewe Sawaad.”

Sawaad (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamwambia:

“Umeniumiza ewe Mtume wa Allaah na Mola wako Amekuleta kwa ajili ya kusimamisha haki na uadilifu, kwa hivyo uniache na mimi nikulipizie katika mwili wako.”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akalifunua tumbo lake na kumwambia:

“Jilipie kisasi chako.”

Sawaad akalikumbatia tumbo la Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huku akilibusu.

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza:

“Kipi kilichokupeleka ukafanya hivi?”

Akasema:

“Ewe Mtume wa Allaah, mambo ndiyo kama unavyoyaona (tumo vitani) na mimi nilipenda tendo langu la mwisho kabla sijafa liwe kuugusa mwili wako.”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea dua nzuri.

Baada ya kuwapanga watu wake sawa na kuwataka wasianze kupigana mpaka atoe amri, akawaambia:

“Wakianza kuja, anzeni kuwarushia mishale na msitoe panga zenu mpaka wawe karibu nanyi kabisa.”

 

Jeshi La Watu Wa Makkah

Usiku ule baadhi ya Maquraysh walijaribu kutaka kunywa maji katika mahodhi waliyoyajenga Waislamu, lakini kila aliyejaribu kuyasogelea aliuliwa, isipokuwa mtu mmoja aitwae, Haakim bin Hizaam, huyu aliachwa na alisilimu baadaye na akawa Muislamu mwema.

Maquraysh walimtuma ‘Umayr bin Wahab Al-Jahamiy aende kuchunguza nguvu za jeshi la Waislamu. Akawa anazunguka mbali na jeshi hilo akiwa juu ya farasi wake, huku na kule, kisha akarudi kwa wenzake na kuwaambia:

“Jeshi lao ni kiasi cha watu mia tatu na zaidi kidogo, lakini naona kesho mtihani utakuwa mkubwa sana, maana watu hawa hawana pa kukimbilia, na hawana cha kupoteza, wanajua kuwa wao watauliwa tu. Hawana isipokuwa panga zao tu, na nyuma yao jangwa tupu, kwa hivyo inaelekea watapigana kwa ushujaa na hawatokubali mmoja wao auliwe bila ya yeye naye kuua mtu mmoja kati yenu, kwa hivyo tazameni wenyewe.”

Pakatokea mzozo mkubwa baina ya Maquraysh, wengi wao wakamtaka Abu Jahl arudi na jeshi lake Makkah, na kwamba hapakuwa na haja ya kupigana na jeshi la Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Lakini Abu Jahl kwa haraka akafanikiwa kuuzima moto huo na kumlaumu ‘Umayr kwa kumwambia:

“Umeingiwa na hofu wewe ulipouona uso wa Muhammad, pale ulipokuwa ukiyachunguza majeshi yake ndiyo sababu ukaja na uwoga na unataka kututia na sisi uwoga huo.”

Akaweza kuwaingiza watu wake mori wa vita, kwa kuwakumbusha kuuliwa kwa ‘Amru bin Al-Hadhramiy na kwamba lazima walipe kisasi chake.

 

Majeshi Yanakabiliana

Asubuhi ya siku ya Ijumaa tarehe kumi na saba mwezi wa Ramadhaan, mwaka wa pili baada ya Hijra, majeshi hayo mawili yalipambana. Allaah Aliwafanya Waislamu walione jeshi la makafiri kuwa ni wachache ili wasiwaogope na akawafanya makafiri wawaone Waislamu pia kuwa ni wachache ili wasiwaogope na kurudi nyuma, yote haya ili kitendeke kile Anachokitaka (Subhaanahu wa Ta’alaa).

Allaah Anasema:

وَإِذْ يُرِيكُمُوهُمْ إِذِ الْتَقَيْتُمْ فِي أَعْيُنِكُمْ قَلِيلًا وَيُقَلِّلُكُمْ فِي أَعْيُنِهِمْ لِيَقْضِيَ اللَّـهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا ۗ وَإِلَى اللَّـهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ ﴿٤٤﴾ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا لَقِيتُمْ فِئَةً فَاثْبُتُوا وَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٤٥﴾

“Na mlipokutana Akakuonyesheni machoni mwenu kuwa wao ni wachache, na Akakufanyeni nyinyi ni wachache machoni mwao, ili Allaah Atimize jambo lilio kuwa liwe. Na mambo yote hurejezwa kwa Allaah.

Enyi mlioamini! Mkikutana na jeshi, basi kueni imara, na mkumbukeni Allaah sana ili mpate kufanikiwa.”

Al-Anfaal 44-45

 

Majeshi yalipoanza kupambana, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaingia ndani ya lile hema, yeye na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) peke yao, na hapana mwengine aliyeingia humo isipokuwa wao, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaanza kuomba dua huku akisema:

“Mola wangu hawa Maquraysh wamekuja kwa jeuri na kiburi chao, wakikupinga na kumkadhibisha Mtume wako, Mola wangu nitimizie yale uliyoniahidi, Mola wangu watu hawa wakishindwa leo, basi hutaabudiwa tena…” Kila vita vikipamba moto, naye huongeza kuomba dua.

Akawa anaendelea kuomba mpaka nguo yake ya begani ikamwanguka, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akaiokota na kumvisha tena huku akimwambia:

“Inatosha ewe Mtume wa Allaah, Ushamuomba vya kutosha Mola wako.”

Kisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasimama penye mlango wa Ariysh aliyojengewa akawa anaisoma aya 45 Suratul Qamar:

سَيُهْزَمُ الْجَمْعُ وَيُوَلُّونَ الدُّبُرَ

 “Wingi wao huo karibuni watashindwa na wataendeshwa mbio na watageuza migongo wanakimbizana.”

 

Mubaaraza (Mapambano Kabla Ya Vita Kuanza)

Kwa kawaida kabla ya vita kuanza, Waarabu walikuwa na tabia ya kuanzisha Mubaraza, na maana yake ni, mtu mmoja au wawili au watatu hutoka kutoka kila upande na kuanza kupambana wao kwanza kila mmoja na mwenzake mpaka wauane, kisha vita ndiyo vinaanza. Mapigano haya kwa kawaida ndiyo yanayotoa picha ndogo ya mwisho wa vita.

