03-Swabrun Jamiyl: Subira Katika Mitihani Kwa Ujumla
03 - Subira Katika Mitihani Kwa Ujumla
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hamkalifishi mtu jambo lolote isipokuwa kwa wasaa wake. Na Anapomkidhia mja Wake kufikwa na misiba na mitihani huwa ni kheri kwake kwani malipo yake ni ya duniani na Aakhirah. Kwa kafiri, misiba na mitihani ni kizuizi kwake kutokuweza kuendelea na shughuli zake za kikawaida. Ama Muumini huwa ni mapumziko ambapo hupata fursa zaidi kumdhukuru Rabb wake kwa kumshukuru, kusubiri na kutegemea malipo ya kufutiwa madhambi yake, au kupandishwa daraja Peponi au kupata mapenzi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) n.k. kama ilivyothibiti katika Qur-aan na Sunnah.
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ (رضي الله عنه) إِنَّ نَاسًا مِنْ الْأَنْصَارِ سَأَلُوا رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَأَعْطَاهُمْ. ثُمَّ سَأَلُوهُ فَأَعْطَاهُمْ. ثُمَّ سَأَلُوهُ فَأَعْطَاهُمْ حَتَّى نَفِدَ مَا عِنْدَهُ. فَقَالَ لَهُم حِينَ أَنْفَقَ كُلّ شَيْءٍ بِيَدِه: ((مَا يَكُونُ مِنْ خَيْرٍ فَلَنْ أَدَّخِرَهُ عَنْكُمْ وَمَنْ يَسْتَعْفِفْ يُعِفَّهُ اللَّهُ وَمَنْ يَسْتَغْنِ يُغْنِهِ اللَّهُ وَمَنْ يَتَصَبَّرْ يُصَبِّرْهُ اللَّهُ وَمَا أُعْطِيَ أَحَدٌ عَطَاءً خَيْرًا وَأَوْسَعَ مِنْ الصَّبْرِ)) متفق عليه
Kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Watu fulani miongoni mwa Answaar walimuomba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye akawapa. Kisha wakamuomba tena naye akawapa. Kisha wakamuomba tena naye akawapa, mpaka akamaliza chote alichokuwa nacho. Akawaambia baada ya kuwa ameshatoa kila kitu: ((Kheri yoyote niliyonayo siwezi kuwanyima, na mwenye kujizuia [kuomba] Allaah Atamjazi kwa kutokuomba, na mwenye kujikwasisha Allaah Atamkwasisha, na atakayejisubirisha Allaah Atampa subira. Hakuna yeyote aliyepewa zawadi bora na ilio kunjufu zaidi kuliko subira)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
La muhimu ni kwamba Muumini avumilie mtihani pale mwanzo anapopata taarifa ya msiba au mtihani. Hivyo ndivyo alivyofunzwa mwanamke aliyekuwa akilia mbele ya kaburi alozikwa kipenzi chake:
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: مَرَّ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِامْرَأَةٍ تَبْكِي عِنْدَ قَبْرٍ فَقَالَ: ((اتَّقِي اللَّهَ وَاصْبِرِي)) قَالَتْ: إِلَيْكَ عَنِّي فَإِنَّكَ لَمْ تُصَبْ بِمُصِيبَتِي وَلَمْ تَعْرِفْهُز فَقِيلَ لَهَا: إِنَّهُ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ. فَأَتَتْ بَابَ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَلَمْ تَجِدْ عِنْدَهُ بَوَّابِينَ فَقَالَتْ: لَمْ أَعْرِفْكَ. فَقَالَ: ((إِنَّمَا الصَّبْرُ عِنْدَ الصَّدْمَةِ الْأُولَى)) متفق عليه
وفي رواية مسلم "تبكي على صبي لها"
Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimpitia mwanamke analia mbele ya kaburi. Akamwambia: ((Mche Allaah na usubiri!)). Yule mwanamke akasema: “Niondokee, kwani hujafikwa na msiba kama wangu!” Wala hakumjua. Akaambiwa: “Huyo alikuwa ni Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Akaenda hadi katika mlango wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na hakuwakuta mabawabu [walinzi] akamwambia: “Nilikuwa sikujua kama ni wewe”. Akamwambia: ((Hakika subira wakati wake ni pale mwanzo wa kupata na msiba)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
Na katika riwaayah ya Muslim imesema: “Alikuwa akimlilia mwanawe”
Katika Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zimetajwa fadhila zake mbali mbali ambazo hakika Muumini anapozitambua hutuliza moyo wake, akapokea majaaliwa aliyokadiriwa na Rabb wake Aliyetukuka akakinai, akaridhika na akashukuru. Hapo ndipo itakapothibiti kwake kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:
((عَجَبًا لإَمْرِ الْمُؤْمِنِ إِنَّ أَمْرَهُ كُلَّهُ خَيْرٌ, وَلَيْسَ ذَاكَ لإَحَدٍ إلاَّ لِلْمُؤْمِنِ. إِنْ أَصَابَتْهُ سَرَّاءُ شَكَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ, وَإِنْ أَصَابَتْهُ ضَرَّاءُ صَبَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ)) مسلم
