01-Swabrun Jamiyl: Maana Na Aina Za Subira

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

01-Maana Na Aina Za Subira

  

 

Subira imegawika katika sehemu nne:

 

 

1. Subira katika utiifu.

 

Inahusiana na 'amali anazotenda mja kwa kutumia mwili (vitendo vya 'ibaadah) au ulimi wake (kumdhukuru Allaah).

 

 

2. Subira katika maasi.

 

Ni kuacha kutenda jambo lisilokuwa lenye kuridhisha kwa kutumia mwili au ulimi wake. 

 

 

3. Subira katika Qadhwaa na Qadar: (Yaliyohukumiwa na Yaliyokadiriwa) na Allaah:

 

Ni kuzuia nafsi isiungulike au isihamanike au isighadhibike kutokana na mitihani inayomsibu mtu.

 

 

4. Subira kutokana na maudhi ya watu.

 

Ni subira kutokana na maudhi ya watu ni kuzuia nafsi, ulimi na viungo visilipize maovu anayotendewa mtu. Kusubiri kote huko ni kwa ajili ya kupata radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَاصْبِرْ نَفْسَكَ مَعَ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ﴿٢٨﴾ ۖ 

Na isubirishe nafsi yako pamoja na wale wanaomuomba Rabb wao asubuhi kabla jua kucha na jioni, wanataka Wajihi Wake. [Al Kahf: 28]

 

 

Ibnul-Qayyim amemsikia Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah akisema:

 

“Subira katika kutekeleza maamrisho na Allaah ni jambo zito na lilikamilika zaidi kuliko subira katika kujiepusha na yaliyoharamishwa. Kwani maslaha yanayopatikana kwa kutenda maamrisho Yake Allaah yanapendwa zaidi na Allaah kuliko kuacha maasi. Na madhara yanayopatikana kwa kuacha kutekeleza maamrisho ya Allaah ni makubwa na yanachukiza zaidi mbele ya Allaah kuliko madhara ya kuwepo na maasia.” [Madaarij As-Saalikiyn]

 

 

1-Subira Katika Utiifu

 

Kunahitajika subira katika utiifu kwani baadhi ya ‘ibaadah zina tabu na mashaka na nyinginezo zinahitaji imani na azimio la nguvu hata nafsi iridhike. Mfano mtu anapoamka usiku akiwa hakushiba usingizi lakini pamoja na hayo anajitahidi kuamka kwa ajili ya Qiyaamul-layl (kisimamo cha usiku kuswali) au kuamka mapema kwenda Msikitini na pengine hali ya hewa ni baridi kali, au Swawm masiku marefu ya joto kali, au kuitolea mali yake aipendayo Zakaah na Swadaqah, au kuvumilia misukusuko inayopatikana katika kutekeleza ‘ibaada ya Hajj n.k. Yote hayo ni  ‘ibaadah na anaifanya kwa ustahmilivu. Mifano yake ni kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ ﴿٤٥﴾

Na tafuteni msaada kupitia subira na Swalaah; na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu. [Al-Baqarah: 45]

 

وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا﴿١٣٢﴾ ۖ 

Na amrisha ahli zako Swalaah, na dumisha kusubiri kwayo. [Twaahaa: 132]         

 

 تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿١٦﴾

Mbavu zao zinatengana na vitanda, wanamuomba Rabb wao kwa khofu na matumaini, na katika yale Tuliyowaruzuku wanatoa.  [As-Sajdah: 16]

 

 

 

2-Subira Katika Maasi

 

Mja anahitaji subira katika maasi kwani binaadamu hukabiliwa na yaliyo haramu na machafu; mfano kula ribaa na mali za mayatima, kuchukua haki za watu ikiwa ni mali au heshima ya mtu, kuzuia ulimi usitaje ya upuuzi au ghibyah (kumteta, kumsengenya mtu), an-Namiymah (kufitinisha) na kila aina ya maneno maovu. Hayo ni baadhi ya mambo ambayo nafsi hutamani kujiridhisha isikie raha na kutimiza matamanio yake, na shaytwaan humtia wasiwasi na kuiamrisha hiyo nafsi itende maovu hayo kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ النَّفْسَ لَأَمَّارَةٌ بِالسُّوءِ﴿٥٣﴾

Hakika nafsi ni yenye kuamrisha sana maovu. [Yuwsuf: 53]

 