Katika mapigano haya, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwatoa upande wa Waislamu, ‘Aliy bin Abi Twaalib, ‘Ubaydah bin Haarith na Hamzah (Radhiya Allaahu ‘anhum), na upande wa makafiri wakatoka, ‘Utbah na ndugu yake Shaybah, na Al-Waliyd mtoto wa ‘Utbah – wote wakiwa watu wa ‘ailah moja. Katika mapigano hayo, Hamzah (Radhiya Allaahu ‘anhu), alimuua mpinzani wake Utbah.  Kisha ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu), alimuua mpinzani wake Shaibah. Lakini ‘Ubaydah (Radhiya Allaahu ‘anhu), yeye na mpinzani wake, wote wawili walijeruhiana wakaanguka chini, na ‘Aliy na Hamzah (Radhiya Allaahu ‘anhum) waliwahi kumrukia Al-Waliyd na kumuua kisha wakamuokoa mwenzao na kumvuta nyuma na kumrudisha katika kambi ya Waislamu. Lakini hatimaye kutokana na damu nyingi iliyomwagika alifariki dunia siku nne baada ya vita vya Badr kwa homa ya manjano.

Zipo khitilafu katika riwaya mbali mbali zilizopokelewa na wanahistoria juu ya nani kapambana na nani katika mubaaraza ya vita hivi, lakini riwaya inayokubalika zaidi ni hii iliyotolewa na Imaam Ahmad na Abu Daawuud inayosema kuwa ‘Aliy bin Abi Twaalib alipambana na Shaybah na Hamzah alipambana na ‘Utbah na ‘Ubaydah bin Al-Haarith alipambana na Al-Waliyd bin ‘Utbah.

Waqafaat At-Tarbawiyah uk.189

 

Mashambulio

Mapigano haya yalimaanisha mwisho mbaya wa jeshi la washirikina. Kwa sababu wamepoteza watatu katika wapiganaji wao wakubwa kwa mpigo mmoja, na kwa kawaida waarabu walikuwa na itikadi ya kuvipima vita kutokana na mapigano ya mwanzo (Mubaraza). Kwa ajili hivyo wakawavamia Waislamu kwa ghadhabu na kwa nguvu zao zote, na Waislamu wakapambana nao kwa ujasiri mkubwa.

Wakati huo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawatokea Waislamu na kuwaambia:

“Naapa kwa yule ambaye nafsi ya Muhammad ipo mikononi pake, yeyote atakayepigana nao leo kisha akauliwa akiwa katika hali ya subra, bila ya kurudi nyuma, basi Allaah Atamuingiza Peponi.”

‘Umayr bin Al-Hammaam (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akila tende, mara baada ya kusikia maneno hayo akasema:

“Hivyo baina yangu na baina ya kuingia Peponi ni kupigana na kuuliwa na watu hawa na tende hii ndiyo inayonichelewesha?”

Akazitupa tende zake, akaingia vitani, akapigana mpaka akauliwa.

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasogea mbele, akachota gao la mchanga, akawakabili Maquraysh, kisha akasema:

“Zimeangamia nyuso zao.” Kisha akawarushia.

Allaah Anasema:

فَلَمْ تَقْتُلُوهُمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ قَتَلَهُمْ ۚ وَمَا رَمَيْتَ إِذْ رَمَيْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ رَمَىٰ ۚ وَلِيُبْلِيَ الْمُؤْمِنِينَ مِنْهُ بَلَاءً حَسَنًا ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿١٧﴾ ذَٰلِكُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ مُوهِنُ كَيْدِ الْكَافِرِينَ

“Hamkuwaua nyinyi lakini Allaah ndiye Aliyewaua. Na wewe hukutupa, pale ulipotupa, lakini Allaah ndiye Aliyetupa, ili awajaribu Waumini majaribio mema yatokayo Kwake. Hakika Allaah ndiye Msikizi na Mjuzi.

Ndio hivyo! Na hakika Allaah ni Mwenye kudhoofisha vitimbi vya makafiri.”

Al-Anfaal - 17 18

 

Kisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia Swahaba zake:

“Wakazieni vizuri! inukeni muifuatilie Pepo ambayo upana wake tu ni sawa na mbingu na ardhi.”

Kisha akaondoka na kurudi penye Ariysh yake aliyojengewa.

Mapambano makali yakaanza baina ya makundi mawili hayo, na ushindi ukawa wa Waislamu. Wakauliwa waliouliwa katika vigogo vya Maquraysh na wakatekwa waliotekwa.

Haya ni mapambano ya pekee ambayo Malaika walishiriki, akiwemo Jibriyl (‘Alayhis Salaam). Baadhi ya Maswahaba walisema:

“Siku hiyo tulikuwa tukiona vichwa vikikatika tu na kuruka huku na kule, hatujui nani anayevikata.”

Allaah Anasema:

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ أَنِّي مُمِدُّكُم بِأَلْفٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُرْدِفِينَ ﴿٩﴾ وَمَا جَعَلَهُ اللَّـهُ إِلَّا بُشْرَىٰ وَلِتَطْمَئِنَّ بِهِ قُلُوبُكُمْ ۚ وَمَا النَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِندِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿١٠﴾ إِذْ يُغَشِّيكُمُ النُّعَاسَ أَمَنَةً مِّنْهُ وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّنَ السَّمَاءِ مَاءً لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ وَيُذْهِبَ عَنكُمْ رِجْزَ الشَّيْطَانِ وَلِيَرْبِطَ عَلَىٰ قُلُوبِكُمْ وَيُثَبِّتَ بِهِ الْأَقْدَامَ ﴿١١﴾ إِذْ يُوحِي رَبُّكَ إِلَى الْمَلَائِكَةِ أَنِّي مَعَكُمْ فَثَبِّتُوا الَّذِينَ آمَنُوا ۚ سَأُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُوا الرُّعْبَ فَاضْرِبُوا فَوْقَ الْأَعْنَاقِ وَاضْرِبُوا مِنْهُمْ كُلَّ بَنَانٍ ﴿١٢﴾ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ شَاقُّوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ وَمَن يُشَاقِقِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿١٣﴾ ذَٰلِكُمْ فَذُوقُوهُ وَأَنَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابَ النَّارِ ﴿١٤﴾

“Mlipokuwa mkimuomba msaada Mola wenu, naye akakujibuni kuwa: Kwa yakini Mimi nitakusaidieni kwa Malaika elfu wanao fuatana mfululizo.