((Ajabu ya jambo la Muumin kwamba kila jambo lakeni kheri. Na halipatikani hili isipokuwa kwa Muumin. Anapofikwa na jambo zuri hushukuru nayo ni kheri kwake na anapofikwa na jambo lenye madhara husubiri nayo ni kheri kwake)) [Muslim]
Miongoni mwa fadhila hizo:
1-Atakutana na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) akiwa hana tena madhambi:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: (( مَا يَزَالُ الْبَلاَءُ بِالْمُؤْمِنِ وَالْمُؤْمِنَةِ فِي نَفْسِهِ وَوَلَدِهِ وَمَالِهِ حَتَّى يَلْقَى اللَّهَ وَمَا عَلَيْهِ خَطِيئَةٌ)) الترمذي وقال حديث حسن صحيح
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mtihani utaendelea kumpata Muumini mwanamume na Muumini mwanamke katika nafsi yake na watoto wake, na mali yake mpaka akutane na Allaah akiwa hana dhambi)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan Swahiyh].
2-Alama ya mapenzi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) - Humtakia kheri mja Anapompa mtihani duniani.
عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) قَال:َ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم: َ(( إِذَا أَرَادَ اللَّهُ بِعَبْدِهِ الْخَيْرَ عَجَّلَ لَهُ الْعُقُوبَةَ فِي الدُّنْيَا وَإِذَا أَرَادَ اللَّهُ بِعَبْدِهِ الشَّرَّ أَمْسَكَ عَنْهُ بِذَنْبِهِ حَتَّى يُوَافِيَ بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ)) وَ قال النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِنَّ عِظَمَ الْجَزَاءِ مَعَ عِظَمِ الْبَلَاءِ وَإِنَّ اللَّهَ إِذَا أَحَبَّ قَوْمًا ابْتَلَاهُمْ فَمَنْ رَضِيَ فَلَهُ الرِّضَا وَمَنْ سَخِطَ فَلَهُ السَّخَطُ)) رواه الترمذي وقال حديث حسن
Kutoka kwa Anas kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Anapompendelea mja Wake kheri, Humharakishia adhabu duniani. Na Allaah Anapomtakia mja Wake shari Humzuilia dhambi zake hata Amlipe Siku ya Qiyaamah)). Na amesema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Hakika malipo makubwa kabisa yapo pamoja na mtithani mkubwa, na hakika Allaah Anapopenda watu Huwapa mtihani. Basi atakayeridhika atapata radhi (za Allaah) na atakayechukia atapata ghadhabu)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan]
3-Alama ya imani
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((مَثَلُ الْمُؤْمِنِ كَمَثَلِ الزَّرْعِ لاَ تَزَالُ الرِّيحُ تُمِيلُهُ وَلاَ يَزَالُ الْمُؤْمِنُ يُصِيبُهُ الْبَلاَءُ. وَمَثَلُ الْمُنَافِقِ كَمَثَلِ شَجَرَةِ االأرْزِ لاَ تَهْتَزُّ حَتَّى تَسْتَحْصِدَ)) متفق عليه
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mfano wa Muumini ni kama mti ulio na rutuba, upepo unaupiga huku na kule, na ataendelea Muumini kufikwa na mitihani. Na mfano wa mnafiki ni kama mti wa seda [aina ya mti wa mbao ya mkangazi], hautikisiki hadi ung’olewe wote mara moja)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
4-Alama ya taqwa na daraja ya juu mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
عَنْ سَعْدِ بْنِ أّبِي وّقَّاصٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ: أَيُّ النَّاسِ أَشَدُّ بَلآءً؟ قَالَ: ((الأَنْبِيَاء، ثُمَّ االأَمْثَلُ فَالأَمْثَلُ، فَيُبْتَلَى الرَّجُلُ عَلَى حَسَبِ دِينِهِ. فَإِنْ كَانَ دِينُهُ صُلْبًا اشْتَدَّ بَلآؤُهُ، وَإِنْ كَانَ فِي دِينِهِ رِقَّةٌ ابْتُلِيَ عَلَى حَسَبِ دِينِهِ. فَمَا يَبْرَحُ الْبَلاَءُ بِالْعَبْدِ حَتَّى يَتْرُكَهُ يَمْشِي عَلَى الْأَرْضِ مَا عَلَيْهِ خَطِيئَةٌ)) أخرجه الترمذي) وقال: حسن صحيح. وابن ماجه وصححه الألباني
Kutoka kwa Sa’iyd bin Abi Waqqaasw (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nilisema: “Ee Rasuli wa Allaah! Watu gani wanaopata mitihani migumu zaidi? Akasema: ((Manabii, kisha mfano wake, na mfano wake. Hupewa mtihani mtu kulingana na Dini [imani] yake. Ikiwa Dini yake ni imara, mtihani wake huwa mkubwa. Na ikiwa Dini yake ni dhaifu hupewa mtihani kulingana na Dini yake. Husibiwa sana na mtihani mmojawapo hadi atatembea ardhini bila ya kuwa na dhambi)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan Swahiyh, Ibn Maajah, na Al-Albaaniy kadhalika kasema ni Swahiyh].