Hapo ndipo mja anapohitajika kufanya jihaad ya nafsi ajizuie na afanye subira na kutokuiendekeza nafsi yake. Imethibiti hili katika Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ فَضَالَةَ بْنِ عُبَيْدٍ (رضي الله عنه)  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ فِي حَجَّةِ الْوَدَاعِ: ((أَلاَ أُخْبِرُكُمْ  بالْمؤُمِن؟ مَنْ أَمِنَهُ النَّاسُ عَلَى أَمْوَالِهِمْ وَأَنْفُسِهِمْ  وَالْمُسْلِم  مَنْ سَلِمَ  النَّاسُ  مِنْ لِسَانِهِ وَيَدِهِ وَالْمُجَاهِدُ مَنْ جَاهَدَ نَفْسَهُ فِي طَاعَةِ اللَّهِ  وَالْمُهَاجِرُ مَنْ هَجَرَ الْخَطَايَا وَالذَّنُوبَ)) أحمد والحاكم قال الألباني  "إسناد صحيح" سلسلة الأحاديث الصحيحة

 

Kutoka kwa Fadhwaalah bin ‘Ubayd ((Je, nikujulisheni kuhusu Muumini? Ni yule anayeaminiwa na watu juu ya mali zao na nafsi zao. Na Muislamu ni yule anayeweka amani kwa watu kwa ulimi wake na mkono wake. Na mpiganaji jihaad ni yule anayefanya jihaad ya nafsi yake katika kumtii Allaah, na mhamaji hijrah ni yule anayehama makosa na madhambi)) [Ahmad na Al-Haakim. Kasema Imaam Al-Albaaniy katika Silsilatul-Ahaadiyth Asw-Swahiyhah: “Hii isnaad ni Swahiyh”]

 

 

Ndio maana Jannah (Pepo) ikawa si wepesi kuipata kwani imezungukwa na mazito na magumu (kuyatenda), na moto ukawa wepesi kuufikia kwa kuzungukwa na matamanio kama alivyotuelezea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth Al-Qudsiy:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ عَنْ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((لَمَّا خَلَقَ اللَّهُ الْجَنَّةَ وَالنَّارَ أَرْسَلَ جِبْرِيلَ إِلَى الْجَنَّةِ فَقَال: انْظُرْ إِلَيْهَا وَإِلَى مَا أَعْدَدْتُ لِأَهْلِهَا فِيهَاز  قَالَ:  فَجَاءَهَا وَنَظَرَ إِلَيْهَا وَإِلَى مَا أَعَدَّ اللَّهُ لِأَهْلِهَا فِيهَا.  قَالَ:  فَرَجَعَ إِلَيْهِ قَالَ: فَوَعِزَّتِكَ لَا يَسْمَعُ بِهَا أَحَدٌ إِلَّا دَخَلَهَا. فَأَمَرَ بِهَا فَحُفَّتْ بِالْمَكَارِهِ. فَقَالَ: ارْجِعْ إِلَيْهَا فَانْظُرْ إِلَى مَا أَعْدَدْتُ لِأَهْلِهَا فِيهَا  قَالَ: فَرَجَعَ إِلَيْهَا فَإِذَا هِيَ قَدْ حُفَّتْ بِالْمَكَارِهِ  فَرَجَعَ إِلَيْهِ فَقَالَ: وَعِزَّتِكَ لَقَدْ خِفْتُ أَنْ لَا يَدْخُلَهَا أَحَدٌ. قَالَ: اذْهَبْ إِلَى النَّارِ فَانْظُرْ إِلَيْهَا وَإِلَى مَا أَعْدَدْتُ لِأَهْلِهَا فِيهَا.  فَإِذَا هِيَ يَرْكَبُ بَعْضُهَا بَعْضًا.  فَرَجَعَ إِلَيْهِ فَقَالَ: وَعِزَّتِكَ لَا يَسْمَعُ بِهَا أَحَدٌ فَيَدْخُلَهَا. فَأَمَرَ بِهَا فَحُفَّتْ بِالشَّهَوَاتِ فَقَالَ: ارْجِعْ إِلَيْهَا فَرَجَعَ إِلَيْهَا فَقَالَ: وَعِزَّتِكَ لَقَدْ خَشِيتُ أَنْ لَا يَنْجُوَ مِنْهَا أَحَدٌ إِلَّا دَخَلَهَا)) الترمذي و قال حديث حسن صحيح – ابو داود والنسائي