Na Allaah Hakufanya haya ila kuwa ni bishara na ili nyoyo zenu zituwe. Na haupatikani ushindi ila kutoka kwa Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu, na Mwenye hikima.

Alipokufunikeni kwa usingizi uwe ni uaminisho kutoka kwake, na Akakuteremshieni maji kutoka mbinguni ili kukusafisheni kwayo na kukuondoleeni uchafu wa Shaytwaan, na kuzipa nguvu nyoyo zenu, na kuitia imara miguu yenu.

Mola wako Alipowafunulia Malaika: Hakika Mimi ni pamoja nanyi, basi watieni nguvu walioamini. Nitatia woga katika nyoyo za waliokufuru. Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole.

Hayo ni kwa sababu wamemuasi Allaah na Mtume Wake. Na mwenye kumuasi Allaah na Mtume Wake basi Allaah ni Mkali wa kuadhibu.

Ndio hivyo! Basi ionjeni! Na bila shaka makafiri wana adhabu ya Moto.”

Al-Anfaal – 9 – 14

 

Kifo Cha Abu Jahl

Abu Jahl alipoona majeshi yake yanaanza kurudi nyuma akawa anapiga kelele akisema:

“Wasikutisheni hao, msiogope kwa kuwa ‘Utbah na Al-Waliyd wameuliwa, leo hatuondoki hapa mpaka turudi nao Makkah tukiwa tumewafunga kamba wote hawa.”

Anasema ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf (Radhiya Allaahu ‘anhu): “Nilipokuwa nimesimama vitani nikageuka kutazama kuliani na kushotoni kwangu nikidhania nitaona watu wazima wamesimama nami ili tusaidiane wakati vita vikipamba moto, lakini nikavunjika moyo nilipowaona watoto wadogo wawili wamesimama mmoja kushotoni na mwengine kuliani kwangu. Nikasema moyoni mwangu: “Leo sina pa kuegemea.” Yule mtoto aliye kuliani pangu akaniomba niiname apate kuniuliza ili yule mwenzake asisikie. Akaniuliza:

“Ami! Yupi kati yao Abu Jahl?”

Nikamuuliza:

“Ewe mwana wa ndugu yangu, unamtakia nini Abu Jahl?”

Akanijibu:

“Nimesikia kuwa anamtukana Mtume wa Allaah, WaLlaahi nikimuona basi sitomwacha, lazima nitamuua.”

Na mtoto aliye kushotoni pangu akaniuliza vile vile kama mwenzake, na nikamjibu kama nilivyomjibu mwenzake na akasema yale yale aliyosema mwenzake, na nilipomuona Abu Jahl nikawaambia: “Yule rafiki yenu mnayemtafuta.”

Wote kwa pamoja panga mkononi wakamvamia na kumpiga kwa mapanga mpaka wakamuua, kisha wakakimbilia kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumjulisha. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza:

“Yupi kati yenu aliyemuua?”

Kila mmoja akasema:

“Mimi ndiye niliyemuua.”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:

“Hebu nione panga zenu.”

Akazitazama kisha akasema:

“Kweli, nyote mumeshirikiana katika kumuua.”

Kisha akasema:

“Al laa ilaaha illa Huwa” mara tatu.

Kisha akasema:

الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي صَدَقَ وَعْدَهُ ، وَنَصَرَ عَبْدَهُ ، وَهَزَمَ الأَحْزَابَ وَحْدَهُ

Alhamdu liLlaahi Lladhiy swadaqa wa’adahu, wa naswara ‘abdahu, wa hazamal ahzaaba wahdahu”.

Tunamshukuru Allaah Aliyesadikisha waadi Wake, Akampa ushindi mja Wake, na Akawashinda makundi peke Yake.

 

Katika vita hivi waliuliwa Maquraysh sabini, na wengine sabini walitekwa, na katika waliouliwa alikuwemo Firauni wa umma huu – Abu Jahl na pia ‘Utbah bin Rabiy’ah na mwanawe Al-Waliyd na nduguye Shaybah na wengi wengineo.

Na miongoni mwa mateka alikuwemo Al-’Abbaas – ami yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na ‘Aqiyl bin Abi Twaalib, - kaka yake ‘Aliy bin Abi Twaalib na Nawfal bin Al-Haarith, na Umayyah bin Khalaf na wengi wengineo.

Hawa wote walikuwa upande wa Maquraysh.

 

Mizoga Ya Makafiri

Baada ya vita kumalizika, Waislamu wakawazika Mashahiyd wao na idadi yao walikuwa kumi na nne, kisha wakaichukua mizoga ya washirikina na kuitupa katika kisima kisichokuwa na maji kilicho karibu na mahali palipotokea mapambano hayo.

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Anawasemesha Maiti Wa Quraysh

Usiku wa manane Waislamu walimsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amesimama penye kile kisima walichotupa mizoga ya Mushrikina akiwasemesha kwa ukali:

“Enyi mlio kisimani! ubaya ulioje mliokuwa nao jamaa zangu nyinyi kwa Mtume wenu! Mlinikadhibisha wakanisadiki watu (kweli), mkanitoa katika mji wangu, wakanipokea watu (kweli), mkanipiga vita wakanisaidia watu (kweli), je! Sasa nyinyi kweli mumekwisha pata yale aliyokuahidini Mola wenu? Ama mimi nimepata kweli yale aliyoniahidi Mola wangu.”

Maswahaba wakamuuliza:

“Ewe Mtume wa Mwenyei Allaah, unazungumza na watu washakuwa mizoga?”

Mtume  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

“Wao wanasikia kuliko nyinyi haya niliyowaambia isipokuwa hawawezi kujibu.”

 

Bishara Njema

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa haraka sana aliwatuma watu waende Madiynah kuwapa habari za ushindi wao mkubwa juu ya Makafiri.

Usaamah bin Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema:

“Zilitufikia habari tulipokuwa tukimzika Bibi Ruqayyah (Radhiya Allaahu ‘anha) binti wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mke wa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Zayd bin Haarithah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipoingia Msikitini, watu walimzunguka huku akisema kwa furaha:

“Amekwisha uliwa ‘Utbah bin Rabiy’ah na Shaybah bin Rabiy’ah na Abu Jahl”, akawa anawataja mmoja mmoja katika vigogo vya Maquraysh waliouliwa Badr.

Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema:

“Nikamuuliza , Baba yangu; Unasema kweli?”

Akanijibu:

“Naam, kweli mwanangu.”

 

Kuondoka Badr

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), aliondoka Badr pamoja na mateka wao na ngawira zao na alipofika karibu na Madiynah alisimamisha msafara katika bonde la Safra akawagawia Waislamu ngawira yao sawa sawa na kila anapoukaribia mji wa Madiynah, alikuta makundi kwa makundi ya watu waliosimama pembezoni mwa njia wakimpongeza.

Allaah Anasema:

إِذْ أَنتُم بِالْعُدْوَةِ الدُّنْيَا وَهُم بِالْعُدْوَةِ الْقُصْوَىٰ وَالرَّكْبُ أَسْفَلَ مِنكُمْ ۚ وَلَوْ تَوَاعَدتُّمْ لَاخْتَلَفْتُمْ فِي الْمِيعَادِ ۙ وَلَـٰكِن لِّيَقْضِيَ اللَّـهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا لِّيَهْلِكَ مَنْ هَلَكَ عَن بَيِّنَةٍ وَيَحْيَىٰ مَنْ حَيَّ عَن بَيِّنَةٍ ۗ وَإِنَّ اللَّـهَ لَسَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٤٢﴾ إِذْ يُرِيكَهُمُ اللَّـهُ فِي مَنَامِكَ قَلِيلًا ۖ وَلَوْ أَرَاكَهُمْ كَثِيرًا لَّفَشِلْتُمْ وَلَتَنَازَعْتُمْ فِي الْأَمْرِ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ سَلَّمَ ۗ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ

“Kumbukeni pale mlipokuwa nyinyi kwenye ng'ambo ya karibu ya bonde, na wao wakawa ng'ambo ya mbali, na msafara ulipokuwa chini yenu. Na ingelikuwa mmeagana mngelikhitalifiana katika miadi. Lakini (mkakutana) ili Allaah Atimize jambo liliokuwa lazima litendeke, kwa sababu aangamie wa kuangamia kwa dalili zilizo dhaahiri, na asalimike wa kusalimika kwa dalili zilizo dhaahiri. Na Allaah ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.

Kumbuka Alipokuonyesha usingizini mwako kwamba wao ni wachache - na lau Angelikuonyesha kuwa ni wengi, mngeliingiwa na woga, na mngelizozana katika jambo hilo.

Lakini Allaah Kakuvueni. Hakika Yeye ni Mwenye kuyajua yaliyo vifuani.

Al-Anfaal – 42 –43

 

Matukio Mbali Mbali

Baada ya vita kumalizika, Musw’ab bin ‘Umayr   (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuona ndugu yake Abu ‘Aziyz aliyekuwa upande wa makafiri akiwa ametekwa na amefungwa kamba. Akamwambia yule aliyemfunga kamba:

“Mfunge vizuri huyo kwa sababu mama yake ana mali nyingi anaweza kumkomboa,”

Ndugu yake akamwambia:

“Huko ndiko kuwapa usia mwema ndugu yangu?”

Musw’ab akamwambia:

“Huyu aliyekukamata ni ndugu yangu zaidi kuliko wewe.”

 

Baada ya maiti za makafiri kutupwa kisimani, Abu Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘anhu) mwana wa ‘Utbah bin Rabiy’ah alikuwa na huzuni sana. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza:

“Unaona vibaya juu ya baba yako, (kwa vile ni kafiri na ametupwa kisimani na wenzake)?”

Abu Hudhayfah akasema:

“Laa WaLlaahi, ewe Mtume wa Allaah, isipokuwa baba yangu alinifanyia fadhila nyingi sana na alikuwa akinipenda, nikadhani kwa ajili hiyo naye atasilimu, na nilipomuona kuwa amekufa kafiri, ndio nikahuzunika.”

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea dua kumtakia kila la kheri.

 

Wale watoto wawili waliomuua Abu Jahl nao wana kisa chao.

Walipokuja kutaka kushiriki katika vita, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimkubali ndugu mkubwa akamkataa yule mdogo.

Mdogo akasema:

“Ewe Mtume wa Allaah, kwa nini umemkubali kaka yangu na mimi hukunikubali?”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

“Kwa sababu umri wako ni mdogo.”

Akasema:

“Lakini siku zote tukipigana mieleka, mimi namshinda kaka yangu.”

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

“Hebu piganeni mieleka nikuoneni.”

Wakapigana na yule mdogo akamshinda mkubwa wake, ndipo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomkubali.

 

‘Umar bin Al-Khattwaaba (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuua siku hiyo mjomba wake Al-’Aasw bin Hishaam, aliyekuwa upande wa makafiri.

 

Fundisho

Allaah Anasema:

وَلَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّـهُ بِبَدْرٍ وَأَنتُمْ أَذِلَّةٌ ۖ فَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

“Na Allaah Alikunusuruni katika (vita vya) Badr. Hali nyinyi mlikuwa dhaifu. Basi mcheni Allaah ili mpate kushukuru (kila wakati kwa neema zinazokujieni).”

Aali ‘Imraan – 123

 

Allaah Anatufundisha hapa kuwa ni Yeye tu mwenye kuleta nusura, na ni Yeye tu Anayestahiki kukimbiliwa wakati wa dhiki, badala ya kuwakimbilia viumbe dhaifu.

Na hili ni somo kwa wale ndugu ambao wanapokumbwa na tatizo, wanaikimbilia ile dua ya Hal Badiri (Ahl Badr) ambayo ndani yake yanatajwa majina ya Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) walioshiriki katika vita hivyo, na kuomba msaada kutoka kwao badala ya kumuomba Aliye na Nguvu (Subhaanahu wa Ta’alaa).

Allaah Aliwapa ushindi Waislamu katika vita hivi juu ya uchache wao, wakati katika vita vya Hunayn, vilivyofuatilia baada ya kutekwa mji wa Makkah, kwa mara ya mwanzo Waislamu walipigana wakiwa idadi yao kubwa zaidi kuliko ya makafiri lakini waliendeshwa mbio na makafiri mpaka Allaah Alipowateremshia utulivu kutoka Kwake.