Aina yoyote ile ya mtihani huwa ni kheri kwa Muumini, kwani bila ya kufikwa na mitihani haitatambulika imani ya Muumini na pia kusingekuwa na fadhila kama hizo tulizoahidiwa ikiwa ni kwa kupewa mtihani mkubwa mno au mdogo mno kwa kadiri yoyote ile atakayojaribiwa nayo mtu, ikiwa ni wa kuhusu nafsi, kifo, maradhi, maudhi, au kupoteza mali, au maafa, au njaa n.k. Hata uwe mtihani huo japo ni mdogo kiasi cha mwiba, kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنهما) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَا يُصِيبُ الْمُسْلِمَ مِنْ نَصَبٍ وَلاَ وَصَبٍ وَلاَ هَمٍّ وَلاَ حُزْنٍ وَلاَ أَذًى وىَ غَمٍّ حَتَّى الشَّوْكَةِ يُشَاكُهَا إِلاَّ كَفَّرَ اللَّهُ بِهَا مِنْ خَطَايَاهُ))
Kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Muislamu hatopatwa na tabu, wala maradhi, wala hamu wala huzuni wala udhia wala ghamu [sononeko] hata mwiba unaodunga isipokuwa Allaah Humfutia madhambi yake kwa sababu ya hayo)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Ibnul-Qayyim (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake Al-Fawaaid kuhusu maisha haya ya duniani na njia ya kuelekea kwa Allaah na mitihani anayokabiliana nayo Muumini. amesema: “Ee usiyekuwa imara, uko wapi na njia hii? Njia ile ambayo Aadam alitaabika, na Nuwh alilia kwa huzuni, na Al-Khaliyl [Ibraahiym] alirushwa motoni, na Ismaa’iyl alilazwa chini kuchinjwa, na Yuwsuf aliuzwa kwa bei ndogo mno na akabakia jela miaka kadhaa, na Zakariyyah alichinjwa kwa msumeno, na bwana mtawa Yahyaa alichinjwa, Ayyuwb aliteseka na madhara makubwa, na Daawuwd alilia kupita kiasi, ‘Iysaa aliwaponyesha masikini maradhi yao akatembea na mnyama mwitu kwa ajili hiyo, na mateso mangapi ya kila aina aliteseka Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akielekea katika njia? Nawe unaishi kwa burudani na mchezo?” [Al-Fawaaid 1:42]
Ndugu Muislamu, kumbuka kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
لَا تَحْسَبُوهُ شَرًّا لَّكُم ۖ بَلْ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ﴿١١﴾
Msiichukulie kuwa ni shari kwenu, bali ni kheri kwenu. [An-Nuwr: 11]
Na pia:
وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢١٦﴾
Na asaa mkachukia jambo na hali lenyewe ni kheri kwenu. Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui. [Al-Baqarah: 216]
Basi vumilia kwa subira njema ndugu Muislamu na usikate tamaa katika kutaraji rahmah ya Allaah kwani Nabiy Ya’quwb aliwapa usia wanawe alipofikwa na msiba kwamba:
وَلَا تَيْأَسُوا مِن رَّوْحِ اللَّـهِ ۖ إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِن رَّوْحِ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ ﴿٨٧﴾
na wala msikate tamaa na faraja ya Allaah; hakika hawakati tamaa na faraja ya Allaah isipokuwa watu makafiri. [Yuwsuf: 87]