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Alipoumba Jannah na moto, Alimtuma Jibriyl Jannah Akimwambia: Iangalie na angalia matayarisho Nliyoyatayarisha kwa ajili ya wakaazi wake. Akasema (Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Kwa hivyo alikuja kuiangalia na kuangalia matayarisho Allaah Aliyofanya kwa ajili ya wakazi wake. Akasema: Akarejea kwa Allaah na kusema: Kwa Utukufu Wako, hakuna atakayesikia (habari yake) ila tu ataingia (Peponi). Kisha Akaamrisha izungushwe (ihusishwe) mambo magumu watu wasiyoyapenda, Akasema: Rejea na angalia yale Niliyoyatayarisha kwa ajili ya wakaazi wake. Akasema: Kisha akarejea na akakuta imezungukwa na mambo magumu watu wasiyoyapenda. Hapo alirejea kwa Allaah na akasema: Kwa utukufu Wako, nina khofu hakuna hata mtu mmoja atakayeingia. Akasema: Nenda motoni ukauangalie na uangalie matayarisho Yangu kwa ajili ya wakaazi wake. Akaona ulikuwa na matabaka moja juu ya tabaka jingine. Akarejea kwa Allaah na akamuambia: Kwa Utukufu Wako hakuna hata mmoja ausikiae (sifa zake) atakayeingia. Kisha Allaah Aliamrisha Uhusishwe na shahawaat (matamanio ya nafsi). Kisha Allaah Akamuambia: Rejea tena (motoni). Alirejea tena na akasema: Kwa Utukufu, wako nakhofia kuwa hapatakuwa na yeyote atakayenusurika nao)) [At-Tirmidhiy akasema ni Hadiyth Hasan, na Abu Daawuwd na An-Nasaaiy]

 

 

 

3-Subira katika Qadhwaa na Qadar (Yaliyohukumiwa na Yaliyokadiriwa) na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

Majaaliwa yanaweza kuwa katika yale ya kheri au ni katika mitihani inayomsibu mtu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَنَبْلُوكُم بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً﴿٣٥﴾ ۖ 

Na Tutakujaribuni kwa mitihani ya shari na kheri. [Al-Anbiyaa: 35]

 

فَأَمَّا الْإِنسَانُ إِذَا مَا ابْتَلَاهُ رَبُّهُ فَأَكْرَمَهُ وَنَعَّمَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَكْرَمَنِ ﴿١٥﴾

Basi mwana Aadam pale Rabb wake Anapomtia mtihanini, Akamtakaramu na Akamneemesha, husema: “Rabb wangu Amenitakarimu.”

 

وَأَمَّا إِذَا مَا ابْتَلَاهُ فَقَدَرَ عَلَيْهِ رِزْقَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَهَانَنِ ﴿١٦﴾

Ama Anapomtia mtihanini, Akamdhikishia riziki yake, husema: “Rabb wangu Amenidunisha.” [Al-Fajr: 15–16]

 

Aina hii ya Subira inahusiana pia na aina za misiba inayomsibu mtu ikiwa ni kifo cha mpenzi wake, mali, maradhi, shida, huzuni, dhiki, maafa n.k.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٥﴾

Na bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao. Na wabashirie wenye kusubiri.

 

الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ﴿١٥٦﴾

Wale ambao unapowafika msiba husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.”

 

أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ ﴿١٥٧﴾

Hao zitakuwa juu yao Barakah kutoka kwa Rabb wao na rahmah, na hao ndio wenye kuongoka. [Al-Baqarah: 155–157]

 

 

 

4-Subira Kutokana Na Maudhi ya watu:

 

Miongoni mwayo, inayohitajia subira ya hali ya juu ni dhulma na maudhi ya watu. Na ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Ametaja kuwa subira ya aina hii inahitajika azimio la nguvu kuvumilia na kutokulipizia na kusamehe watu wanaosababisha  hayo:

 

وَلَمَنِ انتَصَرَ بَعْدَ ظُلْمِهِ فَأُولَـٰئِكَ مَا عَلَيْهِم مِّن سَبِيلٍ﴿٤١﴾

Na bila shaka anayelipiza kisasi baada ya kudhulumiwa, basi hao hawana sababu ya kulaumiwa.

 

 

إِنَّمَا السَّبِيلُ عَلَى الَّذِينَ يَظْلِمُونَ النَّاسَ وَيَبْغُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿٤٢﴾

Hakika sababu ya kulaumiwa ni juu ya wale wanaodhulumu watu na wanakandamiza katika ardhi bila ya haki. Hao watapata adhabu iumizayo.