Hakupata Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka na jeshi kubwa kuliko la siku hiyo, alipotoka na watu elfu kumi na mbili, hata Waislamu wakawa wanasema:

“Hatutoshindwa leo kwa sababu ya uchache wetu” (kwa vile tuko wengi leo hatutoshindwa).”

Na Allaah Anasema:

لَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّـهُ فِي مَوَاطِنَ كَثِيرَةٍ ۙ وَيَوْمَ حُنَيْنٍ ۙ إِذْ أَعْجَبَتْكُمْ كَثْرَتُكُمْ فَلَمْ تُغْنِ عَنكُمْ شَيْئًا وَضَاقَتْ عَلَيْكُمُ الْأَرْضُ بِمَا رَحُبَتْ ثُمَّ وَلَّيْتُم مُّدْبِرِينَ

“Bila shaka Allaah Amekunusuruni katika mapigano mengi, na siku ya Hunayn (pia) ambapo wengi wenu ulikupandisheni kichwa, lakini haukukufaeni chochote, na ardhi ikawa dhiki juu yenu ingawa ilikuwa yenye wasaa, kisha mkageuka mkarudi nyuma”

At-Tawbah – 25

 

Anasema Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Llah): “Katika vita vya Yarmuuk, ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwaambia Waislamu:

“Mtakapotaka msaada katika vita hivi, basi muandikieni Abu ‘Ubaydah.” Vita vilipoanza, wakamuandikia Abu ‘Ubaydah aje kuwasaidia kwa sababu walikuwa katika hatari. Abu ‘Ubaydah akawaandikia yafuatayo:

“Imenifikia barua yenu ikitaka msaada kutoka kwangu, lakini mimi nitakujulisheni yule Atakayeweza kukusaidieni mkapata ushindi kuliko nitakavyoweza kukusaidieni mimi; - Allaahu ‘Azza wa Jalla – ombeni msaada kutoka kwake mkitaka kupata ushindi, kwa sababu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Alipewa ushindi na Allaah siku ya Badr akiwa na watu wachache kuliko nyinyi. Itakapokufikieni barua yangu hii, piganeni nao na wala msiniandikie mimi.”

Anasema Iyaadh Al-Ash‘ary, mwenye kuisimulia kisa hiki:

“Tukapambana nao na tukawashinda, na tukapata ngawira nyingi siku hiyo.

 

Mateka Wa Badr

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa baada ya kutekwa waliotekwa siku ya Badr, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwauliza Abu Bakr na ‘Umar: “Mnaonaje juu ya (tuwafanye nini) hawa mateka?” Abu Bakr akasema: “Ewe Mtume wa Allaah, hawa ni wana wa ami zetu na jamaa zetu, naona bora tuwatoze fidia ili tuwe na nguvu dhidi ya makafiri, na huenda Allaah Akawahidi wakaingia katika Dini ya Uislamu.” Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamgeukia ‘Umar na kumuuliza: “Unaonaje ewe mwana wa Al-Khattwaab?” Akasema: “Hapana WaLlaahi, sikubaliani na rai ya Abu Bakr, bali naona uturuhusu tuwakate vichwa vyao. Umruhusu ‘Aliy amkate kichwa (kaka yake) Aqiyl, na uniruhusu mimi nimkate kichwa (shemeji yangu) fulani, ili Allaah Aelewe kuwa hatuna mchezo dhidi ya makafiri, kwani hawa ni viongozi wa makafiri na vigogo vyao.”

Alisema ‘Umar: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akafuata rai ya Abu Bakr akapokea fidia, na hakupendezewa na rai yangu. Na siku ya pili yake nikawakuta Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Abu Bakr wamekaa wanalia. Nikasema: “Ewe Mtume wa Allaah, niambieni kwa nini unalia wewe na sahibu yako ili kama kitaniliza na miye pia nilie na kama hakitoniliza basi nijilize tu kama mnavyolia.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ninalia kutokana na kufuata rai ya sahibu zako ya kuchukua fidia.”

Allaah Aliteremsha iliyokubaliana na rai ya ‘Umar bin Al-Khattwaab Aliposema:

مَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَكُونَ لَهُ أَسْرَىٰ حَتَّىٰ يُثْخِنَ فِي الأرْضِ ۚ تُرِيدُونَ عَرَضَ الدُّنْيَا وَاللَّـهُ يُرِيدُ الآخِرَةَ ۗ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٦٧﴾ لَّوْلا كِتَابٌ مِّنَ اللَّـهِ سَبَقَ لَمَسَّكُمْ فِيمَا أَخَذْتُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿٦٨﴾

Haimfalii Nabii yeyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda barabara katika nchi. Mnataka vitu vya dunia, na Allaah Anataka Akhera. Na Allaah ni Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima.

Lau isingelikuwa hukumu iliyokwisha tangulia kutoka kwa Allaah ingelikupateni adhabu kubwa kwa vile mlivyochukua.

Al-Anfaal – 67

 

Mpango Wa Kumuua Mtume Wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

Baada ya kushindwa vibaya katika vita vya Badr, wababe wawili walikutana mjini Makkah kupanga mpango wa kumuua Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na majina yao ni ‘Umayr bin Wahab Al-Jumuhiy na Safwaan bin Umayyah, na Umayyah huyu alikuwa mtu muovu sana aliyekuwa akimfanyia vitendo vya udhia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) walipokuwa Makkah.

Safwaan akasema: “WaLlaahi maisha hayana kheri tena baada ya watu wetu waliouliwa na kujeruhiwa.”

‘Umayr akasema: “Umesema kweli WaLlaahi, lau kama si deni nilokuwa nalo na watoto ninaowaogopea wasije kupotea, ningekwenda mpaka kwa Muhammad na kumuua, kwani nina mwanangu mateka kwao.”

Safwaan akasema: “Mimi nitakulipia deni lako na wanao nitawachanganya na wanangu.”

‘Umayr   akasema: “Basi usimwambie mtu yoyote (nakwenda Madiynah kumuua Muhammad).”

Kisha ‘Umayr   akautoa upanga wake na kuupaka sumu, kisha akaifunga safari ya kuelekea Madiynah. Alipokuwa panapo mlango wa Msikiti wa Madiynah akimfunga farasi wake, ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akizungumza na kundi la Waislamu juu ya mafanikio yao katika vita vya Badr akamuona, akasema: “Mbwa huyu adui wa Allaah hakuja isipokuwa kwa shari. Akamkamata, kisha akaingia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), akamuambia: “Ewe Nabii wa Allaah! Adui wa Allaah ‘Umayr   amekuja panga mkononi.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: “Muingize ndani.” ‘Umar akawaambia watu wa Madiynah: “Muingizeni kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) lakini tahadharini naye kwani hana mwamana khabithi huyu.”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomuona akiingizwa huku ‘Umar bin Al-Khattwaab amemwekea upanga shingoni pake akamuambia: “Uondoe upanga. Sogea karibu ewe ‘Umayr.” Akasogea huku akiamkia: “Asubuhi njema.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: “Allaah Ametukirimu kwa maamkio yaliyo bora kuliko hivyo ewe ‘Umayr, nayo ni Salaam maamkizi ya watu wa Peponi.”

Kisha akamuambia: “Kipi kilichokuleta ewe ‘Umayr?” Akasema: “Nimekuja kumkomboa mateka aliye mikononi mwenu, kwa hivyo mtendeeni vyema.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: “Na huo upanga uliouficha?” Akasema: “Mungu aulani upanga, kwani umetuletea kheri gani?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: “Niambie kweli. Umekuja kwa ajili gani?” Akasema: “Hakikunileta isipokuwa hilo tu.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: “Bali ulikaa wewe na Safwaan bin Umayyah mkiwakumbuka waliokufa katika vita vya Badr, kisha ukasema: ‘Lau kama si deni nilokuwa nalo na watoto ninaowaogopea wasije kupotea, ningekwenda mpaka kwa Muhammad na kumuua, kwani nina mwanangu mateka kwao.” Na Safwaan akakuambia kuwa yeye atayashughulikia yote hayo, deni lako na watoto wako ikiwa utaniua, lakini Allaah Ndiye Aliyekufanya usiweze kuyatimiza.”

‘Umayr akasema: “Nashuhudia kuwa wewe ni Mtume wa Allaah. Tulikuwa tukikukadhibisha juu ya habari za mbinguni ulizokuwa ukituletea na Wahyi uliokuwa ukiteremshiwa, na jambo hili hajakuwepo mwengine isipokuwa mimi na Safwaan. WaLlaahi naelewa kuwa hapana aliyekupa habari hizi isipokuwa Allaah. Namshukuru Allaah Aliyeniongoza katika Uislamu na kunifikisha hapa aliponifikisha.” Kisha akaitamka shahada ya haki, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Mfundisheni ndugu yenu mambo ya Dini yake na mfundisheni Qur-aan na mwachieni huru mfungwa wake.”

Akarudi Makkah na kuwalingania watu katika Dini, na watu wengi walisilimu mkononi mwake.

 

Bani Qaynuqaa Wanavunja Mkataba

Kama ilivyo kawaida yao Mayahudi siku zote ni kwenda kinyume na mikataba na makubaliano. Haya yalikuwepo hata kabla ya kuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), wakaendelea nayo tabia hiyo wakati wake Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na hadi hivi sasa Mayahudi wanajulikana kuwa ni watu wanaopenda kwenda kinyume na mikataba na kuivunja, kila wanapojiona kuwa wana nguvu au wapo wanaowategemea wanaoweza kuwasaidia.

Baada ya Waislamu kushinda katika vita vya Badr, chuki ilizidi kuunguza nyoyo zao. Mayahudi wa kabila la Bani Qaynuqaa waliokuwa wafanya biashara maarufu na matajiri, wakiishi katika mtaa wao Madiynah mjini pamoja na Waislamu, waliuvunja mkataba waliotiliana sahihi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na hawa walikuwa na jeshi la wapiganaji mahodari wapatao mia saba, na mojawapo ya makubaliano ya mkataba ilikuwa; ‘Pande zote (Mayahudi na Waislamu) zisitendeane maovu.’

Baada ya vita vya Badr, chuki walioificha nyoyoni mwao waliidhihirisha kwa kuwafanyia istihzai Waislamu na kuwatupia maneno ya chuki, na wakati mwingine waliwafanyia maskhara hata wanawake wa Kiislamu wanaokwenda kununua katika maduka yao.

Anasema Ibn Hishaam, kutoka kwa Abu ‘Awn, kuwa siku moja mwanamke wa Kiarabu alikwenda kununua dhahabu kwa Mayahudi, wakamtaka aufunue uso wake. Mwanamke alikataa, na alipokuwa amekaa hana habari, mmoja kati ya Mayahudi alimjia kwa nyuma akichukua ncha ya chini ya nyuma ya nguo yake na kuifunga na sehemu ya juu ya mgongo, na alipoinuka alikashifika utupu wake. Mayahudi wakamcheka na mwanamke akapiga ukelele. Mwanamume wa Kiislamu aliyekuwepo mahali pale alimuua yule Myahudi, na Mayahudi walikusanyika wote kwa pamoja na kumuua Muislamu yule.

Ibn Hishaam 2/47,48

 

Anasema Al-Mubaarakpuri: “Siku ya Jumamosi tarehe 15 Shawwaal mwaka wa pili wa Hijra, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwazunguka Mayahudi hao muda wa siku kumi na tano, Allaah Akaingiza khofu ndani ya nyoyo zao, wakasalimu amri na kukubali masharti yote ya Waislamu.

Mali yao ikataifishwa, wakafukuzwa Madiynah, wakahamia mji unaoitwa Azru’a uliopo Syria. Waliishi hapo muda kisha wakatoweka.”

Ar-Rahiyq Al-Makhtuum – Uk.216

 

Fundisho

Anasema Al-Ustaadh ‘Abdul-Hamiyd Jaasim Al-Balaliy:

“Ukelele aloupiga mwanamke yule ulisikilizwa na wenye masikio yenye kusikia, na nyoyo zinazopiga zenye uhai na wivu na hisia na ari. Ukelele ule ulipokewa na wanaume, si wale wanaojifanya kuwa wanaume. Ukelele ule uliasisi (ulianzisha) mwamko wa kuilinda heshima ya wanawake wa Kiislamu. Kwani tokea siku ile heshima ya mwanamke wa Kiislamu ilikuwa ikilindwa. Mamilioni ya Waislamu walikuwa wakiusikia ukekele wa mwanamke yeyote na kuuitikia huku wakiungana pamoja kwenda kumsaidia kokote aliko, kila mmoja wao akiona kuwa heshima ya mwanamke huyo ikivunjwa ni sawa na kuvunjika heshima yake, hata kama hapana uhusiano wowote wa damu baina yao, isipokuwa uhusiano wao ni katika Tawhiyd (kumpwekesha Allaah).