 

وَلَمَن صَبَرَ وَغَفَرَ إِنَّ ذَٰلِكَ لَمِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ﴿٤٣﴾

Na atakayevuta subira na akasamehe, hakika hilo bila shaka ni katika mambo ya kuazimiwa. [Ash-Shuwraa: 41–43]

 

 

Juu ya kuwa imeruhusiwa kulipiza dhulma au mateso, lililo bora zaidi ni kuvumilia kwani huko ni kwa ajili ya kupata Radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kutegemea malipo mema. Na juu ya hivyo ni dalili ya taqwa na kuwa na sifa ya ihsaan  ambayo inampatia fadhila Muislamu ya kwamba Allaah Yu pamoja naye daima. Anasema hayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَإِنْ عَاقَبْتُمْ فَعَاقِبُوا بِمِثْلِ مَا عُوقِبْتُم بِهِ ۖ وَلَئِن صَبَرْتُمْ لَهُوَ خَيْرٌ لِّلصَّابِرِينَ﴿١٢٦﴾

Na mkilipiza, basi lipizeni kulingana na vile mlivyoadhibiwa. Na mkisubiri, basi bila shaka hivyo ni bora kwa wenye kusubiri.

 

وَاصْبِرْ وَمَا صَبْرُكَ إِلَّا بِاللَّـهِ ۚ وَلَا تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَلَا تَكُ فِي ضَيْقٍ مِّمَّا يَمْكُرُونَ﴿١٢٧﴾

Na subiri (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), na haiwi subira yako isipokuwa kupitia kwa Allaah. Na wala usiwahuzunukie, na wala usiwe katika dhiki kutokana na njama wanazozifanya. 

 

 

إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الَّذِينَ اتَّقَوا وَّالَّذِينَ هُم مُّحْسِنُونَ﴿١٢٨﴾

Hakika Allaah Yu Pamoja na wenye taqwa, na wale ambao wao ni wenye kufanya ihsaan. [An-Nahl: 126–128]

 

 

Aina hii ya subira inawahusu pia walinganiaji Dini yetu ya Kiislamu, pale mtu anapoamrisha mema na kukataza maovu kama Luqmaan alipomuusia mwanawe:   

 

يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا أَصَابَكَ ۖ إِنَّ ذَٰلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ ﴿١٧﴾

 “Ee mwanangu! Simamisha Swalaah, na amrisha mema na kataza ya munkari, na subiri juu ya yale yatakayokusibu. Hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa. [Luqmaan: 17]

 

 

Na hii ni sifa miongoni mwa sifa za Manabii kwani walivumilia walipokadhibishwa na kuudhiwa na kaumu zao kwa kila aina ya maudhi hadi ikawa ni huzuni kubwa kwao. Nabiy Nuwh ('Alayhis-Salaam) alifanyiwa istihzaai na watu wake. Nabiy Luutw  ('Alayhis-Salaam)    alipata maudhi ya kashfa kutoka kwa watu wake. Nabiy Ibraahiym ('Alayhis-Salaam) aliingizwa kwenye moto na watu wake na akatengwa mbali. Nabiy Yuwsuf ('Alayhis-Salaam) alitaka kuuliwa na nduguze, akaingizwa kisimani, kisha akauzwa kwa bei ndogo mno, kisha akazuliwa kashfa ya mke wa Waziri, akaingizwa jela miaka kadhaa. Nabiy Swaalih ('Alayhis-Salaam) alikadhibishwa na watu wake kuhusiana na miujiza ya ngamia. Nabiy Muwsa ('Alayhis-Salaam) alipata maudhi kuanzia kwa Fir’awn hadi watu wake. Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-Salaam) alipata maudhi na kutaka kuuliwa na watu wake. Na maudhi mengi mbali mbali yalimfikia Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoudhiwa na watu wake Maquraysh wa Makkah hadi kifua chake kikawa na dhiki mno na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akampooza kwa kumwambia:      

 

وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ﴿٩٧﴾

Na kwa yakini Tunajua kwamba kifua chako kinadhikika kwa yale wanayoyasema. [Al-Hijr: 97]

 

Manabii wote hao walivumilia, wakasubiri na wakaweka dhanna nzuri kwa Rabb wao na kuamini waliyoahidiwa na wakaendelea na ulinganiaji wao wa Dini, na wakapata radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na wakawa ni wenye kushinda na kufaulu duniani na Aakhirah.

 

Share