Na wakati Al-Mu’utaswim alipokuwa Khailfa wa Waislamu, mwanamke wa Kiislamu aliyevunjiwa heshima na Warumi alipiga ukelele akisema: “Waa Mu’utaswimaa,” (Ewe Muutaswim). Habari zilipomfikia Mu’utwasim, moyo wake ulipiga kwa nguvu huku damu ikimuenda mbio, akakusanya jeshi kubwa lililofunga safari ndefu kuelekea nchi aliyopiga ukelele mwanamama yule wa Kiislamu ili kumtia adabu adui yule na kuirudisha heshima na kulipwa haki yake mwanamke yule, kisha akarudi nchini kwake baada ya kumshinda adui na kumjulisha kuwa hivi ndivyo itakavyokuwa kwa yeyote mwenye kuvunja heshima ya Muislamu.

Lakini wakati wetu huu, kelele ngapi zinapigwa wala haziwezi kuzipenya kuta za majumba ya viongozi waliokaa kimya. Kelele za ndugu zetu wa Palestina zinazopigwa kila siku dhidi ya Mayahudi, kelele za Wanawake wa Kiislamu wanaoishi ndani ya kambi za wakimbizi huko Lebanon na kelele nyingine kutoka Afghanistan na kutoka katika sehemu mbali mbali ulimwenguni, lakini hapana wa kuzisikia. Keshakufa Al-Mu’utaswim hayupo tena, kwa hivyo kelele za dada zetu hazijapata nyoyo zenye wivu zinazoitikia wala hata damu yenye kuchemka.

 

Vita Vya Uhud

Hazikuwa na tena raha wala hazikuweza kutulia nyoyo za washirikina wa Makkah baada ya kushindwa katika vita vya Badr. Walikuwa katika mikutano yao yote wakizungumza namna ya kulipa kisasi dhidi ya Waislamu. Wakatia azma kuwa lazima vita vipiganwe kwa ajili ya kulipa kisasi chao na kuziosha huzuni zao.

Waliokuwa na nashati na hamasa zaidi katika kutayarisha vita hivi upande wa washirikina ni ‘Ikrimah bin Abi Jahl, Safwaan bin Umayyah na Abu Sufyaan bin Harb na ‘Abdullaah bin Abi Rabiy’ah. Walitayarisha jeshi kubwa lililokusanya watu wa makabila maarufu ya Bani Kinaanah na Tihama na mabedui wa Ahaabish na makabila mbali mbali ya Kiarabu, waliowajaza chuki nyoyoni mwao kwa njia ya khutbah kali kali na kuwaajiri washairi wenye kuhamasisha akiwemo mshairi maarufu Abu ‘Izzah aliyetekwa katika vita vya Badr lakini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuacha huru bila kumtoza fidia baada ya kutoa ahadi kuwa hatopigana tena dhidi ya majeshi ya Kiislamu. Mshairi huyo alikubali kushirikiana na washirikina baada ya kuahidiwa kuwa akirudi vitani yuhai atapewa utajiri mkubwa na kama atauawa basi binti zake watapewa malezi mazuri.

Kutokana na uovu wao huu Allaah Anasema:

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ لِيَصُدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ فَسَيُنفِقُونَهَا ثُمَّ تَكُونُ عَلَيْهِمْ حَسْرَةً ثُمَّ يُغْلَبُونَ ۗ وَالَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ يُحْشَرُونَ

“Hakika wale waliokufuru hutoa mali yao ili kuzuilia Njia ya Allaah. Basi watayatoa, kisha yatakuwa juu yao majuto, na kisha watashindwa. Na wale waliokufuru watakusanywa kwenye Jahannam.”

Al-Anfaal – 36

 

Baada ya kutimia mwaka mmoja tokea vita vya Badr, washirikina waliweza kukusanya jeshi kubwa la wapiganaji wapatao elfu tatu. Waliondoka Makkah wakifuatana na wanawake wapatao kumi na tano pamoja na ngamia elfu tatu na farasi mia mbili pamoja na ngao mia saba.

Mkuu wa majeshi alikuwa Abu Sufyaan na mkuu wa wapanda farasi alikuwa Khaalid bin Waliyd, akisaidiwa na ‘Ikrimah bin Abi Jahl (kabla ya wote hawa kusilimu).

Al-’Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu), ami yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa keshasilimu kwa siri, baada ya kuona jeshi likiondoka, alimjulisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuandika barua aliyompa mjumbe wake aliyeweza kulikata jangwa lenye umbali wa kilomita mia tano kutoka Makkah hadi Madiynah kwa muda wa siku tatu na kumkabidhi barua hiyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwpo Msikiti wa Qubaa.

Ubay bin Ka’ab (Radhiya Allaahu ‘anhu) ndiye aliyemsomea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) barua hiyo, aliyemtaka asimhadithie mtu, kisha akarudi haraka Madiynah kwa ajili ya mashauriano na viongozi wa watu wa Muhaajiriyn na Answaar.

Waislamu wakawa wanachunguza na kufuatilia harakati zote za jeshi la washirikina huku wakijiandaa kwa kunoa panga zao na kukusanya kila kinachoweza kukusanywa katika wanyama wa kupanda na wa kuchinja kwa ajili ya mapambano hayo, wakati huo huo kila mara wakipeleka doria kupeleleza wasije wakavamiwa ghafla.

 

 

 

 


[1] Al-Bidaayah wan-Nihaayah juz.2 mlango wa ‘Q’iswat Saba-a’.

 

[2] Anasema mwanachuoni maarufu Swafiyur-Rahmaan Al-Mubaarakpuri mwandishi wa kitabu cha Ar-Rahiyq Al-Makhtuum kuwa;”Inavyojulikana ni kuwa Bibi Haajar alikuwa Mtumwa wa mfalme wa Misri, lakini kutokana na tahakiki iliyofanywa na mwanachuoni maarufu anayeitwa Al-Qaadhiy Muhammad Sulaymaan Al-Mansuur imethibiti kuwa Bibi Haajar hakuwa mtumwa, bali alikuwa binti wa Mfalme huyo wa Misri”.

[3] Al-Bidaayah wan-Nihaayah mlango wa ‘Shajarat tuba’ juz, 2.

[4] Fat-hul Baariy juz, 3 mlango wa Hijjah.

[5] Mji huu hivi sasa upo chini ya utawala wa Saudia, lakini wakati huo ulikuwa ndani ya utawala wa Yemen.

 

[6] Haadhal Habiyb’ uk. 35.

 

[7] Swahiyh Muslim mlango Naar yadkhuluhal jabbaaruun’

[8] Muslim – mlango wa ‘swifat allatiy yu’araf biha fid duniya ahlul jannah wa ahlun naar’ (juz.4)

 

[9] Fat-hul Baariy – Kitabul Manaaqib – Bab hadith ‘Amru bin Nufayl.

 

[10] Haadhal Habiyb – Abu Bakr Al-Jazaairiy uk.48

[11] Muslim – mlango wa ‘sifat allatiy yu’araf biha fid duniya ahlul jannah wa ahlun naar (juz.4). As-Suyuutwiy katika Al-Jamail Asw-Swaghiyr hadithi nambari 414. Al-Haythamiy katika Az-Zawaaid hadithi nambari 49/10. Atw-Twabaraaniy – Al-Kabiyr na Al-Awswat 34027. Ibn Hajar – Al-Iswaabah – hadithi nambari 4645, uk. 95.

[12] As-Suyuutwiy katika Al-Jamail Asw-Swaghiyr hadithi nambari 414.

[13] Hadithi hii imedhoofishwa na Ibn Hajar katika Al-Iswaabah Juzuu ya 4.

[14] Al-Bukhaariy.

 

[15] Qaaf – 2-4.

[16] Al-Maaidah – 90.

[17] Mujama’ Al-Amthaal kilichoandikwa na Abul Fadhl Midani namba 2925.

[18] Waqafaat Tarbawiyah – uk.34.

[19] Al-Anfaal - 63

[20] Aali ‘Imraan - 103

[21] Ar-Rahiyq Al-Makhtuum – uk.40

[22] Siyratu Ibn Hishaam- juzuu 1 ‘kuzaliwa kwa ‘Abdul-Muttwallib.

[23] Al-Bidaayah wan-Nihaayah – juzuu ya 2 mlango wa ‘Tajdiyd hufar zamzam. Ibn Hishaam juzuu 1, uk. 278 (lafdhi ya Al-Bidaayah wan-Nihaayah) kama ilivyoelezwa na mwana historia Ibn Is-haaq.

[24] Taarikh Atw-Twabariy juz.2 uk. 239 - 240

[25] Suratul Fiyl

[26] Waqafaat Tarbawiyah – Ahmad Farid uk.47

[27] Mukhtasar Siyratur Rasuul kilichoandikwa na Shaykh ‘Abdullaah An-Najdiy uk.13

[28] Ibn Hishaam – 1/162-163

[29] Hivi ndivyo ilivyoelezwa na waandishi wa Siyrah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘‘alayhi wa sallam),  ama Ibn Ish-aq yeye anasema kuwa tukio hili lilitokea wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘‘alayhi wa sallam) alipokuwa na umri wa miaka mitatu. Ibn Hishaam – 1/164-165

[30] Muslim – Mlango wa Israa 1/92

[31] Ibn Hishaam – 1/168

[32] Ibn Hishaam 128/1

[33] Ipo khitilafu baina ya maulamaa juu ya hadithi hii. Imaam Adh-Dhahabiy na Al-Haakim wao wamesema kuwa ni hadithi sahihi, lakini hadithi hii imedhoofishwa na Ibn Kathiyr katika Al-Bidaayah wan-Nihaayah 287/2

[34] Mukhtasar ya Siyrah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) - ‘Abdullaah An-Najdiy – uk. 15-16

[35] Ibn Hishaam 1/113-135. Na Mukhstasar Siyrat Ar-Rasuul Shaykh ‘Abdullaah An-Najdiy uk.30-31

[36] Ibn Hishaam –1/166

[37] Ibn Hishaam – 1/187 - 188

[38] Ibn Hishaam – 1/189 - 190

[39] Ibn Hishaam 1/190-191 - Fat-hul Baariy 7/507. Zipo khitilafu katika riwaya hizi na sisi tumechagua zinazokubalika zaidi.

[40] Ibn Hishaam 192/12. Swahiyh Al-Bukhaariy mlango wa Fadhila za mji wa Makkah na majengo yake 315/1

 

[41] Rahmatul Lil ‘Aalamiyn 1/47 – Ibn Hishaam 1/235 - 236

[42] Fat-hul Baariy-1/27

[43] Swahiyh al Al-Bukhaariy 1/2,3

[44] Ibn Hishaam – 1/237-238

[45] Suratul Mudaththir 1-5

[46] Swahiyh Al-Bukhaariy – 2/733

[47] Haadhal Habiyb, Abu Bakr Al-Jazaairy uk.95

[48] Muslim katika mlango wa Iymaan na Al-Bukhaariy katika ‘Manaaqib al-Answaar’

[49] Muslim (7/3) kitabu cha Al-Iymaan na At-Tirmidhiy kitabu cha At-Tafsiyr

[50] Muslim katika kitabu cha Al-Iymaan na At-Tirmidhiy katika At-Tafsiyr (12/172)

[51] Waqafaat Tarbawiyah uk.120-121

[52] Al-Bukhaariy - mlango wa Halaawatul Iymaan

[53] Muslim 227/16

[54] Muslim

[55] Ar-Rahiyq Al-Makhtuum uk.139

[56] Ar-Rahiyq Al-Makhtuum – uk.174

[57] Al-Bukhaariy

 

[58] Muslim

[59] Al-Bukhaariy

[60] Al-Bukhaariy 1/6

[61] Al-Bukhaariy na Muslim

[62] Al-Bukhaariy

[63] Al-Bukhaariy na Muslim

[64] At-Tirmidhiy na Abu Daawuud

Share